PIPI YA KIJITI NI HATARI KWA MWANAO: CHUKUA TAHADHARI! | JIFUNZE UJASIRIAMALI

PIPI YA KIJITI NI HATARI KWA MWANAO: CHUKUA TAHADHARI!

Sikuwahi hata siku moja kufikiria kama pipi za kijiti zinazopendwa sana na watoto, wakati mwingine hata na watu wazima kuwa zinaweza kuwa hatari kiasi hiki, mpaka pale niliposhuhudia mkasa huu ambao kama nisingelikuwepo karibu na tukio labda mtoto ninayemzungumzia asingelikuwa hai leo hii.

Nikiwa pembeni mwa duka moja la rejareja mahali fulani alikuja mtoto wa kike kama wa miaka mitano 5 hivi huku akiwa ameongozana na mwenzake nadhani ni lazima atakuwa mdogo wake ambaye yeye ‘kalikuwa kadogo’ zaidi kwa kukadiria labda anaweza akawa na mwaka  mmoja au na nusu hivi. Dada mtu baada ya kununua alichokuwa ametumwa, alimchukulia na mdogo wake pipi ya kijiti, akaimenya na kumpa, kisha kakaiweka mdomoni.

Ile pipi, kijiti kilichomoka na kuiacha pipi yenyewe mdomoni mwa mtoto bila yule mwenzake yaani dada mtu  kufahamu ni nini kilichokuwa kikiendelea. Kwa bahati nzuri walikuwa wamesimama pale pale, mimi mara moja nikashtuka kumuona yule mtoto wa mwaka mmoja na nusu akihangaika lakini pasipo kuweza kutoa sauti yeyote. Kilichokuwa kimetokea ni kwamba, lile bonge la pipi baada ya kile kijiti cha kushikia kuchomoka, mtoto alishindwa kuitema ile pipi kutokana na ukubwa.

Watoto wakifurahia pipi za vijiti.
Pipi ikajaa tele mdomoni, mtoto kutoa sauti hawezi wala kuitema pia hawezi. Nadhani kilichokuwa kikimsaidia labda ni pua ambazo zilimuwezesha kutoa na kuvuta hewa. Sasa mwenzake naye akawa ameshagundua kuna kitu kilikuwa kimempata mdogo wake lakini kutokana na utoto naye nafikiri hakuweza kupambanua mara moja ni kitu gani ambacho angeweza kukifanya ili kumnusuru. Alibaki akihangaika kuingiza kidole mdomoni mwa mtoto kwa woga lakini asiweze kuutanua vya kutosha kuifikia pipi.


Na mimi ndipo nilipobaini kwamba yule mtoto pipi ilikuwa imeshamkaba nikamkimbilia haraka! Nilipojaribu kupenyeza vidole mdomoni mwa mtoto alikakamaa mdomo kama vile mamba kameza kipande cha gogo. Ilinibidi kutumia nguvu kidogo pasi na huruma nikihofia lile bonge la pipi lisije likasukumizwa zaidi kooni. Mungu mkubwa! hatimae nilifanikiwa kuitoa ile pipi huku katoto kale masikini machozi yakiwa yalishaanza kumlengalenga. 

1 Response to "PIPI YA KIJITI NI HATARI KWA MWANAO: CHUKUA TAHADHARI!"

  1. Ubarikiwe kwa kuokoa maisha ya kachanga hako, ni Mungu alikusogeza karibu

    ReplyDelete