UJENZI WA MABANDA YA KISASA YA SUNGURA ULIVYO RAHISI NA NAFUU KWA MFUGAJI ANAYEANZA.

Kujenga banda bora na la kisasa la kufugia sungura ndiyo kitu cha kwanza kabisa mfugaji wa sungura anayetaka kuanza kuwafuga sungura anachotakiwa kuanza nacho. Mafanikio ya biashara ya ufugaji wa sungura hutegemea kwa kiasi kikubwa mabanda au vizimba vinavyotumika kuwatunza sungura.

Banda la kutunzia sungura halihitaji kuwa la gharama kubwa sana ikiwa ndiyo kwanza unaanza lakini pamoja na hivyo linapaswa kuwa imara kwa ajili ya usalama na maisha bora kwa sungura wako. Hivyo ujenzi wa rahisi wa mabanda ya sungura yanayokidhi sifa hizo unapaswa ufanywe kwa kutumia malighafi na vifaa vinavyoweza kupatikana kwa urahisi kwenye mazingira uliyopo.

Aina za mabanda ya sungura (vizimba vya kufugia sungura)
Ujenzi wa mabanda ya sungura hauna kanuni maalumu, kikubwa tu ni sungura kupata eneo salama na la kutosha kuishi raha mustarehe, lililokuwa na hewa ya kutosha, eneo la kucheza hasahasa kuruka, kusimama wima na kujinyoosha  huku kukiwa na urahisi wakufanya usafi katika banda kwani sungura wanataka usafi, na hawatakiwi kabisa kuishi katika eneo lililokuwa chafu.

Dhana ya banda bora la kisasa ni kutimiza matakwa hayo ya nafasi ya kutosha , usalama na usafi, hivyo banda lako la sungura au nyumba ya kuishi sungura  wako unaweza ukaiijenga vyovyote vile utakavyoamua kwa kutumia malighafi na vifaa utakavyomudu kupata ilimradi tu umetimiza vigezo na masharti hayo.

Mabanda ya sungura unaweza ukayaweka katika mafungu tofauti kulingana na aina ya sakafu au pia unaweza kuyapanga kulingana na aina ya ufugaji wa ndani au wa nje.

SOMA: Soko la Sungura Tanzania linakua kwa kasi kuliko uzalishaji wenyewe wa sungura.

Mabanda yenye sakafu ya waya.
Aina hii ya mabanda, sakafu wanakokaa sungura hutengenezwa kwa waya mesh au wavu ambao huruhusu kinyesi na mkojo kupita kwa urahisi na kwenda kudondokea juu ya bati au chombo kama trei lililolala mshazari hatimaye uchafu huo hukingwa na kukusanywa kwenye vyombo maalumu kwa ajili ya kuuzwa hasa mkojo au kinyesi kutumika kama mbolea.
 
Mabanda mengine bora ya kisasa ya kufugia sungura.
Uzuri au faida kubwa ya aina hii ya mabanda ni kwamba mfugaji unapata urahisi mkubwa wakati wa kufanya usafi wa mabanda na mabanda hubakia kuwa masafi muda wote.

Ubaya wa aina hii ya ujenzi wa mabanda ya waya ni sungura kukosa raha, kwani sungura kwa asili yake  hawajaumbwa kuishi juu ya sakafu ya waya, asili yao ni kukanyaga juu ya sakafu ngumu kama ardhi na ndani ya mapango wanayopendelea kuchimba wenyewe juu ya ardhi. Unapotumia aina hii ya mabanda basi unashauriwa kutenga eneo dogo uweke sakafu ngumu kama mbao au bati kwa ajili ya sungura kupumzika au kukanyaga pasipo usumbufu.

Mabanda yenye sakafu ngumu.
Mabanda yenye sakafu ya namna hii ndiyo sungura wanayopendelea zaidi na tena sungura hufurahi zaidi endapo sakafu itakuwa ya udongo kusudi waweze kuchimba mashimo ya kujificha lakini haishauriwi kabisa kutumia udongo kwani watakupa tabu sana pindi wakizaa au wakati utakapotaka kuwashika.

Hukimbia na kuingia kwenye mapango hayo kujificha na hata wakati mwingine wanaweza wakachimba mashimo yenye urefu mkubwa wakapitiliza na kwenda kutokeza mbali na lilipokuwa banda lenyewe. Hii ni hatari pia kwani wanaweza wakapotea, kuibiwa au kuliwa na wanyama wa porini.

Ukiweka sakafu ngumu basi inabidi utumie malighafi ngumu kama sementi/zege, mbao au bati na juu unaweka matandiko ya nyasi ngumu au nyuzinyuzi za katani, maranda ya mbao hayafai sana kwani yanaweza kuharibu mapafu ya sungura.

Faida kubwa ya aina hii ya sakafu ni sungura kujisikia raha zaidi watembeapo juu yake lakini ubaya wake upo katika kuweka banda katika hali ya usafi. Wakati wa kufanya usafi bandani itakubidi uhamishe sungura wote kwenda eneo jingine ndipo uweze kufanya usafi vizuri jambo linaloongeza ugumu wa kuwashughulikia.
Banda dogo la sungura lenye sehemu ya ndani na nje.
Mabanda ya nje na ya ndani.
Kama ilivyokuwa kwa kuku sungura pia wanaweza wakafugwa ndani tu au nusu ndani nusu nje. Sungura ni wanyama wanaopenda wakati mwingine kujificha hivyo hata kama unawaweka banda la wazi la nje lakini ni lazima ndani ya banda hilo uwawekee eneo au maumbo wanayoweza wakajificha ndani yake wanapojisikia hawako salama sana. Mabanda ya ndani yanaweza yakatumika kwa ajili ya sungura kupumzika na kulala, kisha ya nje wakatumia kucheza na kula.

Ukubwa (saizi ya mabanda ya sungura)
Sungura wanahitaji kulala, kula , kunywa maji, kucheza, kujificha na kujisaidia haja kubwa na ndogo. Eneo linalopendekezwa la kizimba au banda la kufugia sungura ni mita za mraba 12au wastani wa meta za mraba 1, ina maana kwa wastani upana unatakiwa kuwa mita 1 na urefu mita 1 au futi 6 kwa 2.

Sungura anahitaji pia eneo kwa ajili ya kucheza, kwa hiyo jumla ya eneo lote lisipungue futi za mraba 40 mpaka 60. Sungura anaposimama wima anatakiwa masikio yake yasiguse juu kwenye paa hivyo urefu kutoka chini kwenye sakafu hadi juu kwenye paa unatakiwa kuwa sentimita 60 mpaka 90. Hayo ni makadirio tu ya chini, sungura wanahitaji eneo kubwa hata zaidi ya hilo ili kujinafasi kwa uhuru zaidi.

Mpenzi msomaji, kama ulikuwa hujagundua faida za kufuga sungura, hebu soma makala hii isemayo Sungura wa mbegu na wa nyama wanapatikana Mbezi Kwa Msuguri kwa bei nafuu. Ushauri wangu kwako:-  fuga sungura wana faida kubwa na hawahitaji eneo kubwa kama wanyama wengine, sungura pia wanakula vitu ‘simple’ sana kama vile, nyasi na maganda ya vyakula kama ndizi, kunde, matikiti na maboga, tena kwa kiasi kidogo tu kwa siku. Uzaaji wao ni wa haraka na watoto wengi kuanzia 6 mpaka 8 kwa wakati mmoja. Soko halina shaka unauza kuanzia manyoya, mpaka mkojo.

Unaweza kuanza hata na sungura wawili tu dume na jike na kama utapenda kuanza leo, nakushauri anza na banda kwanza walao la sungura wawili na kisha ukimaliza ndipo utafute sungura kwa ajili ya mbegu. Sungura wazuri na wanaolipa ni wale wa kisasa au chotara ambapo huwa na uzito mkubwa tofauti na sungura wa kienyeji.

0 Response to "UJENZI WA MABANDA YA KISASA YA SUNGURA ULIVYO RAHISI NA NAFUU KWA MFUGAJI ANAYEANZA."

Post a Comment