VIPAJI, UWEZO, AKILI NI VITU WATU TUNAZALIWA NAVYO AU KUJIFUNZA? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

VIPAJI, UWEZO, AKILI NI VITU WATU TUNAZALIWA NAVYO AU KUJIFUNZA?


vipaji uwezo na akili
Huwa tunawaona watu duniani wenye vipaji, akili na uwezo wa wa aina mbalimbali kama vile wanamuziki, wanamichezo, wasanii, viongozi  na hata watu waliobobea katika taaluma mbalimbali kama  sayansi, uchumi, sheria, utabibu na saikolojia kiasi ambacho hata mtu unadiriki kutamani na wewe ungelikuwa kama walivyo, lakini kuna siku hata moja umewahi kujiuliza kama watu hawa wamejaliwa tu na Mwenyezi Mungu na kuzaliwa wakiwa na vitu hivyo au walikuja kuvipata hapa duniani baada ya kuzaliwa?

Utafiti mwingi umekwishawahi kufanyika katika maeneo mengi ya dunia kuhusiana na swali hili na majibu yake kwa kweli yanastaajabisha. Hata kwa mtu wa kawaida unaweza ukaangalia nyuma maisha yako ulikotoka, watu uliosoma nao na wale uliokua nao rika moja, utagundua kwamba baadhi ya watu walikuja kubadilika na kuwa tofauti kabisa na vile walivyokuwa awali, akili, vipaji na uwezo wao ulikuja kuonekana kuwa tofauti au kinyume kabisa na vile ulivyodhania watakuwa.


Hebu tuchukua mfano mmoja wa mtu anayeaminika kuwa ndiye mwenye akili nyingi zaidi duniani(IQ kubwa) . Mtu huyo anayejulikana kama Christopher  Michael Langan alipimwa na kukutwa na kiwango cha IQ 195 karibu asilimia 30% juu zaidi ya IQ aliyokuwa nayo mwanasayansi mkubwa zaidi duniani, Albert Einstai, IQ ya mtu wa kawaida ni 80 mpaka 120. Langan alipozaliwa alianza kuongea akiwa na miezi 6 tu. Akiwa shule ya msingi ilibidi arushwe madarasa ya juu kutokana na uwezo wake wa akili usiokuwa wa kawaida. Akiwa sekondari ilimbidi ajifunze peke yake kutokana na kukorofishana na walimu wake waliodai hawawezi kumfundisha mtu anayewazidi akili, na chuoni nako alliamua kuacha akidai kwamba alikuwa na uwezo wa kuwafundisha Maprofesa wake vizuri zaidi kuliko wao walivyoweza kumfundisha yeye.

Lakini pamoja na uwezo huo mkubwa kiakili aliokuwa nao Langan unafahamu ni kitu gani kilichokuja kumtokea katika maisha yake baadae? endelea kusoma nitakusimulia punde kidogo.


Tukirudi kwenye hoja yetu ya msingi kwamba vipaji, uwezo na akili nyingi binadamu huwa wanazaliwa navyo?, jibu ni HAPANA. Kipaji kama ilivyokuwa ujasiriamali watu hukikuza katika mazingira wanamoishi baada ya kuzaliwa. Ni ukweli kila mtu huzaliwa na kiasi fulani cha vitu hivyo lakini ili kuja kubobea kunahitaji juhudi na maarifa.

Ingawa mtu anaweza akazaliwa akiwa na fursa fulani zinazochochea zaidi vitu hivyo kama vile mtu kuzaliwa IQ yake ikiwa kubwa, umbile lililokaa kimichezo, mtoto anayezaliwa katika familia yenye uwezo wa kumpa elimu nzuri au mtaji, wengine huzaliwa wakiwa na sauti nzuri, sura na umbile zuri nk. Vyote hivi ijapokuwa vinaweza kumpa mtu fursa nzuri ya kufanya mambo makubwa lakini mhusika ni lazima afanye kazi ngumu ya kuvikuza vinginevyo atabakia tu vile vile kama watu wengine waliozaliwa hawana hivyo vitu.


Ili mtu aweze kufanya mambo makubwa ni lazima atambue wazi ni kitu gani anachomudu kukifanya kisha kuanzia pale aanze kukuza na kuendeleza kipaji au uwezo huo kwa njia za kujifunza, kujitoa mhanga, nidhamu na kujitolea muda mwingi wa kutosha kukifanyia mazoezi kipaji hicho.

Kuna watu wengi tu duniani walizaliwa wangali hawana fursa yeyote ile, hawakuwa na sauti nzuri, hawakuwa na akili nyingi darasani IQ, hawakuwa na miili iliyokaa kimichezo, Wengine walizaliwa hata hawana baadhi ya viungo mwilini lakini baadae walikuja kuwa wabobezi katika fani zao. Hii inamaanisha nini? Inamaanisha kwamba binadamu anaweza akawa chochote kile anachotamani kuwa ikiwa tu atachagua kuwa hivyo.

Lakini ni kwanini watu wengi hushindwa kufikia viwango vya juu katika vipaji au fani zao? Sababu mojawapo ni kwamba siyo jambo rahisi mtu kuweza kufikia viwango vya juu, inahitajika juhudi nyingi na kwa asili sisi binadamu tulivyoumbwa huwa hatupendi kufanya vitu vigumu.


Katika kitabu changu nilichoandika kiitwacho “SIRI ZA KUJIFUNZA ELIMU YA PESA NA MAFANIKIO KWA UFANISI”(nadhani wale wote waliojiunga kwa email katika blogu ya jifunzeujasiriamali wanakifahamu) katika ukurasa wa 15 nikinukuu kutoka kitabu kingine kiitwacho Outliers nilisema kwamba, kitu kinachowatofautisha matajiri waliofanikiwa na sisi watu wa kawaida ni masaa(MUDA) wanayotumia katika fani au vipaji vyao. Mwandishi alitolea mifano ya wanamuziki wa kundi la The Beatles, Steve Jobs na Bill Gates akisema kwamba  wote walitumia karibu masaa elfu 10(10,000) katika fani zao kabla hawajafanikiwa kufanya mambo makubwa yaliyowafanya kuonekana wabobezi katika fani zao.

Sasa hetu tena turudi kwenye ile stori yetu ya Christopher Langan, mtu mwenye IQ kubwa kabisa duniani na hatma yake. Kilichokuja kumkuta mtu huyu ni kwamba alikuja kuishia tu kuwa mtu wa kawaida akifanya kazi za kubeba mizigo, wakati mwingine aliajiriwa kama mlinzi, baunsa na hadi hivi leo amebakia tu kuwa mtu maarufu kwa kuwa na akili nyingi lakini hakuna cha maana alichoweza kukifanya maishani tofauti na watu wengine kama kina Bill Gates Steve Jobs, Albert Einstain na wengineo ambao hawakuwa na kiwango kikubwa cha akili kama alichokuwa nacho Langan lakini mambo waliyoyafanya ni makubwa mno, waliweza kubobea katika fani zao. Siri yao kubwa siyo nyingine bali ni kujitoa kikamilifu kwa vitendo, nidhamu, na kujifunza kwa bidii.


Hii ni habari njema sana kwa kila mtu anaye ‘struggle’ kwani ni dhahiri kabisa kwamba hatuna tena kisingizio cha kuwa chochote kile tunachopenda, visingizio kama vile; sijazaliwa na kipaji hiki, mimi darasani sikufanya vizuri, sina uwezo, IQ yangu ni ndogo nk. Unachohitaji ni maamuzi na kisha kujitolea kwa moyo wako wote kuwa kile unachotaka uwe.

Kwa mfano unataka kuwa mwandishi mzuri, huna budi  kutumia masaa yako mengi kufanya mazoezi ya kuandika bila ya kujali shuleni ulipata alama gani katika somo la lugha.

Ninao mfano mzuri mimi binafsi wa wanafunzi wangu ninaowafunza jinsi ya kuandika mpango wa biashara katika Group la Whatsap la MICHANGANUO-ONLINE, wengine ni wanafunzi katika vyuo mbalimbali na wengine hunitumia kazi zao ili niweze kuwapa ushauria au kuzipitia na kuwakosoa pale walipofanya makosa.

Mmoja alinitia moyo sana baada ya kunitumia mchanganuo wa biashara yake aliyokuwa ameshasahihishiwa na mkufunzi wake, aliniambia chuoni alichagua swali hilo la kuandika mchanganuo wa biashara baada ya kujiunga na masomo yangu na kudai masomo hayo yalikuwa msaada mkubwa kwa yeye kufanya vizuri assignment ile.Ijapokuwa alikuwa amepewa maksi nzuri tu na mwalimu wake baada ya kuupitia nilikuta kuna baadhi ya sehemu alikuwa amefanya makosa na nikamshauri alitakiwa kufanya kitu gani. Alinishukuru sana na kusema ule ndiyo uliokuwa mchanganuo wake wa kwanza kuwahi kuandika.

Nilimpa siri ya kuwa bora katika uandishi wa michanganuo kuwa ni kufanya mazoezi ya kuandika michanganuo zaidi kwani kwa kadiri alivyojitahidi  katika mchanganuo wake huo wa kwanza bila shaka atakuja kuwa mbobezi hata kunipita endapo ataandika michanganuo miwili mitatu zaidi.


Hivyo kubobea katika fani, kipaji au uwezo wa aina yeyote ule hakuna uhusiano wowote na kile mtu anachozaliwa nacho kutoka tumboni mwa mama yake bali hutokana tu na juhudi zako za makusudi na kujitambua kuwa ni nini unachotaka kukifanya.    



…………………………………………....

Ndugu Msomaji, napenda kukujulisha kwamba masomo ya kila siku katika lile group letu la Whatsap yanaendelea kila siku na wiki hii tutaanza tena semina za kuandika michanganuo ya biashara zinazolipa hatua kwa hatua. Kama utapenda kujiunga basi lipia ada yako sh. Elfu 10 kupitia namba za simu 0712202244  au 0765553030 kisha tuma ujumbe wa “NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO” na tutakuunganisha muida huohuo pamoja na kukutumia vitabu, masomo na semina zote zilizopita.    

0 Response to "VIPAJI, UWEZO, AKILI NI VITU WATU TUNAZALIWA NAVYO AU KUJIFUNZA?"

Post a Comment