ONGEZA THAMANI KWENYE BIDHAA/HUDUMA ZAKO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

ONGEZA THAMANI KWENYE BIDHAA/HUDUMA ZAKO

Haijalishi ni biashara ya aina gani unayofanya, iwe unauza bidhaa mfano mchele au hata unauza huduma kama vile kuosha magari, kama mjasiriamali makini , unatakiwa kuhakikisha unaifanya bidhaa/huduma yako iwe na kitu cha ziada (Thamani zaidi) kwa wateja wako.


NI KWA NAMNA GANI UTAONGEZEA BITHAA/HUDUMA ZAKO THAMANI?
Mathalani unauza mchele, watu wengi wamezoea kununua mchele na kabla ya kuuinjika jikoni ni sharti kwanza wauchambue na wakati mwingine kuupembua ili kuondoa mchanga na mawe. Kitendo hiki huchukua muda na usumbufu na hata ikiwa mpishi mwenyewe ni mvivu basi walaji kazi wanayo wakati wanapokuwa mezani, utaona kila mmoja akimumunya mithili ya kibogoyo jambo linalo ondoa kabisa hamu ya kula hata kama pilau au ubwabwa wenyewe umeungwa vipi.



Sasa mjasiriamali kwa kutathmini matatizo yote hayo, hata kama  mchele wako unautoa Kyela,  unaweza ukauongezea thamani  kwa kuhakikisha kwanza kabla ya kuwauzia wateja unauchambua vizuri kwa kuondoa mawe yote na mchanga. Usiishie tu hapo vile vile unaweza ukaufungasha vizuri na vifungashio ulivyoandaa maalumu vyenye nembo anuani, na jina lako la biashara. Usiniulize utavitoa wapi, wapo watu ambao ni kazi zao, wafuate wanakuprintia vizuri, kitu kinaonekana kama vile kimetoka Dubai, kumbe ni hapa hapa.

Utakapouza kilo moja sh. 2,000/- hata kama bei ya kawaida dukani ni sh 1,500/- wateja wakishagundua ile thamani uliyoongeza nakuambia wengine itabidi uwafungie katika mifuko laini kwa kuishiwa vifungashio maana wateja watazidi uwezo wako wa kuandaa vifungashio.

Hali ni hiyo hiyo ikiwa unatoa huduma, tuchukulie mfano wewe unatoa huduma za maliwato na eneo la stendi fulani, wawekee wateja karatasi maalumu toilet paper hata ikiwa kuna maji ya kutosha. Wateja wanaofika kuoga, hebu fikiria ni kitu gani kinachoweza kuwatatiza.



Kwa mfano wateja wengi baada ya kuoga hupenda kujifuta lakini maliwato nyingi za stendi hamna mataulo na hata yakiwepo ni vigumu kuhakikisha usafi wake. Weka mataulo mengi yakutosha na yawe safi, waulize wateja ikiwa watapenda huduma ya taulo lililokuwa safi na salama kwa malipo ya ziada, utashangaa jinsi ambavyo wateja wengi watahitaji huduma hiyo ya ziada. 

Kuongeza thamani ndiko kunakotutofautisha wajasiriamali katika nchi za dunia ya tatu hasa Africa kusini mwa jangwa la sahara na wenzetu kutoka nchi kama Uchina, Ulaya na Amerika ya kaskazini. Malighafi husombwa huku na kupelekwa huko, wao wanachokifanya pekee ni kuongezea thamani tu, zikirudi bidhaa huku kama nguo tunapigana vikumbo kuzigombea pale mtaa wa Kongo. Kwa nini hiyo thamani tusiongeze wenyewe?.

0 Response to "ONGEZA THAMANI KWENYE BIDHAA/HUDUMA ZAKO"

Post a Comment