EBOLA: TUACHANE NA DAWA ZA KIZUNGU TURUDI KWENYE ASILI, KIKOMBE CHA BABU NA MUAROBAINI?. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

EBOLA: TUACHANE NA DAWA ZA KIZUNGU TURUDI KWENYE ASILI, KIKOMBE CHA BABU NA MUAROBAINI?.

Muathirika wa virusi vya Ebola
Nikiwa katika harakati zangu za ujasiriamali mitaani leo nilipita mahali fulani mara nikasikia mabishano makali yaliyokuwa yakiendelea baina ya vijana waliokuwa wamesimama kibarazani mwa duka moja. Mmoja wao aliyeonekana akiongea kwa msisitizo mkubwa alikuwa akijaribu kuwaaminisha wenzake kwamba Gonjwa hatari la Ebola limeletwa na wazungu ili kuja kuwapunguza Waafrika.

Aliendelea kudai kwamba Wazungu siyo watu wazuri, kwani hata Ukimwi nao ndio hao hao waliouleta. Akitoa sababu ni kwa nini madai hayo ni kweli alisema kuwa, haiwezekani wakashindwa kupata dawa. “Kwanini Wazungu wanaopatwa na ebola wakipelekwa kwao wanapatiwa dawa na hatimaye hupona lakini waafrika wanaachwa wakifa?, aliuliza kijana huyo kwa hasira akimaanisha baadhi ya wale madaktari waliopona baada ya kupewa madawa ya majaribio.

Nilishindwa kujizuia baada ya kusikiliza upotoshaji ule uliopitiliza, nikasogea karibu na mimi nikawa miongoni mwa wanamjadala. Nilimuuliza yule mtoa mada ikiwa kama alikuwa anafahamu kwa mara ya kwanza ugonjwa huu ulikoanzia lakini hakuonekana kuvutiwa na swali langu. Niliendelea kumuuliza ikiwa kama hao Wazungu ndio wanaowatuma Waafrika kula wanyama pori jamii ya nyani, popo na hata sokwe. 

Mjadala huu ulinikumbusha mambo mengi, Waafrika tunayowasingizia Wazungu kuwa ndiyo waliotusababishia. Hata matatizo ya kiuchumi yanayotokana na ufisadi uliokithiri mpaka hivi karibuni tumekuwa tukiendelea kuulaumu ukoloni wa wazungu kwamba ndio uliotusababishia hata baada ya miaka zaidi ya 50 ya uhuru kupita.

Utakumbuka hata chanjo za magojwa mbalimbali zimekuwa zikikataliwa maeneo mbalimbali kama Nigeria, hata na hapa Tanzania kuna wakati watu walizua madai ya ajabu kama hayo ya kupinga.Matokeo ya ujinga huo tumeshuhudia wenyewe juzi juzi katika janga hilihili la Ebola linaloendelea huko Afrika ya Magharibi, Kusinimashariki mwa nchi ya Guinea wahamasishaji takribani  saba wakiuwawa kinyama kwa silaha za jadi wakati walipokuwa wakihamasisha jamii kujikinga na Ebola kwa kile kinachotajwa kuwa ni hofu juu ya wahamasishaji hao kutumwa na Wazungu kuja kueneza ebola kusudi wagonjwa wanapowekwa karantini basi wapate kuchukua viungo vyao mbalimbali kama maini figo na moyo kwa ajili ya kwenda kuwatibu wazungu.

Mtoto mgonjwa akitoroshwa kituoni na ndugu zake huku wakiwa wamembeba.
Si hivyo tu, makundi mengine ya wananchi wenye hasira kali huko Liberia na Guinea kwa nyakati tofauti yalivamia vituo vya waathirika wa ebola wakabeba magodoro  yaliyojaa damu na majimaji  toka kwa waathirika na kutokomea nayo kusikojulikana. Inasemekana wagonjwa nao walitoroka lakini wakaja tena kurejea baada ya siku mbili. Hebu fikiri !, Ni kwa kiasi gani watu hao walivyoambukizwa ebola kijinga na ni idadi kubwa kiasi gani ya wananchi wengine waliokwenda kuambukizwa huko mitaani.

Tatizo kubwa kwetu sisi Waafrika ni ujinga na kukumbatia imani potofu zisizokuwa na misingi yeyote ile ya kisayansi. Ugojwa wowote ule unaosababishwa na virusi ni vigumu sana kuutibu hata na kwa hao Wazungu wenyewe. Ndio maana wanafanya kila liwezekanalo usiweze kuenea katika nchi nyingi zaidi. Lakini binafsi nadhani kwa kiasi wenzetu Wazungu walivyokuwa makini na pasipokukumbatia imani za kishenzi kama tufanyavyo sisi Waafrika hata ugojwa huu ufike kwao hautaweza kusambaa kama vile ulivyofanya huku kwetu Afrika.

Mazishi ya mtu aliyekufa kwa ebola.
Tusipokuwa makini na upotoshaji wa watu wachache kama  kijana Yule Waafrika tutaendelea kuandamwa na majanga mengi ambayo uwezo wa kuyathibiti tunao wenyewe. Majanga kama vile Ebola, Ukimwi, mauaji ya Albino na vikongwe, watu kuchunwa ngozi nk. Tutaendelea kuwasingizia Wazungu kuwa ndio wanaotusababishia kumbe ni sisi wenyewe.

Tunadai eti ni kwa nini wazungu wasigundue dawa ya ebola na kama ungelilipuka huko kwao basi wangefanya juu chini kupata dawa. Madai haya siyo kweli hata kidogo kwani wanasayansi hawana mipaka wala hawabagui rangi, kazi ya kuvumbua dawa hufanywa na wanasayansi na wala siyo wanasiasa.

Ingelikuwa hivyo ndivyo basi hata magonjwa kama malaria na mengineyo kibao yaliyopatiwa dawa na wazungu hao hao basi yasingelikuwa  mpaka leo hii yamepatiwa ufumbuzi kwani hata mengine kama Malaria wala huko kwao siyo ‘ishu’ sana kama ilivyokuwa huku Afrika.

Gunduzi za kisayansi hazina mipaka ya kiitikadi wala kigezo kingine chochote kile, Muislamu, Mkristo, Mbudha, mhindi, Asiyekuwa na dini yeyote, wote wananafasi sawa ya kubuni na kugundua kitu chochote chini ya jua. Halikadhalika ndivyo hivyo hivyo ilivyo kwa mataifa liwe ni kutoka Magharibi, Mashariki, au Mashariki ya kati. Sasa kinachokuja kuleta tofauti tu ni ELIMU. Mataifa ya Magharibi yameendelea ni shauri ya kuzingatia suala la elimu.
 
Boko Haram "Elimu ya Magharibi ni Haramu" wakiwa wamebeba silaha kali za kivita zilizotengenezewa huko huko Magharibi.

Na ukitaka kujua ukweli kwamba Elimu na maarifa hayabagui, angalia Uchina ipo Magharibi? Mbona sasa inakaribia kuipiku Marekani kwa teknolojia. India haipo Magharibi lakini hata hazijapita siku mbili wameiduwaza Dunia baada ya kufanikiwa kurusha chombo kwenda kuizunguka sayarinyekundu ya Mars.

Irani, taifa tena la Kiislamu kutokana na kuanza kuzingatia elimu na maarifa wamefikia hata hatua ya kuunda Nyuklia na ni hivi karibuni tu, tumeambiwa nao wamezindua dege lao lisiloendeshwa na rubani maarufu kama Drawns. Sasa huo umagharibi na Umashariki sijui Uislamu na Ukristo uko wapi hapo?

Dawa mseto hii tunayoitumia leo hii hapa, (mchanganyiko wa mti wa Artemisinin na viasili vinginevyo) haijagunduliwa Magharibi na wazungu. Ni Wachina, tena Wamarekani wenyewe na ujanja wao wote iliwabidi watumie mbinu kali za kijasusi kwa miaka karibu 10 kuweza kupenya ndani ya ngome ya jeshi la kikomunisti la China wakati huo kusudi waweze kupata siri za mti wa Artemisia unaozalisha dawa hiyo. Wachina baada ya kuigundua hawakukubali ijulikane na Mataifa ya Magharibi hasa Marekani.

Na ikiwa basi sisi Waafrika tumechoka na tiba za Wazungu na tunadhani ya kuwa wanatuletea magonjwa yasiyotibika kwa kisingizio cha chanjo na vifaa vingine vya tiba, basi hatuna haja ya kuwa wala na hospitali, tuamue kurudi kwenye miti yetu ya asili kama kikombe cha Babu na wengineo.

Tusijidanganye kama wanavyofanya Boko Haramu na ISIS, kuwa eti kila kitu cha Kimagharibi ni haramu (sikatai kweli kuna vitu vingine ni haramu)  wakati huohuo wakitumia Mtandao wa intaneti kama njia yao kuu ya kujitangaza na kueneza propaganda za itikadi zao. Sasa najiuliza kwani kompyuta, simu, mtandao wa intaneti  na hata silaha wanazotumia kuulia watu, siyo teknolojia za Kimagharibi?  Kwanini basi wasirudi kwenye asili  wakatumia zana za enzi zile kama majambia, visu na hata njia za mawasiliano kama kupeleka habari kwa barua kwa kutumia wakimbia kwa miguu, farasi, ngamia na njiwa?

Tusiwe kama Ngamia kujichimbia kichwa mchangani akidhania yu salama, il-hali kiwiliwili kingali nje. Boko haram, au hata kikundi/mtu mwenye itikadi nyingine yeyote ile, badala ya kuwa mnafiki na kudai eti elimu, iwe ya kimagharibi, mashariki au kokote kule ni haramu anaweza akaitumia elimu hiyo hiyo anayoipinga kwa mazuri ya kujenga  imani yake hiyo. 

Hamna elimu haramu wala mbaya kutoka upande wowote ule wa Dunia ilimradi tu inatumiwa kwa lengo la kujenga na wala siyo kubomoa. Kila upande una mazuri yake na ndiyo maana Shirika la elimu na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO huwa linahifadhi maeneo yote Duniani ya kihistoria na yanayowakilisha tamaduni mbalimbali pasipo kubagua Magharibi, Mashariki, Kusini wala Kaskazini, dini, rangi wala kabila.


*Mpendwa msomaji wa makala hii, kwanza nikushukuru kwa kutembelea blogu hii ya jifunzeujasiriamali. Pia napenda kukujulisha kwamba baada ya kimya kidogo kilichotokana na kazi kubwa ya ‘kuredisign’  tovuti, blogu na cover za vitabu kusudi viweze kuwa na muonekano mpya, sasa tumerudi tena kuendelea na jukumu la kubadilishana na wewe mawazo zaidi kuhusiana na namna ya kuboresha biashara zetu ndogondogo kwa lengo la kuondokana na umasikini hasa wa kipato unaotutesa watu wengi.

Kuna watu wengi wametoa mapendekezo yao nini kifanyike, na moja lilikuwa ni hilo tulilomaliza la kubadilisha majina. Wapo pia mlioshauri, kwa nini blogu hii isingezungumzia masomo ya ujasiriamali tu peke yake tukaachana na habari mbalimbali, hili nalo tumelizingatia ila, habari zitawekwa hasa zile zenye mahadhi yanayohimiza ujasiriamali, biashara na ubunifu na usisahau pia kuwa wengi katika timu ya watendaji wetu ni wana fani ya uandishi-habari  hivyo ‘jasiri haachi asili’

Kwa wewe ambaye unapendelea zaidi masomo ya ujasiriamali na biashara, basi ukiingia humu kwenye blogu moja kwa moja tembelea ukurasa 'page' (label) iliyoandikwa "Masomo" pale juu kabisa, na humo utapata mfululizo wote wa masomo yote muhimu. 


Ahadi zote tulizotoa, kama kutoa mfululizo wa makala zinazohusu mafanikio ya watu maarufu na wasanii, kitabu cha think and grow Rich katika lugha ya Kiswahili, vyote sasa siyo tu, ukae mkao wa kula bali nakuambia, anza kula sasa hivi, vyote vimekwisha wiva.

0 Response to "EBOLA: TUACHANE NA DAWA ZA KIZUNGU TURUDI KWENYE ASILI, KIKOMBE CHA BABU NA MUAROBAINI?."

Post a Comment