SIRI YA KUFANIKIWA BIASHARA YA KUUZA VINYWAJI BARIDI VYENYE FAIDA NDOGONDOGO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SIRI YA KUFANIKIWA BIASHARA YA KUUZA VINYWAJI BARIDI VYENYE FAIDA NDOGONDOGO

kuuza vinywaji baridi kwa rejareja

Kwenye group la masomo ya kila siku yenye maudhui ya pesa na michanganuo ya biashara kuna mdau mmoja ameuliza swali kuhusiana na biashara ya rejareja akaomba samahani akijua alikuwa nje ya maa lakini kumbe yupo sahihi kwani tunakaribisha swali lolote lile ilimradi tu lihusu Biashara, ujasiriamali au Michanganuo ya biashara yeyote

Aliuliza kama ifuatavyo bila kupunguza wala kuongeza chochote;

Jinsi ya kufanikiwa katika uuzaji wa vinywaji baridi

 Habari boss

Samahani kiongozi

Naomba kuuliza swali ambalo lipo nje ya mada

Naomba kujua uliweza vipi kufanikiwa katika uuzaji wa vinywaji baridi?

Maana kwa ninavyofahamu mim hii biashara faida yake ni ndogo sana

Faida yake ni kuanzia elfu moja mpaka elfu mbili kwa kreti zima la soda

Ulifanikiwa vipi katika hali hii??

 

MAJIBU:

Bila samahani na swali lako wala halipo nje ya mada hata kidogo maanake humu kwenye group la Michanganuo-Online mtu unaweza ukauliza swali lolote lile juu ya michanganuo ya biashara, Ujasiriamali na Biashara za rejareja kwa ujumla wake

Majibu: Siri ya mafanikio biashara ya kuuza vinywaji baridi rejareja


Tukirudi kwenye swali lako ni hivi;

Kwa upande wangu binafsi, nadhani wewe ni mmoja kati ya watu waliowahi kusoma kitabu changu kiitwacho MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LA REJAREJA, kitabu chenye kila kitu mjasiriamali wa biashara yeyote ile ya rejareja na siyo duka tu anachopaswa kujua ili biashara yake iweze kupata mafanikio

Ni ukweli binafsi mimi nimefanya biashara ya duka la rejareja kwa muda wa miaka 12 na hunidanganyi chochote kuihusu hii biashara. Nimeuza vinywaji vya baridi hususani soda, maji na juisi lakini pia nimeuza bidhaa nyingine mbalimbali za dukani kama vile mchele, unga wa sembe/dona, sukari, chumvi, viberiti, sindano, uzi, mshumaa, mafuta ya taa, pini na orodha ni ndeee......fu, siwezi nikavitaja vyote hapa patajaa sijamaliza.

Kuna vigezo vingi huamua faida katika biashara ya duka au tuseme biashara za rejareja kwa ujumla, mtaji wa biashara ya vinywaji, eneo la biashara, aina ya wateja watakaonunua kwako nk. Aina za biashara ndogondogo nyingi zina tabia hii ya kuathiriwa na vigezo hivyo nilivyovitaja.

Kama ulivyosema mwenyewe faida katika vinywaji baridi kwa rejareja siyo kubwa kivile na siyo kwenye vinywaji tu peke yake bali ni katika karibu kila bidhaa ya rejareja faida siyo kubwa sana. Kwa uzoefu wangu vitu vingi vya rejareja unaweza kupata faida kuanzia asilimia 5% mpaka 35% hivi ya mauzo.

Hii inamaanisha kwamba kwa mfano ukiuza bidhaa ya shilingi 100 basi utapata faida kati ya shilingi 5 mpaka shilingi 35 na si zaidi sana ya hapo. Tuchukulie mfano wa soda, kwa soda zinazouzwa shilingi 600 rejareja kreti yake duka la jumla inauzwa shilingi 12,000/= hivyo ni sawa na kusema jumla soda moja umenunua shilingi 500/= faida kwa chupani sh. 100/=

Ili uweze kujua ni asilimia ngapi ya mauzo chukua faida igawe kwa bei ya kuuzia = 100/600 kisha jibu zidisha kwa 100 = asilimia 16.6% Ungepata jibu hilohilo kama ukichukua jumla ya faida ya soda zote kisha ugawe kwa jumla ya mauzo ya soda kreti lote; 2,400/16,800 x 100 = 16.6%

Kwa soda zinazouzwa shilingi 700 kreti lake jumla utanunua sh. 13,500/= sawa na soda moja sh. 562.5/= Faida kwa soda moja ni sh. 137.5/= Kujua ni asilimia ngapi ya mauzo chukua faida gawa kwa bei ya kuuza kisha zidisha mara 100 = 137.5/700 x 100 = 19.64% Pia nayo ukitumia jumla ya faida ya kreti zima ukagawa kwa  jumla ya mauzo ya kreti zima x 100 unapata asilimia hiyohiyo  19.64%

Kwa hiyo unaweza kuona kwamba hizi asilimia 16.6% na 19.64% zipo katika ile ‘range’ tuliyosema ya asilimia 5% mpaka 35%

 

Ni kanuni inayofanya kazi kwa biashara za rejareja Duniani kote na si hapa Tanzania tu. Hata ukienda Marekani sijui china ni hivyohivyo.

SIRI YA KUFANIKIWA BIASHARA YA KUUZA VINYWAJI BARIDI VYENYE FAIDA NDOGONDOGO

Sasa basi kama hivyo ndivyo unawezaje kufanikiwa ama kupata faida kubwa kwenye biashara hii ya vivyaji baridi rejareja?

1. Kuuza kwa wingi (Mass selling)

Haiwezekani uone mafanikio kwa kuuza rejareja soda tu peke yake mahali pasipokuwa na bidhaa nyingine yeyote ile labda iwe pale mahali unapouzia basi soda zinatoka kwa wingi sana pengine unauza hata kreti 10 mpaka 15 kwa siku.

Naweza kukuambia kwamba mimi binafsi wakati nafungua biashara yangu ya rejareja kwa mara ya kwanza kabisa pale maeneo ya Msimbazi Karikakoo kipindi hicho mtu ukiwa na eneo pale ulikuwa na uwezo wa kuishi kwa kuuza soda tu peke yake bila ya kuuza kitu kingine chochote kile kutokana na wingi wa watu katika eneo lile na kumbuka kama nilivyoeleza na picha nikaweka kwenye kitabu hicho uliona nilivyoanza na friji moja tu la kampuni ya Pepsi na kikabati kidogo cha kioo tena nje bila hata fremu lakini uliona nini baada ya mwaka mmoja?

Naomba nikuulize tena, kwanza unajua nini kuhusiana na biashara za rejareja? Kama ulisoma vizuri kitabu changu hicho utakumbuka pale mwanzoni kabisa nilizungumzia aina za biashara za rejareja nikataja kuanzia Kioski mpaka Supermarket na Hypermarkets ambazo ndiyo ngazi ya juu kabisa ya biashara hizi za rejareja duniani.

Sasa hebu tazama soda na maji huuzwa mpaka kwenye Masupermarket na hayo Mahypermarkets, mbona usiwasikie wakisema kwavile soda na maji vina faida kidogo basi wanaachana navyo wauze tu vitu vyenye faida  kubwa? Wewe unazungumzia soda yenye faida karibia asilimia 20%, kuna vocha faida haifiki hata asilimia 3% na bado watu wanauza na tena wengine hata hutegemea mauzo ya vocha peke yake bila ya vitu vingine kuishi mjini. Siri pekee hapa ni maajabu ya kuuza vitu kwa wingi (Mass sales) Kumbuka vinywaji baridi ni bidhaa mtu anaweza kunywa kila siku hivyo wasiwasi wa kudoda ni mdogo sana ikiwa eneo (location) lina watu wa kutosha

2. Mchanganyiko wa Bidhaa mbalimbali (Diversity)

Watu hawategemei faida kwenye bidhaa moja tu ya rejareja mfano soda au maji, katika duka zima au kioski chako au supermarket yako au hata genge lako, hutauza bidhaa moja tu hapana. Kama mimi nilivyofanya kwenye kikabati changu siku ya kwanza kabisa pale mtaa wa Msimbazi Kariakoo, ukitazama vizuri utaona mle ndani ya kikabati kulikuwa na boksi la Panadol, Hedex, mifuko ya keki na Clips za viazi. Sikutegemea faida ya zile soda kwenye friji la Pepsi tu peke yake. Faida kidogokidogo kutoka katika bidhaa zote nilizoziweka hatimaye iliweza kunifanya nione faida niliyokuwa nikiipata ni kubwa.

HITIMISHO

Kwahiyo ndugu yangu Yassin biashara ya kuuza rejareja vinywaji baridi vyenye faida ndogondogo siri yake kubwa ili ufanikiwe kuiona faida kubwa ni kuhakikisha unatekeleza mikakati hiyo miwili niliyoitaja hapo juu, wapo watu wametajirika kwa biashara hizihizi na wengine kupata mitaji mikubwa ya kuanzisha biashara nyingine za mamilioni ya pesa kupitia kwanza kuuza vinywaji baridi kwa rejareja.

Naamini majibu yangu yanaweza kuwa na msaada kwako.

ASANTE SANA,

PETER TARIMO 



SOMA NA HIZI HAPA: 

1. Jinsi ya kujua faida ya duka la rejareja kila sikujioni unapofunga hesabu

2. Mtaji wa biashara ya duka la rejareja: Nianze nashilingi ngapi ili nifanikiwe?

3. Nataka kufungua duka la rejareja la mahitaji ya kilasiku katika jamii, mbimu gani naweza kutumia kufanikisha?

4. Mchanganuo wa biashara ya genge la kisasa la matunda,mbogamboga na vyakula

0 Response to "SIRI YA KUFANIKIWA BIASHARA YA KUUZA VINYWAJI BARIDI VYENYE FAIDA NDOGONDOGO"

Post a Comment