BIASHARA YA MAZAO YA CHAKULA: UNGA MCHELE SUKARI MAHARAGE NA MAFUTA YA KULA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA YA MAZAO YA CHAKULA: UNGA MCHELE SUKARI MAHARAGE NA MAFUTA YA KULA

Je unazijua fursa nyingi zilizomo ndani ya sekta nzima ya biashara ya mazao ya chakula au nafaka?

Haijalishi watu ni masikini kiasi gani ,wala hali ya kiuchumi ni mbaya kiasi gani, lakini chakula na hasa hasa nafaka kitabakia kuwa hitaji la msingi kabisa la binadamu likifuatiwa na mavazi na malazi. Katika biashara zote, biashara ya kuuza mazao ya chakula kama vile mahindi, mchele, unga wa sembe na dona, maharage, sukari, unga wa ngano na mafuta ya kula ndiyo itakayokuwa ya mwisho kudorora.

Mazao ya vyakula, hususani yale ya nafaka kama mahindi, mpunga, ngano, mtama, mihogo, maharage na jamii zake, pamoja na ulezi vimekuwa na mchango mkubwa sana katika kuongeza fursa za kiuchumi kutokana na sababu kubwa kwamba vyakula hivi ni muhimu kwa binadamu wote duniani bila ya kujali rangi, dini, kabila wala eneo analotoka mtu. Kuanzia Afrika, Asia, Ulaya, Australia, mpaka Marekani ya kusini na Kaskazini, hakuna mtu asiyetumia nafaka hizi.

Sekta hii hufanya kazi katika ngazi tofauti kwenye jamii, kuanzia, ngazi ya kaya ambao mara nyingi hawa ni wakulima wadogowadogo wanaozalisha mazao haya kwa kiasi kidogo tu kwa ajili ya chakula cha kujikimu na familia zao na mara chache kwa ajili ya kuuza kupata fedha kwa ajili ya kununulia mahitaji mengine madogomadogo ya familia. Kuna wakulima wakubwa au makampuni yanayolima mazao ya chakula kwa ajili ya biashara, makampuni ya ndani na wafanyabiashara wakubwa wanaonunua na kuuza mazao ya chakula ndani na nje ya nchi na makampuni makubwa mengine hujihusisha na biashara hii kwa namna moja au nyingine kwa ajili ya soko la Kimataifa.

Wapo wafanyabiashara wanaojihusisha na kununua nafaka kama mahindi na mpunga halafu huenda kukoboa au kusaga, biashara ya kukoboa na kusaga mahindi kwa mfano ni maarufu sana jijini Dar es salaam hasa maeneo ya Manzese na Tandika. Wafanyabiashara hao hasa kina mama wengi wamenufaika sana na biashara hii na huwapatia kipato na faida nyingi. Kuna wanaojihusisha na utengenezaji wa vifungashio tu pamoja na kuweka nembo na wapo wanaojihusisha na uuzaji peke yake. Hawa wanamiliki maduka ya kuuza unga, mchele na nafaka nyinginezo kama maharage nk.


Katika mgawanyo katika sekta ya biashara ya mazao ya biashara, utakuta ni mamilioni ya watu, karibu asilimia 90 ya watu wote katika nchi zinazoendelea kama Tanzania hujihusisha kwa namna moja au nyingine na biashara au ukuzaji wa mazao ya chakula. Lakini bado kuna tatizo moja, watu wengi wanalalamika sekta hii kutokuwa na tija ya kutosha, watu hao wengi watakuambia, kilimo bwana hakilipi, mazao ya chakula ni biashara kichaa haitabiriki, wengine watakuambia kilimo cha mazao kinahitaji mtaji kama biashara zingine hivyo hawana uwezo wa kupata mitaji nk.

Wakati watu hao hasahasa wale wanaoishi mijini wakilalamika na kutoa sababu hizo kibao, bado wapo na wanaendelea kuishi mijini huku wakilalamika kupanda kwa bei ya unga wa sembe na dona. Ukiwauliza wanadhani sababu ya chakula kuwa bei juu kiasi hicho ni nini, wanakujibu majibu wasiyokuwa na uhakika nayo kama vile, mvua haikunyesha ya kutosha, wakulima hawana pembejeo, serikali mpya imekuja na sera mpya ya kupandisha vyakula bei, watu wengi wamekimbilia mijini, shamba hakuna tena walimaji, ni mbinu ya madalali wa mazao kujipatia faida kubwa nk.

Ni kweli pamoja na kwamba ukame unaweza kuwa chanzo kikubwa cha kupanda kwa kasi kwa mazao ya chakula hasa mahindi na mazao yake kama unga wa dona, unga wa sembe na pumba za kulishia wanyama, lakini swali moja la kujiuliza ni kuwa,  mbona mazao mengine kama mpunga hayakuathirika kiasi hicho? Ina maana huo ukame ulichagua mahindi na maharage  peke yake? Labda unaweza ukasema ni kwa sababu watu wengi hapa Tanzania chakula chao kikubwa ni ugali.

Sababu zote hizo kwa mfano ingelikuwa ni nchi zilizoendelea sidhani kama zingelikuwa na nguvu kama hapa kwetu, usalama wetu wa chakula kwa ujumla haupo imara na  hii haiwezi kuwa ni kutokana na sababu hizo zilizotajwa hapo juu, Watanzania kuna hatua tunatakiwa kuchukua ikiwa tutataka kuondokana na hali kama hii nyakati zijazo.

Kama Taifa lilivyoamua kuachana na kutegemea umeme wa maanguko ya maji kama wa mabwawa ya mtera, Kidatu na mengineyo baada ya majanga ya umeme kama yaliyosababisha Richmond, Dowans  na skendo zingine kibao za uneme, katika suala la mazao ya chakula pia zinatakiwa zichukuliwe hatua na mikakati mbalimbali. Na hatua hizo si kuiachia tu serikali peke yake, ni suala linalotakiwa kuchukuliwa kwa uzito na wadau wote kwenye sekta wakiwemo wakulima, wafanyabiashara ya mazao ya kilimo, makampuni mbalimbali na mashirika makubwa.

Tatizo kubwa la nchi kama Tanzania hatutumii teknolojia kuhifadhi mazao, kwa mfano mahindi yakishavunwa yangeweza kuhifadhiwa vizuri na kisha kuja kuuzwa baadae wakati wa upungufu wa mahindi lakini hili hufanyika kwa kiasi kidogo sana tena na serikali, kwa upande wa wafanyabiashara siyo wengi wanaofanya hivyo husubiri kwenda kununua tu yaliyokwisha hifadhiwa.

Ikiwa kama utaamua kuwa serious na biashara ya nafaka kwa kutumia teknolojia zinazowezesha mazao kama mahindi kukaa kwa muda mrefu pasipo kuharibika, unaweza kutengeneza pesa nyingi sana katika kipindi cha muda mfupi tu.


Wakulima wadogo kwa upande wao wakisha vuna mahindi mengi wengine huyatumia  bila mpango mzuri mfano kutengenezea pombe za kienyeji na kuyauza bei rahisi jambo linayoyafanya yaishe ndani ya kipindi kifupi. Utakachokifanya ni kuwekeza fedha zako kwenye ununuzi wa mahindi au na nafaka nyinginezo kama maharage kipindi cha mavuno kisha unayahifadhi  kitaalamu kwa muda wa miezi kadhaa tu au mwaka halafu unaangalia vipindi vyenye upungufu wa mazao ndipo unauza.

Kilimo cha mahindi pia watu wamekuwa wakitegemea mvua zaidi, na zinapokuwa haba na mavuno nayo huwa haba. Tazama zao kama mpunga na ngano, mchele na ngano huzalishwa kwa wingi na makampuni makubwa tena kwa kiasi kikubwa kwa njia za umwagiliaji na ndiyo sababu hata unaweza ukaona mazao haya hayawezi kuathirika sana na ukosefu wa mvua kama ilivyokuwa kwa zao la mahindi.

Faida za kutumia makampuni makubwa kuwekeza katika biashara ya uzalishaji na uuzaji wa mazao ya chakula ni kwamba, huzalisha ajira wakati huo huo yakihakikisha usalama wa chakula unakuwepo. Makampuni makubwa yanakuwa na mitaji mikubwa hivyo kuwa na uwezo mkubwa pia katika uhifadhi na utunzaji wa mazao hayo kabla ya kuuzwa au kutumiwa katika shughuli za kuzalisha bidhaa nyingine. Yanakuwa pia na uwezo mkubwa wa  usafirishaji wa mazao katika maeneo mbalimbali ya nchi yanakohitajika au nje ya nchi.

Ndiyo maana nasema bado fursa ni kubwa katika sekta hii tofauti na vile watu wengi mijini wanavyofikiri. Mwaka huu wafanyabiashara waliothubutu tu hata kuanzisha biashara ya kuchukua mazao kutoka mikoa inayozalisha nafaka kwa wingi kama vile, Mbeya, Ruvuma, Sumbawanga, Morogoro na Iringa wengi wao wanacheka, hawawezi kukuelewa ukiwaambia eti biashara zimedorora kwani katika maduka yao kila kukicha watu ni foleni, utasikia wakisema, “nipimie unga kilo 5”, “ nipimie mchele kilo 10”, wengine, “naomba mchele wa mbeya super”, maharage ni shilingi ngapi?”, sembe imepanda tena?” nk.

SOMA: Utaongezaje thamani kwenye bidhaa zako?

Tabia ya watu kupenda kula unga wa sembe nayo kwa kiasi fulani inachangia uhaba wa chakula hususani mahindi kwani kiasi kinachopotea kwenye pumba  baada ya mahindi kukobolewa ni kikubwa, wanaofanya biashara ya kukoboa na kusaga mahindi wanafahamu sana ni kiasi gani cha pumba kinachopotea. Na kwa bahati mbaya zaidi ugali au unga wa mahindi yaliyokobolewa ni hatari kwa afya za walaji. Unaweza kuona unga wa sembe kuwa ni mzuri machoni au unapokula lakini kiafya ni majanga makubwa, ni chanzo kikubwa cha magojwa yasiyoambukiza kama kisukari, presha na hata unene kupita kiasi. Ingawa dona nayo wakati mwingine inaweza kuwa siyo nzuri sana endapo mahindi yatasagwa bila ya kuaosha vizuri, lakini kama yatasafishwa kikamilifu na kuondolewa yale yaliyoharibika ndicho chakula kizuri chenye afya.


Kuna kasumba nyingine ya watu kutokupenda kula baadhi ya vyakula kwa kuviona kama ni vyakula duni vinavyostahili kuliwa nyakati za njaa tu, vyakula kama vile ugali wa muhogo, ugali wa mtama, uwele na magimbi. Tumezoea kula ugali wa mahindi, wali, viazi, ndizi, mihogo ya kukaanga au ya kuchemsha, tambi na kande tu, wakati vyakula kama ugali wa mtama ni chakula kizuri sana chenye virutubishi vingi na nyuzinyuzi zinazosaidia usagaji mzuri wa chakula tumboni.

Fursa nyingine kubwa kwa wanaopenda kuanzisha makampuni ya kudili na mazao ya chakula hasa nafaka ni kama hii ya kuhakikisha kwa mfano kampuni yako inakuja na mbinu na mikakati mipya ya kijasiriamali kama vile kusaga nafaka na kuzifungasha(pack)  katika ubora wa hali ya juu, mandhari ya kuvutia mahali unapofanya shughuli hizo ukizingatia mtu ni afya. Kuwa na nembo(logo) yako mwenyewe iayokutambulisha kibiashara ni muhimu pa. Kwa ujumla hakikisha kampuni yako inakuwa tofauti na kampuni au biashara nyingine zinazojihusisha na biashara ya mazao ya chakula au nafaka.Ukishakuwa na jina, (brand) yako nzuri unaweza ukauza bidhaa zako kama ni unga wa mahindi unga wa ulezi, unga wa mtama, mafuta ya kupikia, maziwa au chochote kile kinachohusiana na nafaka au chakula nchi nzima na hata nje ya nchi kama vile unavyowaona makampuni kama akina Azam, METL, Azania, Tanga Fresh na wengineo .

..............................................................................................


HUDUMA NA VITABU KUTOKA SELF HELP BOOKS TANZANIA

1. Kitabu cha Michanganuo na Ujasiriamali.sh. 20,000/= hardcopy na sh 10,000/= softcopy

2. Kitab: Siri ya mafanikio biashara ya Dula la rejereja sh. 10,000/= hardcopy na sh. 5,000/=softcopy

3. Mifereji 7 ya pesa na siri matajiri wasiyopenda kuitoa 
sh. 5,000/=hardcopy na sh. 3,000/=softcopy\4. Kujiunga na masomo ya Semina ya kuandika michanganuo ya biashara sh. 10,000/=


5. Huduma na mafunzo ya kuanzisha kampuni ndogo ya uchapishaji vitabu, hardcopy na softcopy kwa gharama nafuu ya shilingi elfu 50 tu, pamoja na gharama za kuchapa vitabu vya kuanzia sokoni shilingi elfu 50 nyingine, jumla inakuwa sh. 100,000/= unaingiza kitabu chako(hardcopy) sokoni pamoja na blogu inayofanya kazi kila kitu utakayotumia kuuza softcopy. Kila kitu utafundishwa na utakuwa ukipewa sapoti ya karibu baada ya mafunzo. Unapelekwa maeneo yote muhimu yanayohusiana na uchapaji wa kitabu chako mguu kwa mguu na mkufunzi. Kwa kitabu cha kurasa zaidi ya 120 gharama ni tofauti.

6. Mafunzo kwa vitendo ya kuanzisha blogu inayofanya kazi, na itakayoanza kuwa na watembeleaji siku chache baada ya kuanza. Unafundishwa mwenyewe mpaka umeelewa kila kitu. Gharama yake ni shilingi elfu 30 mpaka umeelewa na blogu yako kukamilika.


TUNAPATIKANA MBEZI KWA MSUGURI JIRANI NA STENDI

SIMU:  0712 202244    AU   0765 553030

4 Responses to "BIASHARA YA MAZAO YA CHAKULA: UNGA MCHELE SUKARI MAHARAGE NA MAFUTA YA KULA"

 1. Nashukuru kwa darasa hili limenihamasisha zahidi kama kijana mwenye nia ya kujiajiri hasa katika biashara ya mazao, ningependa kununu vitabu vyote vi3 ila soft copy navipataje?

  ReplyDelete
  Replies
  1. Asante pia Mr. Son John Joram, softcopy za vitabu hivi unaweza kuzipata kupitia email na malipo unafanya kupitia namba za simu 0712202244 au 0765553030 jina, ni Peter Augustino Tarimo

   Delete
 2. Kwa kwel ujumbe n mzuri Sana , ttzo lipo kwenye uthubutu na usimamizi hapo tulio wengi huwa tunafeli

  ReplyDelete
  Replies
  1. Basi hatuna budi kuvifanyia kazi vitu hivyo 2 kwa dhati kabisa ili kuhakikisha tunafanikiwa katika maisha yetu. Asante mr. Unknown kwa kucomment hapa

   Delete