BANDA LA KUKU 100 WA KIENYEJI: VIPIMO, RAMANI, PICHA NA JINSI YA KULIJENGA KWA UBORA

Banda la kisasa la kuku 100 wa kienyeji

Katika maswali ya wasomaji wa blogu ya jifunzeujasiriamali wanayoniuliza, nimekuwa napata maswali yanayojirudia mara kwa mara kuhusiana na jinsi ya kujenga mabanda ya kuku. Wakati fulani hata niliandika Makala hii isemayo, UJENZI WA MABANDA YA KUKU ISIWE KIKWAZO CHA WEWE KUANZISHA BIASHARA YA UFUGAJI WA KUKU. Hata hivyo siku za hivi karibuni nimeendelea kupokea maswali na changamoto kutoka kwa wafugaji wa kuku wapya na hata wale wa zamani pia wakitaka kufahamu au kupata ramani, michoro na hata vipimo vya banda bora na la kisasa la kuku linavyoweza kuonekana.

Hapa nitaanza kwanza na maswali waliyoniuliza wadau hao wa kuku kwa kuyaandika ikiwa ni pamoja na kuweka screenshots za meseji walizonitumia, 

1. Mdau wa kwanza aliuliza  hivi;

Je, naweza kupata ramani au mchoro au picha za banda la kuku la kuanzia ambalo linaweza kuchukua kuku 1000 hadi 2000?

Na screenshot yake ni hii hapa;2. Mdau wa pili yeye aliniuliza kama ifuatavyo;

Hi Mr. Tarimo, nimesoma taarifa zako kwenye Google nimezipenda sana. Mimi nataka kuwa mjasiriamali wa ufugaji wa kuku tena mkubwa ila sijui chochote kuhusu kuku na nataka nianze kwenye ujenzi wa banda la kuku la kisasa na la bei nafuu. Nahitaji msaada wako nianzeje pia niwe  kwenye group?

Screenshot yake ilikuwa hivi;

Banda la kuku la gharama nafuu

Baada ya kuona maswali hayo kwanza ningependa kuandika kile nilichowajibu kwa haraka haraka halafu tena nitaelezea kwa ufasaha kabisa banda la kuku 100 linatakiwa kuwa na ukubwa kiasi gani.

SOMA: Ujenzi wa mabanda ya kisasa ya sungura ulivyo rahisi na nafuu kwa mfugaji anayeanza

1. Majibu kwa mdau wa kwanza

Banda la kuku halihitaji kuwa na shepu au mtindo wa kipekee Sana bali tu liwe imara,  sehemu za kulia chakula, kunywea maji, kulala mfano mabembea nk. Pia lipitishe hewa safi vizuri na sakafu nzuri.

Vipimo vya banda zingatia kuku 6 mpaka 10 kwenye mita moja ya mraba. Yaani mita 1 upana kwa mita 1 urefu.

Kama ni kuku wa kienyeji ni vizuri ukatumia kuku 6 kwenye mita moja ya mraba ambapo kwa idadi ya kuku 2000 utahitaji mita za mraba; 2000/6 sawa na mita za mraba 333. Mita za mraba 333 ni sawa na urefu,(makadirio) mita 18 na upana mita 18 au urefu mita 20 na upana mita kama 16 hivi.

SOMA: Kilichokuwa nyuma ya pazia, ufugaji wa kuku wa kienyeji(kuku wa asili)

Screenshot ya majibu hayo nihii hapa;

banda la kuku linatakiwa kuwa gharama kubwa sana?


2. Majibu ya swali kwa mdau wa pili 2

Mabanda si lazima yawe ya hali ya juu sana, cha kuzingatia kwanza ni vipimo, saizi ya banda inayoendana na idadi ya kuku unaotaka kuwafuga na kingine ni uimara wa banda wa kuwakinga na hatari zozote zile kama vile wanyama hatari, baridi, jua, upepo na mvua.

SOMA: Shilingi milioni 5 itatosha kufuga kuku wangapi wa mayai? Naomba mchanganuo

Unaweza kujenga kwa kumtumia fundi yeyote mtaani kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi kwenye mazingira uliyopo.

Screenshot ya jibu hilo ni hii hapa chini;

Banda la kuku unaweza kumtumia fundi yeyote mtaani na vifaa vinavyopatikana kwa urahisi


Majibu kwa ujumla ya jinsi ya kujenga banda la kuku linalofaa kufugia kuku: ujenzi, vipimo, ramani na picha ya mabanda

Ukitazama katika majibu yote mawili kwa wadau hapo juu utagundua kwamba kitu cha msingi sana kabla hujajenga banda lako la kuku ni idadi ya kuku unaotaka kufuga pamoja na saizi ya banda. Ni lazima kwanza ujue katika eneo la ukubwa fulani wanatakiwa kukaa kuku wangapi. Kwa kifupi unatakiwa kujua kuku mmoja anatakiwa aishi kwenye eneo la ukubwa gani.

Sasa kitaalamu kabisa ni kwamba kuku wa umri/aina tofauti watahitaji pia eneo la ukubwa tofauti, mathalani  banda la vifaranga 100 haliwezi kuwa sawa na banda la kuku wa mayai 100. Halikadhalika pia banda la kuku wa kienyeji 20 haliwezi kulingana na banda la kuku wa kisasa 20 walio na umri huohuo sawa na wenzao wa kienyeji. Hivyohivyo banda la kuku wa nyama 200 haliwezi likawa sawa na banda la kuku chotara 20 ingawa idadi na umri vinaweza kuwa ni vilevile.

Lakini kwa ujumla ni kwamba mabanda ya kuku wakubwa kitaalamu wawe ni kuku wa kisasa, wa kienyeji au wa mayai, katika mita moja ya mraba wanatakiwa kuishi wastani wa kuku 6 mpaka 10. Hii inamaana kwamba kwa kuku wa kienyeji watahitaji eneo la nafasi kubwa zaidi kushinda wale kuku wa kisasa. 

Hivyo katika wastani huo, ule wa chini kabisa kuku 6 ndio utakaofaa zaidi kwa kuku wa kienyeji na ule wa juu zaidi kuku 10 utafaa zaidi kwa kuku wa kisasa wawe wa nyama au hata wa mayai. Na kwa upande wa kuku chotara basi unaweza ukawaweka hapo katikati labda tuseme kuku 7 au 8 katika mita ya mraba moja .Mita ya mraba 1 hapa namaanisha (Mita moja urefu x Mita moja Upana).

SOMA: Chakula cha kuku wa kienyeji kina tofauti yeyote na kile cha kuku wa kisasa?

Kwa upande wa kuku wadogo vifaranga unaweza ukapunguza vipimo hivyo banda la ukubwa wa mita moja mraba likawa na vifaranga hata zaidi ya 15 hamna shida ingawa pia kuna vipimo vyake maalumu.

SASA NI VIPI UTAJUA UKUBWA WA BANDA KULINGANA NA IDADI YA KUKU UNAOTAKA KUFUGA?

Njia nyepesi zaidi na rahisi ya kukuwezesha kujua idadi ya kuku wako itahitaji eneo la ukubwa wa mita ngapi za mraba ni hii ifuatayo;
Kwanza weka msimamo unataka kuku wako wabanane au wawe huru kiasi gani. Ukitaka wawe huru sana tuseme kama kuku wa kienyeji basi wewe weka idadi ya kuku wako kwenye mita moja ya mraba kuwa 6 au hata 5 ukitaka. Kisha sema hivi; 

Ikiwa kuku 6 = Mita 1 ya mraba, Je kuku(…………) (taja idadi ya kuku wako hapo) watahitaji mita ngapi za mraba? Kisha chukua idadi ya kuku wako gawa kwa 6 na jibu ndio mita za mraba unazohitaji.

MFANO: BANDA LA KUKU WA KIENYEJI 100 LIWE NA UKUBWA WA MITA NGAPI ZA MRABA?

Kuku 6      =   Mita ya mraba 1
Kuku 100  =   Mita ? za mraba?

Chukua kuku 100 /6  = 16.6
Kwahiyo kuku 100 watahitaji mita za mraba 16.6 ambazo ni sawa na wastani wa Mita 4 upana na Mita 4 Urefu au Mita 8 urefu na mita 2 upana.

Unaweza ukaamua kutafuta ukubwa wowote ule wa eneo linalohitajika kulingana na idadi yako ya kuku unaotaka kufuga.

SOMA: Hydroponic fodder: jinsi ya kuotesha majani ya mifugo katika trei za aluminium na plastiki bila udongo

Ikiwa unataka pengine kufuga kuku wa kisasa wa nyama punguza ukubwa wa banda na ufanye angalau kuku 10 wakae kwenye mita moja ya mraba hivyo kwa kuku 100 wa kisasa watahitaji banda la ukubwa wa; 100/10 = mita za mraba 10 au (Upana mita 2 x Urefu mita 5) nk.

JINSI YA KUJENGA BANDA LA KISASA LA KUKU
Hakuna kanuni/formula maalumu inayotakiwa kufuatwa ili mtu aweze kutengeneza banda la kuku iwe ni banda la kuku wa kienyeji, banda la kuku wa nyama, banda la kuku wa mayai, banda la kuku wa kisasa, banda la kuku chotara banda la vifaranga au hata banda la bata na ndege wengineo wafugwao, ila kitu kikubwa tu cha kuzingatia hapa ni uimara wa banda kuhakikisha kuku wanakuwa salama wasidhurike na hatari zozote wala hali mbaya ya hewa lakini pia wapate eneo la kutosha la kucheza, kula na kulala.

Materials za kujengea mabanda ya kuku yaweza kuwa ni kitu chochote kile kinachofaa kujengea mfano kuna mabanda ya kuku ya mbao na misumari, mabanda ya kuku ya udongo(tofali za udongo au za sementi), banda la kuku la mabanzi na hata mabanda ya kuku ya nyavu na miti au mbao.  Kuna watu wengine hufikiri banda la kuku la ghorofa ndio zuri na la kisasa zaidi lakini wala siyo lazima liwe ni banda la ghorofa, banda la kuku la gharama nafuu tu linatosha kabisa endapo litakidhi sifa zote zile zilizotajwa pale juu bila kusahau bembea wajirushe hapo usiku wakati wa kwenda kulala.

RAMANI YA BANDA LA KUKU LA KISASA
Watu wengine hufikiria labda kuna ramani za kisasa sana za mabanda ya kuku kama zilivyokuwa ramani za kisasa na tata(complex) za majumba ya kulala au ya kuishi binadamu. Lakini ukweli ni kwamba, kwa mfugaji wa kawaida unayetaka pengine kufanya ufugaji wa kuku wa kienyeji kibiashara kama ule niliouelezea katika mchanganuo wangu maarufu wa ufugaji  bunifu wa kuku wa kienyeji, basi huna haja ya kumtafuta mkandarasi wa majengo akudizainie banda lako la kuku, wala vifaa na material za bei ghali.

SOMA: Kupata faida kwenye ufugaji wa kuku wa kienyeji au wa kisasa mfugaji mjanja hutumia mbinu hizi

Wewe cha kufanya tu ni kuhakikisha ukishapata vifaa (material) zako za bei nafuu, unamtafuta fundi au kama wewe ni mtundu kama mimi wala huna haja ya kumtafuta fundi bali wewe piga hesabu kuku wako wanahitaji ukubwa wa eneo gani kisha anza kuchimba mashimo au kuweka msingi na ujenge kitu kama ukumbi(hall). Baadae ndani ya lile hall kata vyumba unavyohitaji kulingana na aina za kuku uliokuwa nao.

Kama ni kuku wa aina moja tu basi huna haja ya kukata vyumba wala nini, wewe wawekee mahitaji yao yote ndani kulingana na idadi yao kisha wamwage huko wahangaike wenyewe. Hakikisha lakini banda lina vigezo vyote nilivyotaja, usalama, nafasi ya kutosha, hewa(madirisha ya nyavu), kuwakinga na  hali yeyote ile mbaya ya hewa pamoja na sakafu nzuri, mabembea nk.

…………………………………………

*Ufugaji wa kuku ni miradi unayoweza kuianza kwa mtaji wowote ule mdogo au mkubwa ulio nao lakini ukitaka mafanikio makubwa na ya haraka, basi huna budi kutafuta mtaji wa kutosha na uzoefu, Mafunzo kama haya ya kwenye mitandao si mabaya yanamsaidia mtu kupunguza ule muda atakaotumia kujifunza kwa vitendo ila vitendo ni lazima piga ua ili ujifunze mwenyewe changamoto na fursa zilizopo na si kuhadithiwa.

Baada ya muda wa vitendo angalao kufuga kwanza kuku wachache kwa miezi kadhaa, sasa unaweza kuwekeza muda na fedha zako nyingi kwenye miradi hii, hapo ndipo unapoweza kuona mafanikio makubwa na ya haraka ya ufugaji wa kuku, lakini vinginevyo unaweza kuishia tu kufuga kuku kwa ajili ya kitoweo/mboga au jogoo wa kuchinja Krismasi, Mwakampya na Idi, basi.

Nimeandaa michanganuo ya biashara hizi za ufugaji wa kuku kitaalamu na kiubunifu yenye kila kitu kuanzia muhtasari, changamoto mpaka makisio yote ya fedha, michanganuo hiyo ipo mitatu (3), kuku wa mayai, kuku wa nyama na kuku wa kienyeji. Kila mchanganuo bei yake nauza shilingi elfu 10 lakini nina offa ya muda mfupi kwa wale wote wanaojiunga na Group langu la Whatsapp la masomo ya kila siku ya Fedha na Michanganuo.

Kwa members wanaojiunga nawauzia kwa  sh. Elfu 10 tu michanganuo yote 3, hivyo mtu anakuwa amesevu sh. Elfu 20. Offa kama nilivyosema haitadumu muda mrefu kwani group lenyewe nalo nafasi zimebaki chache. Karibu kama utapenda nikutumie na kukuunganisha na group. Mawasiliano yangu ni; Simu/waTsap: 0765553030 au  Simu/sms: 0712202244 . Asante sana
Peter Augustino Tarimo

0 Response to "BANDA LA KUKU 100 WA KIENYEJI: VIPIMO, RAMANI, PICHA NA JINSI YA KULIJENGA KWA UBORA"

Post a Comment