JINSI YA KUANDAA MCHANGANUO WA BIASHARA YENYE MAFANIKIO, MAENEO 6 MUHIMU YA KUZINGATIA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI YA KUANDAA MCHANGANUO WA BIASHARA YENYE MAFANIKIO, MAENEO 6 MUHIMU YA KUZINGATIA


Wajasiriamali tumezoea dhana kwamba Mpango wa biashara ni kitu kinachohitajika tu pale tunapokwenda katika taasisi za fedha au benki kuomba mikopo kwa ajili ya kuendelezea biashara zetu. Lakini kitaalamu mpango wa biashara ni zaidi ya hivyo.

Mpango wa biashara au mchanganuo wa biashara kama wengi tulivyozoea kuuita ni muhimu sana katika suala zima la usimamizi wa biashara unayokusudia katika kupanga malengo yaliyokuwa wazi ya kampuni au biashara yako na kuelezea kikamilifu jinsi utakavyoyafikia malengo hayo.


Mchanganuo wa biashara siyo tukio la mara moja bali ni andiko linaloweza kupitiwa mara kwa mara na kufanyiwa marekebisho kila wakati inapohitajika kulingana na mabadiliko nayo yanavyotokea katika biashara. Biashara inafanana na kitu kinachoishi, hubadilika, kukua na hata wakati mwingine hufa. Ni njia bora kabisa ya kuelezea ni wapi biashara yako inakoelekea.

Katika uandaaji wa mchanganuo wako wa biashara yapo maeneo ambayo yanatakiwa kupewa umuhimu wa kipekee ili kuweza kuunganisha sehemu nyingine zote za mpango huo na kuleta maana au uhalisia unaotarajiwa. Maeneo hayo ni haya yafuatayo;


1. UTAFITI
Tenga muda wa kutosha kufanya utafiti wa kina kuihusu biashara yako  kufahamu mambo mbalimbali(facts) ili mwisho wa siku utakapokuja kuziunganisha sehemu zote na sura za mchanganuo wako ziweze kuleta mantiki.

2. DHANA/MAKISIO(ASSUMPTIONS)
Tengeneza makisio ya kina(detailed assumptions). Msingi mkubwa wa mpango wa biashara wowote ule uliokuwa mzuri unasimama juu ya dhana imara ambazo zitakuwezesha kufanya makisio yako kwa usahihi. Makisio au dhana hizo ni sawa na dira inayokuongoza katika kujua matokeo ya wakati ujao au kukuwezesha ‘kuigiza’ vile biashara yako itakavyokuwa hapo baadae.


Mjasiriamali unapotengeneza makisio/dhana zako unatakiwa kufanya hivyo ukizingatia vitu muhimu vitatu ambavyo ni;

1.  Mauzo
2.  Gharama zinazobadilika
3.  Gharama zisizobadilika(za kudumu)

Katika vitu hivyo vitatu unatakiwa uonyeshe ni kwanini vimekuwa kama vilivyo, kwa mfano dhana kwenye mauzo yako unaweza ukaonyesha miezi fulani ni makubwa pengine kutokana na kwamba ni msimu wa mavuno au sikukuu nk. Pia dhana katika gharama unaweza ukakisia ni asilimia fulani ya mauzo kulingana na utafiti wako ulivyoufanya, uzoefu na hesabu za kipindi cha nyuma au biashara nyingine zinavyofanya kwenye sekta hiyo.


Unapoweza kuunganisha na kuhusianisha vyema dhana zako na malengo yako itakusaidia pia katika kuweka mikakati mahsusi ya masoko na kubaini ni rasilimali kiasi gani zinazohitajika ili kutimiza malengo ya biashara hiyo uliyojiwekea. Kila kitu katika mchanganuo wako wa biashara kinatakiwa kufungamana pamoja na kuhusiana.

3. MAHITAJI YA KUANZIA(KIANZIO)
Eneo hili ni nyeti sana wakati wa maandalizi ya mchanganuo wa biashara yeyote ile. Haitoshi tu kusema kwamba, tunahitaji shilingi 20,000,000 bali ni muhimu pia kuelezea kwa undani hiyo milioni ishirini itatumika kwa ajili ya vitu gani, onyesha gharama mbalimbali  za kuanzia kama vifaa, gharama za awali, eneo, mtaji wa kazi, jumla yake ni kiasi gani. Hii itamfanya msomaji wa mchanganuo wako kuona kweli ulifanya utafiti wa kutosha. Onyesha pia na chanzo cha mahitaji hayo ni nini(Mtaji ulikoutoa)


4. TAARIFA REJEA.
Taarifa rejea au vyanzo ulivyotoa taarifa za kutengeneza mchanganuo wako kwa mfano, upembuzi yakinifu, utafiti wa soko, taarifa za washindani wako na taarifa juu ya sekta uliyopo. Hii ni kama vile ushahidi wa kutia nguvu kile unachokieleza katika mchanganuo wako. Msomaji anategemea kuona alama(tanbihi) inayoelekeza chanzo cha maelezo yako.

Toa maelezo mafupi na yenye kueleweka kwa urahisi kwani wadau wengi mfano wakiwemo watu wa mabenki hawapendi maelezo marefu sana yasiyokuwa na tija, wanachotaka ni ukweli(facts) tu.

5. USIMAMIZI WA RASILIMALI WATU
Eneo hili ni wajasiriamali wengi hawalipi uzito unaostahili wanapoandika michangauo ya biashara zao, wakati ukweli ni kipengele muhimu sana ambacho ndicho kilichokuwa na changamoto kubwa zaidi kwa mjasiriamali wa leo hasa unapoajiri wafanyakazi katika soko la ajira lisilotabirika. Ni lazima uonyeshe kwa usahihi ni kwa jinsi gani utavutia wafanyakazi  walio na ujuzi watakaohudumia biashara yako.

Unatakiwa pia uonyeshe mchoro wa mfumo wa utawala pamoja na mahitaji ya rasilimaliwatu kama vile mikakati ya kuajiri wafanyakazi wa kudumu au vibarua wa muda mfupi.


6. OMBA USAIDIZI KUTOKA NJE.
Ni jambo la busara kuandaa mwenyewe mpango wa biashara yako kwa kuwa ni wewe mwenyewe ndiye unayeijua biashara yako vyema kuliko mtu mwingine yeyote yule, lakini unashauriwa hata kama umeandaa mwenyewe baada ya kumaliza kuandika basi umtafute mtu unayemuamini atakayekusaidia kuupitia mchanganuo huo ili kama kuna makosa au udhaifi mwingine wowote ule akushauri kuurekebisha au kuboresha.

…………………………………………….

Mpenzi msomaji wa makala hizi, napenda kukujulisha pia kwamba katika GROUP letu la WHATSAP la MICHANGANUO ONLINE, masomo ya kila siku usiku saa 3 yanayohusiana na Michanganuo na Mzunguko wa fedha bado yanaendelea kama kawaida na kuelekea nusu ya pili ya mwaka huu tunatarajia kuwa na semina kabambe za kuandika hatua kwa hatua michanganuo ya zile biashara zenye fursa kubwa ya kuleta faida haraka.

Leo hii tarehe 22 July ndani ya Group tutakuwa na somo la pesa lisemalo, “SEHEMU 6 SALAMA ZAIDI ZA KUTUNZIA FEDHA ZAKO, JE CHINI YA GODORO NA VIBUBU NAZO ZIPO?”

Karibu usikose somo hili na kila siku kwa masomo mengine mazuri yatakayokupa uelewa mpana zaidi wa pesa. Kiingilio ni shilingi elfu 10 tu kwa muda wote na tunakutumia offa ya vitu mbalimbali vikiwemo vitabu maarufu 2 vya michanganuo kwa kiingereza na Kiswahili pamoja na semina zilizopita na michanganuo kamili mbalimbali. Ukitaka kulipia unaweza kutuma pesa moja kwa moja katika moja ya namba hizo hapo chini au

Tuwasiliane kwa,
SIMU: 0712202244
WATSAP: 0765553030

Peter Augustino Tarimo   

0 Response to "JINSI YA KUANDAA MCHANGANUO WA BIASHARA YENYE MAFANIKIO, MAENEO 6 MUHIMU YA KUZINGATIA"

Post a Comment