KABLA YA KUKOPA MKOPO WA BIASHARA YAKO, PAMBANA KIUME KWANZA USIJE KUUMBUKA BURE | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KABLA YA KUKOPA MKOPO WA BIASHARA YAKO, PAMBANA KIUME KWANZA USIJE KUUMBUKA BURE

USHAURI WA KIBIASHARA:
Leo rasmi nimeanzisha kipengele cha ushauri baada ya kuwa kwa muda mrefu nikitoa ushauri mbalimbali wa kibiashara pasipo kuuweka hapa katika blogu ya jifunzeujasiriamali, ingawa nakumbuka siku za nyuma kabisa nilipoanzisha tovuti ya jifunzeujasiriamali.com nilichapisha katika tovuti hiyo ushauri wangu kwa dada mmoja aitwaye Katarina juu ya biashara ya utengenezajiwa sabuni, shampoo, batiki na unga wa lishe. Bonyeza maandishi hayo kuusoma ushauri huo.

Ushauri ule kwa Katarina ulitokea kuwa maarufu sana na uliowafungua masikio wajasiriamali wengi kuwa, ujuzi wa kutengeneza bidhaa peke yake tu hautoshi kusimamisha biashara iliyokuwa imara. Mtu atahitaji pia na maarifa ya biashara kama mbinu za kutafuta masoko nk. ndipo biashara yake iweze kufanikiwa.

Nilifurahi ushauri ule kwa Katarina hata ulisaidia wadau mbalimbali wakiwemo hata na watoa semina  na waalimu wa ujasiriamali wa kutengeneza bidhaa na vitu mbalimbali kwa ujumla kuanzisha sambamba na semina zao mafunzo ya msingi ya biashara kama mbinu za masoko, mitaji, uendeshaji biashara, uongozi nk.

Mfumo tutakaoutumia sasa hivi ni kama ule ule niliokuwa nikiutumia kipindi hicho nilipomshauri Katarina, yaani, mtu ananitumia swali lake kwa njia ya meseji au barua pepe, e-mail na kisha mimi swali hilo ama changamoto hiyo ninaijibu kupitia makala ndani ya blogu hii kama ilivyokuwa makala hii utakayokwenda kuisoma  hivi punde. Siyo lazima jina lako tulitaje kwenye makala labda uturuhusu mwenyewe, tunaweza pia kutaja jina kwa ufupisho tu ama jina moja.

Tukija moja kwa moja kwenye swali la leo, linatoka kwa msomaji wa jifunzeujasiriamali mkoani Arusha, Bw. R. S Seibul anayeuliza hivi;

 “Mimi ni mfugaji, lakini miezi mitatu iliyopita nimeanzisha biashara ya kuuza vifaa vya ujenzi wa nyumba ambayo naona mtaji wake ni kidogo mno siwezi kuweka vifaa vyote vinavyohitajika na wateja. Sasa swali langu ni kwamba, naweza kwenda kukopa benki ipi iliyokuwa na masharti na riba nafuu kuliko zingine, hapa Arusha kuna mabenki mengi kama,(anataja majina ya baadhi ya mabenki), tafadhali nishauri niende benki ipi isiyokuwa na makato mengi.”

Majibu.
Ndugu yangu Seibul, kwanza nikupongeze kwa kuamua kuongeza Mifereji yako ya kipato baada ya kugundua kipato unachokipata kutokana na kazi ya ufugaji haitaweza kukukomboa moja kwa moja na lindi la umasikini. Wazo lako la kuongeza mtaji kwa kwenda kukopa benki ni zuri na ambalo ndiyo njia pekee ya wewe kuweza kutoka haraka kimaisha, kwa maana nyingine ni kama ‘shortcut’ au njia ya mkato ya kuufikia uhuru wako kifedha. Lakini njia hiyo ya mkato inakupasa uipite kwa umakini wa hali ya juu sana, usijeteleza halafu ukajikuta unadumbukia kwenye ‘dimbwi kubwa la tope.’

SOMA: Ukisoma hapa huwezi tena kuwalaumu Mabenki na Taasisi za fedha.

Kwanza kabla hujaanza hatua  kuelekea Benki yeyote ile, na ninaamini mabenki karibu yote yanafanana kimasharti, ni kama vile watoto wa baba mmoja ‘BENKI KUU’ wala mtu eti asije kukudanganya kuwa kuna benki ya biashara iliyokuwa na masharti nafuu na riba kushinda nyingine. Tofauti zao utakuta ni ndogondogo sana na wala haziwezi zikamsaidia sana mkopaji anayetafuta unafuu dhidi ya benki nyingine.

Unajua ndugu Seibul, sisi wakopaji kitu ambacho tungelipenda sana tukipate kutoka mabenki na taasisi za fedha si kingine bali unafuu wa riba, masharti nafuu ya urejeshaji kwa mfano hata ikiwezekana kusogeza kidogo mbele siku za marejesho tuseme labda kama mtu kapangiwa kurejesha mwanzoni mwa mwezi basi mtu huyo angependelea arejeshe hata katikati ya mwezi bila kusumbuliwa. 

Kwa bahati mbaya kabisa vitu hivi mabenki na taasisi za fedha ndivyo vitu wanavyovichukia kushinda kitu kingine chochote kile. Isitoshe hata serikali yenyewe kupitia bunge imeweka sheria inayozuia uzembe wa namna hiyo kwa wateja wanaokwenda kukopa amana za watu zilizowekwa katika mabenki kuzuia zisipotee kirahisi.

SOMA: Siri ya Mabenki kila kona jijini unaijua?

Kwa mantiki hiyo basi ili mtu uweze kuwa rafiki mzuri wa benki inakupasa kuzingatia mambo hayo hasahasa urejeshaji kwa wakati na usio suasua. Ina maana kwamba kama ni biashara unakwenda kuikopea pesa, basi uhakikishe kwanza biashara  hiyo inao uhakika wa kuwa na wateja wa uhakika watakaoiwezesha kuzalisha fedha zitakazotosheleza kurejesha mkopo pamoja na kujiendesha yenyewe pasipo kutegemea chanzo kingine chochote kile cha pesa inapofika siku yako ya marejesho ya mkopo.

Na biashara ya namna hiyo inatakiwa iwe ni biashara ambayo imekwisha kuwa na uzoefu angalao wa kipindi kirefu kidogo, siyo miezi 3 tu.

Basi au la uwe na uhakika wewe mwenyewe kwamba ikijakutokea kuyumba kwa biashara basi unayo njia nyingine mbadala ya kupata pesa za marejesho bila kuathiri masuala mengine kama mahitaji yako na familia au biashara nyingine uliyokuwa nayo. Kulingana na ulivyonieleza bila shaka wewe unayo mifugo pengine na shamba na sina shaka yeyote kwamba kama utakwenda benki basi ni lazima watake uweke mali zako hizo kama dhamana kwanza kabla hawajakukopesha, na hili ni kwa taasisi au benki yeyote ile bila kujali sijui ina masharti nafuu au nini.

SOMA: Je Mtanzania Unakopesheka na Taasisi za fedha?

Ushauri wangu kwako Bwana Seibul ni kwamba, Pambana kwanza kiume kabla hujaamua kwenda Benki, hebu angalao fanya hiyo ‘hardware’ kwa miezi mingine 3 uone inakwendaje. Je, ina faida?, na mzunguko wake wa pesa taslimu upoje?, vitu vinachukua muda gani kumalizika tangu uvinunue? nk. Ukishajiridhisha kwamba biashara yako hiyo inao uwezo wa kurejesha kiasi cha marejesho ya mkopo unaotaka kuomba basi “RUKSA”, nenda ukachukue mkopo wako.  

Ila pia uchunge sana suala la usimamizi wa biashara pindi baada ya kuchukua mkopo wenyewe usijeajiri wajanja wakakomba mtaji wako wote na mkopo wenyewe. Kuajiri sisemi ni kubaya ila tu uwe karibu na uhakikishe unamuwekea vipimo kila baada ya muda fulani ufanye tathmini ya mali na mtaji wako.

SOMA: Kufanya biashara na mtaji wa kubabaisha ni sawa na kulima kwa jembe lisilokuwa na mpini.

Usiombe kuja kufilisiwa na benki, ni kitu kinachouma sana lakini pia kwa upande mwingine mkopo ni nyenzo muhimu mno katika kufanikisha biashara yeyote ile kama makala hii hapa ya “Siri matajiri wasiyopenda kuitoa inavyosema. Dhana ya kupambana kiume itakusaidia kwanza kuzijua changamoto zote zinazohusiana na biashara ya uuzaji wa vifaa vya ujenzi ikiwa ni pamoja na kiasi cha pesa zinazohitajika ili utakapokopa basi usije ukayumba kimaamuzi.

Utakuwa umekwisha komaa na changamoto zote za kuendesha biashara hiyo ukiwa na mtaji kidogo hivyo hautakuja kuthubutu kuchezea fedha utakazokopa benki. Kwa kupambana kiume kwanza kabla ya kwenda kuomba kupigwa ‘tafu’ na benki au taasisi yeyote ile ya fedha kutakuepusha na kuja kuumbuka bure ikiwa mambo yatakuja kwenda ndivyo sivyo.

Kuhusiana na ni Benki ipi uende ukakope, mimi sioni kama ni ‘ishu’ sana, kwani karibu mabenki yote yana masharti na vigezo vinavyofanana, ila utakapofika muda wa kwenda kukopa wewe mwenyewe unaweza ukaamua kufanya utafiti kwa kwenda katika mabenki kadhaa ukawauliza na kisha baadaye ukaoanisha vigezo na masharti yao halafu unaweza kuona ni benki ipi inakuvutia zaidi ya nyingine.

Je, una swali lolote kuhusiana na biashara ambalo ungependa kupata ufafanuzi hapa kwenye blogu ya jifunzeujasiriamali wakati huo huo ufumbuzi huo ukiwasaidia na wadau wengine?. Basi usisite kututumia changamoto yako hiyo, tutakutafutia majibu kwa kina na siyo lazima kuchapisha jina lako kamili, waweza kutumia vifupisho au jina moja tu ukipenda.

Tuma kupitia E-mail:                    jifunzeujasiriamali@gmail.com

Au meseji kupitia namba: 
0712 202244 au 0765 553030

Pia nachukua nafasi hii kuwajulisha wale wote wanaohitaji vitabu kutoka kwetu kwamba vitabu vyote 'Hard copy' au vya karatasi sasa vipo vimeshakamilika, kwa wale waliokuwa wameweka oda na ambao watapenda kuagiza ni wakati sasa wa kufanya hivyo.

Kwa wateja wa Dar es salaam unaweza kuagiza uletewe mpaka pale ulipo. 

Vitabu vyetu,

"MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI", "MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA" pamoja na "SIRI YA MAFANIKIO BIASHARA YA REJAREJA"

Ni vitabu kamwe visivyopitwa na wakati(Books of all times) Vimebeba maudhui ambayo popote pale Duniani hata uende Ulaya, Marekani, Asia na Australia yatafanya kazi ile ile ambayo yatafanya hapa Tanzania. Jitahidi walao kupata nakala moja kati ya vitabu hivi.

Bei ya vitabu vya karatasi(hardcopy) kwa Michanganuo ya Biashara na Ujasiriamali... ni Sh. 20,000/=, Mifereji 7 ya Pesa .....ni Sh.4,000/= na Siri ya Mafanikio ya Biashara ya Rejareja...ni Sh. 10,000/=  

Kwa wateja wetu walioko Mikoani tunawatumia vitabu kupitia mabasi yaendayo mikoani(mkoa wowote ule) ila bei ya kitabu panaongezeka gharama kidogo za kutuma kitabu ambapo kwa mikoa ya mbali mara nyingi hufika mpaka Sh. 10,000/= kwa kifurushi kimoja na Sh. 5,000/= kwa mikoa iliyokuwa karibu mfano Morogoro.

Wewe ulieko Mkoani huna haja ya kuwa na wasiwasi wa kupotea kwa kitabu, kwani uzoefu wetu unaonyesha hakuna kabisa uwezekano kama huo. Hata hivyo Self Help Books tunabeba dhamana yote tunapomuuzia mteja kitabu. Tunahakikisha mteja kitabu kimemfikia vinginevyo basi pesa yake inarudishwa na ni kitu ambacho bado hakijawahi kutokea katika mamia ya vitabu tulivyokwishawahi kutuma mikoa mbalimbali.

0 Response to "KABLA YA KUKOPA MKOPO WA BIASHARA YAKO, PAMBANA KIUME KWANZA USIJE KUUMBUKA BURE"

Post a Comment