BIASHARA 7 NZURI MWAKA 2019: CHAGUA 1 UINGIZE FAIDA NA KIPATO CHA ZIADA KWA URAHISI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA 7 NZURI MWAKA 2019: CHAGUA 1 UINGIZE FAIDA NA KIPATO CHA ZIADA KWA URAHISI


BIASHARA NZURI 2019
Kama kuna kitu matajiri wanachokijua zaidi kuliko vitu vingine vyote basi ni PESA. Hali kadhalika masikini nao PESA ndio kitu wasichokifahamu kuliko vitu vingine vyote. Ninapoyasema hayo simaanishi kuijua pesa katika maana ya noti au sarafu hapana bali namaanisha kuwa na uelewa wa ndani kabisa wa jinsi unavyoweza kuzalisha na kuzisimamia pesa zako kikamilifu.

Kutimiza azma hiyo mtu anahitaji kitu kimoja tu nacho ni mfumo utakaomwezesha kuingiza pesa na kuzisimamia, mfumo huo si mwingine bali ni BIASHARA. Unaweza leo hii ukapata bahati ya kuwa na pesa nyingi labda kutokana na kushinda bahati na sibu au vyovyote vile lakini nakuhakikishia kama hautaziwekeza fedha hizo kwenye biashara na biashara hiyo ukaiiwekea mfumo mzuri wa usimamizi, pesa hizo hata ikiwa ni bilioni moja nakupa miaka michache tu utarudi palepale ulipokuwa mwanzo.



Hata kama utasema uzitumie ukizibanabana, mwisho wake kama hazizai zitakwisha tu na hutakuwa na cha kuendelea tena kuweka kama akiba. Kuna gharama mbalimbali za maisha na hizi hazikwepeki. Lakini habari njema ni kwamba kupitia biashara uwezo wa mtu kuingiza pesa zaidi hauna ukomo, ndio maana leo hii nimekuletea orodha ya biashara 7 unazoweza kuzifanya mwaka huu mpya wa 2019 kama njia ya kujiingizia kipato cha ziada. Haijalishi unafanya shughuli zako nyingine ajira ama biashara, unaweza kuchagua moja.

Kitu cha pekee sana katika orodha yangu hii leo ni kuwa biashara hizi nimezichagua kulingana na urahisi katika kuzisimamia, kwa maana nyingine ni biashara ambazo zinaweza kuanzishwa lakini mmiliki usitumie muda wako mwingi kuzihudunia na zikawa zinakupa kipato kama kawaida. 


1.Biashara ya kuuza Bidhaa au Huduma Mtandaoni.
Sipendekezi njia ngumu sana ya kuanzisha duka la mtandaoni hapana, nataka ufanye kitu kinachowezekana katika mazingira ya kawaida kabisa. Unaweza kufungua blogu au tovuti lakini bado kwa mtu wa awaida kabisa inaweza kuwa vigumu. Hivyo nitakutajia njia rahisi kabisa. Siku hizi karibu kila mtu mwenye smartphone yupo pia kwenye mtandao wa kijamii kama siyo facebook basi ni twitter, Insta, youtube au mtandao mwingine wowote ule.

Mitandao hii tunayoipenda sana katika kuwasiliana kijamii unaweza ukaitumia pia katika kutangaza na kuuza bidhaa yeyote ile au huduma unazozalisha mwenyewe au hata unazochuuza kutoka kwa watu wengine. Tena unaweza hata kuuza kitu ambacho hunacho mkononi, ni mali kauli tu, ukishampata mteja unamuunganisha na mwenye mzigo au unafuata mzigo na kumpelekea kwa makubaliano ya kupata cha juu.


Kuna watu wengi sasa hivi wanauza simu, vyombo vya ndani, madawa, ili hali hawana hata kioski, mteja akihitaji kitu wanampelekea au kumtumia kwa njia ya mabasi. Siri kubwa ya biashara hizi ni kujijengea jina(Branding). Kuna watu wanadili hata na ubuyu tu peke yake na wanapata pesa kuliko mtu mwenye duka kubwa. Hakuna biashara iliyo na urahisi kwenye usimamiaji kama hizi za kwenye mtandao kwani kila kitu una uwezo wa kukidhibiti kiteknolojia, unaweza kupanga muda maalumu wa kuhudumia wateja wako nk. Pia karibu kila kitu kinachouzwa katika maduka na magulio ya kawaida ya jadi unaweza pia ukakiuza mtandaoni kuanzia vitabu, magari, vifaa vya kielektroniki, vyakula, orodha ni ndfu unaweza mwenyewe kutaja chochote unachokijua.

2.Kuanzisha kiwanda kidogo.
Dhana ya viwanda ikiwa ndio inashika kasi Tanzania sasa hivi, mtu yeyote anaweza akanufaika na fursa hiyo kubwa kwa kuchukua hatua mbalimbali kama vile, kufungua kiwanda chenyewe, kuuza malighafi mbalimbali za kutengenezea bidhaa mfano, sabuni za vipande, sabuni za maji, dawa za chooni, batiki, unga wa lishe, juisi za matunda, nguo, keki, crips, ubuyu, tambi nk.


Au pia unaweza hata ukaanzisha darasa la kufundisha jinsi ya kutengeneza vitu mbalimbali kama una ujuzi kupitia mitandao  ya kijamii kama magroup ya wasap na facebook, blogs nk. Unaweza pia ukaanzisha darasa mahali ukajitangaza kuwa unatoa mafunzo ya namna ya kutengeneza kitu fulani ilimradi tu uonyeshe watu kwa vitendo ule utaalamu unaotaka kuwafundisha.

Urahisi wa usimamiaji katika biashara hii upo katika uhuru wa kuchagua ni muda gani ufanye kazi zako, unaweza kuamua uzalishaji uufanye muda wa jioni au usiku baada ya kazi zako. Mauzo nayo unaweza kuyafanya kwa jumla na hivyo kutopata usumbufu wa kutumia muda mwingi, labda wateja unawaambia waje siku maalumu kuchukua mzigo au unawapelekea walipo. Ni rahisi pia kuajiri mtu wa mauzo kwani utakuwa na vitu vinavyohesabika baada ya kazi ya uzalishaji kuifanya mwenyewe.

3.Biashara za vyakula.
Biashara ya chakula ni sekta kubwa unayoweza kuchagua eneo dogo linalokufaa kulingana na mazingira yako(a niche) na kujikita kikamilifu. Na uzuri wa chakula ni kwamba ni bidhaa inayotumiwa kila siku na kila mtu, mtu akila leo kesho ni lazima atakula tena, hivyo kama umemuuzia chakula kizuri leo kesho atakutafuta tena.


Unaweza kurahisisha usimamizi kwenye biashara ya chakula kutegemeana na ni eneo lipi umejikita. Kwa biashara ya ziada lenga maeneo yale ambayo hayatakupa usumbufu kusimamia. Unaweza kwa mfano katika biashara za chipsi au mgahawa ukatengeneza mfumo utakaokuwezesha wewe usiwe pale muda wote na ukafungua hata matawi mawili au zaidi kupata faida kubwa zaidi. Wengi hutumia mtindo wa “daladala”, kufungua ofisi na kumkabidhi meneja kila kitu yeye akuletee hesabu maalumu tu usiku huku ukikagua aseti zako pale mara kwa mara basi.

4.Usafirishaji wa Abiria na mizigo.
Kama unao mtaji hii bado ni biashara itakayolipa mwaka 2019 kutokana na mahitaji makubwa ya huduma hizo nchini.Watu kila siku wanahitaji kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, barabara zinaongezeka na kuboreshwa katika awamu hii ya uongozi kuliko awamu nyingine yeyote. Utahitaji usimamizi imara tu kutengeneza faida nzuri mwaka 2019 iwe ni bodaboda, bajaji, daladala, basi au hata malori ya mizigo.


Urahisi hapa kwenye usimamizi unakuja pale inapowezekana kumwajiri mtu akafanya kazi na kukuletea hesabu tu ingawa kunaweza kuwa na changamoto za hapa na pale lakini, uwongo unaweza kuingiza pesa huku ukiendelea na majukumu yako mengine pasipo kutoa jasho jingi.

5.Ufugaji wa kuku, sungura, samaki na ndege wengine wafugwao.
Urahisi kwenye usimamizi wa biashara hii ni kwamba unaweza kuwashughulikia mifugo wako muda wa asubuhi na jioni tu na ikifika wakati wa mauzo ukatenga siku maalumu ambayo haupo kazini au kwenye biashara yako kuu. Pia kumwachia msaidizi ni rahisi kwani mifugo ni kitu unachoweza kuhesabu kwa urahisi.

6.Kilimo cha mbogamboga na matunda kama nyanya, pilipili hoho, bamia, kisamvu na matembele.
Ukiwa na uwezo wa kufunga green house, itakurahisishia sana katika usimamizi na uendeshaji kwani hautahitajika ukae pale masaa yote kutokana na kazi kurahisishwa na mfumo wa umwagiliaji wa matone(drip irrigation system). Pia hakuna uhitaji mkubwa wa kuondoa magugu kama ilivyo kwa bustani za kawaida kutokana na kuwepo kwa matandazio ya kisasa ya nailoni yanayozuia magugu kuota.


7.Biashara za nyumbani.
Hapa kama ilivyokuwa kwa mtandao wa Intaneti, nyumbani ni ukumbi unaoweza kufanya biashara za aina nyingi sana pasipo kulazimika kulipa kodi wala kuingia gharama nyingine nyingi. Urahisi katika usimamiaji wa biashara hizi utategemea ni nani utakayemwachia hiyo biashara pale nyumbani unapoondoka. Ikiwa kwa mfano unayemwachia ni mwenza wako, mke au mume inakuwa rahisi sana kwani wote mnakuwa na lengo moja. Lakini pia unaweza ukamwachia mtumishi wa nyumbani kuangalia biashara kwani nyingi huwa ni biashara ndogo zinazohesabika kirahisi.

Ifuatayo ni orodha ya biashara ndogondogo unazoweza kuanzisha nyumbani, kibarazani au hata ndani ya ua wako.
·       Vitafunwa mbalimbali
·       Ice cream na lambalamba
·       Kuuza barafu
·       Kukodisha vitu kama viti, maturubai, vyombo nk.
·       Uuza mkaa na kuni
·       Kuuza pumba kwa ajili ya kulishia mifugo
·       Kuuza maji ya bomb/kisima.


Hitimisho.
Wakati biashara ya ziada inaweza kuwa ni njia nzuri ya kuongeza kipato chako pia vipo vitu kadhaa nya kuzingatia;
1.  Zingatia malengo ya kuanzisha biashara yako ya ziada, ikiwa ni ya muda mrefu kama vile siku moja kuja kuifanya ndio biashara yako ya kudumu basi ianze taratibu huku ukiifanyia utafiti wa kina ili uifahamu nje ndani. Ila kama unalenga tu la kupata pesa za kukidhi haja fulani ya muda mfupi huna haja ya kufanya utafiti wa kina sana.

2.  Kumbuka pia kwamba biashara ya ziada haiwezi kukupa utajiri wa haraka, ingawa zina uwezo wa kumtajirisha mtu lakini haziwezi kufanya hivyo kimiujiza kwa siku mbili tu au tatu, ni lazima uwe mvumilivu, uweke juhudi kuhakikisha unatoa thamani ya kutosha kwa wateja na wala siyo kujidanganya eti inaweza kukutoa muda mfupi tu ujao.


.....................................................

Ndugu msomaji wa makala hii ikiwa unapenda kujifunza zaidi masomo yahusuyo fedha na michanganuo ya biashara, basi karibu kwenye group letu la wasap na email kwa kiingilio cha sh. elfu 10 upate masomo yote tangu mwezi Januari na pia nafasi ya kujifunza kwa mwaka wote wa 2019 bila kulipa zaidi.

Namba za kulipia ni 0765553030 au 0712202244 kisha tuma ujumbe, "NIUNGANISHE NA GROUP LA MICHANGANUO-ONLINE"

Ikiwa hutumii wasap masomo tutakutumia kwa njia ya email.

Mwisho wa offa hii ni Desemba 30, wahi kabla group halijajaa kwani zimebaki nafasi chache. Masomo ni kila siku saa 3 usiku.

Kwa vitabu bora kabisa na Michanganuo ya biashara iliyokwisha andikwa tayari tembelea; SMART BOOKSTZ

1 Response to "BIASHARA 7 NZURI MWAKA 2019: CHAGUA 1 UINGIZE FAIDA NA KIPATO CHA ZIADA KWA URAHISI"