MCHANGANUO WA BIASHARA YA GENGE LA KISASA LA MATUNDA, MBOGAMBOGA NA VYAKULA


Muuza genge akihudumia wateja gengeni kwake
Kabla sijakwenda kukuletea muhtasari wa mchanganuo mzima wa biashara ya genge la kisasa la matunda, mbogamboga na vyakula la Duble M FRESH, hapa chini nitatoa maelezo kidogo kwanza kuhusiana na sekta nzima ya biashara hii ya genge, faida, uanzishaji wake na wateja wa genge kwa ujumla.


Matunda na mbogamboga ni mazao ya chakula ya biashara yenye faida kubwa. Wengi hudhani ni biashara za vijijini lakini ukweli ni kwamba watu wanaoishi mijini ndio wateja na walaji wakubwa wa mazao haya. Katika mikoa inayokua kwa kasi kubwa kama vile mikoa ya Dodoma, Dar es salaam, Arusha, Mbeya na Mwanza mazao ya chakula na hususani matunda na mboga mboga yamekuwa ni biashara ya mtaji mdogo inayowaingizia wajasiriamali pesa nyingi na ni tegemeo la watu wengi kuliko biashara za mtaji mkubwa.


Katika orodha ya Michanganuo ya biashara zilizopo katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, tumeweka michanganuo ya biashara ndogondogo za mitaji midogo kuanzia elfu 50(50,000), laki mbili(200,000) mpaka laki tano(500,000) lakini pia kuna mipango ya biashara kubwakubwa za mtaji kuanzia milioni 20, milioni 50 na kuendelea. Katika orodha hiyo kuna biashara ya GENGE LA MATUNDA NA MBOGA iitwayo MMFRESH au DOUBLEM FRESH. MMFRESH ni genge la kisasa lililopo katika Manispaa ya Kinondoni eneo la Sinza.

Uzuri wa biashara ya genge ni kwamba, mtaji wa biashara ya genge siyo lazima uwe mkubwa sana na hauhitaji kukodi fremu ya gharama kubwa kama ilivyokuwa kwa biashara zingine kama biashara ya duka la rejareja. Kuna watu huamua kuanzisha duka genge na wengine huanzisha magenge tu peke yake. Tofauti ya vitu hivi viwili ni kwamba, duka genge huuza mchanganyiko wa bidhaa za matunda, mbogamboga, vyakula na bidhaa nyingine za madukani wakati genge tu peke yake huuza matunda na mbogamboga au na vyakula kidogo.


Faida ya biashara ya genge:
Biashara ya genge inalipa faida karibu nusu kwa nusu ya mtaji ulionunulia mali. Hapa namaanisha kwamba unaweza ukanunua kwa mfano tikiti maji shilingi elfu moja(1,000) na ukaja kuliuza kwa shilingi elfu 2(2,000) halikadhalika unaweza ukanunua ndizi shilingi mia ukaiuza shilingi mia mbili, hapo watu husema umepata faida nusu kwa nusu.

Eneo la kuweka biashara ya genge
Kama ilivyokuwa kwa biashara nyingine za rejareja mfano wa biashara ya duka, eneo ndio kigezo muhimu kushinda kila kitu. Jinsi ya kuanzisha biashara ya genge la matunda na mboga ni lazima genge lako ulifungue katika eneo unalojua lina watu wengi au makaazi ya watu ili uweze kupata wateja wa kutosha.


Usajili, kodi, TIN namba na sheria mbalimbali
Biashara ya genge watu wengi huanzisha bila hata ya kwenda TRA wala mahali pengine popote pale kujisajili au kukata leseni na vibali mbalimbali kama zilivyo biashara nyingine. Si kama vitu hivyo havihitajiki, la hasha bali ni kutokana na sababu kwamba biashara ya genge inachukuliwa kama ni biashara ndogondogo isiyozidi mtaji wa shilingi milioni 4. Biashara za udogo huu mara nyingi serikali huwa haihangaiki nazo kwenye suala la kodi wala leseni ingawa pia kuna magenge mengine yanauza mauzo makubwa hata zaidi ya maduka.

Kuna ushuru unaodaiwa na serikali za mitaa pamoja na tozo nyingine mbalimbali mfano za usafi wa jiji nk..Lakini pia genge lako likikua sana kutoka hatua ya genge la kawaida na kupita hatua ya genge duka maafisa wa kodi na leseni wanaweza wakakutembelea na kukutaka ukakate vitu hivyo.


Bidhaa za genge:
Bidhaa za genge ni matunda ya aina zote kama nyanya, maembe, machungwa, limao, ndimu, nanasi, ndizi mbivu mapeasi, tikiti, mabungo, ukwaju, mapapai nk., mbogamboga mfano, mchicha, kabeji, spinachi, matembele, karoti, pilipili hoho, pilipili kali, matango, bilinganyi nk. , baadhi ya vyakula kama vile, ndizi mbichi, mchele, maharage, unga, viazi vitamu, viazi mviringo, dagaa wakavu, samaki, dagaa wa kukaanga, viungo vya aina mbalimbali kama iliki, mdalasini, karafuu na bizari.

Mtaji wa kuanzisha genge:
Ukiwa na eneo tayari iwe ni kibarazani kwako au kandokando ya barabara, genge la matunda na mbogamboga unaweza kuanza hata ukiwa na shilingi elfu kumi(10,000). Lakini kama ninavyoshauri mara kwa mara kuanzisha biashara yeyote ile hakuna mtaji maalumu unaoweza kuambiwa na mtaalamu au mtu mwingine yeyote kwamba mtaji kiasi fulani ndio unatosha kuanza.


Kitakachokujulisha ni mtaji wa shilingi ngapi uanze nao ni malengo na maono yako uliyokuwa nayo kichwani. Na vitu hivi maono na malengo ndio mpango wako wa biashara unayotaka kuifanya na wala siyo makisio(projections) kama wengi wanavyodhani ingawa makisio ni sehemu tu ya mpango wa biashara yako uandike usiandike. Kwa urahisi kabisa ukitaka kujua unahitaji mtaji kiasi gani wa kuanza biashara yako, orodhesha mahitaji yote(gharama) ambayo ungependa biashara yako iwe nayo na jumla ya mahitaji hayo ndiyo mtaji unaohitaji, basi hamna zaidi.

Soko/Wateja wa biashara ya genge
Biashara ya kuuza genge wateja wake wakubwa ni ni kina mama wa majumbani walio na familia. Hata kama utamuona mtoto au baba akija gengeni kwako kununua mahitaji basi ujue kuna uwezekano mkubwa nyuma yake kaagizwa na mama(mwanamke) ambaye ndiye mpishi pale nyumbani vinginevyo basi watakuwa ni wateja wachache wanaume wanaoishi ubachela au wanafunzi wa vyuo. Hivyo basi katika mkakati wako wa soko ni lazima uwalenge kina mama zaidi kama utataka kufaulu biahsra hii.

MWANAMKE AKINUNUA VITU GENGENI KWA AJILI YA FAMILIA
Wanawake ndio wateja wakubwa wa biashara ya genge.


Baada ya kuona kwa ufupi biashara ya genge ilivyo sasa tutakwenda kuona Muhtasari wa mpango wa biashara ya genge la matunda na mbogamboga la MMFRESH, genge lililopo Sinza Kinondoni Dar es salaa. Mchanganuo huu mzima unapatikana katika kitabu cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI, kitabu kilichosheheni kila kitu mjasiriamali anachohitaji ili kufanikisha biashara ya kisasa. Mbali na michanganuo ya biashara mbalimbali kina masomo mengine yote ya biashara na ujasiriamali sehemu moja.


MUHTASARI WA MPANGO WA BIASHARA YA GENGE (MMFRESH)
Genge la matunda na mboga ‘fresh’ maarufu kama DoubleMfresh au (MMFresh) ni genge ambalo dhamiria yake kuu ni kuboresha afya za watu wa Kinondoni kwa njia ya kuwauzia mboga mboga na matunda yenye ubora wa hali ya juu na ambayo hutoka shambani muda mfupi.

DoubleMfresh hadi kufikia mwaka wake wa 4 litakuwa na matawi  mengine matatu kila moja katika kila tarafa zinazounda manispaa nzima ya Kinondoni, lengo likiwa ni kila mwana Kinondoni aweze kufurahia huduma hizi karibu na nyumbani anakoishi badala ya kuzifuata masoko yaliyokuwa mbali.

Genge litamilikiwa na Bwana Omar Masoud Othman mwenye uzoefu mkubwa katika biashara  ndogondogo hususani biashara ya dagaa, samaki na mazao yatokanayo na bahari, uzoefu huo aliupata kutoka kwa marehemu  wazazi wake ambao walifariki dunia kutokana na ajali ya meli ya MV Spice iliyotokea Septemba 10 mwka 2011 huko Nungwi Visiwani Unguja.

Mwaka 2012 ndipo alipoamua kulifunga genge la wazazi wake kisiwani Pemba na mtaji wote kiasi cha shilingi milioni 2 akauhamishia jijini Dar es Salaam ambapo anatarajia kufungua Genge la kisasa katika  kitongoji cha Sinza Kumekucha kilichopo ndani ya tarafa ya Magomeni na baadaye katika Tarafa nyingine zote tatu za Wilaya ya Kinondoni yaani, Kinondoni yenyewe, Kibamba na Kawe.

Bidhaa zitakazopatikana gengeni MMFresh ni pamoja na mbogamboga na matunda karibu aina zote, nafaka aina mbalimbali pamoja na bidhaa zitokazo baharini kama vile samaki waliokaushwa na dagaa.

Soko la matunda na mbogamboga jijini Dar es Salaam hususani maeneo ya Sinza ni kubwa na lina endelea kukua kadiri idadi ya watu nayo inavyozidi kuongezeka. Wilaya ya kinondoni kwa mujibu wa tovuti ya Jiji la Dar es Salaam idadi yake ya watu inakisiwa kufikia watu 1,900,000 Mwaka 2012 kwa ongezeko la asilimia 4.1% kila mwaka.

Mkakati wa soko wa MMfresh utalenga zaidi katika kuwavutia wateja wale wenye kipato cha kati kwa kufanya mambo mbalimbali yatakayowajulisha na kuwavutia ikiwamo, kutengeneza na kusambaza kadi maalumu kwa majirani siku ya ufunguzi rasmi, kubandika matangazo mitaani pamoja na kutoa zawadi na nyongeza kwa wateja na watoto wadogo katika zile siku za mwanzo mwanzo.

Mauzo katika miaka mitatu ya mwanzo yanakisiwa kama ifuatavyo, mwaka 2012 shilingi 10,800,000/=, 2013 shilingi 16,200,000/= na shilingi 24,300,000/= mwaka 2014. Asilimia ya faida ghafi kwa mauzo ni 45% miaka yote mitatu. Faida halisi katika kila mwaka inakisiwa kuwa 280,000/=, 2510,000 na 4,705,000. Chini ni chati inayoangazia kwa ufupi makisio hayo.

1.1    Dhamira kuu.
Dhamira kuu ya DoubleMFresh ni kuboresha afya za watu wa maeneo ya Sinza na Kinondoni kwa ujumla kwa kuwauzia mbogamboga na matunda yaliyokuwa “fresh” kutoka shambani. Hatutauza mbogamboga na matunda yaliyolala ili kuhakikisha wateja wetu wanapata bidhaa bora na safi. Hii itawavutia wateja wengi waendelee kuja kila siku na kusababisha bidhaa kutokulala ovyo.

1.2    Malengo:
MMFresh linatarajia kufikia malengo yafuatayo baada ya kufungua genge lake la kwanza pale kumekucha.
(1)       Kufungua magenge mengine yapatayo matatu ifikapo mwaka wa nne.
(2)       Kufikisha faida ya sh.4,705,000/= mwishoni wa mwaka 2014.
(3)       Kufungua duka la rejareja ifikapo mwaka wa tano.

1.3    Siri za mafanikio:
Mambo yatakayosababisha DoubleMFresh kupata mafanikio ni haya yafuatayo:
(i)          Kuuza mbogamboga na matunda yaliyokuwa na ubora wa hali ya juu.
(ii)        Kutengeneza maumbo yanayovutia kwa ajili ya kupanga bidhaa.
(iii)      Kupanua soko kwa kufungua matawi maeneo mengine.
(iv)      Kutoa huduma nzuri ambazo zitavuka matarajio ya wateja.

2.    Maelezo kuhusu Biashara:
DoubleMFresh litamilikiwa na Bwana Omar Masoud Othman na litaanza rasmi na mtaji wa Sh. 2,000,000/= ambazo ni gharama pamoja na bidhaa za kuanzia biashara.2.1  Umiliki wa Biashara:
DoubleMFresh litamilikiwa na Bwana Omar Masoud Othuman. Bwana Omar amejifunza biashara ndogondogo kutoka kwa wazazi wake kisiwani Pemba tangu akiwa anasoma. Mwaka 2012 ndipo alipohamia jiji Dar es Salaam baada ya wazazi wake kufariki dunia. Aliendelea na uuzaji wa samaki na dagaa mitaani aliowachukua feri mpaka sasa anapotarajia kufungua Genge la kisasa katika mtaa wa Sinza kumekucha………………………………………….

Mchanganuo mzima wa biashara hii ya Genge la matunda, mbogamboga na vyakula.(MMFRESH) pamoja na michanganuo ya biashara nyingine nyingi zinazolipa unapatikana katika kitabu chako cha MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI.


JINSI YA KUKIPATA KITABU HIKI NA BEI.

KITABU CHA KARATASI(HARDCOPY) ni sh. elfu 22 kwa wateja walioko Dar es salaa na tunawapelekea mpaka walipo. Mikoani tunatuma kwa njia ya mabasi ila gharama ya basi huongezeka kutegemeana na basi na eneo mteja alipo.


KITABU NAKALATETE(SOFTCOPY)
Tunatuma popote pale mteja alipo kwenye simu au kompyuta yake na bei ni shilingi elfu kumi(10,000/=)

Kwa mawasiliano, namba zetu ni hizi; 

Whatsap/Simu: 0765553030

au Simu/sms: 0712202244

Peter Augustino Tarimo

0 Response to "MCHANGANUO WA BIASHARA YA GENGE LA KISASA LA MATUNDA, MBOGAMBOGA NA VYAKULA "

Post a Comment