MCHANGANUO WA BIASHARA YA KUUZA CHIPSI, JE, UNAJUA GHARAMA YA SAHANI MOJA MPAKA INAFIKA MEZANI NI SH. NGAPI?

Ukisikia biashara ya mtaji mdogo yenye faida kubwa basi biashara ya kuuza chipsi ni moja ya biashara hizo. Hivi ulikuwa unajuabiashara ya chipsi kuku, soda inavyolipa dar? Basi kama ulikuwa hulijui hilo fuatana na mimi leo katika Makala hii ili uweze kulijua, unakula sahani ya chipsi kavu au chipsi mayai huku ukishushia na soda baridi, je wajua sahani hiyo moja ya chipsi mpaka inaingia mezani imegharimu kiasi gani cha fedha?.


Unamuona muuza chipsi akipokea hela nyingi unasema, “Du jamaa anapiga pesa sana ngoja na mimi nianzishe banda langu la kuuza chipsi, je unajua ni mahitaji ya shilingi ngapi utakayotakiwa uwe nayo kabla hujaanza? Na je unajua mtaji wako wa chipsi utarudi baada ya muda gani kupita? Unajua ili uweze kurudisha ghara zote za siku ulizotumia unatakiwa uuze angalao sahani ngapi za chipsi kwa siku(Break eve point)?. Vipi kuhusiana na vifaa vya kupikia chipsi, unajua bei ya jiko la kukaangia chipsi ni shilingi ngapi, jiko la kupikia chipsi na mayai, bei ya kabati la chipsi, makarai, jiko la kuchomea mishikaki, frying pan, sahani nk.?

SOMA: Mchanganuo wa biashara ya car wash, kuosha magari mtaji na vifaa vinavyohitajika.

Je unajua ni gharama zipi za uendeshaji wa biashara ya chipsi unazotakiwa kuzilipa? Unatakiwa kujua gharama kwa mfano, bei ya gunia la viazi mbatata/viazi ulaya, bei ya mafuta ya kukaangia chipsi, bei ya mkaa au nishati utakayotumia iwe ni umeme, gasi au Maranda ya mbao. Bei ya trei la mayai, bei ya viungo mbalimbali utakavyotumia kutengenezea saladi(kachumbari) au chachandu kwa ajili ya kuongeza hamu na ladha kwenye chipsi zako wateja wavutiwe zaidi kwako nk.

Baada ya kufahamu vitu vyote hivyo sasa utatakiwa kujua unaweza ukapata faida kiasi gani katika mradi wako huu wa kukaanga chipsi au Vihepe kama watoto wa mjini wanavyoita hasa wanafuzi wa mashule na vyuo ambao ni wateja wakubwa sana wa chipsi katika miji mikubwa kama Dar es salaam na kwingineko.

SOMA: Biashara ya mgahawa wa chakula, mchanganuo na mtaji mdogo wa kuanzia

Faida utakayoipata itategemea sana ENEO lako la biashara likoje, ikiwa ni eneo lenye mzunguko mkubwa wa watu mfano stendi ya mabasi, katika eneo la starehe na burudani kama bar au club, karibu na shule au karibu na chuo, basi mauzo na faida yako itakuwa kubwa sana na nzuri. Lakini ikiwa ni eneo tu la kawaida mtaani faida inaweza kuwa ya kawaida(wastani)

Ili kunogesha biashara yako ya chipsi unatakiwa kama unao uwezo basi uweke na bidhaa nyingine mfano juisi, soda au vinywaji vingine vya kushushia, kuwa na biashara ya juice pembeni au hata biashara ya kuuza soda na maji sambamba na biashara yako ya chipsi itakuongezea faida zaidi. Biashara ya chipsi vilevile inataka uwe na bidhaa ambatani kama vile mishikaki, kuku wa kukaanga au wa kuchoma, firigisi, samaki, soseji na ndizi. Bidhaa hizi ambatani zitaifanya faida yako kuongezeka zaidi.

SOMA: Biashara 7 nzuri za kufanya zitakazokuingizia pesa hata kama umelala

Sasa ili kujua hayo yote unapaswa kwanza kufanya utafiti wa biashara ya chipsi ambao kwa mujibu wa kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIMALI Utafiti wa biashara yeyote ile siyo chipsi tu, mtu unatakiwa kuuliza watu mbalimbali, kutembelea sehemu mbalimbali kupata taarifa anuai zinazohusiana na biashara unayotaka kuifanya pamoja na kusoma au kusikiliza machapisho yeyote yenye taarifa za biashara yako unayotaka kuifanya. Kwa kifupi kabisa hivyo ndivyo utafiti wa biashara au upembuzi yakinifu unavyoweza kufanyika wala huhitaji kuwa na digrii ya uchumi ndipo ufanye utafiti wa biashara yako.

Hatua ya pili unatakiwa uandae mpango wa biashara yako, hii ukiweza kuandika katika karatasi ni vizuri zaidi lakini pia watu wengi huifanya tu vichwani mwao na kuanza ndio maana utakuta watu wengi hawana kitu kinachoitwa mpango wa biashara ulioandikwa, siyo hawafanyi kabisa mpango wa biashara hapana, bali hufanyia vichwani na kutekeleza moja kwa moja kuokoa muda.

SOMA: Sababu kuu tano(5) kwanini uandike mpango wa biashara yako kwanza kabla hujaianzisha biashara yenyewe

Kinachosababisha watu wengi kutokuandika mipango ya biashara zao kwenye karatasi mara nyingi ni udogo wa biashara zenyewe, utakuta mtu anataka kufanya biashara ya mtaji wa laki moja sasa anaona yanini kusumbuka na tafiti na michanganuo, ila ukweli ni kwamba vitu hivyo huwa anavifanya kimya kimya kichwani mwake bila hata ya yeye mwenyewe kujua kama amevifanya. Ni lazima vifanyike, kamwe hamna namna nyingine unavyoweza kuanza biashara bila utafiti na mpango.

Sasa tukirudi kwenye mchanganuo wa biashara yetu ya chipsi kuku, mayai na chipsi kavu, hapa nitaanza kwa kuweka mahitaji ya kuanzisha biashara ya chipsi ya mtaji wa kawaida kwenye eneo la kawaida uswahilini, siyo maeneo ya ‘kishua’ yanayohitaji mtaji mkubwa sana.

SOMA: Naanza hatua kwa hatua kuandika mchanganuo wa biashara ya ufugaji wa kuku wa nyama

Mchanganuo kamili wa biashara yetu ya chipsi tutaandika hatua kwa hatua kwa njia rahisi kwenye group letu la Whatsapp la MICHANGANUO-ONLINE siku ya leo tarehe 3/6/2020 usiku saa 3 mpaka saa 4 lakini hapa chini nitakwenda kuweka mahitaji yote na gharama za kuanzia tu, nitaweka gharama za kudumu za mradi wa chipsi, gharama za uendeshaji na pia nitaainisha ni gharama zipi za moja kwa moja na zipi ni gharama zisizokuwa za moja kwa moja katika mradi/biashara hii. Ndani ya group tutafafanua zaidi pamoja na kuandika hatua kwa hatua kuanzia muhtasari mpaka ripoti ya faida na harasa.

Katika group la MICHANGANUO-ONLINE tumeanzisha utaratibu wa kuandika michangauo ya biashara zenye fursa kubwa na faida hatua kwa hatua, michanganuo hii inaweza kuwa mifupi au mirefu kulingana na aina ya biashara husika lakini tutajitahidi michanganuo hiyo iwe mifupi na iliyo na maana kwa mjasiriamali anayetaka kuiweka katika vitendo mara moja bila kuchelewa. Tutakuwa tukizingatia zaidi vipengele vile vya mpango wa biashara muhimu vinavyomrahisishia mtu kufanya utekelezaji haraka. Michanganuo hiyo mtu anaweza akaiendeleza na kuifanya michanganuo kamili mirefu kwa urahisi zaidi.

SOMA: Huna muda wa kutosha kuandika mpango wa biashara? tumia njia hizi 3

Kabla sijaorodhesha mahitaji ya mradi wetu wa chipsi katika eneo la uswahilini lakini lililo na watu wa kutosha, nitaainisha kwanza Gharama mbalimbali ambazo mara nyingi watu huwa zinawachanganya. Kumbuka nimesema mradi huu ni wa uswahilini lakini hata ikiwa unataka kuanzisha biashara yako ya chipsi ‘ushuani’, tuseme labda maeneo ya watu wenye kipato kikubwa kama vile masaki, Sinza, Ilala nk. basi unaweza tu ukatumia mfumo huohuo wa kuorodhesha mahitaji yako yote na kitakachobadilika hapo ni bei tu za vitu mbalimbali mfano wewe badala ya kuweka kabati la chipsi la shilingi laki mbili basi weka la laki 8 au milioni kabisa. Na katika listi ongeza na gharama za vitu kama AC, mayonnaise, sofa na kodi ya eneo kubwa kuanzia laki 2,3 mpaka 5 kwa mwezi badala ya elfu 50 au laki moja nk.

1. Gharama za kudumu:
Hizi ni zile gharama za vifaa, banda na vyombo kama majiko, makarai, kabati, meza na viti ambavyo hutumika zaidi ya mara moja na pengine vinaweza kukaa hata zaidi ya mwaka mmoja
2. Gharama za uendeshaji:
Huu ni mtaji wenyewe wa kuendeshea biashara, ni zile gharama za uendeshaji biashara (vitu au shughuli zinazotumika kwa muda mfupi mfupi, zinaisha na kwenda kununua vingine)

3. Gharama za moja kwa moja:
Gharama hizi zinaweza kuwa pia katika upande wa gharama za uendeshaji au za kudumu lakini ni zile tu zinazohusiana moja kwa moja na uzalishaji wa bidhaa au huduma kwa mfano gharama za ununuzi wa viazi, mafuta, saladi, chumvi, na mkaa.

SOMA: Jinsi ya kuandika mpango rahisi wa biashara kwa muda mfupi ndani ya nusu saa.

4. Gharama zisizokuwa za moja kwa moja:
Gharama hizi pia zaweza kuwa pande zote mbili, upande wa gharama za kudumu au za uendeshaji lakini hazihusiani moja kwa moja na uzalishaji wa bidhaa ama huduma inayozalishwa na mfano mzuri ni gharama kama vile za uchakavu wa vifaa, mishahara, kodi ya pango na matangazo. Gharama hizi hata usipozalisha kitu siku hiyo, mithali umeshaanza biashara yako ya chipsi basi zitatumika tu na hamna namna ya kuzikwepa.

Jinsi ya kutumia aina zote hizo nne za gharama zilizoainishwa hapo juu na ni wapi kila moja inatakiwa kutumika kwemye mpango tutakwenda kuona kwa vitendo katika mchanganuo wetu huo wa biashara ya kukaanga na kuuza chipsi katika Group la Michanganuo-online leo. Vitu vyote tunavyojifunza katika group hili vinahifadhiwa na mara unapojiunga kwa mara ya kwanza unapata fursa ya kuvidownload na kuvisoma hivyo hamna shaka ikiwa ulipitwa na Michanganuo iliyopita.

MCHANGANUO WA MAHITAJI YA KUANZISHA BIASHARA YA CHIPSI ENEO LA KAWAIDA LAKINI LENYE WATU WENGI KAMA BUGURUNI, MANZESE, TANDIKA, MBAGALA RANGI TATU, MBEZI-KIMARA NK.

Nimetaja maeneo yaliyopo Dar es salaam lakini si lazima iwe ni Dar, hata mikoani(mikoa yote) pia mfano huu unafanya kazi hamna shida. Vile vile bei ya vitu mbalimbali na gharama zingine nimekadiria tu, si lazima iwe hivyo kwa upande wako, itategemea maeneo ulipo na jinsi ulivyoufanya utafiti wako. Hata hivyo bei hizi ni za wastani.

Jedwali la mahitaji:
Gharama za kudumu/Vifaa:

Kabati la chipsi 1
150,000
Jiko la kukaanga chipsi 1
65,000
Jiko la kuchomea mishikaki na kuchaganyia chipsi mayai 1
25,000
Karai kubwa 1
18,000
Meza 2 kubwa @ 50,000 na ndogo@20,000
70,000
Viti 4 @ 10,000
40,000
Benchi 1
5,000
Koleo la kuchotea chipsi 1
4,000
Frying pan ya chipsi mayai 2 @ 15,000
30,000
Sahani dazani 2 @ 800
20,000
Beseni
4,000
Vijiko, umma na chuma za mishikaki
10,000
Visu 2 @ 1,500
3,000
Ndoo 2 @ 3,000
6,000
Jumla ndogo
450,000

Gharama za uendeshaji(mtaji)

Kodi (pango) miezi 6 @ 50,000
300,000
Mshahara wa msaidizi siku 3 @ 5,000
15,000
Viazi ndoo 2 @ 15,000
30,000
Mafuta lita 5 @ 3,000
15,000
Nyama ya mishikaki kilo 1
7,000
Kuku 1
6,500
Mkaa gunia moja
45,000
Mayai Trei 2 @ 6,000
12,000
Tomato source 1
2,000
Chili sorce
2,500
Chumvi, pilipili, nyanya na viungo vyote kwa ajili ya kachumbari jumla
6,000
Foil paper/vifungashio
5,000
Dharura
54,000
Jumla ndogo
500,000

JUMLA KUU

950,000

Kwa hiyo kama uonavyo kwenye jedwali letu la mahitaji ya  kuanza biashara ya kukaanga na kuuza chipsi, mtaji unaohitajika ni shilingi laki tisa na nusu(950,000/=)

Gharama za uendeshaji zimekadiriwa kiasi kinachotosha kuanzia, na kwa kuwa kunakuwa na mzunguko wa pesa kila siku vitu viunauzwa na kununuliwa vingine basi mzunguko utaendelea hivyohivyo huku faida ikizidi kuongeza mtaji. Gharama za kudumu hazina haja ya kuongeza nyingine zinatumika zilezile mpaka zitakapochakaa baada ya kipindi cha muda mrefu ambao tutakuja kuona kwenye uchakavu. Tutakwenda pia kuona hatua kwa hatua jinsi ya kukokotoa gharama ya sahani moja ya chipsi mpaka inamfikia mteja mezani ni shilingi ngapi.

SOMA: Ni lini biashara yako itarudisha gharama zote ulizotumia?(break even analysis)

Kuhusu gharama za moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja pia tutakwenda kuzionyesha kwenye mchanganuo wetu kamili wakati tukiandika hatua kwa hatua kwenye group la MICHANGANUO-ONLINE, hapa tumeziweka kwa ujumla tu.

Mpaka hapo ndugu msomaji wa blogu hii ya jifunzeujasiriamali nimefika mwisho wa Makala hii lakini nakusihi hakikisha  umejiunga na group letu hili kwa masomo zaidi ya michanganuo ya biashara na masomo mengine ya fedha yasiyopatikana mahali kwingine kokote. Karibu sana!

...............................................................................


KULIPIA KUJIUNGA NA GROUP UPEWE NA MASOMO NA SEMINA ZOTE ZILIZOPITA, TUMA NENO, “NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO NA OFFA ZOTE MPYA


*Ratiba ya Group la Michanganuo-online

SIKU
SOMO/MADA
Jumatatu
Somo la fedha
Jumanne
General/Vitu mchanganyiko
Jumatano
Michanganuo
Alhamisi
General/Vitu mchanganyiko
Ijumaa
Somo la Fedha
Jumamosi
General/Vitu mchanganyiko
Jumapili
Michanganuo

Siku za vitu mchanganyiko au general huwa tunajifunza chochote kutoka kwa yeyote katika group pamoja na matangazo mbalimbali ya biashara za wadau


Siku za masomo ya fedha na Michanganuo masomo maalumu kuhusiana na mada hizo hutolewa na wataalamu mbalimbali usiku kuanzia saa 3 mpaka saa 4 au 5

1 Response to "MCHANGANUO WA BIASHARA YA KUUZA CHIPSI, JE, UNAJUA GHARAMA YA SAHANI MOJA MPAKA INAFIKA MEZANI NI SH. NGAPI?"