UNAWEZAJE KUYAKABILI MAGUMU, MAANGUKO NA MIKASA YA KUTISHA MAISHANI KAMA HII? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UNAWEZAJE KUYAKABILI MAGUMU, MAANGUKO NA MIKASA YA KUTISHA MAISHANI KAMA HII?


MIKASA NA MATESO YA KUTISHA
Binadamu wote hakuna hata mmoja anayeweza akadai kutopitia vitu hivi katika muda wa maisha yake, sote tumepitia huko na hata ikiwa bado basi ujue kuna siku. Mambo magumu maishani, mikasa ya kukatisha tamaa na maanguko kwenye yale tunayopanga kuyafanya ni vitu ambavyo hata wale watu wanaodhania kwa kuishi kwa tahadhari ya hali ya juu kupitiliza wanaweza kuvikwepa huja kugundua kumbe hawako sahihi. Unaweza leo hii ukawa unafurahia neema, lakini kumbe hujui kesho kuna janga gani litakukuta.

Ni nani aliyefahamu katika harakati za marudio ya uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni msichana asiyekuwa na hatia Ackwilina Ackwiline angefikwa na mkasa wa kifo akiwa ndani ya basi akielekea kurudisha fomu za maombi yake ya kazi? Janga limetokea na kwa hakika maumivu na uchungu walio nao ndugu wa huyu binti hasa wazazi wake hauwezi kupimika. Wanaona ni kama vile hakuna tena njia yeyote ya kutokea, wanahisi hawana nguvu tena ya kusonga mbele na maisha yao, kila kitu kimegeuka na kusimama kimya, haviendi mbele wala kurudi tena nyuma!


Ukweli wa mambo ulivyo ni kwamba sisi binadamu uwezo wetu wa kuzuia mambo mabaya au mikosi kutukuta ni mdogo sana, ingawa yapo mengine yanayoweza kusababishwa na uzembe au kwa makusudi na wanadamu wenzetu. Na huo ni upungufu ambao sisi kama binadamu hatuwezi kuubadilisha kirahisi. Sasa binadamu bada ya kupitia magumu yote hayo na mikasa anapaswa kufanya kitu gani?

Katika mazingira kama haya wapo wanaoshindwa kabisa kukabiliana nayo wanaamua hata kujitoa uhai au wanapatwa moja kwa moja na matatizo ya akili, msongo wa mawazo na wakati mwingine matatizo ya moyo au kiharusi(stroke). Lakini kumbuka pia kwamba katika kila anayekumbwa na mikasa ya kutisha namna hii, maanguko, ugonjwa usiopona, kutengwa na jamii kwa sababu yeyote ile au njaa na majanga ya kila aina, kunakuwa na njia iliyojificha nyuma ya majanga hayo ambayo kama utaweza kuiona basi unaweza tena kupona na kurudia hali yako ya kawaida kama ulivyokuwa zamani, na hii ndiyo imekuwa ikisababisha watu wengi hata baada ya kupatwa na mikasa ya kutisha maishani lakini baadae hupona na kupata tena mpenyo upya wa maisha yao huku wakisahau kama waliwahi kukumbwa na mikasa hiyo.


UNAPOKUMBWA NA MIKASA AU MAGUMU YEYOTE MAISHANI.

Fahamu kabisa ya kwamba sisi binadamu tulivyoumbwa tumewekewa uwezo wa ajabu ndani yetu wa kupona tena taratibu kutoka janga lolote lile na kurudia hali zetu za kawaida kama vile minyoo wa ardhini walivyo, unapomkatakata kwa jembe ukidhani tayari umemmaliza kabisa, vile vipandevipande huenda tena kujikuza upya na kuwa minyoo kamili inayoweza kutembea kama zamani. Pamoja na maumivu yote anayoyapata unapokuwa ukimkatakata, lakini kumbe ndiyo njia yake ya kujiongeza.

Ili kuondokana na hali ya magumu, mikasa na maanguko ya kimaisha, jiulize maswali yafutayo;

1.  Najifunza nini kutokana na mkasa/tukio hili?
2.  Nitatumia mbinu gani au njia gani kukabiliana na tatizo kama hili wakati ujao kama litanitokea tena?
3.  Kuna njia/fursa au mpenyo wowote unaoweza kujitokeza katika mazingira ya tukio hili?

Kwa kadiri utakavyojitibu mapema(kukubaliana) na hali halisi iliyokuwepo mbele yako ndivyo na uwezekano wa kurudia hali yako ya kawaida au kupona nao utakavyoharakishwa. Uwezekano tena wa kurudia hali yako ya kuishi kwa furaha, mafanikio, afya na amani. Vitu vilivyotoweshwa na giza nene la mikosi, dhuluma, maanguko, mikasa na roho mbaya ya binadamu wanaojipenda wenyewe kuliko wenzao.


Wakati mwingine muda unahitajika, waswahili husema “Muda ni dawa ya kila kitu”, unahitaji kupata muda wa kupona majeraha hayo mabaya. Huhitaji wala mtu yeyote kukushauri ni njia ipi uifuate zaidi ya ujasiri wako mwenyewe, kuamua uendelee kuteketea katika maanguko haya yaliyokwishatokea kwa kuruhusu magonjwa ya moyo, kiharusi na kujinyonga au uamue kupona taratibu njia pekee Mwenyezi Mungu aliyotupa Wanadamu ya kujiondoa katika magumu, mikasa na maanguko ya kila aina yanayotokea hapa Duniani.

Maisha yeyote mtu utakayoamua kuishi yawe ni ya furaha, amani, mafanikio, utajiri, uchungu, magumu, kukatisha tamaa, yote yataamuliwa na jinsi utakavyokabiliana na nyakati hizi chungu katika maisha. Fahamu kuwa haupo peke yako, mimi, yule na hata mwingine tumewahi kupitia nyakati ngumu kama hizi. JIPE MOYO UTASHINDA!!!

0 Response to "UNAWEZAJE KUYAKABILI MAGUMU, MAANGUKO NA MIKASA YA KUTISHA MAISHANI KAMA HII?"

Post a Comment