SIRI YA MIKOPO NA CHANZO CHA WATANZANIA KUOGOPA MNO KUKOPA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SIRI YA MIKOPO NA CHANZO CHA WATANZANIA KUOGOPA MNO KUKOPA

Heri ya Mwaka Mpya Ndugu Msomaji wa Makala hii !

Tunapoukaribisha mwaka 2022 kuna mambo mengi tutanayoyaacha nyuma yetu lakini pia ni lazima tukubali kwamba kuna mengine kamwe hayataweza kufutika kwenye mawazo yetu kwa urahisi siku za hivi karibuni na moja kati ya matukio hayo ni kama vile kuondokewa na wapendwa wetu, kuugua na hata kupatwa na majanga makubwamakubwa.

Kwahiyo nichukue nafasi hii kuwakumbuka hasa Wadau wenzetu ambao siku kama ya leo mwaka jana waliweza kusoma ujumbe wangu wa mwaka 2021 lakini kwa bahati mbaya leo hii hatuko nao tena, Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa Amani Amina.

Wiki inayoisha nchini kuna habari ‘ilitrendi’ (kushika sana kasi) kuhusiana na deni la Taifa, huku kila mtu akisema lake. Ijapokuwa si nia yangu kuonyesha upande ninoegemea lakini pia kama haki yangu ya msingi na kama Mwananchi siyo vibaya nami nikatoa maoni yangu kidogo katika mtazamo wa Kijasiriamali.

Siyo siri Watanzania wengi tunaogopa sana mikopo na sababu kubwa ya hofu hii si nyingine bali ni UKOSEFU WA ELIMU YA KUTOSHA YA FEDHA. Wanaoujua utamu wa kukopa na kufanyia kazi mikopo kwa malengo waliyokusudia huwa siri hii wengi hufa nayo mioyoni, katu hawamdokezei mtu mwingine kirahisi.

Unapokuwa unatumia rasilimali za watu wengine kukuingizia pesa zaidi ni sawa na kuwatumikisha watu wengine bila ya wao wenyewe kujua kama unawatumikisha ilimradi tu unatumia akili. Wakati wa utumwa wajanja (Mabwana) waliwatumia watumwa kama mitaji, lakini leo hii unaweza kuwatumikisha watu wengine kwa kutumia rasilimali na nguvu zao kwa akili bila ya kuwashurutisha.

Dhana ya kukopo haipo kwa mtu mmojammoja tu peke yake bali hata katika ngazi ya Nchi(Mataifa). Tatizo kubwa linalotuponza Mataifa maskini ya Afrika na kuonekana kila mara kutiwa kitanzi na mikopo tunayopokea Magharibi na Mashariki ni tatizo la matumizi ya mikopo hiyo. Kama tu ilivyo kwa mtu mmojammoja, Mataifa hayo nayo baada ya kuchukua mikopo, fedha hizo huwa haijulikani bayana zinakokwenda wala zinachofanyia ni nini.

Tena isitoshe hakuna ufuatiliaji wa nguvu na uwajibishwaji kwa wahusika kwa upotevu wa hizo fedha, hata kukiwa na uwajibishwaji kidogo wahusika hawalazimishwi kurudisha mali na pesa iliyopotea zaidi ya kufungwa miaka miwili, mitatu na wakitoka jela wanakwenda kutafuna pesa walizoiba kama kawaida.

Kachunguze Wamarekani na Wachina mikopo ndiyo iliyowafikisha pale walipo leo baada ya kuitumia kwa nidhamu katika miradi yenye tija. Badala ya sisi kuanza kulumbana eti ikiwa tukope au tusikope, mimi nafikiri ulikuwa ni muda muafaka kujiuliza tutumie mbinu na mikakati ipi kudhibiti mianya ya wizi wa fedha tutakazokopa ili zisipotee kirahisi, zizalishe na mwishowe zirejeshwe kule zilikokopwa.

Kama tunakopesheka na fursa ya kukopa tunayo kwanini tulaze damu wakati mzunguko wa fedha ndani ni kidogo kiasi hicho?

Tukiachana na hayo ya deni la Taifa, mimi napenda zaidi kudili na mtu mmojammoja katika suala hili. Kwanza ikiwa kama wewe ni mjasiriamali mdogo, mwaka 2022 funguka kabisa, toka nje ya ‘miboksi’ uliyojilundikia miaka yote ! Tambua kuwa kwa mtaji wako mwenyewe kidogo biashara haitaweza kupiga hatua yeyote ile ya maana. Unahitaji rasilimali kubwa zaidi.

Kitu ninachoshauri hapa  si mtu akimbilie benki au taasisi kubwa kubwa za kifedha kiholela tu hapana, hawatakukopesha kirahisi hivyo. Hebu kaa chini kwanza kisha jiulize swali hili, “JE, HIVI MIMI NINAKOPESHEKA”

Mtu kukopesheka haimaanishi kuwa wewe unamiliki sijui nyumba au mali isiyohamishika hapana, Kukopesheka watu huangalia kwanza UAMINIFU WAKO na hiki ndicho chanzo cha ule usemi kwamba, UAMINIFU NI MTAJI.

Siku zote mimi huwa nasema kwamba ili mtu kujenga hali ya kukopesheka, anzia katika ngazi ya chini kabisa, usipende shortcut. Unaanzia wapi sasa? Ukiona huwezi hata kumkopa jirani yako shilingi elfu mbili upatapo tatizo dogo na ujue pia utapata shida sana kujaribu kukopa kwenye kikundi cha VICOBA au hata vile vya upatu wa kienyeji -michezo. Kuaminika kunaanzia huko. Na usipoaminika pia hukopesheki popote.

Ikiwa bado hujajijengea uwezo wa kukopesheka nakushauri usisubiri anza hata kesho kwa kujiunga na mikopo ya chini kabisa ya vikundi vidogovidogo, vicoba nk. bila kujali utakopa kiasi gani cha fedha kwa kuanzia lengo lako likiwa ni kujenga kwanza uwezo wa kukopesheka na tabia ya kujiwekea akiba. Wakati huo lenga kukopa katika taasisi kubwa zaidi au benki kadiri muda unavyokwenda na uwezo wako wa kukopesheka unavyoongezeka.

Mara tu utakapofanikiwa kukopa benki au taasisi kubwa ya kifedha mara moja, endelea kudumisha hali yako nzuri ya kukopesheka na uaminifu bila kujali kiwango cha mkopo unachopata kama ni kikubwa au kidogo. Kidogokidogo utaanza kuona mtaji siyo tatizo kubwa tena kwako kwa kuwa unao uwezo sasa wa kuupata unapouhitaji. Lakini hali hii ni lazima iambatane na mtu kujifunza siku zote elimu ya kifedha hasa matumizi mazuri, kujiwekea akiba na kuwekeza katika bishara zenye faida.

HITIMISHO

Siri ya mikopo ipo kwenye matumizi yake, Ikiwa kwa namna yeyote ile utashawishika kutumia pesa za mkopo nje ya lengo mahsusi la mkopo wenyewe, kataa kabisa, ni bora ukaurejesha mkopo mzima mzima kama ulivyo bila ya kuufanyia chochote huku ukibakia na deni la riba peke yake kuliko kuufanyia vitu tofauti na vile ulivyoombea.

Waliofaulu na mikopo mara nyingi huungana na wale waliofeli na mikopo kuwaogopesha wale wasiojaribu hata siku moja kukopa kwa kuwaaminisha  kwamba mikopo ni kitu hatari sana wanachostahili wajanja wachache tu, badala yake wangeliwapa somo ni kwa namna gani wanaweza wakakopa bila ya kuhatarisha rasilimali zao nyingine kwa kuwa wote waliofeli na waliofaulu wanao uzoefu kwenye kukopa. Usiogope kukopa bali ogopa majaribu ya kutafuna fedha za mkopo.

……………………………………

Niemeongeza muda kidogo kwa ajili ya OFFA ya vitabu vyote 5 vya SELF HELP BOOKS TZ na Michanganuo ya Biashara, mwisho utakuwa ni tarehe 10 January 2022

Pia Group letu la Watsap, MASTERMIND GROUP-2022 bado kidogo tufunge kuunganisha watu na kuanza masomo na semina rasmi. 

Ukihitaji Vitabu tu na Michanganuo lipa sh. Elfu 10 kupitia 0765553030 au 0712202244 Peter Augustino, kisha tuma neno “NATAKA OFFA YA VITABU TU”

Na ukihitaji na kuungwa na kwenye group tuma neno “NATAKA OFFA YA VITABU NA GROUP”

 

Soma Hapa Baadhi ya Meseji za Shuhuda za Waliojipatia OFFA Hii

 


SOMA PIA NA HIZI;

1. Je, Mtanzania unakopesheka na Taasisi za fedha au Benki?

2. Kuendesha biashara bila mtaji wa kutosha ni sawa na kulima kwa jembe lisilokuwa na mpini

3. Njia 7 za kupata Mtaji wa biashara unayoipenda

0 Response to "SIRI YA MIKOPO NA CHANZO CHA WATANZANIA KUOGOPA MNO KUKOPA"

Post a Comment