USIDHARAU PESA HAKUNA PESA NDOGO | JIFUNZE UJASIRIAMALI

USIDHARAU PESA HAKUNA PESA NDOGO

Kama kuna jambo linalotugharimu maishani na kutufanya wengi wetu kuendelea kudidimia katika bahari ya umasikini, basi ni hili suala la kudharau pesa ndogondogo na kudhani hazina athari yeyote kubwa kiuchumi katika maisha yetu ya kila siku.

Ukweli huu kwa kweli mimi  binafsi ijapokuwa nilikuwa naujua lakini ilikuwa ni juju tu na kinadharia zaidi mpaka hivi leo asubuhi nilipokutana na tukio moja lililonifanya nibaki nikistaajabu na kujiuliza, “Hivi kweli kwa kipindi chote hiki nilichoishi hapa duniani kuna jambo ninalolifanya na linalonigharimu kiasi hiki pasipo mimi mwenyewe kushtuka hata chembe?” Tukio lenyewe tena wala si kubwa na la ajabu sana ni maisha ya kawaida kabisa ila tu cha ajabu hapo ni funzo lenyewe linalotokana na tukio hilo.

Ilikuwa leo asubuhi yapata kama saa mbili na nusu hivi, nikiwa katika eneo langu la biashara, nikamsikia jirani yangu tuliyepanga fremu eneo moja, yeye ni kinyozi akiniita kuniuliza tufanyeje, kwani umeme, ‘LUKU’ ulikuwa tayari  umekwisha. Alikuwa ameongozana na mteja aliyekuwa anataka kunyoa. Mteja huyo hakuwa mgeni machoni pangu, ni mfanya biashara maarufu sana wa kusafirisha mizigo kwenda mikoani. Sina haki ya kumtaja jina lake hapa kwani sijamuomba wala kumpa taarifa kuwa nitaandika makala itakayomhusu.

Tukiwa watatu tukijadili njia rahisi na ya haraka ya kupata umeme, kwenda kituo cha mafuta au kununua kwa njia ya simu, mara alifika dada mmoja,(simfahamu) akawa anamuulizia kinyozi mwingine mwenzake na huyu niliyekuwa najadili naye suala la LUKU.Kinyozi huyu mwingine yeye huwa shughuli zake zaidi siyo kunyoa bali ‘hudili’ zaidi na kusuka ‘Dread’ za akina mama. Alimjibu ya kwamba hajafika, dada akamuomba ampigie simu ili awahi kuja kwani alihitaji kusuka ‘dread’ kwa ajili ya shughuli itakayofanyika leo hii hii.

Yule kinyozi aliinua simu yake akaiweka sikioni kana kwamba anampigia yule kinyozi mwenzake kama yule dada alivyomuomba, huku akizunguka zunguka aliitoa simu sikioni na kuitazama kisha akatamka, “Huyu bwana hapatikani, naona bado atakuwa amelala, na leo kulivyokuwa na mawingu atafika hata saa nne hapa”

Masikini dada wa watu hakuwa na la ziada zaidi ya kujiondokea kimya kimya huku akiwa amejikatia tamaa. Sijui kama labda kulikuwa na msusi mwingine aliyekwenda kusuka kwake au aliamua aende zake kwenye shughuli bila kusuka dread, hakuna aliyefahamu tena hilo.

Baada tu ya kutupa kisogo yule ‘mdada’,  kinyozi alitamka, “Hata ningelimpigia kweli, akajua ni huyu dada, asingelikuja ng’o!, tunamjua vizuri huyu dada hatoi hela, akitoa sh. 1500/-  au sh. 2000/-  huondoka akilalamika kutwa. Bora nimemdanganya aondoke zake asituletee mikosi asubuhi asubuhi hii.”

Sasa hapa ndipo nilipopata somo lenyewe, baada tu ya yule kinyozi kumaliza kuzungumza yule tajiri wa malori ya mizigo yaendayo mikoani, sikutarajia kabisa alichokisema, kwanza alistushwa sana na kauli aliyokuwa ameitoa yule kinyozi, kisha akasema, “Hiyo elfu mbili siyo ndogo, unafikiri akitoa hivyo mara siku 30 au miezi miwili ni sh. ngapi?, kama unakubali kuipokea inamaana inatosha, huna sababu ya kuidharau, hamna hela ndogo”

Nilitafakari hali ya kiuchumi bwana yule aliyokuwa nayo nikajaribu kuilinganisha na shilingi elfu mbili anazosema siyo ndogo kwa kweli nikastaajabu sana, lakini nilipata jawabu ni kwa nini watu wengine hufanikiwa katika maswala ya pesa na wengine kubakia vilevile miaka nenda miaka rudi. Ni kutokana na kuthamini kila senti wanayoipata.


Huyu mfanyabiashara alishangazwa sana na kuona watu wa hali ya chini kabisa wakidharau shilingi elfu mbili mpaka kufikia hatua ya kumdanganya mteja ilimradi tu “amewaondolea nuksi asubuhi asubuhi ya kuwaletea elfu mbili”

0 Response to "USIDHARAU PESA HAKUNA PESA NDOGO"

Post a Comment