MAADUI WAKUBWA WA BIASHARA YAKO USIOWADHANIA HATA KIDOGO (KIKULACHO…) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MAADUI WAKUBWA WA BIASHARA YAKO USIOWADHANIA HATA KIDOGO (KIKULACHO…)



Wahenga hawakukosea waliposema; Kikulacho kii nguoni mwako na mchelea mwana kulia hulia yeye. Haya ndiyo yaliyomkuta kijana mmoja aitwaye Sam, mfanyabiashara mdogomdogo wa matunda na mbogamboga kama nyana, vitunguu, kabeji, karoti, pilipili hoho na matango katika maeneo ya mbezi mwisho.

Sam kwa muda mrefu alikuwa akijihusisha na biashara ya kuuza matunda na mbogamboga katika eneo la Mbezi mwisho lakini mwaka huu mwezi ule wa 6 alipata wazo la kutanua zaidi biashara yake kwa kwenda kuomba mkopo kutoka katika taasisi moja ya fedha iliyopo palepale Mbezi mwisho. Baada ya kujiunga na kikundi cha watu wengine wanne walikwenda katika taasisi hiyo na wakakubaliwa kupewa kila mmoja shilingi laki tatu na nusu(350,000/=) fedha ambazo Sam alikuwa na malengo ya kufungua tawi la biashara yake ya matunda na mbogamboga eneo jingine.

SOMA: Kushuka bei ya mchele, kilo moja hatuuzi, tunaanzia kilo 5 na kuendelea.

Baada ya kufanya utafiti wa kina alibaini kuwa tawi la biashara yake mpya angeliweka eneo jingine tofauti na Mbezi Mwisho na akaamua tawi hilo afungue maeneo karibu na stendi ya Kwa Msuguri. Ingawa maeneo hayo ni hifadhi ya barabara hata hivyo haikumzuia kuweka biashara yake hapo kwani asingeliweka banda la kudumu. Wafanyabiashara wengi huweka vibanda vya muda ambavyo inakuwa rahisi kuhamishia eneo jingine pale serikali inapowataka kufanya hivyo ili kupisha ujenzi wa barabara au shughuli nyingine zozote zile za umma.

Kijana Sam huku akiendelea na biashara katika “goli” lake la zamani pale Mbezi Mwisho, aliiba muda wake kidogo kwa siku mbili tatu, na kwenda kusimamia ujenzi wa meza kwa ajili ya biashara yake hiyo mpya. Alijenga meza safi pale stendi kwa Msuguri akitumia fedha alizotoa kwenye biashara yake kiasi cha shilingi laki moja na nusu hivi. Kumbuka wakati huo bado ndio anafanya mchakato wa kupata zile fedha sh. 350,000/= kutoka taasisi ya fedha.

SOMA: Je, unakopesheka na taasisi za fedha au benki?

Bada ya kukamilisha ujenzi wa  meza na kuweka turubai la kuzuia jua na mvua sasa alianza kazi nyingine ya kumtafuta mtu atakayeuza kwenye biashara hiyo kwani asingeweza kuwa Mbezi kwenye biashara yake ya zamani na wakati huohuo tena awe Kwa Msuguri kwenye biashara mpya. Mwishowe alifanikiwa kumpata kijana mmoja mdogo aliyemaliza darasa la saba hivi karibuni, ukimwangalia anaweza kuwa na umri wa miaka 15 hivi.

Baada ya kuchukua ule ‘mzigo’(fedha) kutoka katika taasisi waliyokopa, mara moja alikwenda kuagiza bidhaa mbalimbali akianza na matenga 2 ya nyanya, gunia la viazi mviringo, gunia la vitunguu, karoti na mbogamboga na matunda mengine madogomadogo. Alinunua pia na mzani kwa ajili ya kuwapimia wateja wanaopenda kununua vitu kama nyanya, viazi au vitunguu kwa kilo. Meza ilipendeza sana kwa mpangilio wa vitu vilivyoenea vyote hata wateja wakaanza kuhama kutoka magenge mengine ya jirani na kuja kununua vitu pale.

SOMA: Kweli huduma hii kwa wateja ni Customer care au ni customer Kero?

Mama lishe na baba lishe wote wa eneo lile wengi walikimbilia pale, na ungewasikia wakisema, “Huyu dogo anauza vitu bei rahisi sana na ukiomba kuongezewa siyo mchoyo hata kidogo”. Wakati yote hayo yakiendelea Sam alikuwa bize na biashara yake ya zamani kule Mbezi mwisho na alifika pale tu muda wa kwenda kuchukua bidhaa zilizokwisha. Bidhaa hazikuwa zikikaa muda mrefu, akileta nyanya leo siku ya kwanza, ya pili zimeisha! Halikadhalika na vitu vingine ilikuwa ni hivyohivyo.

Kuna kitu kingine cha ajabu nilichoshuhudia kwa yule ‘dogo’ muuuza genge, jirani palikuwa na vijana wauza chipsi na supu waliojenga ukaribu wa ajabu na huyu dogo, kila muda unapofika walimletea vyakula bila hata yeye kuagiza, asubuhi walimletea supu chapatti na chai. Mchana chipsi, kuku na mayai pembeni, na jioni walimletea kongoro au paja la kuku na chipsi kidogo.

SOMA: Unajua biashara ya chipsi kuku, mayai na soda inavyolipa Dar?

Haikuwa rahisi mtu wa pembeni labda kumpa kijana yule tahadhari yeyote kwani kwanza huelewi yeye na mwenye biashara wana uhusiano gani na wala wakati akiletewa hivyo vyakula kulikuwa hamna dalili yeyote ya yeye kukataa, walikuwa wanacheka kama kawaida.

Jambo jingine lililoanza kunipa tashwishi ni siku moja kumsikia yule dogo akimlalamikia muuza chipsi mmoja akimwambia; “Mimi sipendi bwana, kwanza nakudai hela zangu nyingi tu, kila ukichukua, baadae unasema umeshanilipa, mimi nakuachia Mungu tu ndiye atakayekulipa

Du! Kauli aliyoitoa yule dogo ilinishtua sana nikaanza kuhisi dhahiri kuwa yule Dogo alikuwa akinyanyaswa kwa namna fulani na wafanyabiashara waliomzunguka bila tajiri yake kugundua na walitumia udogo wake na ugeni wake katika biashara kumkandamiza na kujinufaisha isivyokuwa halali na mali zilizokuwa pale gengeni.

SOMA: Ukijua gharama halisi za wafanyakazi kwenye biashara yako utawafukuza!

Baadae ilikuja kubainika kuwa kumbe wale vijana wauza chipsi walikuwa wamefikia hatua ya kuja kujichukulia chenji wenyewe katika droo ya pesa ya huyu dogo hata bila ridhaa yake. Dogo wakati mwingine akitoka kidogo kwenda haja, akija mteja gengeni vijana wa chipsi hujiuzia kama shamba la bibi na kuweka fedha mifukoni mwao.

Binafsi kwa kuwa eneo hilo nilikuwa nikifika tu kwa muda kwa ajili ya kuangalia na mimi maendeleo ya biashara yangu niliyokuwa nimemwachia mtu, baada ya kugundua picha ile niliazimia kumtafuta Sam kwa kuwa tulikuwa tukifahamiana japo si sana, nimueleze jinsi ambavyo angeweza kuzuia uharamia uliokuwa ukifanyika pale kwenye biashara yake.

Wakati nikiwa katika harakati hizo za kuonana naye siku mbili tatu nilisikia kuwa ile meza ilikuwa imefungwa na dogo alikuwa ametimuliwa kwa upotevu wa karibu mtaji wote wa shilingi laki tatu na nusu ndani ya muda mfupi tu. Sam aliamua kuifunga ile biashara na kuelekeza zaidi nguvu zake katika biashara yake ya zamani kule Mbezi mwosho ili angalao aweze kumudu marejesho ya ule mkopo ambao bado ni mbichi kabisa.

Biashara ya Sam haikufa kutokana na ukosefu wa mtaji wa kutosha, wala haikufa kutokana na kukosa wateja wa uhakika. Biashara ile ilikufa kutokana na ukosefu wa usimamizi makini, kijana aliyewekwa pale hakupewa mafunzo stahiki na wala tajiri yake hakujishughulisha angalao kufanya uchunguzi mapema wa jinsi muenendo wa biashara ile ulivyokuwa. Aidha pia alishindwa kuweka mfumo madhubuti wa mahesabu ambao ungemuwezesha kubaini mapema zaidi upotevu wa pesa kabla hali haijawa mbaya kiasi kile.

SOMA: Jinsi ya kusimamia hesabu katika biashara ndogo unayomwachia mfanyakazi akuuzie.

Angeweza kwa mfano wakati anaanza, kumwekea mafungu kadhaa tu ya vitu mbalimbali, mfano mafungu 20 ya viazi, mafungu 30 ya nyanaya, vitunguu nk. kisha jioni achukue hata nusu saa au lisaa la kuja kufanya tathmini kujua ameuza mafungu mangapi na ni mafungu mangapi yaliyobakia. Hata hawa vijana wauza chipsi na majirani waliokuwa wakimiminika gengeni hapo kujichukulia vitu kwa bei ya mteremko na nyongeza kubwa bila shaka walishatambua biashara ile haikuwa na usimamizi makini na yule dogo hakuwa kabisa anafahamu kama anafanya makosa makubwa.

Maadui wa biashara yako hawawezi kutoka mbali, wakati mwingine ni baadhi ya walewale wateja wanaofika kukuungisha, inawezekana wengine hata wasijue kama wanakuumiza kwa kuwa mteja siku zote yeye hupendelea unafuu lakini kazi kubwa ya kuzuia madhara yanayoweza kuletwa na wateja wa namna hiyo ni yakwako wewe mjasiriamali kwa kuamua kuweka sera imara zitakazoiongoza biashara yako hata ikiwa wewe haupo pale umemuachia mtu mwingine.

SOMA: Kama unaona ni kazi ngumu kusimamia hesabu za biashara yako, bora uachane nayo vinginevyo utavuna mabua.

Kwa mfano unaweza kuandika katika karatasi mambo yote asiyotakiwa kuyafanya mfanyakazi wako ukampatia akakaa na hiyo karatasi mfukoni au ukabandika ukutani ili ajikumbushe kila siku. Vitu kama vile, Utoaji holela wa chenji, kuruhusu mtu akope, kutoruhusu mtu mwingine yeyote afanye mauzo kwenye biashara hata ikiwa ni ndugu yake, matumizi binafsi kama chakula nk. Ni lazima kila kitu uwe na utaratibu wake na utaratibu huo uhakikishe unafuatwa vinginevyo mfanyakazi huyo hakufai mwachishe utafute mwingine kabla mtaji wako haujamalizika kama wa Sam. 

...........................................................

Kwa vitabu  katika lugha ya kiswahili kutoka SELF HELP BOOKS tembelea, SMART BOOKS TZ 

Kujiunga na Group la masomo ya kila siku Wasap(0765553030) MICHANGANUO-ONLINE, kuhusiana na mzunguko wa fedha kwenye biashara na Michanganuo ya biashara mbalimbali bunifu zinazolipa, toa kiingilio chako sh elfu 10 Kupitia namba za simu, 0765553030 au 0712202244 kisha tuma ujumbe wa "NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO 

Kupata kitabu maarufu cha KANUNI YA KUJIFUNZA ELIMU YA PESA NA MAFANIKIO KWA UFANISI na vitabu vingine vingi bila malipo yeyote, 'free of charge', Jiunge(subscribe) katika blogu hii kwa kubonyeza hapa, >>>JIUNGE NA BLOGU HII. kisha ufuate maelekeza pamoja na kucheki email yako.

0 Response to "MAADUI WAKUBWA WA BIASHARA YAKO USIOWADHANIA HATA KIDOGO (KIKULACHO…)"

Post a Comment