UGAIDI NI KIMBELEMBELE CHA MAREKANI NA UINGEREZA KUENEZA DEMOKRASIA DUNIANI. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UGAIDI NI KIMBELEMBELE CHA MAREKANI NA UINGEREZA KUENEZA DEMOKRASIA DUNIANI.

Maandamano ya Hong Kong kudai Demokrasia


Ni mtazamo wangu,

Ni kimbele mbele hihikihiki kilichosababisha Iraq kutumbukia katika lindi la maafa makubwa, kwa kisingizio cha kuleta demokrasia. Afganistan, lLibya, Misri, na sasa Syria na Ukraine. Koote huko tangu wapandikize maafa hayo wala hakujatulia, moto bado ungali unawaka, pasipokuwa na hata chembe ya aibu, Obama na Cameroon wanadiriki eti kutamka,   “Tupo pamoja na wanaoandamana nchini Hong Kong kupinga sera za  China Bara dhidi ya sheria zake za kuchagua wagombea katika jimbo lake hilo“.

Cha ajabu kabisa ni pale Mataifa haya ya Magharibi yanapojifanya kuwasaidia wale wanaojiita wanademokrasia    ‘pro-democracy’na  kisha bada ya kufanikiwa kuziondoa serikali zinazodaiwa kuwa za kidikteta, wanageuka kuwa magaidi hatari, ukitaka kuona mifano angalia Syria, Iraq na  Libya. ISIS  ni mfano mzuri na makundi yanayoisumbua serikali dhaifu ya Libya iliyojigamba kumng‘oa  Muhamar Gadafi. Magaidi na wenye uroho wa kutawala hujinufaisha sana na vuguvugu la kudai demokrasia kwani wanajua hakuna kitu kingine Mataifa ya Magharibi wanachopenda kama madai ya demokrasia hasa katika nchi zile zinazoonekana kuiminya.

Wako radhi kusaidia chochote, kwa gharama yeyote ile hata ikiwa ni kwa kulipa gharama kubwa kama wanayoilipa sasa kule Iraq na Syria. Kwa nini hawajifunzi tu?  Kwa maoni yangu binafsi sasa naona funzo watalipata kutoka Uchina, endapo wataendelea na ujinga wao huo wa kila mara kudai wapo pamoja na wadai demokrasia hata ikiwa wanamageuzi hao ni kikundi cha wahuni wenye malengo yao binafsi kama ilivyokuwa syria na Libya. Sifikiri kama Xi Jinping atakubali kirahisi rahisi tu himaya yake kuchezewa.
 
Waandamanaji wakiwa barabarani.
Hivi kwa mfano watokee watu leo katika jimbo mojawapo la Marekani mfano jimbo la Virginia, litake kujitenga, au kudai demokrasia na madaraka zaidi, Obama atakubali kirahisi? Wanahistoria wanakumbuka jinsi Marekani ilivyopigana vita chungu karne ya 18 katika harakati za kuzuia mpasuko baina ya majimbo ya Mashariki na Magharibi. Sasa iweje leo hii wanakuwa wa kwanza kushadidia mipasuko na utengano katika nchi za wenzao?. Uingereza kukosa kuogopa aibu sidhani kama juzi wangekubali ile kura ya maoni ya Scotland, hata ushindi wa London dhidi ya kura hiyo kama isingelikuwa vitisho vya Waingereza, Wascotish ni lazima wangeshinda.

Hali ni hiyo hiyo katika nchi kama Uhispania, jimbo linalolilia kujitenga la Catalonia limefanya hivyo kwa miongo mingi pasipo matumaini, na hata kura ya maoni walioahidiwa itafanyika wiki hii kama wenzao Scotland, nayo katika hali ya kutatanisha Mahakama kuu imeisitisha, wameshashitukia kura hiyo itapita. Kusema ukweli hakuna nchi inayopenda kumegeka megeka bila sababu ya msingi, hivyo Uchina na Hong Kong ingeachwa iamue maswala yake pasipo kuingiliwa na Mataifa ya kigeni.


Putin kwa hasira aliamua kuinyakua Kremia kwa nguvu, ni kwa sababu hizi hizi baada ya nchi za Magharibi kuunga maandamano yasiyokuwa na kikomo yaliyomng’oa Viktor Yokunovych aliyekuwa akiungwa mkono na Urusi. Namuunga mkono Rais wa Iran Hassan Rouhan aliyesema juzi katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuwa ”Magaidiwanatengenezwa na zile nchi zinazojidai kueneza Demokrasia Duniani“

0 Response to "UGAIDI NI KIMBELEMBELE CHA MAREKANI NA UINGEREZA KUENEZA DEMOKRASIA DUNIANI. "

Post a Comment