CHAKULA CHA KUKU WA KIENYEJI KINA TOFAUTI YEYOTE NA CHA KUKU WA KISASA? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

CHAKULA CHA KUKU WA KIENYEJI KINA TOFAUTI YEYOTE NA CHA KUKU WA KISASA?


jinsi ya kuchanganya chakula cha kuku
Katika safu yetu ya USHAURI, leo msomaji wetu kutoka Mbinga aliuliza swali lifuatalo,

Naomba kufahamu ikiwa chakula hiki cha kuku wa kisasa kama naweza kuwalisha kuku wa kienyeji bila madhara yeyote. Je ipo tofauti yeyote kwenye utengenezaji wa chakula kwa ajili ya kuku wa kisasa na wa kienyeji?

MAJIBU.
Virutubisho vinavyohitajika katika mwili wa kuku wa kisasa ndivyo hivyohivyo vinavyohitajika katika mwili wa kuku wa kienyeji, hivyo kuku wa kienyeji anapokula chakula kilichotayarishwa kwa ajili ya kuku wa kisasa hawezi akadhurika na tena iwapo utampa kwa kiasi kinachostahili ndio atakua vizuri na kunenepa kuliko hata angejitafutia mwenyewe chakula kwa kuchakura ardhini.


Tofauti kubwa iliyokuwepo kati ya ulaji wa kuku wa kienyeji na ule wa kuku wa kisasa ni kwamba kuku wa kienyeji kijenetiki ni mstahimilivu zaidi anapokosa virutubisho vya kutosha katika mwili wake kuliko kama ilivyokuwa kwa kuku wa kisasa. Pia kuku wa kienyeji anao uwezo wa kula chakula cha aina moja kwa muda mrefu, nikimaanisha chakula kilichokuwa na virutubisho vya aina moja tu, tuseme labda wanga kwa muda mrefu na asiweze kudhurika au kuonyesha dalili yeyote ya kudumaa kama ilivyo kwa kuku wa kisasa.

Kisayansi siyo kuku tu peke yao, hata viumbe wengine hususani wanyama, ndege, samaki na hata wadudu, wanahitaji virutubisho(viini-lishe) muhimu vikuu vitano kusudi waweze kuishi na kukua vyema. Virutubisho hivyo ni; Wanga, Protini, Mafuta, Vitamini na madini pamoja na maji. Kwahiyo kuku awe ni wa kienyeji au wa kisasa anahitaji kupata makundi yote haya matano ya viinilishe ili aweze kuishi na kukua vizuri kama inavyostahili.


Suala la chakula kwa ajili ya kuku vifaranga(starter), kuku wanaokua(growers), kuku wa nyama(broiler mash) na kuku watagaji(layers mash) na hata finishers hili huzingatia zaidi mahitaji maalumu ya kundi husika kulingana na umri wake. Kwa mfano vifaranga starter mash, mchanganyiko wake wa viinilishe protini huzingatiwa zaidi na kwa kiwango kikubwa kutokana na vifaranga miili yao kuhitaji protini zaidi kwa ajili ya ukuaji wa haraka.

Ni hivyo hivyo na kwa kuku wa mayai wanaotaga, chakula chao ratio yake inatakiwa vitamin na madini kupewa kipaumbele kikubwa hasa madini ya chokaa kutokana na mahitaji ya utengenezaji wa kaka la yai kuhitaji kwa wingi vitu hivyo. Lakini yote kwa yote chakula kwa ajili ya kuku wa aina yeyote ile wawe ni wa kienyeji, wa kisasa, vifaranga au wa mayai ni lazima katika mchanganyiko wa chakula chake makundi yote matano ya vyakula yawemo.


Kwa mfano
1.  Wanga hupatikana kutokana na vyakula kama vile mahindi, mchele, mtama, mihogo, viazi, magimbi, viazi vikuu, ngano, uwele, nk.

2.  Protini hutokana na vyakula vyote vya asili ya nyama kama mabaki ya nyama, ngozi na damu. Vyakula vyote vyenye asili ya baharini kama dagaa, mabaki ya samaki nk. Wadudu kama mchwa, funza, senene na kumbikumbi, Vyakula vyote vya jamii ya mikundekunde kama soya, kunde, maharage mbaazi na choroko.

3.  Mafuta ni vyakula kama vile, mashudu ya alizeti, mashudu ya ufuta, karanga, nyonyo, machicha ya nazi nk. Hata hivyo kuna vyakula vingine utakuta vina mafuta na wanga kwa wakati mmoja au mafuta  na protini.

4.  Vitamini na madini, utakuta vyakula kama vile, chokaa, chumvi, mbogamboga na matunda ya aina mbalimbali.

5.  Maji ya kutosha pia ni muhimu sana kwa kuku wa aina zote wawe ni wa kisasa au wa kienyeji.

Kuku kwa asili hujitafutia chakula mwenyewe kwa kuchakura chini na kula mimea mbalimbali ambapo anapata makundi yote ya virutubisho vinavyotakiwa mwenyewe. Sayansi ya kutengeneza chakula cha kuku kisasa ilitokana na binadamu kuanza kuwafuga kuku kwa kuwafungia ndani ya mabanda.


Fomula ya mchanganyiko wa makundi ya vyakula mbalimbali huchukua nafasi ile ya kuku kujichagulia mwenyewe chakula. Kuku anapochakura anajua kwa usahihi kabisa(automatic) ale kiasi gani cha wanga, protini na madini bila hata ya kupangiwa na mtu yeyote kutokana na jinsi vile mwili wake anavyojisikia ukihitaji virutubisho hivyo.

Lakini hata ikiwa kuku atakosa virutubisho sahihi inavyostahili yeye atakula tu chochote anachokipata ilimradi ameshiba hata ikiwa ni chakula cha aina moja tu. Kwa kuku wa kienyeji unaweza usione madhara yake mara moja lakini kwa kuku wa kisasa wataonyesha kudumaa haraka sana.

Asante sana msomaji wa blogu yetu kutoka Mbinga Mkoani Ruvuma, naamini swali lako nimejitahidi kulijibu.

Ikiwa una swali au changamoto yeyote ya ujasiriamali unaweza kuituma  hapa tukakushauri, ushauri mdogomdogo ni bure hatuchaji chochote na tunapoamua kuuweka hapa katika blogu hatutaji jina la mtu aliyeomba ushauri labda kwa ridhaa yake mwenyewe.

……………………………………………………….

Ndugu msomaji wangu, ikiwa ulikuwa bado hujasoma mchaganuo wetu bunifu wa kuku wa kienyeji, tafadhali nakusihi sana siyo wa kukosa kwani utaweza kufahamu mbinu nyingi sana unazoweza ukazitumia katika kuongeza idadi ya mayai ya kuku wa kienyeji kutoka idadi ya kawaida ya mayai 45-60 kwa mwaka hadi mayai 200 kwa mwaka, pia utapata mbinu za kumfanya kuku wa kienyeji akue haraka pamoja na teknolojia rahisi sana na nzuri ya kuchanganya chakula cha kuku hata ikiwa huna fedha za kununulia mashine ya gharama kubwa.

Mchanganuo huo unapatikana ndani ya kifurushi cha michanganuo 3, kiitwacho, MKOMBOZI CHICKS PLAN 3PACKS ambacho bei yake(softcopy) ni shilingi elfu 10 tu. Ndani kuna michanganuo mingine 2 ya kuku wa kisasa wa mayai na kuku wa nyama.

Ukinunua kifurushi hiki tunakupatia offa ya kitabu chetu maarufu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI(softcopy), masomo, semina zote zilizopita pamoja na kuunganishwa katika GROUP la masomo ya kila siku la MICHANGANUO-ONLINE

SIMU:            0712202244
WHATSAPP: 0765553030  

1 Response to "CHAKULA CHA KUKU WA KIENYEJI KINA TOFAUTI YEYOTE NA CHA KUKU WA KISASA?"

  1. Nashukuru sana kwa huduma yako nzuri ya uelimishaji.
    Naomba unisaidie jambo moja .kwamba ni chanjo gani ambayo kuku wa nyama au bloilers huwaga wanachanjwa ili wasipatwe na mlipuko wa magonjwa

    ReplyDelete