JINSI YA KUTUMIA MAAJABU YALIYOPUNGUZA CORONA TANZANIA KUBUSTI UCHUMI WAKO UNAOSAMBARATIKA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI YA KUTUMIA MAAJABU YALIYOPUNGUZA CORONA TANZANIA KUBUSTI UCHUMI WAKO UNAOSAMBARATIKA


KUPIGA NYUNGU, MWANAUME AKIJIFUKIZA KUTIBU CORONA
Kuna watu mpaka sasa hivi Duniani wanaitukana Tanzania kwamba imekataa kuchukua tahadhari zote zilizowekwa na shirika la Afya Duniani WHO. Watu hao hawaamini hata kidogo kile kilichotokea Tanzania na wanachukulia korona kuisha Tanzania kama vile ni maajabu ya Dunia. Lakini kwa wachache wanaoelewa kama Donald Trump wa Marekani wameishia kimyakimya kufuata nyayo Tanzania ilizopitia.


Naomba usije ukaninukuu vibaya hapo, mimi sijasema Tanzania corona imekwisha kabisa hapana, bali imepungua kwa kiasi cha kustaajabisha na watu wengi kutokuamini kabisa wakiwemo majirani zetu Kenya, Uganda, Rwanda na wengineo. Ingawa Imani za kidini zimetajwa kuhusika na hili lakini mimi katika makala hii sitajikita sana kwenye Imani za kidini ingawa pia kile nitakachokwenda kukizungumzia(IMANI / BELIEF) kinaweza kuhusika na dini kwa namna moja ama nyingine kulingana na mtazamo wa mtu ulivyo.


Kumbuka tu kwamba Imani siyo lazima ihusiane na dini, unaweza ukaweka Imani kwa jambo lolote lile lisilohusiana na dini na ikafanya kazi. Imani ni hali inayofanya kazi ndani ya akili ya Mwanadamu na ina athari kubwa sana kwenye kufanikiwa ama kutokufanikiwa kwake kimaisha. Sibezi Imani za kidini hapa bali nataka tu kuelezea jinsi vile Imani inavyofanya kazi kwa namna ya ajabu katika akili zetu.

Ikiwa majirani zetu Kenya na Uganda hawaiamini Tanzania kama kweli Corona imepungua sembuse nchi zilizokuwa mbali kama Marekani, Ulaya na Asia? Sasa basi ni kitu gani hasa kilichotokea Tanzania hata Corona ikapungua kisi hicho na kuna ukweli wowote kwamba Corona imepungua ama ni propaganda tu za viongozi wa Tanzania kutaka kuficha ukweli wa mambo kijanja kusudi taswira ya Tanzania kibiashara huko nje isije ikaharibika tukakosa hela za utalii, ndege na nyinginezo?


Kujua ikiwa kama ni kweli Tanzania Corona imepungua kwa kiasi kikubwa au la ni rahisi sana kwa mtu unayeishi hapahapa Tanzania lakini siyo kwa mtu aliyeko ughaibuni. Unatakiwa tu kujiuliza maswali machache yafuatayo pale ulipo; Je, ni watu wangapi unaowajua mtaani kwako waliokufa kwa korona ndani ya wiki hii? Au ni watu wangapi maarufu nchini waliokufa au kuambukizwa corona siku za hivi karibuni? Na Je, siku mbili tatu hizi umeshuhudia watu wangapi wakiwa na mafua makali, kikohozi au hata homa kali na matatizo ya kupumua kwa shida?.

Kiukweli nilichoshuhudia mimi binafsi kwa macho yangu hospitali moja ni kupungua sana kwa wagojwa na sababu kubwa inatajwa kwamba ni watu wengi kutouguaugua tena ovyo mafua, vikohozi na minyoo kulikosababishwa na watu kunawa mikono kila mara.


Nilikuwa mmoja kati ya wabishi sugu kwamba corona haiwezi kupungua Tanzania ili-hali wenzetu Kenye wagojwa bado wanaongezeka, lakini baada ya kujiuliza maswali hayo machache niliamua mwenyewe kukaa chini na kuanza kuandika makala hii lengo langu likiwa si kupamba wala kusifia hapana, bali kuchunguza na kuibuka na majibu ya ni mbinu gani hasa iliyotumika mpaka corona Tanzania ikapungua kwa namna ya kustaajabisha hivyo na wala siyo kwa majirani zetu au nchi nyingine yeyote ile Duniani.


Kisha basi mbinu hiyohiyo bila shaka inaweza ikatumiwa na watu mbalimbali kuboost hali zao za kiuchumi zikiwemo pia biashara zao zinazozorota kwa kasi ileile Corona au Covid 19 ilivyosambaratishwa.

Siandiki Makala hii kiushabiki hata kidogo naomba nirudie tena, bali naiandika kisayansi kabisa baada ya kufanya utafiti wa kutosha. Mtu mwingine anaweza akasema labda Peter anataka kuleta tu siasa kwenye jambo hili, pengine kwakuwa kipindi cha kampeni kinakaribia na mengine kibao ya namna hiyo, hapana, hata kidogo, ukilipinga hili ni shauri lako mimi siwezi kukulazimisha, kwanza sina chama mimi bali muumini wa maendeleo ya binadamu.

SASA BASI NI KWA NAMNA GANI UNAWEZA KUTUMIA MAAJABU YALIYOMALIZA UGOJWA WA CORONA TANZANIA KUBUSTI UCHUMI WAKO?

Kwanza kabisa niweke wazi kwamba kilichosaidia sana mapambano ya covid 19 hapa Tanzania ni IMANI waliyojengewa Watanzania juu ya janga hili. Haijalishi ni kiongozi gani aliyebuni mbinu hii lakini mbinu ni mbinu tu ilimradi isaidie kushinda vita.


Ijapokuwa waswahili husema Mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni, siwezi nikasema ni Rais Magufuli aliyefanikisha hili peke yake kwa kuwa tulishuhudia hata viongozi wengine akiwemo Waziri mkuu Mh. Kasim Majaliwa, Waziri wa afya mama Ummy Mwalimu na hata Waziri wa Tamisemi Mheshimiwa Sulleiman Jafo wakihamasisha kauli mbalimbali zilizowajengea Watanzania Imani ya kuushinda ugojwa huu hatari kama vile, “Corona isitutishe”, “zingatieni masharti yote ya shirika la afya Duniani huku mkiendelea kuchapa kazi” “Pigeni nyungu kwelikweli msione aibu” “Kujifukiza, malimao, tangawizi, michaichai, muarobaini bila ya kusahau kumuomba MWENYEZI MUNGU”  na mengineyo mengi.

Kilichowasaidia watu kwa kiasi kikubwa siyo malimao, tangawizi na kupiga nyungu vyevyewe kama vilivyo hapana bali msaada mkubwa ulitokana na ile Imani iliyojengeka akilini mwa watu kwamba Corona isingeliweza kuwadhuru kwa kiasi kile walichokuwa wakidhania kabla. Wasiwasi ungeliweza kupandisha juu idadi ya vifo na wagojwa wa corona lakini Watanzania hawakuruhusu jambo hilo kutawala katika akili zao.


Jinsi imani ilivyo na nguvu ya kubadilisha matokeo ya jambo lolote lile chini ya jua
Kile unachokiamini huwa ndicho kinachokuwa kweli mara zote. Imani zina athari kubwa sana kwenye namna tunavyohisi, kufikiri na kutenda. Ndiyo hutoa taswira ya mambo yote tunayopitia katika maisha yetu;
Ø Imani ndiyo inayotengeneza mawazo/fikra
Ø Mawazo hutengeneza Hisia
Ø Hisia hubadilika kuwa vitendo/kutotenda
Ø Na vitendo sasa ndiyo vinavyohusika na matokeo yeyote yale katika maisha yetu
Mlolongo uko hivi;

IMANI →  FIKRA   HISIA →   VITENDO →  MATOKEO

Watu kimakosa huwa mara kwa mara tunadhania kwamba vitendo ndiyo vyenye uwezo wa kuleta matokeo lakini ni kama tunajidanganya kwa kusahau vitu vingine 3 nyuma yake. Ndiyo sababu tunastruggle(kuhangaika) sana kutafuta matokeo mazuri pasipo mafanikio makubwa kwani vitendo tu bila kingine chochote haviwezi kukufikisha mbali, utakwama njiani.


Na hii ndiyo sababu umeona nchi kama Marekani, Uingereza Italia na nyinginezo zilizokimbilia kutekeleza vitendo kama lock down nk. hazikuweza kupata matokeo mazuri pamoja na kuwa wana rasilimali nyingi. Walisahau vitu vingine 3 nyuma, Imani, fikra na hisia. Hapa chini nitaonyesha hatua zote 5 jinsi Tanzania ilivyozitumia kikamilifu na kufika hapa ilipofikia na janga hili la corona, na kisha baadae nitakwenda kutoa mfano mwingine wa mtu anavyoweza kupata matokeo bora kabisa kwenye jambo jingine lolote lile kama biashara, uchumi nk.

Kwenye matokeo yeyote yale maishani yawe mabaya au mazuri, hebu rudi kinyumenyume ukianza na MATOKEO yenyewe kisha chunguza matokeo hayo yametokana na VITENDO gani?, halafu Vitendo vilisababishwa na HISIA zipi, hisia hizo zilitokana na FIKRA zipi na mwisho tafuta Fikra zilitokana na IMANI ipi. Baada ya kugundua Imani iliyosababisha matokeo, sasa ndipo unapoweza kuamua kubadilisha matokeo hayo ikiwa ni mabaya kwa kubadilisha Imani na si vinginevyo. Ukijidanganya kuanzia kwenye vitendo narudia tena kusema ni lazima tu utafeli kwa mara nyingine, anzia kwenye mzizi wa fitina “IMANI”

Imani ilivyopunguza Corona Tanzania.
Tutaanza na MATOKEO kisha tutarudi kinyumenyume mpaka kwenye IMANI.

MATOKEO:
Matokeo yetu kwenye hili suala la korona ni KUPUNGUA KWA HALI YA UGOJWA/NAFUU KUBWA-Visa siyo vingi tena.

KITENDO:
Ni kitendo gani au vitendo gani Watanzania wanavifanya sasa ambavyo ndio vinavyotupatia matokeo haya tuyaonayo? Bila shaka vitendo ni Kufanya kila aina ya jitihada zinazochangia katika kumaliza janga la corona huku shughuli nyingine za kiuchumi zingali zikiendelea kama kawaida.

HISIA:
Ni hisia zipi Watanzania walizokuwa nazo juu ya vitendo hivyo?
Watanzania hawana wasiwasi na korona wanafanya mambo yao kama ilivyokuwa kabla ya ujio wa corona, hawahofii tena kama corona itawaua wala njaa kutokana na lockdown

FIKRA:
Ni fikra au mawazo gani yanayosababisha hizi hisia?
Corona itaisha kwa kuchukua tahadhari zote za kisayansi, kumtegemea Mungu lakini pia hatua za kienyeji bila ya kujifungia ndani na hata tukiugua tutapona hatutakufa.

5. IMANI
Ni Imani ipi inayosababisha fikra hizo?
Corona isitutishe na wala haina nafasi Tanzania, ni ugonjwa ulioletwa na watu kutoka mataifa ya nje kwa makusudi au bila kukusudia kwa lengo la kutufanya tuogope, tujifungie ndani na mwishowe tufie huko kwa njaa.


Katika kutia Imani hiyo nguvu Rais John Pombe Magufuli alifikia hatua ya kupima corona kwenye mapapai, mbuzi na sungura akakuta vitu hivyo pia vina maambukizi jambo lililowashangaza watu wengi na kuwaongezea Imani kwamba ugojwa huu si bure ni kama vile umepandikizwa. Walizidisha Imani kuwa corona haina madhara kwa kiwango kilichokuwa kimetabiriwa na Mataifa makubwa na matokeo yake ni huu ushindi tunaouona japo corona haijamalizika kwa asilimia 100%. Tungelikazania kwenye vitendo vya 'kujilockdown' leo hii tungelikuwa wapi?

Hivi karibuni Mataifa mengi yamegundua siri kuwa lockdown zisingeliweza kuwa suluhu endelevu ya corona bali suluhu ni kuwajengea watu Imani ya kuishinda corona wakati huohuo shughuli nyingine zikiwa zinaendelea kama kawaida mbinu ambayo Tanzania tulianza nayo tangu janga hili linaanza mpaka sasa hivi ambapo maambukizi yameanza kupungua.

IMANI, IMANI, IMANI, iwe ni ya dini au hata katika jambo jingine lolote lile ikipandikizwa akilini na kugeuzwa hisia mwisho wake hushawishi vitendo vitakavyoleta matokeo tarajiwa. Haiwezekani ukatenda vitendo pasipo Imani wala Hisia yeyote ile vikakuletea matokeo unayoyatarajia, utajikuta tu unaishia njiani, kusuasua au kupoteza kabisa motisha na ari ya kumalizia vitendo hivyo. Matokeo mabaya ni zao la kupanda Imani ambaya kwenye akili zetu, Imani ambayo inashawishi hisia mbaya.


Kitu kikubwa sana walichokifanya viongozi wa Tanzania ni kuwaondolea watu Imani mbaya waliyokuwa wamejijengea kuhusu corona na kuwavika Imani nyingine nzuri juu ya corona, basi hakukuwa na uchawi wala mazingaombwe hapo. Watu wa dini mbalimbali hapa msinifikirie vibaya tafadhali, dini nayo imechangia pakubwa katika vita na janga hili kwani dini pia ni Imani chanya katika kupambana na jambo lolote lile baya duniani.

UTAITUMIAJE IMANI KUBUSTI(KUINUA) UCHUMI/BIASHARA YAKO INAYOSAMBARATIKA?

Hatimaye sasa hebu tuone ni kwa jinsi gani funzo la mapambano ya ugojwa wa corona Tanzania linavyoweza kukusaidia katika mapambano mengine hasa ya kuondokana na umasikini kwa kuinua kipato chako cha fedha.

Tutatumia mlolongo kama uleule tuliouona kuanzia kwenye matokeo kurudi nyuma mpaka kwenye Imani. Tunachokitafuta hapa zaidi ni Imani kwani pasipo kwanza kubadilisha Imani mtu aliyonayo juu ya jambo fulani itakuwa vigumu sana kubadilisha matokeo ya jambo hilo, ataendelea tu kupata matokeo yaleyale milele na milele.

MATOKEO:
Matokeo yetu kwenye suala hili la kiuchumi ni;
Ukata/umasikini/kukosa kipato cha kutosha kuendesha maisha-

KITENDO:
Ni kitendo gani au vitendo gani unavyovifanya vinavyokupa matokeo hayo?
Sipati wateja wa kutosha kwenye biashara yangu kwa sababu sifanyi juhudi za kutosha za masoko kama ambavyo ningelipaswa kufanya

HISIA:
Ni hisia zipi ulizokuwa nazo juu ya hali hiyo?
Nina wasiwasi sitopata wateja wa kutosha na ninaogopa kwamba biashara yangu inaweza ikafa

FIKRA:
Ni fikra au mawazo gani yanayosababisha hisia hizi?
Mimi siyo mjuzi kwenye suala la masoko na wala sipendi kazi hiyo kwani inanifanya nionekane kama vile nawalazimisha watu kununua.

5. IMANI
Ni Imani ipi inayosababisha fikra hizo?
Kazi ya masoko ni ya kulazimisha watu, haina uhalisia na ni watu wenye uchu wa pesa tu ndio wanaopaswa kuifanya.

HITIMISHO
Ukishabaini IMANI inayokusababisha usipate kile unachokitaka maishani basi tayari utakuwa umekaribia sana kupata suluhisho la tatizo lako na utaweza hatimaye kubadilisha matokeo uliyokuwa ukiyapata kila mara.

………………………………………

1.   Kwa Makala bora kabisa usizoweza kuzipata mahali pengine popote pale juu ya fedha na Michanganuo ya biashara, karibu kwenye darasa letu whatsap na telegram, Group la MICHANGANUO-ONLINE tuna masomo kila siku yatakayokujenga kisaikolojia na kukuongezea ubunifu kwenye biashara yako. Kiingilio ni sh. Elfu 10 tu kwa mwaka mzima unapata pia na masomo yote ya siku zilizopita. Lipia kwa 0765553030 au 0712202244 Peter Augustino Tarimo, kisha tuma ujumbe wa “NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO-ONLINE2021” pamoja na CHANNEL YAKE

2.   Kujipatia kitabu cha MAFANIKIO YA BIASHARA YA REJAREJA bonyeza link hiyo.

3.   Kupata VITABU NA Michanganuo ya biashara mbalimbali zinazolipa tembelea duka letu la vitabu mtandaoni la SMART BOOKS TANZANIA

0 Response to "JINSI YA KUTUMIA MAAJABU YALIYOPUNGUZA CORONA TANZANIA KUBUSTI UCHUMI WAKO UNAOSAMBARATIKA "

Post a Comment