UJASIRIAMALI: UBUNIFU NDIYO MSINGI WAKE MKUU NA INJINI YA UCHUMI KATIKA SOKO HURIA. | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UJASIRIAMALI: UBUNIFU NDIYO MSINGI WAKE MKUU NA INJINI YA UCHUMI KATIKA SOKO HURIA.

Ujasiriamali ni nini hasa?
Katika  lugha ya Kiswahili  ujasiriamali  unamaanisha, ujasiri wa kutafuta mali. Lakini tukirudi  nyuma kidogo karne iliyopita kuangalia  maana aliyoitoa mwanauchumi raia wa Austria, “Joseph Schumpeter; Ujasiriamali  maana yake ni Uratibu na Uendeshaji wa shughuli za kibiashara  kwa Ubunifu kwa lengo la kupata Faida na utayari wa kukabilia na Hasara  yeyote itakayojitokeza.

Tofauti iliyopokuwepo kati ya biashara na Ujasiriamali
Biashara ni nini?
Biashara  ni shughuli yeyote ile  halali anayoifanya  mtu kwa lengo  la kupata faida, shughuli hiyo yaweza kuwa uuzaji  wa bidhaa, utoaji  huduma  au uzalishaji bidhaa.Ujasiliamali upo ndani ya biashara, “huwezi kuwa mjasiliamali pasipo kuwa mfanyabiashara lakini unaweza ukawa mfanyibiashara bila kuwa mjasiriamali”.
Umuhimu wa Ujasiriamali.
Kimsingi kila mwanadamu hapa duniani ni mfanyabiashara kutokana na ukweli kwamba shughuli zote azifanyazo mwanadamu zinalenga kuleta faida lakini  kati ya hao wanadamu  utakuta  wapo maskini na matajiri. Kinachosababisha  hali hiyo ni Ujasiriamali.

Kutokana na kila mtu kutamani afanikiwe zaidi ya mwenzake hali ya ushindani hutokea (hali ya kila mtu kutaka kuwafanyia wateja kitu cha ziada kitakachowanufaisha) na baadhi yao hufanya mambo ya ziada  ili kutimiza lengo hilo. Mambo hayo au jambo la ziada ni lazima  liwe gumu na ambalo  wakati  mwingine  humhitaji  mtu  kulifanya kwa bahati  na sibu pasipo kuwa na uhakika asilimia mia moja kuwa atapata faida. Hali hiyo ndiyo huitwa ujasiriamali na siyo kila mtu anaweza kufanya hivyo, ndiyo maana siyo kila mtu anayefanya biashara anaweza akaitwa mjasiriamali.

Hata kabla ya wataalumu kugundua neno ujasiriamali, ujasiriamali ulikuwepo tangu binadamu alipoanza kuishi duniani, tunaweza tukasema ni tangu zama za mawe, wakati mababu zetu walipoanza kutengeneza moto kwa kupekecha vijiti viwili huku wakiokoteza matunda, mbogamboga na mizizi porini.

Hilo limedhihirishwa na maendeleo makubwa kuanzia  zama hizo za kale za mawe mpaka leo hii zama za ‘Intanet’. Bila  shaka kuna baadhi ya Binadamu waliokuwa wajasiriamali waliosababisha mabadiliko hayo ya kiuchumi  na kijamii kutokea.

Katika kundi la watu wengi, haiwezekani wote wakawa wajasiriamali, ni lazima  wawepo wachache watakaoziona fursa za biashara na kuzitumia. Na hao ndio huitwa wajasiriamali.

Katika nchi zilizopiga hatua kubwa katika ujasiriamali, serikali zao zilihamasisha watu kupitia elimu  mashuleni na vyuoni kama njia ya watu kujijengea tabia  za kijasiriamali ili baadaye waweze kuingia katika dunia  ya ushindani. Tabia  na uwezo  wa  watu kuanzisha  miradi  inayolenga kuzalisha  bidhaa na huduma mpya ambazo hazikuwepo  awali inafaa ihimizwe.
Ubunifu  unatakiwa uwe ndiyo msingi wa ujasiriamali badala ya  mazoea  ya kuanzisha  miradi mipya  bila  ya kuongeza vitu vitakavyoboresha  zaidi bidhaa /huduma husika. Vitu hivyo vitakavyoboresha bidhaa huduma vyaweza kuwa bidhaa/huduma yenyewe, mfumo mpya wa masoko, mifumo mipya ya usambazaji, njia mpya za uzalishaji, mifumo mipya ya kitaasisi nk.

Mfano mzuri ni bidhaa na teknolojia mpya zinazoibuka kila siku na kuzifunika zile za zamani, hiyo yote ni kazi ya wajasiriamali. Teknolojia kama ya Intaneti, barua pepe (e-mail) zimechukua mahali pa barua za kawaida na simu za mezani, Player’ za santuri  zinazotumia umeme zilichukua nafasi ya ‘Gramaphones’  zilizozungushwa kwa mkono.

Radio cassettes’ zikachukua mahali pa players. CD/DVD players  zikazipiku cassettes na sasa kuna vitu kama ‘MP3’ na ‘MP4’ players, Iphones, Smart Phones  na simu za mikononi za aina kwa aina zenye uwezo mkubwa wa kupiga muziki, kuonyesha picha na kuunganishwa na Intaneti.

Ujasiriamali ni kama uhai(pumzi) inayosukuma uchumi wa soko huria. Makampuni makubwa hayawezi kuendelea kubakia kileleni mwa soko milele ikiwa hayataheshimu kiini cha ujasiriamali ambacho ni ubunifu. Ni lazima yakubali mabadiliko, yakubali kubomoa ‘yale mambo’ ya kizamani waliyoyazoea na kujenga mapya.

Kinachofanya  Makampuni kama Johnson & Johnson,General Motors, Microsoft, Apple na mengineyo kuendelea kufanya vizuri ni kuachana na tabia za ukiritimba wa “kujifungia”, kutokuogopa mbadiliko, kuanzisha biashara mpya na kufunga ama kuuza zile biashara za zamani ambazo zinaonekana hazizalishi tena faida.






2 Responses to "UJASIRIAMALI: UBUNIFU NDIYO MSINGI WAKE MKUU NA INJINI YA UCHUMI KATIKA SOKO HURIA."