JE, PESA INAWEZA KUTATUA KILA TATIZO DUNIANI AU NDIO CHANZO CHA MATATIZO YOTE? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JE, PESA INAWEZA KUTATUA KILA TATIZO DUNIANI AU NDIO CHANZO CHA MATATIZO YOTE?

Pesa

Huu ni mjadala uliofanyika kwenye Mastermind group la MICHANGANUO-ONLINE 25/1/2022 na unaweza kushiriki kwa kutoa maoni yako wewe upo upande gani. Hapa nimeweka hoja kutoka pande zote mbili, wanaosema pesa inaweza kumaliza kila tatizo na upande wa wale wanaotetea kwamba Pesa ni chanzo cha kila tatizo hapa Duniani. Mwisho kabisa tulipiga kura na kuona ni upande upi ulioshinda mjadala. 

1. Upande wa ndiyo Pesa ni suluhisho la matatizo yote:

 

Mtu wa kwanza

Hebu jaribu kufikiria labda umekumbwa na ugojwa mbaya na wa ajabu, unaofanana na Corona ambao chanjo yake bado haijagundulika bado wala tiba, lakini ukasikia mara kuna dawa imepatikana huko Marekani lakini bei yake ni milioni 10 na unapona kabisa. Huoni kwamba kama huna pesa hapa tumekuzika?

Hebu fikiria zaidi labda umeoa au kuolewa na mweza ambaye hayupo vizuri kifedha, kila siku ugomvi hauishi ndani ya nyumba kisa pesa, kwanini pesa isiwe chanzo cha furaha?

Unataka kuwapeleka wanao shule nzuri na hupendi wapoteze muda wao bure kwenye zile shule za kina kayumba kwa sababu watamaliza darasa la saba hawajui hata kiingereza cha kuombea maji, sasa kwanini pesa isiwe mwarobaini wa matatizo yote duniani?

Jaribu kuvaa viatu vya ombaomba ambaye hana kabisa mahali pa kulala anazurura tu huko mjini, hivi kama leo hii nitakupatia milioni 20 ukaweza kwenda kujinunulia kiwanja cha 20x20 mbagala na bado ukabakiwa na pesa nyingine kwa ajili ya kusimamisha banda lako la mabati (fullsuit), niambie ubaya wa pesa hapo uko wapi?

 

Ni nani duniani asiyependa starehe? Kutembelea vivutio mbalimbali duniani, miji na majiji ukila bata na kunywa vizuri, ukinunua nguo kali pamoja na magari ya kifahari ya bei mbaya. Vitu vyote hivu huwezi kuvipata ikiwa kama mfukoni huna pesa.

 

Kwahiyo tusifanye mchezo jamani na pesa kwani hakuna tatizo isilotatua, tunaisingizia tu bure kuwa ni chanzo cha matatizo kwakuwa hatuna kitu mifukoni.

 

Mtu wa Pili

Pesa inao uwezo wa kutatua matatizo ya mtu kwa asilimia 99% hii inamaanisha kwamba inaweza kukuokolea muda wako kwa asilimia 99 huku ikikuachia asilimia 1% tu ya matatizo yako uyatatue mwenyewe. Kwa mtindo huo unaweza kuona kwamba unamiliki asilimia 100% ya muda wako kutatua asilimia 1% tu ya matatizo yako. Hii haimaanishi kwamba pesa imetatua mataizo yako kwa asilimia 100%? kwa sababu pesa imetatua mataizo yako kwa asilimia 99% na kukufanya mwenyewe utatue asilimia 1% iliyobakia.

 

Mtu wa Tatu

Ikiwa utahitaji chochote kile pesa inaweza kununua, Chakula, malazi, elimu, afya, usafiri, burudani nk. Na ikiwa utapenda kufanyiwa jambo lolote lile, mara zote yupo mtu aliyeko tayari kukufanyia kwa bei stahiki. Ukiwa na pesa unaweza kujipatia huduma ya daraja lolote lile la juu mfano kwenye ndege, gari moshi, Uba, mwendokasi ama usafiri mwingine wowote ule, wewe utapanda first class kila mara na siyo daraja la tatu ama la nne. Ikiwa mtu ni mgojwa karibu ya kufa anaweza akalipia matibabu yeyote yale ya bei ghali kuokoa maisha yake tofauti na mlalahoi wa kawaida.

Sikatai kweli kuna mazingira machache sana pesa inaweza isiweze kutoa msaada lakini tukubali tu ukweli kwamba walio na pesa za kutosha wanaweza kujiandaa vizuri zaidi kabla majanga hayajawakuta na wanakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kukabiliana na madhara yeyote yatokanayo na majanga hayo. Kwa hiyo pesa bwana inaweza kutatua kila tatizo asikudanganye mtu.

 

Mtu wa nne

Pesa ni kila kitu bwana! Ingawa nakubali kwamba pesa ndio chanzo cha maovu makubwa zaidi Duniani, lakini pia ndiyo chanzo kikuu kabisa cha furaha. Nina uhakika pesa inaweza ikatatua kitu chochote kigumu katika maisha yangu, hata naweza nikasema ina uwezo wa kutatua matatizo mengi ya kiakili yanayowakumba watu wengi siku hizi mfano misongo ya mawazo, upweke na hata kuchanganyikiwa akili kunakosababishwa na hali ngumu na duni za kimaisha.

 

Mtu wa Tano

Ndiyo pesa inaweza kusuluhisha karibu matatizo yote. Katika nyakati za zamani inawezekana haikuweza kutatua kila tatizo lakini kwa nyakati hizi za sasa pesa unaweza ukaifananisha na hewa ya Oksijeni au Visa ya kusafiria, huwezi kuishi bila ya pesa utakufa!

a)  Pesa inakupa uhalali wa karibu kila kitu

b)  Pesa inakupa nguvu

c)   Pesa ni kitu kinachoongeza thamani kwenye utu wako

d)  Ukiwa na pesa ni sawa na mtu aliyeketi juu ya gari au baiskeli yenye zile springi za kuzuia mshtuko (Shock absorber) gari ikiruka juu huwezi kuumia kamwe.

Na kwa msaada wake unaweza ukatatua kila tatizo linalokuja mbele yako.

 

Mtu wa sita

Ndiyo pesa inaweza kutatua matatizo yote. Watu wanaweza wakasema kwamba pesa inaweza tu kutatua matatizo kama ya ulipaji wa madeni mbalimbali na kodi za serikali, lakini pia hata unapokuja upande wa suala la mahusiano kwa kutumia pesa mtu unaweza ukanunua urafiki na mapenzi kisha baada ya muda kupita hautaendelea tena kulipa kwakuwa rafiki au mpezi anakuwa keshakuzoea tayari na mmekuwa pengine mke na mume. Pasipo pesa pengine isingeliwezekana kabisa kumpata.

Pesa inatatua kila kitu sema tu tatizo ni watu kushindwa kupata pesa za kutosha kutatulia matatizo yao ndio maana wanatafuta sababu zisizokuwa na mashiko. Binti mdogo mrembo hata wa miaka 17 atakubali kuolewa na mzee wa miaka 70 huku wakiitana baby baby, lakini je, ikiwa mzee wa miaka hiyo asiyekuwa na kitu kabisa kweli si hata wanawake wa umri wake watamkimbia? Tuache masikhara bwana pesa inatisha!

 

2. Upande wa hapana, Pesa ndiyo chanzo cha matatizo yote duniani:

 

Mtu wa kwanza

Pesa ni ibilisi na chanzo cha kila aina ya uovu hapa duniani, ninachokubali tu ni kweli pesa inaweza kukusaidia kulipia baadhi ya vitu fulanifulani  lakini linapokuja suala zima la mahusiano pesa imefeli kabisa, Unaweza kutumia pesa kumnunua mpenzi na marafiki lakini hebu niambie mpaka lini utaendelea kuwalipa? Mapenzi ya kweli kamwe hayawezi kudumishwa na pesa na ingelikuwa ni hivyo basi Bill Gates Bilionea aliyewahi kushika namba moja kwa utajiri Duniani asingetalikiana na mkewe na wakaachana mazima kila mtu na hamsini zake.

Mtu wa Pili

Wewe unasema Bill Gates? Mbona huyo ni chamtoto tu, Bilionea namba moja (1) duniani anayeongoza sasa hivi kwa utajiri mkubwa Bwana Elon Musk anaishi ubachela huu mwaka wa 5 sasa hana mkemaalumu baada ya kuachana na mkewe na isitoshe si mke mmoja keshataliki zaidi ya wake watatu katika nyakati tofauti, hivi kweli mnaosema pesa ni kila kitu kwanini tusiwapeleke mirembe mkapimwe? Pesa itanunua kila kitu lakini haiwezi kabisa kununua furaha, mapenzi wala urafiki. Pesa haiwezi kutatua matatizo yote bali inaweza tu kutatua baadhi ya matatizo.

 

Mtu wa Tatu

Pesa hutengeneza tu njozi za furaha lakini siyo furaha halisi, waliojaliwa kuwa na pesa nyingi wanaweza tu kurahisisha maisha yao lakini pia hilo linaweza kusababisha mataizo. Watu walio na furaha zaidi maishani hudai kwamba chanzo cha furaha yao ukweli kimetokana zaidi na maswala ya kiroho, mahusiano imara, kuweza kukabiliana na matatizo, kitendo cha kuwasaida binadamu wengine waliokuwa na matatizo mablimbali pamoja na kujitoa nje ya ukanda wao wa faraja (step out of their comfort zone)

Kuwa na fedha nyingi sana hutengeneza tu njozi za furaha, na kama tujuavyo sote watu wanaoishi kwa njozi ni hatari sana kwani wanahisi muda wote wao ni wakamilifu wasiokuwa na makosa.

 

Mtu wa Nne

Pesa siyo majibu ya kila kitu tunachohitaji katika jamii zetu, kwa mfano ukiangalia miji mikubwa na tajiri duniani kama vile New York, London na Shangai kuna kiwango kikubwa sana cha uhalifu, wakati katika miji yetu masikini mfano Zanzibar, Dodoma, Bujumbura, Nairobi na Kampala jamii zimetulia na huwezi kusikia matukio makubwa makubwa sana ya uhalifu na mauaji ya kutisha, watu wana furaha pasipokuwa hata na pesa nyingi na wanafanya mambo ambayo watu matajiri wasingeliweza kuwa na wazo la kuyafanya, mambo hayo ni mazuri kwasababu wanayafanya kwa ushirikiano kama binadamu wa kawaida. Kama nilivyotangulia kusema pesa siyo jibu la kila kitu maishani.

 

Mtu wa Tano

Pesa ingelikuwa na uwezo wa kuleta furaha maishani Mastaa na watu mashuhuri duniani wasingejiingiza katika uraibu wa dawa za kulevya, pombe na bangi. Kwa kutumia vitu hivyo wangali na pesa nyingi ni ishara tosha kwamba kuna kitu fulani wanachokikosa katika maisha yao licha ya pesa nyingi wanazozimiliki, hivyo wanajaribu kukitafuta kitu hicho kwenye hivyo vilevi. Kitu hicho si kingine bali ni Furaha. 

 

Mtu wa Sita

Kwa kukazia tu msumari uliogongelewa na msemaji aliyetangulia kusema, ngoja niwataje kabisa live watu mashuhuri waliokuwa na pesa zao hapa Bongo na nje ya bongo lakini waliishia maisha ya kusikitisha. Michael Jackson alikufa mpweke licha ya utajiri wote aliokuwa nao, watu tulitazamia labda kando ya kitanda chake pangelikaa mkewe na watoto wake wawili wakati akikata roho lakini haikuwa hivyo, niambieni huo uzuri wa pesa hapa uko wapi?. Mwimbaji mwingine mashuhuri Whitney Houston na mwanaye wote waliishia vifo vya kusikitisha baada ya matumizi yaliyokithiri ya mihadarati, niambie walikosa kitu gani? Mastaa wa hapa bongo kwa leo nawaweka kiporo lakini wapo pia ambao pesa haikuweza kuwasaidia kwa lolote. 

                                                                              

Je, mpenzi msomaji na wewe una maoni gani? Tafadhali usiache kutushirikisha tuongeze hapo walipoishia wengine lakini pia kura yako ni muhimu ili tuweze kujua sote kwa pamoja ni upande upi utakaoshinda mjadala huu.

Asante sana

Peter Augustino Tarimo

0765553030   

 

Tafadhali piga kura yako hapo chini;

Je, Pesa inaweza kusuluhisha kila tatizo linalomkuta mwanadamu?
Ndiyo Inaweza
Hapana Haiwezi
Created with Quiz Maker


SOMA NA HIZI HAPA;

1. Unahitaji kupata pesa kiasi gani kwa siku ili uweze kuwa na furaha maishani? 

2. Saikolojia ya pesa na kanuni 10 za kufuata ili uwe mtu uliyefanikiwa kimaisha

3. Biashara 7 nzuri za kufanya zitakazokuingizia pesa hata kama umelala

4. Njia 6 za kuondoa woga na stress za pesa katika maishayako

5. Je, ipo kanuni ya mafanikio ya kifedha? Mtazamo wakisaikolojia

0 Response to "JE, PESA INAWEZA KUTATUA KILA TATIZO DUNIANI AU NDIO CHANZO CHA MATATIZO YOTE?"

Post a Comment