BENKI KARIBU KILA KONA YA JIJI LA DAR ES SALAAM, SIRI YAKE UNAIFAHAMU? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BENKI KARIBU KILA KONA YA JIJI LA DAR ES SALAAM, SIRI YAKE UNAIFAHAMU?

Siku hizi sina kawaida ya kwenda kati kati ya jiji la Dar es salaam kama zamani, na sababu kubwa ni kwamba huwa sina kinachonipeleka huko mara kwa mara. Hutokea mara moja moja labda ninapokuwa na wateja wanaohitaji niwapelekee vitabu kama siku ya jana nilipokwenda katika majengo pacha ya Benki kuu ya Tanzania, ‘BOT’ kumpelekea mteja wangu kitabu cha “Michanganuo ya Biashara na Ujasiriamali”.

Awali kwenye simu, mteja huyu aliniambia anaishi Kigamboni hivyo nikifika Feri muda wa saa 10 jioni basi nimsubiri hapo feri lakini nikiwa njiani akanipigia tena simu na kunijulisha kwamba muda huo nimkute pale nje ya majengo ya Benki kuu. Nilipofika pale ilikuwa yapata kama saa 11 jioni hivi, nikapiga namba yake na akanijibu tayari keshaniona nisogee karibu na geti la benki. Kabla sijavuka barabara yeye alikuwa ndani ya geti mle Benki, akatoka haraka akavuka barabara na kuja upande wa pili nilipokuwa nimesimama mimi mkabala na lango la kuingia BOT.


Alikuwa ni kijana mchangamfu sana, baada ya kusalimiana nikampa kitabu na kisha kumuonyesha vitabu vingine, viwili, kile cha “Mifereji 7 ya Pesa” na “Siri ya mafanikio ya biashara ya Rejareja”. Alivipenda na vyote akavinunua kwa pamoja.Nilimuona ni kijana mwenye hamasa ya hali ya juu sana ya mafanikio. Na japo sikuhangaika kumuuliza ikiwa pale Benki kuu anafanya kazi gani, lakini nilifahamu fika kwamba, Benki Kuu hamna kazi ndogo hata kidogo. 

Nilimsihi sana juu ya kuwekeza katika miradi mbalimbali bila kujali ukubwa wake hasa kipindi hiki akiwa katika kazi ya ajira, “Hakuna tena wakati mzuri zaidi wa kuweza kupata mtaji wa kuanzisha biashara kama huu, ambapo umeajiriwa unapata mshahara kila mwezi” Nilimsihi, yeye akawa tu anacheka na kufurahi. “Bwana Peter nimefurahi sana kufahamiana na wewe, nitakupa e-mail yangu uwe unanitumia vitu unavyoandika mara kwa mara” kijana alimalizia, tukaagana na yeye akavuka barabara akikimbia kuelekea kule liliko geti la BOT ambako kuna mwenzake alikuwa akimuita.

Taratibu nilijiondoa hapo majengo pacha ya Benki kuu nikielekea maeneo ya Kanisa la Azania Front ili nikapande usafiri utakaonifikisha kwangu Mbezi. Tayari kigiza kama vile kilikuwa kinaanza kuingia hivi lakini hata hivyo nadhani ilikuwa bado, ni kutokana tu na mawingu yaliyokuwa yametanda angani, kwani hata saa 12 na nusu ilikuwa haijafika vizuri.

Nikiwa nashangaa shangaa hapo maeneo, nje kidogo ya Hoteli ya New Africa (Casino), nikijiuliza, nikapande basi gani, daladala za kawaida au Mwendokasi, ikanichukua takriban dakika 10 hivi bila uamuzi, Mwishowe niliamua nisogee mpaka hapo Posta mpya nikaangalie daladala za kawaida zinazokwenda mbezi. Kila daladala linalokuja ni Temeke, Mwenge na Mmbagala, punde kidogo likaja la Kimara Suka, niaona ‘isiwe tabu, ngoja nijitose ndani kitaenda kueleweka tu huko mbele ya safari’. Niliamua nipande la Kimara Suka ili nikaunganishe jingine la mbezi. Kama kawaida tuliingia garini kwa msukumano mkubwa mpaka shati nililokuwa nimevaa likachafuka, hata sijui ni kitu gani nikajua pengine huenda mlangoni palikuwa na grisi au kuna mtu alishika chombo kichafu kama ndoo ya samaki.


Daladala imekwisha ondoka sasa tukawa tupo mtaani kuelekea maeneo ya Mnazi mmoja, hapa katikati karibu na jengo la TTCL, vijana wanne niliokuwa nimeketi nao siti ya nyuma wakawa wanazungumza kilugha cha kwao mchanganyiko na kiswahili, Kwa haraka haraka mtu ungegundua vijana wale ni wa kutoka kanda ya ziwa na baadhi yao walikuwa wageni hapa jijini, kutokana na mmoja kati yao kuwa alikuwa akiongea kwa simu akimjulisha aliyekuwa wakiongea kuwa yeye kaja Dar kumuuguza ndugu yao hospitali ya Muhimbili.

Mmoja wa vijana hao aliwauliza wenzake, “Mbona huku Dar es salaam kila baada ya nyumba chache utakuta jengo la benki?” Mwingine alijibu, “Siku hizi biashara ya mabenki mijini imekuwa dili sana, siyo kama zamani” Mwingine akadakia; “Inatokana na watu kuendelea, hakuna tena mtu anayeweka pesa kwenye vibuyu kama ilivyokuwa zamani”. Japo sikuchangia chochote lakini nilipenda mjadala ule uendelee lakini mara walibadilisha mada ile wakaendelea ‘kuchapa kilugha cha kwao’. Sikuelewa wanazungumza nini japo nilisikia wakitajatajaneno ‘milioni’ mara kadhaa.


Gari ilikuwa inafika Magomeni Mapipa sasa, wale vijana wakashuka, mle kwenye basi likabakia zogo kubwa, kina dada fulani waliokuwa wameketi mbele yetu wakawa wanawasema wale vijana kwa kutaja kabila lao kuwa ni watu wanaopenda sana kuzungumza lugha ya kwao na popote pale wanapokuwa huwa hawapendi tabu ndiyo maana kwenye siti waliyokuwa wameketi walikuwa wakijiachia kiasi hata abiria wengine waliokuwa wamekaa nao kama mimi kupata kero.

Siti inakaa watu wanne lakini wao walilazimisha tukakaa watano na bado ukaaji wao wanataka wao wote waegemee kitini huku wewe ukijitahidi kujiinamisha mbele, na ni watu walioshiba kwelikweli. “Ukimuona kavaa jaketi, buti na soksi ndefi basi ujue ana pesa, katoka kuuza mifugo au madini, wanapenda kuficha pesa ndani ya majaketi au kwenye viatu ndani ya soksi” alielezea mmoja wa wale kinadada.

Ule mjadala mimi haukunipendeza hata kidogo, nikahisi ule ni kama ubaguzi wa kikabila vile, kitu kisichopendeza hata kidogo na tena isitoshe kama kulikuwa na mtu wa kabila lile mle kwenye gari asingelijisikia vizuri, nikamwambia yule dada, “basi jamani makabila kila moja lina kasoro zake, waacheni vijana wa watu”.

Nilifika zangu Kimara Suka nikashuka na kwenda kupanda daladala lingine lililonifikisha Mbezi kwa Msuguri.

.................................................................................................

Mpenzi Msomaji wa Blogu hii ya jifunzeujasiriamali, Ikiwa utahitaji vitabu vyetu au huduma nyingine yeyote ile kama vile ya Ushauri basi usisite kuwasiliana na sisi kwa namba za simu ya mkononi; 0712 202244, au 0765 553030 au 0689 303098 au unaweza kutumia emai, jifunzeujasiriamali@gmail.co na pia Telegram ni @petertarimo.

Vitabu vyetu vyote sasa unaweza ukavipata popote pale tanzania na nje ya Tanzania kupitia mtandao wa kisasa wa internet, email, Telegram na Watsaap. 

0 Response to "BENKI KARIBU KILA KONA YA JIJI LA DAR ES SALAAM, SIRI YAKE UNAIFAHAMU?"

Post a Comment