NJIA 7 ZA KUPATA MTAJI WA BIASHARA UNAYOIPENDA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NJIA 7 ZA KUPATA MTAJI WA BIASHARA UNAYOIPENDA

Biashara mpya au iliyokwishaanzishwa, zote zinahitaji mitaji ili ziweze kukua. Mtaji unaweza ukawa ni fedha, au rasilimali nyingine yeyote inayowekezwa katika biashara. Upatikanaji wa mtaji ni moja ya mambo yanayokwamisha biashara nyingi na ni changamoto kubwa kwa wale wanaotaka kuingia katika biashra mpya.

Kabla haujaamua ni wapi utapata mtaji, kwanza fanya  tathmini ya mahitaji yote ya  fedha  na rasilimali zitakazohitajika katika  kuanzisha au kuendesha biashara husika. Zoezi hili mara nyingi hufanywa wakati unapotengeneza Mchanganuo wa biashara.

Vyanzo vya mtaji.
Kuna njia nyingi  ambazo mtu anaweza kuzitumia  kupata mtaji kwa ajili ya biashara, zifuatazo ni baadhi ya zile ambazo hutumiwa mara kwa mara;

1. Akiba yako mwenyewe; na hii unaweza ukaipata bada ya kufanya kazi ya ajira, kuuza mali zako unazomiliki mfano nyumba gari, shamba, ngombe au mazao ya shambani, kupewa zawadi au ruzuku n.k. Pia unaweza  ukatumia faida inayotokana na biashara unayoifanya.

2. Kuingia ubia na watu/mtu mwingine ambaye atachangia kiasi   fulani cha mtaji, lakini  ukumbuke umiliki wa biashra utapungua kwani huwezi tena kumiliki kwa aslimia mia moja.

3. Mkopo kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki. Mkopo wa  aina hii  chukua kwa tahadhari, ingawa ni njia nzuri mara nyingi huweza kusababisha ndugu au jamaa mkagombana hata kuuana. Hakikisha unawekeana mkataba wa maandishi kuepuka utata baadaye. 
Njia hii inatumika na watu kwenye jamii katika sura mbalimbali mojawapo na maarufu sana ni upatu au Michezo. Michezo uzuri wake haina riba, lakini ubaya wake ni kule kutokuwa na uhakika na kuaminika, mtu anaweza akachukua wa kwanza na itakapofika zamu ya kuwachangia wenzake akaanza kupiga chenga. Na kwa kuwa hakuweka dhamana yeyote inakuwa vigumu kumlazimisha alipe.

4. Mkopo wa benki/taasisi za kifedha; Hii ndiyo njia inayotumiwa na watu wengi zaidi ukiacha ile ya akiba binafsi kutokana na  taratibu zake kuwa wazi na zisizoleta lawama. Ipo  mikopo ya muda mrefu na mfupi na yote  mkopaji hukatwa riba asilimia fulani.Tatizo kubwa kwenye mikopo ya aina hii ni wajasiriamali wengi hasa wale wadogo kukosa sifa za kukopa  hasa katika suala la dhamana.

5. Karadha; Badala ya kukopa fedha, unakopa zana za kufanyia kazi au vifaa mfano, mashine, gari, friji nk. umiliki wa vifaa hivi hubakia kuwa ni mali ya mkopeshaji, na wewe unayekopa humlipa gharama za kukodi, faida yake ni kwamba fedha ambazo ungenunulia vifaa hivyo unaweza  ukafanyia mambo mengine katika biashara na hivyo kufanya mtiririko wako wa fedha kuwa mzuri zaidi. 

6. Kuuza  madeni kama unadai wateja; unakubaliana na mtu au kampuni nyingine kudai madeni  badala yako.

7. Kukopa kutoka kwa wanao kuuzia malighafi au bidhaa, unaweza ukapokea bidhaa au malighafi baada ya kuuza ndipo ukawalipa fedha zao na hii huweza kuchukua muda wa mwezi mmoja miwili au muda wowote mtakaokuwa mmekubaliana.

1 Response to "NJIA 7 ZA KUPATA MTAJI WA BIASHARA UNAYOIPENDA"