SOKO LA SUNGURA TANZANIA LINAKUA KWA KASI KULIKO UZALISHAJI WENYEWE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SOKO LA SUNGURA TANZANIA LINAKUA KWA KASI KULIKO UZALISHAJI WENYEWE

Je, ulikuwa unajiuliza siku nyingi kuwa ni mradi gani unaoweza ukaufanya na ukakulipa faida kubwa katika kipindi kifupi  kabisa na wakati huohuo gharama za mtaji pamoja na zile za kuendeshea mradi wenyewe kubakia kuwa chini kadiri inavyowezekana?. Basi sasa suluhisho limepatikana usiwe na wasiwasi tena.

Kama kawaida yetu sisi Self Help , kazi yetu ni kuumiza vichwa ili kupata majibu magumu kwa watu mbalimbali wanaohangaika kujinasua kutoka katika makucha makali ya umasikini. Safari hii baada ya kukutana na wadau mbalimbali wanaofanya kilimo cha sungura au tuseme ufugaji wa sungura, tumebaini fursa kubwa mno iliyojificha nyuma ya shughuli hii inayochukuliwa na watu wengi kama kazi ya kitoto kwa wanafunzi wa shule za msingi.


Kwa kifupi tu ni kwamba faida za kufuga mnyama sungura ni kubwa na za haraka kushinda wanyama wengine wote wakiwemo wale maarufu kama kuku, ng’ombe na  hata bata. Sababu ni kwamba, huzaliana kwa kasi ya ajabu, sungura hawana kipindi cha joto, “heat period” kama walivyo wanyama wengine, wao mimba ni muda wowote ule ilimradi tu sungura jike asiwe na mimba kipindi anapopandwa.


Sababu nyingine ni kwamba, sungura huwa hawashambuliwi na magojwa mengi na kwa urahisi kama ilivyokuwa kwa wanyama wengine. Ukidumisha usafi wa mabanda yao vizuri hutasikia hata siku moja sungura akiumwa eti sijui mafua, typhod, wala mdondo. 

Na sababu ya tatu ni kuwa chakula cha sungura upatikanaji wake ni rahisi, hula sanasana nyasi au majani  ya mimea karibu yote yanayopatikana kwenye mazingira yanayozunguka binadamu, wanakula chakula kidogo, kwa mfano ukiwa na sungura 50 inaweza ikakuchukua muda usizidi dakika 15 kuwatayarishia chakula iukiwa nyasi zimekwishatayarishwa.


Sungura unaweza ukawafuga hata ukiwa unaishi katika nyumba ya kupanga kwani hawahitaji eneo kubwa sana. Hawazalishi uchafu mwingi na ni rahisi kufanya usafi katika mabanda yao ikiwa utakuwa umejenga banda la kisasa.

Sungura Bora na wa Kisasa kwa ajili ya nyama na Mbegu.
Kwa upande wa nyama ya sungura ni nyama nzuri zaidi na inayopendekezwa na wataalamu wa afya kuwa ni nyama safi nyeupe isiyokuwa na mafuta mabaya na nzuri hasa kwa kuzuia matatizo mbalimbali ya kiafya kama shinikizo la damu, kisukari na kansa.


Soko la sungura kwa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla ni soko linalokua haraka, ila tatizo kubwa lililokuwepo ni kuibuka kwa watu na makampuni yanayotumia fursa hii kujipatia pesa kijanja kwa kuwarubununi wafugaji wadogo waanzishe ushirika ambao wao ndio watakaosimamia biashara hiyo. Watu hawa hufikia hata hatua ya kuwatoza wafugaji hao viingilio vikubwa, kuwauzia mbegu na chakula kwa bei ya juu na kuwaahidi kuja kununua mazao yao pindi yatakapokuwa tayari lakini mara nyingi huja kuingia mitini na kuwaacha wamekata tamaa bila ya kujua ni nini cha kufanya.

Lakini pamoja na changamoto hizo zote bado ufugaji huu kama watu watahamasisha vya kutosha ulaji wa nyama hii nzuri isiyokuwa na madhara kjiafya hapahapa nchini soko litakuwa kubwa tu kwani bado watu wengi pia hawana uelewa juu ya manufaa na uzuri wa nyama hii na wengine hudhani labda sungura ana makatazo kidini nk. wengine tu hawali kwa sababu hawajawahi kula. Mazao yatokanayo na sungura kama vile, manyoya ngozi na mkojo pia kuna uwezekano wa soko lake nje ya nchi hasa china na nchi za mashariki ya mbali. Inasemekana mkojo wa sungura hutumiwa kutengeneza viua-wadudu wa mazao ya kilimo.


Wachina kwa mfano ni watu wanaopenda mno kitoweo cha nyama ya sungura. Yapo mahoteli hata hapa Tanzania ambayo kama ufugaji utahamasishwa vizuri yanaweza yakawa ni soko zuri sana kwa siku za baadaye kwa ajili ya watalii na wageni wanaofika nchini wakitokea nchi za ukanda huo. Tayari kuna makampuni kadhaa Afrika Mashariki hususani Kenya na Uganda kama vile "Rabbit Republic" ambayo tayari yameshaanza kununua nyama ya sungura kutoka kwa wafugaji wadogo na kwenda kuisindika kwa ajili ya kuuza.

Kama shughuli nyingine yeyote ile, changamoto hazikosekani hasa upatikanaji wa chakula, soko na magonjwa, lakini changanoto hizi siyo kubwa sana, kwa mfano kwa upande wa chakula mfugaji anaweza akajifunza teknolojia ya kuotesha mimea bila kutumia udongo iitwayo hydroponic fodder ambayo huchukua siku 4 mpaka 6 tu kukuza majani mabichi ambayo ni chakula kizuroi sana kwa sungura na kilichokuwa na virutubisho vya kutosha.

Magojwa, sungura huwa wanapatwa na magojwa lakini ikiwa utazingatia usafi inavyotakiwa ni kwa kiwango kidogo sana hata ukilinganisha na mifugo wengine kama kuku. Watu wengi hulalamika soko, lakini kwa kweli soko la sungura ukitangaza watu wakajua unao, hawakai, watu wengi hupenda sana kuwafuga na wengine hupenda kula nyama kwa mara ya kwanza kwani watu wengi hapa Tanzania hawajawahi kuionja nyama hiyo, wanapoelimishwa juu ya faida za nyama yake hasa sifa hii ya kutokuwa na mafuta yanayoweza kusanabisha magojwa mabaya kama magonjwa ya moyo, kisukari na kansa, watu hawana kipingamizi kabisa cha kununua nyama ya sungura

Kwa hiyo ndugu msomaji kama wewe una mapenzi na ufugaji, usiogopeshwe na changamoto ndogondogo zinazoweza kukuzuia usifuge sungura. Unachohitaji ni sungura wako wa mbegu, banda la kisasa la sungura na unaweza ukaanza na idadi yeyote kutegemeana na mtaji wako. Lakini cha kukutahadharisha hapa ni kuwa ujiandae vyema kwa mabanda yakutosha kwani nijuavyo mimi uzaaji wa sungura, unaweza hata kujikuta unakuja kukosa mahali pa kuwaweka.

Mdau unasubiri nini kuanzisha ufugaji huu wenye tija kubwa na usiokuwa na gharama nyingi? Soko linakua kwa kasi, kadiri watu nao wanavyoendelea kupata uelewa juu ya faida za kula nyama nyeupe ya sungura isiyokuwa na madhara.

8 Responses to "SOKO LA SUNGURA TANZANIA LINAKUA KWA KASI KULIKO UZALISHAJI WENYEWE"

  1. Naomba mawasiliano yenu. Nimependa sana pia nahitaji kujua hiyo hydroponic fodder inakuaje?

    ReplyDelete
  2. Tutaandika makala zaidi juu yake hii, mawasiliano yetu ni 0712202244 au jifunzeujasiriamali@gmail.com

    ReplyDelete
  3. Hi,Naomba kujua namna ya kutengeneza Hydroponic Fodder please.

    ASANTE.

    ReplyDelete
    Replies
    1. https://www.jifunzeujasiriamali.co.tz/2018/09/hydroponic-fodder-jinsi-ya-kuotesha.html

      Delete
  4. Naomba kutambua soko la sungura. Mimi niko Tanga, wilaya ya mkinga. Kifupi ni mefurahi kupata elimu ya ufugaji wa sungura. Ahsanteni.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Soko la sungura kama ilivyokuwa kuku inakubidi mfugaji utafute soko mwenyewe kwa njia za kawaida za kujitangaza na kufanya promosheni na kazi hii ni lazima uianze kabla hata hujaanza kufuga na si vinginevyo. Hakuna soko la miujiza kwa bidhaa au mazao yeyote yale kama baadhi ya watu wanavyoaminisha watu.

      Delete
  5. Nahitaji solo nko na sungura nataka kuuza

    ReplyDelete
    Replies
    1. Litafute kwa kuwasiliana na watu wanaohitaji sungura kwa ajili ya kuwafuga au kwa ajili ya kitoweo, ulizia watu waliokuwa karibu nawe, vutia watu kwa kuwaelimisha faida za kula nyama nyeupe ya sungura isiyo na madhara kiafya nk. Hakuna soko la sungura lililojificha mahali mtu anaweza kukupa taarifa zake popote.

      Delete