SEMINA: MCHANGANUO WA UFUGAJI WA KUKU CHOTARA WA NYAMA KIUBUNIFU, SIKU-1(MAANDALIZI) | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SEMINA: MCHANGANUO WA UFUGAJI WA KUKU CHOTARA WA NYAMA KIUBUNIFU, SIKU-1(MAANDALIZI)

kuku aina ya kuroiler
Hii ni sehemu ya semina yetu ya siku ya jana tarehe 25/03/2024 kweny Group maalumu la semina hizi za Ubunifu katika biashara, tulianza na Maandalizi na leo tena TAREHE 26/03/2024 saa 3 usiku tutaendelea na vipengele 3 vya  “MUHTASARI, BIDHAA & BIASHARA” Karibu usikose

Tulianza hivi....................

Habari za muda huu wapendwa katika group letu hili maalumu kabisa kwa ajili ya semina za biashara bunifu mbalimbali. Katika mfululizo huu, leo tunaanza na mchanganuo wa biashara ya ufugaji wa kuku chotara aina ya Kuroiler kwa ajili ya nyama na itatuchukua siku 5 kumaliza tukilenga (focus) hasa ubunifu unaoweza kuifanya biashara hii kuwa yenye faida kubwa tofauti na ufugaji wa kawaida tu uliozoeleka na kila mtu.

Kwa siku ya leo, yale tutakayojifunza ni haya yafuatayo;

1.   Maana ya Mchanganuo/Mpango wa Biashara

2.   Maandalizi ya kuandika Mchanganuo wa biashara ya ufugaji wa kuku chotara kuroiler

3.   Jinsi ya kufanya Utafiti wa soko lako la kuku chotara kuroiler au sasso

4.   Njia 6 za kuandika mchanganuo wa biashara

1. MCHANGANUO/MPANGO WA BIASHARA MAANA YAKE NI NINI?

Ni andiko linaloelezea jinsi biashara yako itakavyoendeshwa. Ni ufupisho wa muundo wa biashara yako, malengo, mikakati na mpango wa fedha.

Ni muongozo unaokusaidia wewe na wadau wengine katika kuelewa jinsi biashara yako itakavyofanikiwa.

Malengo ya Mpango wa biashara

Lengo la msingi kabisa la mpango wa biashara ni kukusaidia kufahamu muelekeo wa biashara yako na hatua utakazochukua ili kufikia malengo. Unakuongezea kujiamini hata kama kutatokea mdororo wa kiuchumi mbele ya safari.

Kazi nyingine za mpango wa biashara ni kama vile;

·      Kuombea mkopo toka taasisi za kifedha na benki

·      Kujaribu wazo la biashara ikiwa kama linawezekana ama la

·      Kupima malengo ya biashara uliyojiwekea na

·      Kusaidia katika kazi ya kuiendesha biashara yako vyema  

2. MAANDALIZI YA KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA YA UFUGAJI WA KUKU KUROILER

KUROILER ni kuku wa aina gani?

Kroiler au Kuroiler ni aina ya kuku chotara wenye sifa zote mbili za kuku wa mayai na kuku wa nyama. Hukua haraka na kutaga mayai mengi kuliko kuku wa kienyeji huku wakiwa na uwezo mkubwa wa kubadilisha chakula chochote kile wanachokula kuwa nyama, hivyo  wanakula kilekile chakula cha kuku wa kienyeji anachokula na kukua muda uleule lakini akiwa na uzito mkubwa zaidi yaw a kienyeji. Hivyo wanakuwa na nyama nyingi kwa kipindi kifupi sana.

Kuku chotara maana yake ni mchanganyiko wa aina mbili tofauti za kuku walio na sifa tofauti kwa ajili ya kupata uzao wa kuku waliokuwa na sifa bora zaidi ya wazazi wao.

Katika ufugaji wa kuku wa kisasa ufugaji wa kuku chotara mtu anaweza akachagua mbegu tofauti apendayo kwa mfano mbali na aina hii ya kuroiler kuna kuku chotara wengine waitwao Sasso, hawa nao wana sifa zinazokaribiana sana na kroiler na asili ya kuku saso ni huko nchini Ufaransa miaka ya 50.

Kuroiler asili yao ni huko nchini India na ni mchanganyiko wa aina ya kuku wa nyama majogoo (broilers)  na matetea aina ya Rhode Island Red  au, Majogoo aina ya White Leghorn na matetea aina ya  Rhode Island Reds.

Baada ya kuamua kichwani mwako sasa unataka kulifanyia kazi wazo la biashara ya ufugaji wa kuku aina ya Kuroiler wa nyama, kitu muhimu kinachofuata ni maandalizi kwa ajili ya kuandaa mpango wa biashara yako. Na si kwa biashara hii tu peke yake bali pia na kwa biashara nyingine zote ni hivyohivyo.

Kwenye maandalizi ya mpango wa biashara ni lazima mtu ufanye kitu kinachoitwa UTAFITI au upembuzi yakinifu, maana yake unafikiria njia tofautitofauti zitakazokuwezesha kulitekeleza wazo lako hili la biashara. Utaanza kutafuta majibu ya maswali mbalimbali juu ya ufugaji wa kuku wa kuroiler kusudi baadae uweze kuchagua yale sahihi katika kuandika mchanganuo wako.

Mfano unaweza kuchunguza mifumo mbalimbali ya ufugaji wa kuku ukabaini ipo 3, Huria, Nusu huria na mfumo wa ndani. Sasa ukishafahamu faida za kila mfumo unachagua utumie mfumo gani mmoja kwenye mpango wa biashara yako, hiyo ndio maana ya kufanya utafiti kupata majibu utakayotumia.

3. NJIA ZA KUFANYA UTAFITI WA BIASHARA YAKO YA KUKU KROILER

Kuna njia kuu mbili za kufanya utafiti wa soko au biashara yako

1. Utafiti wa msingi

2. Utafiti wa Dawati 

1. Katika utafiti wa msingi unazungumza na wadau mbalimbali wanaohusiana na biashara ya ufugaji wa kuku chotara kama vile wanaofuga kuku kama wewe, wafanyabiashara ya kuku chotara na mazao yake, wateja wa kawaida mtaani, maduka ya chakula na vifaa vya kuku na wataalamu wa mifugo. 

2. Njia ya pili ya utafiti wa dawati ni kwa kusoma taarifa mbalimbali zinazohusiana na ufugaji wa kuku chotara kwenye vitabu, majarida, mitandao na vyombo vingine vya habari.

Vipengele muhimu zaidi kwenye biashara ambavyo hufanyiwa utafiti ni vile ambavyo taarifa zake mara nyingi haziwezi zikapatikana ndani ya biashara/kampuni na mfano wake ni kama vipengele vifuatavyo;

                           1.      SOKO

                           2.      BIDHAA

                           3.      USIMAMIZI na

                           4.      FEDHA 

1. soko

Kwa kuwa soko ndio kitu muhimu pengine kushinda vyote ili biashara ifanikiwe ni lazima tufanye uchunguzi iwapo kama wateja watapatikana kweli au la.  

Kwenye soko taarifa tutakazochunguza zinalenga katika kufahamu ukubwa wa soko la kuku wa nyama wa Kuroiler, aina ya wateja watakaonunua kuku, bei, ubora wa bidhaa zilizopo, ushindani na kiasi unachotarajia kuzalisha.

2. Bidhaa (kuku)

Tutachunguza mchakato mzima namna kuku wa Kuroiler wanavyozalishwa kuanzia uandaaji wa banda, vifaranga wa siku moja mpaka kuku wanapouzwa wote. Teknolojia pamoja na mikakati mbalimbali itakayotumika katika kuhakikisha wateja wanapata kuku bora wenye uzito na ladha inayostahili.  

Katika kutafiti jinsi kuku wa nyama Kuroiler wanavyokuzwa unapaswa kuzunguka katika maduka ya vifaa vya ufugaji kuku, kwa wafugaji unaowajua na kwa maofisa mifugo kuulizia bei za vifaranga wa kuroiler, vifaa mbalimbali kama madawa, chanjo, vitamini na chakula kwa ajili ya kulishia kuku hao. Linganisha ufugaji wa kuku wa kienyeji na ufugaji wa kuku wa kisasa kama vile ufugaji wa kuku wa mayai na hata ufugaji wa kuku wa nyama kibiashara. 

3. Usimamizi

Chunguza pia ni kina nani watakaoweza kuuhudumia mradi wako, Je utakuwa ni wewe mwenyewe? Familia au utaamua kumuajiri mfanyakazi? Jibu ndilo tutakaloandika kwenye mchanganuo wako.

4. Fedha

Kwenye fedha kitu cha kwanza tunachunguza mahitaji yote yanayotakiwa gharama zake ni kiasi gani na tutaweza kupata wapi fedha za kugharamia. Kitu cha pili ni kulinganisha mahitaji ya mradi na kiasi cha fedha mmiliki/wamiliki walizokuwa nazo, Ikiwa kiasi hakitoshi au umegundua kiasi hicho kitaishia njiani basi utatathmini uwezekano wa aidha kurekebisha mahitaji au kutafuta vyanzo vingine zaidi vya mtaji.

4. NJIA 3 ZA KUANDIKA MCHANGANUO WA BIASHARA

Unaweza kuandika mpango wa biashara yako kwa kutumia moja kati ya njia hizi 3 zifuatazo; 

1.   Kwa kufuatisha vipengele/sura zinazounda mpango wa biashara(Outlines)

2.   Kwa kutumia Vielezo/Templates

3.   Kwa kutumia Programu/Software maalumu za michanganuo ya biashara 

Hapa kwenye semina hii tutatumia njia ya 1 ya kufuata mfululizo wa vipengele vinavyounda mpango wa biashara. Mlolongo wa vipengele hivyo ni huu ufuatao;  

1.MUHTASARI 

2.MAELEZO YA KAMPUNI / BIASHARA 

3.BIDHAA au HUDUMA

4.TATHMINI YA SOKO

5.MIKAKATI NA UTEKELEZAJI

6.UENDESHAJI

7.MAELEZO YA UONGOZI NA WAFANYAKAZI

8.MPANGO WA FEDHA

9.VIELELEZO / VIAMBATANISHO 

Vipengele hivyo kwa undani tutaona hapo baadae.

Kwa siku ya Leo tunaishia hapa na tutaendelea na sehemu inayofuata siku ya kesho. Hakikisha unapitia kabisa mapema mchanganuo wako wa kuku wa nyama wa Kroiler niliokupatia kusudi wakati tukiandika hatua kwa hatua uwe unafuatilia kipengele kwa kipengele kufahamu namna mpangilio wa kila kipengele unavyotakiwa kuwa.

Pia FOCUS yetu ambayo ni UBUNIFU katika biashara hii bado tutaiona kwenye vipengele vinavyofuata huko mbele, hivyo fuatilia semina hii mpaka mwisho wake.

Asante

Peter



SOMA PIA NA HIZHI HAPA;

1.   Banda la kuku 100 wa kienyeji: vipimo, ramani, picha na jinsi ya kulijenga kwa ubora

2.   Muongozo kamili wa jinsi ya kufuga kuku wa nyama (broilers) kitaalamu- semina siku-3

3.   Ujasiriamali: ubunifu ndiyo msingi wake mkuu na injini ya uchumi katika soko huria.

4.   Kama una biashara ndogo ya mtaji mdogo, hizi hapa njia 11 za kuibusti

5.   Biashara 7 nzuri za kufanya zitakazokuingizia pesa hata kama umelala.


0 Response to "SEMINA: MCHANGANUO WA UFUGAJI WA KUKU CHOTARA WA NYAMA KIUBUNIFU, SIKU-1(MAANDALIZI)"

Post a Comment