WASOMALI KUFANIKIWA BIASHARA NA KUTAJIRIKA: MWENZAO ATOBOA SIRI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WASOMALI KUFANIKIWA BIASHARA NA KUTAJIRIKA: MWENZAO ATOBOA SIRI

Watanzania wenye asili ya kisomali, hata na wengine waishio nchini  kama wakimbizi, ni nadra sana kuwakuta wakiishi maisha magumu kiuchumi. Na si hapa Tanzania tu, bali kote duniani walipo watu hawa wa  jamii ya Kisomali kama vile huko Ulaya Marekani na hata Asia. Licha ya nchi yao kuwa na matatizo makubwa ya kliusalama kwa takriban zaidi ya miaka 20 sasa tangu kupinduliwa kwa dikteta Mohamed Siad Barre  kila wanakokimbilia wengi wao huwakuta wakimiliki biashara kubwakubwa.

Baada ya kufikiria  na kuamua kufanya ‘kautafiti’ kasikokuwa rasmi nimeshangazwa na majibu niliyokutana nayo. Kwanza nilianza kwa kuwadodosa waswahili wenzangu na wengi wao walinipa majibu kama vile, “ Wasomali wengi shughuli zao hazieleweki, ni wajanja sana na hata wakati mwingine hutumia njia haramu kama vile utekaji nyara , usafirishaji na uuzaji wa sila, madawa ya kulevya pamoja na uharamia wa baharini.” Mwingine, “Hawa watu bwana wana ushirikiano mkubwa sana, baadhi ya ndugu huchangiana pesa kusudi mmoja au wawili waende ulaya au nchi yeyote yenye neema, baadaye wanapokwenda kufanikiwa kiuchumi huwatumia ndugu waliobaki nyumbani mitaji na hiyo ndiyo siri yao kuu ya mafanikio”

Kuna waliodiriki hata kusema kuwa , “Wasomali bwana wanapofanya biashara zao huwa wana kawaida ya kuchinja wanyama kama mbuzi na kondoo, sijui kama ni kafara ama kitu gani kwani hata kama unaishi nao jirani hawawezi kukushirikisha. Hugawiana nyama wenyewe kwa wenyewe na wasomali wanaofahamiana, huenda ikawa matambiko hayo ndiyo chanzo cha wao kufanikiwa katika biashara zao”

Baada ya kupata maoni mengi toka kwa wazawa  wa hapa, niliamua nitende haki kama ilivyokuwa sheria ya maumbile kuwa usije ukamhukumu mtu kwa ushahidi wa upande mmoja pekee. Nikaanza na wasomali fulani wanaoishi jirani na ninapofanya shughuli zangu za kila siku.Huwa napenda kupiga nao stori mara nyingi ingawa wengi wao hawakijui Kiswahili barabara.

Kuna mmoja dereva wa malori makubwa   jina sijalishika huwa anapenda sana kunitania, ”wewe mswahili achana na biashara yako hii ya …………….(huitaja biashara yangu)twende zetu Sudani ya Kusini nikakuonyeshe biashara itakayokutajirisha harakaharaka” Na mimi huwa namtania “Wewe Msomali,  mimi siyo mjinga, nani wa kwenda kujiunga na ‘Al Shabaab’? Siwezi kwenda kujifunga mabomu mie niache” Hujaribu kunishawishi nitafune mirungi lakini huwa namwambia, “mimi siyo mbuzi, hebu ondoka hapa wala asije akatokea polisi huko nikaingia mtego usiokuwa wakwangu”.

Kuna kijana mwingine wa Kisomali jina lake Haruni, yeye ni kama vile hajui Kiswahili kabisa hutamka maneno  kwa shida mno, na inaonekana hapa hajakaa muda mrefu, baba yake anamiliki malori makubwa yaendayo Congo, na huniambia kuwa mama yake yupo Marekani na huko wanamiliki nyumba, na umri wake wapata kama miaka 40 hivi. Mwaka jana alisafiri kwenda Marekani  na baada ya miezi michache akarudi tena hapa  Tanzania akasema amekuja kumsaidia baba yake kwenye kampuni yake ya usafirishaji mizigo.

Naye hupenda sana kunitania huku akitumia lugha ya Kiswahili kibovukibovu  kilichochanganyikana na kiingereza. Leo alipofika akaanza kunitania, “Wewe kila siku nikija hapa unaonekana uko ‘sirias’ , hucheki  muda wote umekaa ndani umejiinamia , mimi mwenzio umewahi kuniona nimenuna hivyo muda wote?  toka nje uje ujumuike na watu, uzungumze, pesa hazitafutwi hivyo.” Na mimi sikuchelewa nikamjibu, “ Siyo wewe uliyeniambia siku za mwisho wa wiki ijumaa na Jumamosi hata mkeo hakusemeshi, ni siku zako za kutafakari? Sasa huko siyo kununa ni kitu gani? Hata na mimi nina muda sipendi kusemeshwa natafakari mambo yangu”.

Baada ya utani huo wa hapa na pale, nikajikuta namwambia, sichangamki kutokana na ukata, sina pesa, nawaza jinsi ya kupata pesa. Baada tu ya kutamka sentensi hiyo ndipo yakazuka mazungumzo yaliyokuja kuzaa  wazo lililonisukuma  kuandika makala hii. Aliniambia hivi;

 “Listen, I am forty now, my son, 18 he is in USA studying at  Goverment boarding school, I pay no single pen. I started Saving money when I was 14, after that I invested in business and now I am retired at 40” Akimaanisha kwamba kinachotakiwa  ili mtu uishi maisha mazuri, kwanza anza mapema kujiwekea akiba, kisha itumie akiba hiyo kuwekeza katika biashara hasa hasa ni vizuri zaidi ikiwa utawekeza katika nyumba na ardhi. Utajikuta ukistaafu mapema ukiwa bado kijana wa umri wa miaka 40.

Nilipata jibu kwa nini  Wasomali kama walivyokuwa wenzao Wayahudi  kila sehemu wanapokwenda duniani hufanikiwa kiuchumi na maisha yao hubadilika huku wenyeji walioko pale wakiendelea kuwakodolea macho huku wakisema maneno wasiyokuwa na ushahidi nayo. Kwa kufahamu changamoto walizokuwa nazo huko kwao, hakukaliki, hawana  jingine zaidi ya kuhakikisha fursa yeyote wanayoipata hawaichezei, hawarudii makosa, “wanaamua kuichoma meli  waliyokwenda nayo pale ili wasipate tena wazo la kurudi nyuma,  ni ama wafe au washinde vita, ‘fullstop’”

0 Response to "WASOMALI KUFANIKIWA BIASHARA NA KUTAJIRIKA: MWENZAO ATOBOA SIRI"

Post a Comment