MUONGOZO KAMILI WA JINSI YA KUFUGA KUKU WA NYAMA (BROILERS) KITAALAMU - SEMINA SIKU-3 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MUONGOZO KAMILI WA JINSI YA KUFUGA KUKU WA NYAMA (BROILERS) KITAALAMU - SEMINA SIKU-3

kuku wakubwa wa nyama wiki 4 - 8

Ili uweze kuandika vizuri mchanganuo wa biashara ya ufugaji wa kuku wa nyama kwa ajili ya kuombea mkopo benki ama taasisi yeyote nyingine ile ya fedha, huna budi kufanya utafiti wa kina kuhusiana na biashara nzima ya broilers. 

Kufahamu muongozo kamili wa jinsi ya kufuga kuku wa nyama nayo ni sehemu ya utafiti huo kwani kutakuwezesha kujua vipimo mbalimbali, bei na hata gharama utakazohitaji kwa ajili ya kutekeleza mradi wako kwa mafanikio makubwa na hivyo kurahisisha kazi ya kuandika mpango wenyewe.

Kabla hatujakwenda kuandika mchanganuo wetu wa kuku wa nyama hebu kwanza tuone muongozo wenyewe upoje;

 

BANDA / MALAZI YA KUKU

Katika ufugaji wa kuku aina zote iwe ni kuku wa nyama, kuku wa mayai, kuku chotara au kuku wa kienyeji, banda/nyumba kwa ajili ya kuwahifadhi kuku ndiyo kitu muhimu zaidi kitakachoamua ufugaji wako ufanikiwe ama usifanikiwe. Kuku wanahitaji nyumba au banda bora kwa ajili ya kuwakinga na hali yeyote ile inayoweza kuwafanya washindwe kukua vizuri au kudhurika kwa namna yeyote ile.

Inaweza kuwa ni hali ya hewa ya joto, baridi, upepo, mvua, jua kali, unyevunyevu nk. Pia banda husaidia kuwakinga kuku na hatari mbalimbali mfano wezi, wadudu na wanyama wabaya kama nyoka, mapaka, vicheche, kunguru na mbwa. Banda la kuku linatakiwa liwe na uwezo wa kudumisha hali ya hewa inayohitajika pasipo kutegemea hali ya hewa ya nje ya banda.

Kuna mifumo mikuu mitatu ya ufugaji wa kuku na  hii ndiyo inayoamua banda lako la kuku liwe la namna gani;

1.  Mfumo huria ambao kuku wanajitafutia chakula wenyewe hasa kuku wa kienyeji na huhitaji banda kwa ajili ya kulala usiki tu

2.  Mfumo wa Nusu huria – huu kuku wanafungiwa ndani lakini wanajengewa uzio eneo wanaloweza kuzunguka na kula

3.  Mfumo wa ndani:- Kuku hasa wa kisasa kama broiler na layers hufungiwa ndani moja kwa moja na sakafu hufunikwa kwa matandiko/matandazio au katika cages

 

Vipimo vya banda kwa ajili ya kuku 2000 wa nyama (broiler)

Kitaalamu kuku mmoja wa nyama katika mfumo wa kufugia ndani anahitaji nafasi ya futi moja ya mraba ambayo ni karibu sawa na upana wa rula moja ya sentimita 30 x urefu wa sentimita 30. Kwa vipimo hivyo maana yake ni kwamba mita moja ya mraba(mita 1 x mita 1) inakadiriwa kutosha kuku wa nyama 10. Wengine huweka mpaka kuku wa nyama 12 katika eneo la mita moja ya mraba. Hivyo utaona kwa idadi yetu ya kuku 2000 tutahitaji banda lenye ukubwa wa mita za mraba 200 sawa na upana mita 20 x urefu mita 10. Urefu kwenda juu ni futi saba sawa na mita 2

Unapoanzisha ufugaji wa kuku una machaguo mawili, la kwanza uamue kujenga banda mwenyewe au ukodishe  mabanda yaliyokwisha jengwa tayari.

Banda la kuku wa nyama linatakiwa liwe vipi?

·       Madirisha ya kutosha kuingiza hewa pamoja na mapazia kwa ajili ya kuzuia upepo na baridi nyakati za usiku au hali mbaya ya hewa.

·       Lijengwe urefu wa banda uanzie Mashariki kwenda Magharibi kwa ajili ya kuwakinga kuku na jua kali

·       Banda liwe imara

·       Sakafu ya banda la kuku iwe tambarare na inaweza kuwa ya saruji, udongo au mbao

Sehemu ya kulelea vifaranga (Brooder) / Kiota

Kuku wa nyama wa siku moja mpaka waote manyoya wanatakiwa wakae katika mazingira ya joto lisilobadilika badilika na pia sehemu isiyokuwa na upepo mkali kwani wanaweza kufa. Wanahitaji kiota ambacho ni mduara unaotengenezwa kwa kutumia karatasi gumu, boksi au material yeyote ya mbao pamoja na wavu wenye matundu madogomadogo. Mduara unasaidia vifaranga wasibanane kwenye kona wala wasiende mbali na chanzo cha joto, unaweza kuuongeza kadiri wanavyokua

Kiota kinaweza kuondolewa baada ya wiki moja mpaka mbili pale kuku wanapokuwa wameshaota manyoya na kujitegemea kwa joto la kawaida.

Ikiwa banda ni dogo na hali ya hewa siyo mbaya unaweza tu kuweka vyanzo vya joto vya kutosha bandani na vifaranga wakaendelea kulelewa humo bila ya kuweka viota tangu siku ya kwanza mpaka siku ya mwisho kuku wanauzwa au kuchinjwa.

Kiota kwa ajili ya kulelea kuku wa nyama kiweje?

Chanzo cha joto: chanzo cha joto hakina mjadala kwa vifaranga wa kuku wa nyama kwani ndiyo mbadala wa mama yao ikiwa wangelikuzwa kwa njia ya asili ya kuatamia mayai. Chanzo cha joto kinaweza kikawa ni balbu maalumu ya umeme iliyo na watts 100 au 250, Jiko la mkaa au Taa ya chemli.

Kama unatumia balbu ya umeme itundikwe juu kwa waya  sentimita 35 kutoka sakafu ya banda na inaweza ikapandishwa juu au kushushwa chini kutegemeana na hali ya joto ilivyo. Balbu ikingwe isiguse vifaranga au vitu vinavyoweza kushika moto kwa urahisi kama matandazo.

Ikiwa utatumia jiko la mkaa au taa ya chemli basi iwekwe juu ya tofali futi moja juu vifaranga wasifikie na hakikisha mkaa hautoi moshi au taa haivujishi mafuta. Chanzo cha joto kiwashwe saa 1 mpaka 3 kabla vifaranga havijaletwa.

Joto ndani ya kiota siku ya kwanza linatakiwa kuwa nyuzi 35 za sentigred ( nyuzi 95 F) na linatakiwa kupunguzwa nyuzi 2 za sentigredi(nyuzi 5 F) kila baada ya wiki moja. Tumia kipima joto na ikiwa hauna basi tazama tabia na mwenendo wa vifaranga kwenye kiota. Wakikusanyika sehemu moja karibu na chanzo cha joto ni dalili  joto ni kidogo hivyo ongeza nguvu ya joto kama ni taa ishushe chini kidogo nk.

Joto likiwa kali watakaa mbali na chanzo cha joto huku wakitanua mabawa yao na kuhema harakaharaka. Punguza joto kwa kupandisha taa juu pamoja na kuwapa maji mengi ya kunywa.

Sakafu/Matandazo: Kwa siku ya 1 – 2 magazeti, gunia au mifuko laini hutandikwa juu ya matandazo, isizidi siku 2 kwani miguu ya kuku wa nyama  hutanuka na wanaweza kupata ulemavu hatimaye kutembea kwa shida.

Matandazo  yanatakiwa kuwa na kina cha inchi 3 – 4 kwa ajili ya kunyonya unyevunyevu wa mbolea na kuongeza joto kwa vifaranga lakini yasiwe na chembechembe ndogo sana au vumbi jembamba kwani vifaranga wanaweza wakafikiria ni chakula na kuanza kula makapi.

Kiota kimoja kinaweza kuwa na kuku kuanzia 100 mpaka 250 kulingana na ukubwa au aina ya chanzo cha joto, vifaranga wanatakiwa wawekewe vyombo vya maji na chakula watakavyoweza kutumia kwa urahis mfano kwa chakula unaweza ukatumia mifuniko ya maboksi, matrei ya mayai au trei ndogondogo za aluminium/plastiki mpaka watakapoweza kulia kwenye vilishio vya kawaida(feeders). Vifaranga 25 watumie chombo kimoja cha chakula na maji idadi hiyohiyo.

MAANDALIZI YA KUPOKEA VIFARANGA

Siku kadhaa kabla ya kuwasili kwa vifaranga wako wa kuku wa nyama fanya usafi unaohitajika kwenye banda zima na mazingira yote yanayozunguka eneo la ufugaji. Tumia dawa ya kuulia vimelea wa magojwa kama Dettol kupulizia maeneo hayo pamoja na kusafisha banda na vyombo vyote vya kulia chakula na maji.

Siku moja kabla ya kuwasili kwa vifaranga andaa vyema sehemu ya kulelea vifaranga/kiota (brooder). Tandaza matandazo na juu yake weka magazeti au gunia kwa ajili ili vifaranga waweze kujizoesha kutembea na kula juu yake kwa siku mbili au tatu kabla hawajaachwa watembee juu ya matandazo matupu.

Matandazo yasiwe ni chembechembe ndogo sana wala vumbi kwani yanaweza kuwasababishia vifaranga matatizo ya kupumua. Matandazo mazuri ni randa za mbao zenye ukubwa wa kati, nyasi laini na makapi ya mazao kama mpunga nk.

Washa kabisa chombo chako cha joto kiota kianze kupata joto. Andaa pia vyombo vya kulia chakula, vinyweo vya maji, vitamini na glucose.

VIFARANGA WANAPOWASILI

Vifaranga wanatakiwa waletwe kwa kutumia maboksi maalumu kutoka kwa mtotoleshaji anayeaminika na usiwaweke kwenye gari la kufunika au buti la gari wasijekukosa hewa wakafa. Mara tu wanapowasili hivi wapelekwe moja kwa moja katika sehemu maalumu ya kulelea(Brooder) na vifaranga wapewe maji safi. Ikiwa wataonekana ni wachovu basi maji yachanganywe na glucose na vitamin kuwaongezea nguvu kisha baada ya masaa 4 – 5 ndipo waweze kupewa chakula.

JINSI YA KUWATUNZA VIFARANGA WA KUKU WA NYAMA BAADA YA KUWASILI

CHAKULA:

Kwa siku ya 1 –5 huwa hawali wala kunywa maji mengi sana kwa sababu bado wanakuwa wakitumia virutubisho walivyofyonza kutoka katika ute wa yai wakati wa kuanguliwa.

Zipo aina tatu za vyakula nya kulisha kuku wa nyama  kulingana na kiasi cha virutubisho vilivyokuwepo ndani yake hasa kiasi cha protini navyo ni;

                     1.     Chakula cha kuanzia – Starter

                     2.     Chakula cha kukuzia – Grower

                     3.     Chakula cha kumalizia – Finisher

Vilevile Katika ufugaji wa kuku wa nyama unaweza ukatumia njia mbili za ulishaji wa chakula ambazo ni;

1.          Kuanza na Starter – Grower – Finisher

Katika njia hii wiki mbili za mwanzo unawalisha Starter, Wiki ya tatu Grower na wiki ya nne na kuendelea unawalisha Finisher

2.          Kuanza na Starter  – Finisher

Katika njia hii, wiki mbili za mwanzo unawalisha Starter kisha wiki ya tatu mpaka siku ya mwisho utakapowauza/kuwachinja unawalisha Finisher

Kuku wakiwa kwenye kiota siku ya kwanza mpaka ya tano wapewe chakula muda wote bila ya kupimiwa, baada ya hapo unaweza kuwapa chakula kwa ratiba maalumu mfano kuwawekea chakula kwenye vilishio kwa muda wa masaa 18 na kuondoa chakula kwa masaa 6 au masaa 16 kwa masaa 8 nk.

Wakati wa kubadilisha aina ya chakula usibadilishe ghafla bali anza kuchanganya kila aina nusu kwa nusu au robo kwa robo tatu siku mbili mpaka tano kabla hujabadilisha moja kwa moja.

Hakikisha chakula ni kile tu kilichotengenezwa kwa uwiano sahihi wa virutubisho vinavyostahili au nunua kabisa vyakula kutoka kwa watengenezaji walio na uzoefu na wanaoaminika.

Hakikisha chakula ni freshi, kisicho na unyevunyevu kwani unyevu unaweza kulea kuvu na bacteria wanaosababisha magonjwa hatari kwa kuku.

Baada ya kuku kutolewa kwenye viota wiki moja mpaka mbili watahitaji vilishio na vinyweo vikubwa zaidi ambapo kila kuku 100 watahitaji vilishio 3.

KIASI CHA CHAKULA KUKU MMOJA WA NYAMA ANAKADIRIWA KULA KILA WIKI MPAKA ANAUZWA / KUCHINJWA.

WIKI

Gramu

Wiki ya 1

175

Wiki ya 2

350

Wiki ya 3

455

Wiki ya 4

560

Wiki ya 5

770

Wiki ya 6

910

JUMLA

2240g

 

Kiasi cha chakula kuku wako watakachokula kitategemea ni muda gani utawafuga kuku, kiasi kuku watakachokula mpaka wiki ya nne ni tofauti na kiasi watakachokula mpaka wiki ya tano au sita.

MAJI:

Kuku wa nyama wanahitaji maji safi mara kwa mara. Safisha vyombo vya maji kila siku kuzuia maambukizi ya magonjwa. Weka vyombo (vinyweo) 3 vya maji kwa kila idadi ya kuku 100

 

Kiasi cha maji wanachokunywa kuku 100 kwa wiki

WIKI

Kiasi cha maji kwa kuku 100

WIKI 1

14ltr

WIKI 2

28ltr

WIKI 3

47ltr

WIKI 4

56ltr

WIKI 5

70ltr

WIKI 6

84ltr

WIKI 7

98ltr

 

Kulingana na jedwali hilo hapo juu kwa muda wa wiki 4 mpaka 4 na nusu kuku mmoja anakadiriwa kunywa maji lita 1.75 mpaka lita 2 kutegemeana na hali ya hewa itakavyokuwa. Kukiwa na joto kali kuku watakunywa maji mengi kuliko majira ya baridi na mvua.

MWANGA:

Ili kuomgezeka uzito na uotaji manyoya haraka kuku wa nyama wanatakiwa wawekewe taa usiku na mchana kwa saa zote 24 siku ya 1 mpaka 5, baada ya hapo wapewe saa moja ya giza kwa siku ili kuwazoesha giza wasije wakapatwa na msongo(stress) au kifo ikitokea kukatika kwa umeme ghafla au dharura yeyote ya kuzimika kwa chanzo cha mwanga.

VITAMINI, CHANJO NA MADAWA

·                   Siku ya 1 – 5 vifaranga wawapo kwenye viota wachanganyiwe  glucose na vitamini kwenye maji

·                   Changanya dawa ya kuzuia  mafua au Coccidiosis(Vigostat yenye Ridocox) kwa wiki nne za mwanzo. Kilo moja inatosha mfuko mzima wa chakula

·                   Endelea kuwapa Vitamini katika maji kwa siku zinazofuata hadi wiki moja kabla ya kuwauza ndipo upunguze

·                   Siku ya 7 wape vifaranga chanjo ya Kideri(New castle)

·                   Siku ya 14 wapatie chanjo ya Gumboro

·                   Siku ya 21 rudia chanjo ya Newcastle

·                   Tenga kabisa kiasi cha fedha kwa ajili ya matibabu ya dharura ikitokea kuku wakapatwa na ugonjwa wowote ule utakaohitaji daktari/mtaalamu na dawa

·                   Wapatie kuku dawa kulingana na maelekezo ya mtaalamu/daktari wa mifugo

MATANDAZO/USAFI

Epuka kulowanisha matandazo na endapo maji yatamwagika eneo fulani eneo hilo libadilishwe matandazo mengine makavu mara moja. Kila siku ondoa matandazo yalliyolowana au kugandamana kwa unyevu na kutifua  yale yaliyopo ili yanyonye unyevu vizuri. Matandazo yanaweza kubadiklishwa kwa wiki mara moja au kadiri utakavyoona inahitajika.

KUMBUKUMBU ZA BIASHARA

Kila siku hakikisha unaweka kumbukumbu sahihi za ulishaji wa kuku, kiwango cha ukuaji, madawa, idadi ya kuku wanao kufa na tarehe ya kuchanjwa kuku. Pima uzito kila wiki kwa kuchukua sampuli ya kuku wachache. Kumbuka ufugaji wa kuku ni biashara kama zilivyokuwa biashara nyingine na uwekaji mzuri wa kumbukumbu utakusaidia sana katika ulipaji wa kodi, kutathmini faida au hasara ya mradi wako na kutambua ni wapi gharama ni kubwa ili upunguze.

MUDA WA KUUZA/KUCHINJA KUKU WA NYAMA

Kuku wa nyama huwa tayari kwa kuchinjwa au kuuzwa kuanzia wiki ya 4 na kuendelea mpaka wanamalizika Kuna watu huuza kuku wa nyama kuanzia siku ya 25. Wanapokaa muda mrefu sana bandani gharama za kuwahudumia huongezeka na hivyo bei pia inabidi iongezeke kufidia hizo gharama. Kuku mmoja wa nyama katika umri kuanzia siku ya 25 mpaka ya 35 anakuwa amekula wastani wa kilo 2 za chakula

KIWANGO CHA KUFA KWA KUKU (MORTALITY RATE)

Kwa ujumla kiwango cha kufa kwa kuku wa nyama ni kati ya asiliia 5% mpaka asilimia 12%, hii ina maanisha katika kuku 100 wanaweza kufa kuku watano mpaka 12, zaidi ya hapo kutakuwa na tatizo aidha mlipuko wa ugojwa au wanyama na wadudu walao kuku.

MBOLEA:

Kwa kuku wengi mbolea inaweza kuwa nyingi sana hasa ikiwa unafugia eneo la mjini hivyo ni lazima uwe na njia ya kuihifadhi au kuiuza moja kwa moja kwa wateja watakaoihitaji kama vile wakulima wadogo wa mbogamboga. Kiroba cha kilo 50 cha mbolea ya kuku huuzwa kati ya shilingi elfu 2,000/= mpaka 2,500/=

HITIMISHO

Usije ukatarajia kuku wa nyama kujitafutia chakula wenyewe kama kuku wa kienyeji au kuku chotara wafanyavyo, hivyo kabla hujaanza kufuga kuku wa nyama(broilers) piga mahesabu kabisa ujue zitahitajika kiasi gani cha fedha za kuwahudumia mpaka umri wa kuuzwa ufike, umuhimu sawa na huo pia upo katika soko la kuku wako, tafuta soko kabla hata hujaingiza vifaranga kwenye viota. Zingatia sana vitu hivi 3;- banda bora la kuku wa nyama, ulishaji sahihi na maji safi na salama ya kutosha.

Pamoja na hayo lakini usipuuzie pia mambo yanayoonekana kuwa madogomadogo mfano, idadi ya vifaranga katika kiota, joto na mwanga, kwani vitu hivi vyaweza kuwa na athari kubwa sana katika afya ya kuku na mradi wako mzima.      

0 Response to "MUONGOZO KAMILI WA JINSI YA KUFUGA KUKU WA NYAMA (BROILERS) KITAALAMU - SEMINA SIKU-3"

Post a Comment