KUKUZA BIASHARA YAKE HARAKA, MJASIRIAMALI MDOGO ANAPASWA AJUE VITU HIVI 10 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUKUZA BIASHARA YAKE HARAKA, MJASIRIAMALI MDOGO ANAPASWA AJUE VITU HIVI 10


SUMAKU YA WATEJA KWENYE BIASHARA
Kukuza biashara kutoka chini kabisa ifike hatua ya juu zaidi kunahitaji juhudi kubwa na ubunifu kutoka kwa mjasiriamali mwenyewe ambaye anapaswa kujifunza mbinu za kukuza aina ya biashara anayoifanya. Aina za biashara mbalimbali huhitaji pia mbinu tofauti za ukuzaji kulingana na vigezo mbalimbali kama vile mazingira biashara inapofanyika, aina ya wateja, ushindani uliopo na fursa mbalimbali za kimasoko na kimauzo.

Ili biashara iweze kupata mafanikio haraka na makubwa, mjasiriamali ni lazima afahamu jinsi ya kukuza mtaji mdogo aliokuwa nao na kuigeuza biashara hiyo ya mtaji mdogo aliyoanzisha kuwa biashara kubwa inayolipa vizuri. Hapaswi kabisa kuziogopa au kuzikwepa changamoto za ujasiriamali bali kuzitumia kikamilifu kanuni za ujasiriamali katika kuzipunguza au kuziondoa kabisa changamoto hizo.


Mwanzoni mtu kweli anaweza akaona ugumu kwani itambidi kuvaa kofia zote peke yake nikimaanisha, mjasiriamali kushughulika na mambo mengi mwenyewe kama vile kufanya kazi za mauzo, maswala ya kodi, kuhudumia wateja na kufanya kazi zote zinazohusiana na uendeshaji wa biashara bila msaada kutoka kwa mtu mwingine yeyote yule. Hakuna wa kumsaidia na mwisho wa siku anajikuta yupo hoi huku muda mwingi ukiwa umekwisha.

Lakini kando ya ugumu wote nilioutaja ikiwa mjasiriamali ataamua kukaa chini akavuta hisia zake na kutazama mambo kwa mapana anaweza kwa urahisi kugundua njia anazoweza akazitumia kuikuza biashara yake haraka zaidi na kwa wepesi huku akitengeneza pesa nzuri chapchap na kuwaacha nyuma hatua nyingi mamia ya biashara kama yakwake.


Ingawa kuna mbinu na mikakati mingi inayowezakutumiwa kukuza biashara ndogo haraka, lakini mbinu hizi zifuatazo zinaweza zikaifikisha biashara yeyote ile hatua nyingine kabisa na kwa wepesi. Pamoja na kwamba nyingi ya mbinu hizi mwanzoni zinaweza kumgarimu mtu muda wake mwingi lakini mwishoni zinaweza kuleta mabadiliko makubwa kwa maana ya mauzo na faida kwa ujumla. Ni kama tu ilivyokuwa kwa mambo mengine yote katika maisha kwamba ni lazima mtu awekeze kwanza muda na hata fedha ndiyo aje kuchuma matunda baadae. Mjasiriamali hapaswi kulenga sana mafanikio ya muda mfupi, bali katika mafanikio ya muda mrefu huku akizingatia zaidi faida anayoipata mteja kama msingi mkuu wa mafanikio yake.

Mbinu hizo ni hizi zifuatazo;
1. Tengeneza faneli yako ya mauzo.
Natumaini Faneli unaijua, umewahi kununua mafuta ya taa dukani? Basi kile chombo chenye mdomo wa duara mpana juu halafu chini kinapoingia kwenye chupa ni chembamba. Biashara yeyote ile inatakiwa kuwa na kitu kama hiki, mahali ambapo wateja huja na kukusanyika wengi kisha baadae ‘kupenya’ taratibu na kununua bidhaa/huduma zako. Na biashara yeyote ile iwe ni ya mtandaoni au hata zile biashara za kawaida mfano biashara ya kuuza nguo za mitumba nazo  zina uwezo wa kuwa na faneli.


Biashara kwa mfano hizi za kwenye mtandao wa intaneti, faneli yako inaweza kuwa ni tovuti(website), blogu, email list, group la wasap, nk. kote huko unavutia wateja waje kujua ni nini unachotaka kuwauzia wakipendezwa nacho basi hujipenyeza kwenye mdomo wa faneli yako na kuja kununua, wasipovutiwa huzungukazunguka kwenye faneli na ‘kusepa’ zao kwingine watakaporizika kupenya.

Kwa biashara ya kawaida kwa mfano duka la mtaani la kuuza urembo na vipodozi, faneli yake ya mauzo ni fremu yenyewe ya duka au eneo mjasiriamali anapotandaza bidhaa zake za urembo na vipodozi ili ziweze kuonekana na wateja watarajiwa kabla hawajachukua maamuzi ya kununua. Ikiwa mjasiriamali hatakuwa na sehemu kama hiyo inamuwia vigumu sana kuuza bidhaa au huduma zake kikamilifu.


Faneli ya mauzo inaweza ikafananishwa na sumaku yako ya kuvuta wateja waje kununua kile unachouza na unaweza hata ukatengeneza faneli zaidi ya moja kulingana na uwezo na rasilimali ulizokuwa nazo.

2.Tafiti washindani wako.
Unapoamua kuingiza sokono biashara yako iwe ni bidhaa au huduma, unatakiwa kuwajua vizuri washindani wako(wale wanaouza kitu kinachofanana na cha kwako) Nenda katika faneli zao chunguza ni nini wanachokifanya na utagundua ni nini wanachokuzidi nacho kisha na wewe utakitumia kitu hichohicho huku ukikifanyia maboresho zaidi. Hii ni njia rahisi sana ya kuikuza biashara yako haraka.

3.Tengeneza mfumo wako imara wa huduma kwa wateja utakaokuwezesha kuwa na wateja wa kudumu.
Kumpata mteja mpya ni vigumu mara tatu(3) zaidi kuliko kumtunza mteja yule uliyekuwa naye tayari. Halikadhalika kumuuzia mteja mgeni kitu ni vigumu zaidi kuliko kumuuzia mteja ambaye tayari ulikwishamuuzia tena mara nyingine. Jitahidi sana kuweka vivutio kwa wale wateja uliokuwa nao tayari ili mauzo yako yaongezeke mara dufu na hivyo kukuza biashara haraka.


4.Vumbua fursa mpya katika biashara yako
Kwa kutafiti na kulitambua vizuri soko lako(wateja wako) unaweza kubaini fursa za masoko zaidi ambazo unaweza kuuza bidhaa au huduma zako. Kwa mfano tuseme ulikuwa ukisambaza vifaa vya steshenari mashuleni, unaweza pia kubaini mahitaji ya bidhaa za chakula kama mahindi, maharage, mchele, ngano, sukari na mafuta ya kula kwa shule za kulala boarding au hata zile shule zilizokuwa katika maeneo ya vijijini wanakokula mlo wa mchana.

 5.Tengeneza orodha yako ya wateja na mawasiliano yao(Email list)
Hasahasa orodha ya baruapepe(email list) ni kwa zile biashara za mitandaoni zaidi lakini pia ni jambo zuri likifanyika hata kwa zile biashara za kawaida. Kuwa na orodha ya wateja wako na jinsi ya kuwasiliana nao iwe ni kwa email, facebook, watsap au mtandao wowote ule wa kijamii kama tulivyoona kwenye faneli ya wateja au sumaku ya wateja, ni njia moja ya kisasa kabisa na iliyokuwa bora zaidi ya kukuza haraka biashara yeyote ile duniani katika nyakati tunazoishi sasa.

6.Tengeneza ushirikiano wa kimkakati.
Ushirikiano wa kimkakati na wadau mnaoendana utakuwezesha kupanua zaidi wigo wako wa kupata wateja kwani kushirikiana na makampuni na watu wanaofanya biashara zinazofanana na ya kwako kutakufanya ujuane na wateja ambao isingekuwa rahisi kuwafahamu mwenyewe. Siku hizi kuna makundi(magroup) mbalimbali mitandaoni ambayo hurahisisha sana ushirikiano wa namna hii.


7.Tumia majukwaa, mbalimbali.
Kwanini usitumie majukwaa yaliyojaa tele kutangaza biashara yako? Hapa kwetu kuna facebook, watsap, twitter, Instagram, forums na blogs mbalimbali. Na mengi ya haya majukwaa ni bure kabisa kujitangaza hawachaji hata senti tano.

8.Wape wengine leseni wakuuzie biashara yako.
Unaweza kukuza biashara yako kirahisi sana kwa kuamua kutoa idhini kwa watu wengine kuzalisha au kuuza kile unachokifanya wewe. Kwa mfano umebuni bidhaa fulani ya urembo au kipodozi na kuipa jina lako. Unaweza ukatafuta watu au mtu mwenye uwezo atakayeweza kuzalisha bidhaa hiyo kwa wingi ikiwa ni  pamoja na kuisambaza kwa wingi huku jina lako lilelile uliyoipa mwanzoni likiendelea kutumika kisha mnakubaliana wewe upate asilimia fulani ya faida itakayotokana na biashara hiyo. 


9.Kununua biashara nyingine.
Unaweza ukaamua ili ukue haraka zaidi ukanunua biashara zile zinazoshindana na ya kwako au hata kuungana nazo mkatengeneza biashara moja kubwa. Nayo hii ni njia mojawapo ya kukua haraka kibiashara.

10.Jitanue kimataifa.
Unaweza kuuza hata nje ya mipaka ya nchi au mkoa wako ulipo. Kuvuka mipaka kunaweza kuonekana ni jambo gumu na linalohitaji gharama kubwa lakini ukweli ni kwamba hakuna biashara zilizo na faida kubwa na ya haraka kama biashara za masafa marefu, cheki wanaokwenda China, Dubay au hata wanaosafiri kwenda kuchukua na kupeleka bidhaa hapo Zanzibar wanavyofanya biashara za uhakika ukilinganisha na baadhi ya watu wanaong’ang’ania tu kariakoo au Manzese na sehemu nyingine  jijini Dar es salaam.

Mbinu hizo kumi hapo juu ni kati ya mamia ya mbinu mbalimbali zinazoweza zikatumiwa na wajasiriamali na wafanyabiashara katika kukuza biashara zao haraka na kwa ufanisi mkubwa.

……………………………………

Ndugu msomaji wa makala hii, naandika pia makala nzuri za kuelimisha katika group la whatsap la Michanganuo-online kila siku. Mle tunazingatia zaidi makala zihusuzo mzunguko wa fedha katika biashara na michanganuo ya biashara bunifu zenye fursa za kipekee. Karibu sana jiunge nami huko kama ulikuwa hujajiunga.

Kiingilio ni sh. Elfu 10 tu na unapata uanachama wa kudumu unaoambatana na offa ya kitabu mashuhuri cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, michanganuo maarufu 3 ya kuku(MKOMBOZI CHICKS PLAN 3PACK) pamoja na mfululizo wa masomo yote yaliyopita tokea Januari mwaka huu.

Kujiunga tuma kiingilio chako sh. Elfu 10 kupitia namba 0712202244 au 0765553030 jina hutokea Peter Augustino Tarimo, kisha tuma ujumbe kwa wasap 0765553030 au meseji ya kawaida usemao, “NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO” na nitakuunganisha muda huohuo pamoja na kukutumia kila kitu. Ikiwa hutumii watsap hamna tatizo kwani masomo tunakutumia pia kwenye email utakayotutumia.

Leo hii tarehe 13 Septemba 2018 usiku saa 3-4 katika Group tutakuwa na somo kubwa sana lisemalo “KUKOPA FEDHA ILI UKALIPE DENI KUNAWEZAJE KUBORESHA MZUNGUKO WAKO WA FEDHA KWENYE BIASHARA? Mada hii muhimu tutazungumzia mambo mengi mazito yanayowasumbua vichwa wajasiriamali wengi kuhusiana na kukopa fedha kwa ajili ya kuboresha biashara zao.

Somo litajibu maswali mengi magumu kama vile ni kwanini wajasiriamali wengi wanastruggle(wanahangaika kimtaji mitaani) ili-hali mapesa yamejaa tele mabenki na katika taasisi nyingi za fedha hayana hata wa kuzichukua.

Usikose mtu wangu wa nguvu kama tayari umejiunga na group hilo, na kwa wewe ambaye bado haujajiunga muda upo wa kuhakikisha unawahi mada ikiwa live motomoto, usisubiri kuja kusoma kama makala iliyopita haipendezi sana japo ndio, unaweza kupata somo zima kama lilivyo na mengine yote yaliyopita katika mpango(programu) yetu ya mwaka wote wa 2018, lakini kupata kitu ‘Mubashara’ ndiyo mpango mzima.

Kuweza kupata maelezo juu ya vitabu mbalimbali kutoka Self Help Books Tanzania ltd, bonyeza maandishi haya yafuatayo; >>SMARTBOOKSTZ

1 Response to "KUKUZA BIASHARA YAKE HARAKA, MJASIRIAMALI MDOGO ANAPASWA AJUE VITU HIVI 10"