USHAURI KWA MWANAFUNZI ALIYEHITIMU CHUO/MASOMO ANAYETAKA KUANZA MAISHA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

USHAURI KWA MWANAFUNZI ALIYEHITIMU CHUO/MASOMO ANAYETAKA KUANZA MAISHA


Unapokuwa chuoni au shuleni ni tofauti kabisa na maisha halisi ya mtaani unapokuwa umemaliza masomo na kuanza kazi au biashara. Mambo uliyokuwa ukifikiria unakuta mengine ni kinyume kabisa. Kwa hiyo unatakiwa ufahamu namna ya kukabiliana na hali kama hiyo.


Hapa chini nimeorodhesha baadhi ya dondoo zinazoweza kumsaidia mtu yeyote anayejiandaa kuanza maisha baada ya kuhitimu masomo yake. Kumbuka wakati wa kumaliza masomo ndiyo muda muhimu sana wa kuhakikisha ndoto zako unazisimamia vizuri, hapa ndipo unaanza safari nyingine pengine ngumu zaidi ya ile uliyomaliza. Karibu tusome pamoja.

1.JIEPUSHE KABISA KWANZA NA MIKOPO
Vijana wengi wanapenda sana kumiliki magari, subiri kwanza magari yapo siku zote, usikimbilie kukopa kisa tu na wewe uonekane unamiliki gari kali. Ukitaka kununua gari au kitu chochote kile kitakachogharimu fedha nyingi basi jiwekee kwanza akiba kidogokidogo mpaka pale pesa hizo zitakapotimia ndipo ununue.


Tumia ile kanuni ya kujilipa mwenyewe kwanza kila mwezi, itakusaidia sana katika kutimiza shauku yako hiyo kali(ndoto) badala ya kukimbilia benki au taaasisi za fedha. Kwanza kumbuka unalo deni tayari kama ulisoma kwa mkopo sasa madeni juu ya madeni ni ya nini?

2.KUBALI KUFANYA MAKOSA.
Watu wengi unaowaona leo hii wakiwa na mafanikio makubwa kama wangelikubali kusikiliza sauti za watu zilizokuwa zikiwaambia wanafanya makosa, sidhani kama leo wangekuwa pale walipo. Hawakukatishwa tamaa kirahisirahisi na makosa yao. Funga masikio endelea kuboresha na kurekebisha taratibu.

3.USIIONEE AIBU HALI ULIYOKUWA NAYO.
Unapaswa kuyakubali maisha kama yalivyo. Kwa mfano usione haya kutembeza bidhaa zako mtaani ukiziuza kisa eti unaogopa kuonekana na wale wanaokufahamu, wala usiogope kutembea kwa miguu wakati wa kwenda kazini ikiwa ofisini siyo mbali sana na unakoishi.

4.USIJARIBUI KULINGANISHA MAISHA YAKO NA YA MTU MWINGINE YEYOTE YULE.
Watu mashuhuri au wenye uwezo unaojaribu kujilinganisha nao, niamini wana matatizo yao kama ulivyokuwa na ya kwako. Wanasumbuliwa na matatizo nkibao kwenye mahusiano yao, wana matumizi makubwa kwenye bajeti zao na hata jamii nzima hutegemea mambo makubwa zaidi kutoka kwao kuliko kama ilivyokuwa kwa watu wa kawaida. Huo ni mzigo tosha na hivyo kujaribu eti kujilinganisha nao kamwe hautapata amani ya nafsi


5.KUWA MAKINI SANA UNAPOONA MAFANIKIO YANAKUJIA KIRAHISIRAHISI.
Mara nyingi mafanikio ya namna hiyo ni kama yanakutega vile. Ni lazima kwanza kabla ya kufanikiwa uanguke kwa namna moja au nyingine, vinginevyo hautajua thamani ya mafanikio hayo. Au inawezekana mafanikio hayo yamekutokea kwa bahati na sibu tu. Hebu fikiria ikiwa mbele ya safari utakuja kuanguka na isikutokee tena bahati na sibu, maisha yako yatakuwaje?

6.FANYA KITU CHAKO MWENYEWE.
Bila ya kujali kitu hicho ni kidogo au kikubwa kiasi gani, lakini cha muhimu anzia chini kabisa na jifunze namna ya kukitafutia soko mwenyewe, wala haijalishi unapoanzisha kitu hicho una ajira au hujaajiriwa wewe anzisha tu. Hii itakupa funzo muhimu sana maishani litakalokuja kukusaidia huko mbele ya safari, litakupa ujasiri na kujiamini kwamba hata likitokea jambo lolote baya katika ajira au shughuli uliyokuwa nayo basi unaweza kuingia mstari wa mbele mwenyewe(front)  na kuanza mapambano.


7.JAMBO MOJA LINAPOKWAZA MIPANGO NA NDOTO ZAKO, ISIWE NDIYO MWISHO WA KILA KITU.
Usisimamishe mambo yako mengine yote kwa ajili yake na badala yake jitahidi kuhamishia mawazo yako kwenye mambo mengine chanya zaidi ndipo utaweza kuwa na maisha bora yaliyo na furaha na mafanikio.

8.SAIDIA WATU WENGINE MARA NYINGI KADIRI UWEZAVYO.
Usiwaache katika dhoruba ya mateso kama unao uwezo wa kuwaokoa kutoka wakati mgumu unaowakabili. Mara nyingi utakuja kulipwa kwa njia moja au nyingine wakati ujao. Kumbuka safari yako bado ni ndefu na unao muda mwingi mbele tofauti na mtu aliyekwishakaa muda mrefu mtaani, utakutana na watu wengi baadae hujui kama unayemsaidia leo atakuja naye kukusaidia nini hapo baadae.

9.USIJIHANGAISHE KUFANYA KILA KITU KWA UKAMILIFU WA KIWANGO CHA HALI YA JUU SANA.
Unahitaji tu kutafuta suluhisho la kawaida, mambo makubwa mara nyingi sana hutokana na mambo madogomadogo ya kawaida tu.


10.KUBALI KUFELI KUPO NA KILA MTU HUFELI
Kila mtu katika muda wa maisha yake hapa duniani hufeli wakati mmoja au mwingine, cha msingi ni mtu kutokukata tamaa na kujaribu tena na tena baada ya kuanguka.

11.MWISHO USISAHAU KUWA MAISHA NI MAGUMU USIPOKUWA MAKINI.
Haijalishi kama wewe ni nani, wala unazo fedha kiasi gani, usipokuwa makini si ajabu siku moja ukajikuta maisha yamegeuka chini juu kwako, jitayarishe kila wakati na kuwa makini. Ni nani alijua watu kama kina Michael Jackson, Whitney Huston, Mc Hammer na mifano mingine kibao hata hapa Tanzania wapo, watu hao wangekuja kujikuta katika wakati mgumu kiuchumi kufikia hatua ya kujitoa uhai, wakati mwanzoni walishashika pesa kufuru?

……………………………………………….........

Ndugu msomaji wa makala hizi, karibu pia katika GROUP la masomo ya kila siku la WHATSAPP la MICHANGANUO-ONLINE kule tunajifunza kila siku masomo yahusuyo fedha na michanganuo ya biashara. Pia tunakuwa na semina za mara kwa mara za jinsi ya kuandika Michanganuo ya biashara bunifu zinazolipa haraka. Kiingilio ni sh. Elfu 10 tu, tunakupatia na offa ya vitabu na masomo mbalimbali yaliyopita.

Somo letu la leo tarehe 23 July 2018 litahusu, MBINU ZA KUIFANYA SIKU YAKO IONEKANE INA MASAA 25 BADALA YA 26. Kumbuka masomo ni kila siku, ukitaka kulipia tumia namba za simu 0712202244  au  0765553030 jina hutokea Peter Augustino Tarimo kisha tuma namba ya whatsap au email yako na ujumbe usemao, ‘NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO’






1 Response to "USHAURI KWA MWANAFUNZI ALIYEHITIMU CHUO/MASOMO ANAYETAKA KUANZA MAISHA"