UFUGAJI WA KUKU WA KISASA WA MAYAI VS KUKU WA NYAMA NI BIASHARA IPI INAYOLIPA FAIDA ZAIDI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UFUGAJI WA KUKU WA KISASA WA MAYAI VS KUKU WA NYAMA NI BIASHARA IPI INAYOLIPA FAIDA ZAIDI?


Kuku wa nyama vs kuku wa mayai
Msomaji wetu mmoja kutokea kule mkoani Morogoro  aliuliza swali hili lifuatalo, nami bila kupunguza wala kuongeza neno naliweka hapa kama ifuatavyo,

"Ndugu mshauri napenda sana kufuga kuku lakini nimeshindwa kuamua nianze na kuku wa aina gani, tafadhali ningeomba unijulishe kati ya kuku wa kisasa wa nyama na wale wa kisasa wa mayai ni wepi waliokuwa na faida zaidi ili nianze kwanza na hao ndipo baadae nikipata uwezo niweze kufuga na hao wengine pia. Asante sana nategemea jibu zuri toka kwako."

MAJIBU.
Kutoa  jibu  moja tu kwamba ni kuku wa aina gani, kati ya kuku wa kisasa wa nyama na kuku wa kisasa wa mayai ni yupi kati yao aliye na faida zaidi au wanaolipa zaidi siyo rahisi kabla kwanza ya kuchunguza mazingira mazima ya biashara ya ufugaji wa makundi hayo mawili ya kuku, gharama, muda na vitu mbalimbali vinavyohusika katika mchakato mzima tangu unawaingiza bandani mpaka unaanza kupata faida.

Hebu kwanza tuanze na kutizama kila upande, sifa zake, muda kuanzia wakiwa vifaranga wa siku moja mpaka wanapofikisha umri wa kuleta faida, gharama pamoja na vihatarishi mbalimbali.

KUKU WA NYAMA (BROILERS)
Kuku wa nyama ni kuku wanaofugwa maalumu kwa ajili ya nyama. Muda wao tangu wakiwa vifaranga wa siku moja mpaka kuuzwa ni mfupi, wiki 4 mpaka wiki 8 tu, kwa hiyo ndiyo kusema kwamba kama unataka faida ya harakaharaka basi kuku wa nyama ndiyo suluhisho lake.


Uzuri(Faida) za kufanya biashara ya ufugaji wa kuku wa nyama.
·       Kuku wa nyama pia huhitaji uwekezaji mdogo lakini mapato yake ni makubwa unapolinganisha na muda wake.

·       Faida nyingine unapowalinganisha na kuku wa mayai kwa upande wa magonjwa, kuku wa nyama wanayo nafuu moja kwani kutokana na kipindi chao cha kuishi kuwa kifupi sana hata unapotokea mlipuko wa ugojwa hasara yake siyo kubwa sana kwani unakuwa bado hujawekeza fedha nyingi sana hasa kwenye chakula.
·       Wanao uwezo mkubwa wa kubadilisha chakula wanachokula kuwa nyama haraka na hivyo ukuaji wao pia ni wa haraka.

·       Hauhitaji kiasi kikubwa sana cha madawa na chanjo kutokana na muda wake kuwa mfupi.


Ubaya(Hasara) za kufanya biashara ya ufugaji wa kuku wa nyama.
·       Hatari kubwa ya kufa kwa magonjwa hasa wanapokuwa vifaranga.

·       Wanahitaji uangalizi wa karibu mno na hula chakula kingi katika muda mfupi.

·       Kuku wa nyama usipokuwa makini sana na soko wanaweza kukusababishia hasara kubwa endapo muda wa kuwauza utafika na wakose mtu wa kuwanunua haraka.

·       Ili uweze kupata faida inayoonekana inakubidi mtaji wa kuanzia usiwe chini sana angalao uanze na vifaranga 100 kwenda juu na hata makampuni au wauzaji wenyewe wa vifaranga na mawakala wao huwa wanaanzia kuuza viaranga 100 kwenda juu.


KUKU WA MAYAI.
Hawa ni kuku wanaofugwa kwa ajili ya uzalishaji wa mayai aidha kwa ajili ya kula tu(mayai yasiyorutubishwa na jogoo) ama kwa ajili ya kutotolesha vifaranga(mayai yatokanao na matetea waliopandwa na jogoo).

Uzuri au faida za biashara hii ya ufugaji wa kuku wa mayai.
·       Hatari ndogo ya kufa kwa magonjwa hasa wanapokuwa wameshafikisha umri wa kuanza kutaga.

·       Kuku wa mayai wana faida endelevu na ya uhakika kwa kipindi kirefu kila siku kuanzia wanapoanza kutaga mpaka wanapofikisha wastani wa umri wa miaka 2 wanapokuwa wameanza kuzeeka.

·       Mayai yakichelewa kuuzika kwa siku kadhaa hayawezi kuongeza gharama kama ilivyokuwa kwa kuku wa nyama ilimradi tu yasizidi wiki mbili mpaka 3 muda yanapoanza kuharibika.

Ubaya(Hasara) za kufanya biashara ya ufugaji wa kuku wa mayai.
·       Kuku wa mayai wanahitaji kiasi kikubwa cha mtaji kwani unahitaji kuwekeza fedha nyingi zaidi ya miezi minne kabla haujaanza kuuza mayai.

·       Hasara huwa kubwa ukitokea mlipuko wa ugojwa kipindi wameshaanza kutaga.

·       Huhitaji madawa na chanjo nyingi.


Unaweza pia ukalinganisha uzuri wa biashara ya kuku hawa kwa kutumia kigezo cha wastani wa faida inayopatikana ndani ya kipindi fulani mfano kipindi cha mwezi au mwaka mmoja ukitumia idadi sawa ya kuku. Kwa mfano hapa mimi nitatumia idadi ya kuku 100 kuona kwamba katika kipindi cha mwezi mmoja wastani wa faida katika kila kundi ni kiasi gani.

Ni hesabu rahisi ambayo sitatumia gharama zote bali nitatumia zile gharama kubwa na muhimu kama chakula tu, gharama nyinginezo nitachukulia kwamba hazibadiliki kwa pande zote 2 (I assume to remain constant on both parties)


WASTANI WA FAIDA KWA KUKU WA NYAMA KWA MWEZI
Gharama(Chakula) kwa kuku mmoja
Wiki ya 1 mpaka ya 3, starter kg 1.1
Wiki ya 3 mpaka ya 6, Finisher  kg 3.4
Jumla wiki zote 6 kuku 1 atakula wastani wa  kg 4.5

Kuku 100 watakula kg 4.5 x 100 kg 450 sawa na mifuko 9 ya kilo 50, kila mfuko wastani wa sh. Elfu 45
Hivyo Kuku 100  kwa wastani watakula chakula cha sh. 405,000 kwa wiki 6

Mauzo ya kuku
Kuku 100 @ sh. 6000 = 600,000

Faida
Faida kwa wiki 6 = 195,000. Kwa wiki 1 = 32,500
Kwa mwezi au wiki 4 =
Sh. 130,000

WASTANI WA FAIDA KWA KUKU WA MAYAI KWA MWEZI
Gharama za chakula kwa kuku mmoja.
Wiki ya 1 mpaka ya 8 starter gramu 1,760
Wiki ya 8 mpaka ya 18 Grower, gramu 14,900
Wiki ya 18 mpaka wiki ya 90 layers gramu 65,520
Jumla kuku mmoja atakula gramu, 82,180 sawa na kilo 82.2


Kwa kuku wote 100 watakula kilo 82.2 x 100 = kg 8,220 sawa na mifuko 164.5 ya kilo 50 kila mmoja. Mfuko mmoja = sh. 45,000
Hivyo kuku wa mayai 100 katika muda wote wa wiki 90  watakula chakula cha wastani wa sh.
45,000 x 164.5 =
7,402,500

Mapato
Mauzo ya mayai kwa wiki 72 au siku 504 za utagaji
Kila siku wastani wa mayai 85 x siku 504 = mayai 42,840
Sawa na trei 1,428. Kila trei bei yake ni sh. 9,000
Jumla ya mauzo ya mayai ni sh 9,000 x 1428
12,852,000

Mauzo ya kuku waliokwishazeeka
Wastani wa kuku 95 x sh.7000 = 665,000
Jumla ya mapato yote ya mradi ni sh. 12,852,000 + 665,000 =

13,517,000

Faida
Faida kwa kipindi chote cha wiki 90 ni’
Mapato yote – Gharama zote
13,517,000 - 7,402,500 =
6,114,500

Faida kwa wiki moja = 6,114,500 gawa kwa wiki 90 = 67,930
Faida kwa mwezi mmoja au wiki 4 = 67,930 x 4 =
Sh. 271,720


HITIMISHO
Kwa haraka haraka ukitazama matokeo ya hesabu hapo juu utagundua ya kwamba kuku wa mayai wastani wa faida yake kwa mwezi ni kubwa shilingi 271,720 kushinda wenzao kuku wa nyama shilingi 130,000 kwa mwezi. Wastani wa faida kwa kuku wa mayai ingawa ni kubwa kwa mwezi lakini hupatikana baada ya kipindi kirefu tofauti na kuku wa nyama ambao huchukua kipindi cha wiki chache tu.

Kwahiyo kabla hujahitimisha kwamba ni kuku aina gani wenye faida zaidi, unapaswa kujipima katika vigezo vifuatavyo kutokana na jibu la swali hili kuwa na majibu tofauti kulingana na mtu na mazingira yake aliyonayo.

Muda ulio nao.
Jichunguze ikiwa labda kama upo bize sana na mambo mengine mengi. Kwa mfano biashara ya kufuga kuku wa mayai haitaweza kufanikiwa wala kuwa na faida kwako ikiwa kama huna muda wa kutosha kuwahudumia katika kipindi chote cha miaka 2 kwa hiyo chaguo lako kama huna muda ni kufuga kuku wa nyama(broilers)

Kiasi cha mtaji uliokuwa nao.
Kuku wa mayai wanahitaji mtaji mkubwa wa kuanzia pamoja na uwekezaji katika vifaa mbalimbali utakavyohitaji kama mabanda, vitalu, vyombo nk. na fedha hizi hazitakiwi eti ukazitafute wakati ukiwa umeshaanza vifanga wakiwa bandani hapana. Unapaswa kuwa nazo zote mfukoni au benki. Kama mtaji wako ni wa wasiwasi usije ukadhubutu kuanzisha biashara ya ufugaji wa kuku wa mayai labda uanze na idadi ndogo sana ya kuku kulingana tu na mtaji uliokuwa nao.


Nguvu kazi iliyopo.
Je utaajiri mtu/watu au utaendesha biashara ya ufugaji wa kuku mwenyewe?. Ni kina nani watakaokusaidia? Kwakuwa kuku wa nyama wanachukua kipindi kifupi sana ni rahisi kuendesha mradi hata kama ni wa idadi kubwa ya kuku ukiwa mtu mmoja peke yako lakini kwa upande wa kuku wa mayai ni lazima utahitaji wasaidizi. Kwahiyo kama huna msaidizi wa uhakika siyo vizuri kuanzisha biashara ya ufugaji wa kuku wa mayai, unaweza kuja kula hasara.

Na mwisho kabisa ni kwamba ikiwa unao uwezo wa kutosha katika vigezo vyote vilivyoainishwa hapo juu unaweza pia ukaamua kufuga aina zote 2 za kuku, kuku wa mayai(Layers) sambamba na kuku wa nyama(Broilers).

Natumaini ndugu yangu uliyeuliza swali hili majibu haya yatakuwa yamekupa mwanga wa kuamua ni kuku wa aina gani utakaoanza nao dhidi ya wengine, siwezi moja kwa moja kukushauri uanze kufuga aina gani kwa kuwa mazingira na uwezo wako siwezi kujua yapoje, hivyo ni juu yako wewe mwenyewe kuamua kulingana na vigezo nilivyokuanishia hapo kwenye majibu ya swali hili. 

ASANTE SANA. 
Peter A. Tarimo
Mshauri na mwandishi.

……………………………………………………

Je, unataka kuanzisha biashara ya ufugaji wa kuku lakini hujui ni gharama na mahitaji kiasi gani vinatakiwa? Usije ukadanganywa kwamba eti ukifuga kuku unahesabu faida tu hapana, kuna gharama mbalimbali pia unazopaswa kuzijua kabla na njia unazoweza kuzitumia kusudi uweze kupata faida kubwa. Kuyajua maswala hayo yote unahitaji kufanya utafiti na kuandaa mpango wa biashara yako ya ufugaji wa kuku hata bila ya kuandika kwenye karatasi, unaweza kupanga kichwani kwako tu ilimradi ufahamu ni jinsi gani unavyopanga.

Kwa kusoma michanganuo iliyokwishaandaliwa tayari unapata picha halisi ni jinsi gani uandae mpango wako. Tuna michanganuo ya kuku wa aina zote, kuku wa mayai, kuku wa nyama na kuku wa kienyeji ambayo inaweza kuwa msaada mkubwa kwako katika kuandaa mradi wako mwenyewe.

Chakufanya tu ni wewe kutuma malipo ambayo ni shilingi elfu 10 kwenye namba 0712202244 au 0765553030 na sisi tunakutumia kifurushi chenye michanganuo yote 3 muda huohuo. Jina hutokea Peter Augustino Tarimo.



1 Response to "UFUGAJI WA KUKU WA KISASA WA MAYAI VS KUKU WA NYAMA NI BIASHARA IPI INAYOLIPA FAIDA ZAIDI?"

  1. Woow ushauli mzur lakin nilihitaji kufahamu kuwa ni fedha kiasi gan inapaswa kuwa nayo unapohitaj kuanzà

    ReplyDelete