JINSI UNAVYOZUIA MAFANIKIO MAKUBWA MAISHANI KWA KUHANGAIKA NA VITU VIDOGOVIDOGO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI UNAVYOZUIA MAFANIKIO MAKUBWA MAISHANI KWA KUHANGAIKA NA VITU VIDOGOVIDOGO


MAMBO MAKUBWA MAISHANI
Binadamu kila wakati tumekuwa tukisaka siri za mafanikio maishani lakini chakushangaza sana ni kwamba wengi wetu badala ya kulenga yale mambo ambayo ndiyo yanayoweza kutufikisha kwenye mafanikio ya kweli tunakuwa tukihanganika na vitu vidogovidogo sana ambavyo havina uwezo wa kutuletea maendeleo yeyote yale ya maana.

Matone ya kawaida ya mvua hayajawahi kumuua wala kumuumiza mtu lakini si ajabu hata kidogo kumkuta mtu akikimbia mvua barabarani kwa kasi ya ajabu akitafuta mahali pakavu pa kujificha lakini wakati mwingine akiwa katika barabara hiyohiyo haogopi kabisa kupishana kwa karibu na magari ambayo yana uwezekano mkubwa wa kukatisha uhai wake.


Hali ni hivyohivyo ilivyo kwa upande wa afya zetu, unaweza ukamkuta mtu anajali kupita kiasi kujikinga na magonjwa madogomadogo hata yale yanayotibika kirahisi kabisa kama kikohozi na mafua(simaanishi tusijikinge na magojwa hapana) lakini cha kushangaza mtu huyohuyo ndiye utakayemkuta akifanya ngono zembe(mapenzi holela na watu tofautitofauti) bila hata ya kuchukua tahadhari yeyote kama kuna magonjwa hatari ya zinaa yanayoua kama ukimwi nk.

Nimetoa mifano hiyo 2 makusudi nikitaka kuonyesha kwamba hata katika suala zima la mafanikio yetu binadamu kiuchumi bado wengi wetu tunalenga mno katika vitu vidogovidogo ambavyo katu haviwezi kuwa na uwezo wa kututoa pale tulipo na kutufikisha kwenye ‘nchi ya ahadi’ mahali pazuri zaidi au palipo na mafanikio.


Hebu jiulize, unaweka vipaumbele vyako katika vitu gani linapokuja suala la pesa na mafanikio?. Mfano kijana anayemaliza shule au chuo sasa na kuanza mara moja kuweka malengo ya kujiwekea akiba kwa ajili ya ununuzi wa rasilimali(asseti) zenye uwezo wa kumzalishia pesa baadae, miaka kumi mbele utakuja kumshangaa kijana huyu hutampata tena atakuwa mbali kiuchumi kuliko yule anayewaza kutumia kila senti anayoipata kula raha.

Mtu kufikiria namna unavyoweza kuwekeza pesa zako na ni wapi uziwekeze ni moja ya kitu muhimu sana katika maisha ya binadamu kwani ndiyo hatimaye huamua mustakabali mwema wa maisha yake kiuchumi.


Lakini utakuta mtu badala yake anaanza kufikiria vitu  vidogovidogo vya muda mfupi mfupi tu kwa mfano, “nitakula nini kesho”, “mpenzi wangu anataka nimnunulie rasta na hereni za dhahabu, nitapata wapi pesa za kumnunulia”, “nyumbani hatujala nyama huu ni mwezi wa pili sasa..”.nk. Mtu anahofia vitu ambavyo wala sio tishio kabisa katika maisha yake na ni vya kupita muda mfupi. Imefikia mahali watu sasa tuweke hofu zetu katika mambo yanayotutisha kweli na kuweka mipango na mikakati ya kukabiliana nayo


Kuna matishio ya ukweli kama vile homa, kuugua magojwa yanayohitaji gharama kubwa, badala ya kuwaza tu vitu vidogovidogo kama michango ya harusi, vipaimara au ngoma za viduku mitaani, tuanze kufikiria utaratibu wa kujikatia bima za afya kwa familia zetu na sisi wenyewe, matishio ya magojwa yanayohitaji fedha nyingi ni ya ukweli wala siyo hadithi kama wengi tunavyoweza kufikiria. Umeshashuhudia mara ngapi wapendwa wako au hata watu unaowajua wakipoteza maisha kisa tu kukosa gharama za matibabu  zinazoeleweka?

Si kama nahukumu au kutishia hapana, bali hii ndiyo asili yetu sisi binadamu kuhangaika na vile vitu vilivyopo mbele yetu kwa wakati ule tulio nao tu hata kama havina umuhimu kihivyo. Watu wanaofanikiwa mara nyingi hulenga katika yale mambo mazito yaliyo na umuhimu mkubwa katika maisha yao hata ikiwa mambo hayo wanayatarajia miaka mingi ijayo. Mfano wa mambo hayo ni kama haya yafuatayo;

1.  Kupata kazi nzuri
2.  Kuwekeza katika vitegauchumi na biashara zitakazowalipa vizuri baadae
3.  Kujenga mahusiano mazuri na watu wale uwapendao na mnaoonana mara kwa mara.
4.  Kuwa na afya nzuri
5.  Kuishi maisha unayoyataka kila siku

Mambo haya makubwa, kila mtu anaweza akawa nayo yakwake tofauti na mwingine lakini yote kwa yote mtu anatakiwa kuwa na malengo yake makubwa maishani atakayohakikisha akili yake yote inayawaza mpaka pale atakapoyatimiza na wala siyo mambo madogomadogo yasiyokuwa na tija yeyote maishani.

……………………………..

Ndugu msomaji wangu, makala zako kuhusiana na Mzunguko wa fedha na Michanganuo ya biashara katika group la Wasap la MICHANGANUO-ONLINE bado zinaendelea kila siku, karibu njoo ujiunge kwa shilingi elfu 10 tu upate na masomo mengine yote yaliyopita pamoja na kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI free of charge.

Tunakupa na michanganuo maarufu 3 ya ufugaji wa kuku aina zote pamoja 1 wa kilimo cha matikiti maji bila malipo yeyote ya ziada. Pia utaunganishwa na group hilo la wasap na kuwa miongoni mwa wajasiriamali  makini karibu 100 wanaojua kile wakitakacho maishani(MASTERMINDGROUP)

Ikiwa hutumii wasap hamna shida kwani masomo utapata kupitia email yako.

Leo Septemba  10 2018 usiku saa 3 tutakuwa na somo lisemalo; “BIASHARA YENYE FURSA KUBWA NA YA KIPEKEE NCHINI ISIYOJULIKANA BADO NA WATU WENGI”

ASANTE SANA,

Peter Augustino Tarimo

self help books Tanzania

0765553030
  

0 Response to "JINSI UNAVYOZUIA MAFANIKIO MAKUBWA MAISHANI KWA KUHANGAIKA NA VITU VIDOGOVIDOGO"

Post a Comment