BIASHARA NDOGO ZILIZOSAHAULIKA: BUSTANI NDOGO YA MIWA JIJINI DAR ES SALAAM | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA NDOGO ZILIZOSAHAULIKA: BUSTANI NDOGO YA MIWA JIJINI DAR ES SALAAM


Bustani za miwa ya kutengeneza juisi
Unaweza kushangaa nazungumziaje miwa jijini Dar es salaa wakati maeneo kibao makubwa yapo sehemu mbalimbali nchini Tanzania kama vile kule Morogoro, Mbeya, Tanga, Mwanza na Ruvuma ambayo mtu unaweza ukalima zao la miwa tani kwa matani na kuisafirisha kuja hapa Dar es salaa kuiuza, sawa na wafanyavyo wafanyabiashara wengi wa miwa wanaoleta miwa jijini kwa ajili ya kutengeneza juis ya miwa ambayo hupendwa sana hasa nyakati za kiangazi kama hizi.


Lakini lengo langu katika mfululizo wa makala hizi za BIASHARA ZILIZOSAHAULIKA au ZISIZOPEWA KIPAUMBELE KIKUBWA LAKINI ZINA FURSA KUBWA YA KUTENGENEZA FAIDA, lengo hasa ni kuibua fursa ambazo zinawezakuwa zipo lakini watu wengi hasa wa vipato vya chini hawazifahamu. Ndiyo ni kweli kilimo cha zao la miwa siyo fursa iliyojificha, maeneo kibao mikoani miwa hulimwa kwa ajili ya kutengenezea sukari na mingine kusafirishwa kwenda maeneo mengine wasiyolima kwa wingi kama jijini Dar es salaa kwa ajili ya kutengenezea juisi za miwa.

Katika miradi au biashara ninazodai zimesahaulika ninachowakumbusha watu ni kwamba biashara inaweza ikawa ni ya kawaida sana lakini wewe kwa kuongeza ubunifu fulani ukaifanya kuonekana kama vile ni biashara iliyosahaulika. Kwa hiyo mimi mantiki yangu kubwa hapa ni kuibua ubunifu ambao kwa mazingira ya kawaida mtu unaweza ukadhani hakuna fursa yeyote ile. Mfano ni mtu mmoja nilikuwa nikipiga naye stori kuhusiana na miwa hii hii, nikamweleza, unajua bustani ya miwa inaweza ikamuongezea mtu kipato kwa urahisi sana akiwa hapahapa Dar. Lakini yeye alinibishia na kusema hivi, “wewe si mzima, ukalime miwa dar wakati hapo Morogoro mashamba ya miwa yamejaa mahekari kwa mahekari utamuuzia nani?”


Nilijaribu kumueleza kwanini nilikuwa nasema vile, nikamuambia kwamba, miwa ni zao ambalo soko lake halina mashaka, unapofika sokono mara nyingi utawakuta wanunuzi wamepanga foleni wakisubiri kununua miwa kwa ajili ya kwenda kutengeneza juisi ya miwa na hamna msimu wowote utakuta miwa ikidoda sokoni iwe kiangazi au masika. Na nikamweleza pia kwamba ninaposema bustani za miwa jijini Dar es salaam simaanishi mtu akaweke bustani ya miwa maeneo kama kariakoo, posta, buguruni au hata Manzese hapana, haiwezekani.

Juisi ya muwa ni nzuri kwa afya
Juisi safi na halisi ya miwa.
Dar ina maeneo kibao ambayo bado yanafaa kwa kilimo cha bustani za mbogamboga na matunda. Watu wanaoishi kwa mfano maeneo ya Kiluvya, Kimara, Mbezi, Chanika, Kigamboni, na maneo yote ya pembezoni mwa jiji wanaweza kuwa na bustani ndogondogo za matunda na mboga au hata miwa kama ninayozungumzia.

Kwanini miwa? Pamoja na soko lake la uhakika jijini Dar, lakini miwa haihitaji uangalizi mkubwa sana kama yalivyokuwa mazao mengine ya bustani kama mbogamboga na matunda. Huhitaji mbegu ya kisasa sana kwani unaweza kuchagua tu muwa mzuri ukaukatakata vipande na kupanda pingili zako. Tatizo kubwa katika kilimo cha bustani ya miwa ni mchwa, lakini mchwa wanaweza kudhibitiwa kirahisi sana kwa kutumia njia za asili kama vile majivu au kwa kununua dawa kidogo inayopimwa katika maduka mengi ya pembejeo za kilimo ukachanganya na maji kisha ukapaka pingili za muwa kabla hujazipanda ardhini.


Muwa hauhitaji maji mengi sana na unaweza, ukishaota ukaweka matandazio kuzuia maji mengi ardhini kuchukuliwa na jua kama mvuke. Ukishapanda wewe kazi yako kubwa labda ni kuja kupalilia tu siku moja moja mpaka unavuna. Unaweza ukaweka mbolea kidogo ya kuku, ngombe au hata mbolea za chumvichumvi kama vile UREA, CAN nk. Muwa hukomaa baada ya miezi 12, mwaka mmoja mpaka miezi 16 na utajua kama muwa umeshakomaa pindi majani yake yanapobadilika na kuwa rangi ya njano na muwa huwa na urefu wa mita 2 mpaka mita 4.

Mradi kama huu si kwamba ni biashara unayoweza ukasema utaitegemea moja kwa moja kiuchumi, kama niliyotangulia kusema mwanzoni kwamba biashara hizi naziita biashara zilizosahaulika na lengo lake hasa ni kuongeza tu mzunguko wa fedha katika kaya au familia kwani katika familia kunapokuwa na njia tofautitofauti na nyingi za kuongeza kipato mwisho wa siku familia inaondokana na umasikini kuliko kutegemea chanzo kimoja tu cha mapato.

Kama muwa hauhitaji muda mwingi kuukuza wala gharama kubwa, lakini mwisho unapokomaa unakuwa na uwezo wa kupata hapo hata shilingi elfu 5, sasa kwanini usijaribu kupanda kama una kaeneo nyumbani kwako? Licha ya kupata pesa lakini pia muwa unaweza kuliwa na wanafamilia kama chanzo kizuri cha madini na inasemekana pia maji yake yanasafisha figo.

Kumbuka pia kwamba mwaka huu niliahidi kuwa katika makala zetu kwenye blogu hii na kampeni  zetu zote katika mitandao ya kijamii tutahamasisha zaidi njia za kuongeza mzunguko wa fedha katia biashara zetu na mifukoni mwetu kwa ujumla katika kutimiza malengo yetu.


Ndiyo maana hata katika GROUP LETU LA WHATSAPP LA MICHANGANUO ONLINE kila siku pamoja na kuwa na masomo ya MICHANGANUO lakini pia tunakuwa na somo la KUONGEZA MZUNGUKO WA FEDHA katika biashara zetu na kujifunza nidhamu ya hali ya juu ya kutunza fedha.

0 Response to "BIASHARA NDOGO ZILIZOSAHAULIKA: BUSTANI NDOGO YA MIWA JIJINI DAR ES SALAAM"

Post a Comment