MWAKA 2020 ISHI KAMA TAI, USIKUBALI TENA KUISHI KAMA KUNGURU | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MWAKA 2020 ISHI KAMA TAI, USIKUBALI TENA KUISHI KAMA KUNGURU

NDEGE TAI
Kwanza kabisa ndugu mdau wa blogu hii napenda Kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuvusha salama mwaka 2019, ni imani yangu kama  unasoma hapa basi ni miongoni mwa waliovuka salama hata ikiwa kulikuwa na changamoto za hapa na pale. 

Kipekee pia nikushukuru wewe kwa kuwa nasi 2019 yote na nikuombe kwa mara nyingine tena kuendelea kuwa nasi 2020 kwani tunatarajia kuwa na mambo mzuri na muhimu zaidi hasa katika sekta ya Viwanda (The 2020 Tanzania Industrial Revolution is Possible, Play your Part ! )

Pamoja na kwamba kila mwaka inapofika mwezi January tumekuwa tukijiwekea Malengo lakini wengi wetu inakuuwa vigumu kuyatimiza yote kikamilifu ifikapo Desemba. Pamoja na hayo lakini malengo yatabakia kuwa ni kitu muhimu na kisichoweza kukwepeka kabisa katika maisha.

SOMA: Jinsi ya kupanga malengo ya biashara au maisha yanayotimizika kwa ufanisi

Watu wataendelea kujiwekea malengo iwe ni January, June au Oktoba lakini tu kitu kimoja kinachowatofautisha wale wanaofanikisha malengo yao kikamilifu na wale wasiofanikisha vizuri ni njia wanayotumia(approach) katika kuyatekeleza malengo yao. Nakumbuka mwaka jana muda sawa na huu baada ya kuwatakia wasomaji wa blogu hii heri ya Krismasi na Mwakampya niliandika makala ambayo nilisisitiza umhimu wa mtu kuishi kama Mbayuwayu(Mwaka 2019 ishi kama mbayuwayu) 

Mengi sana yamewahi kuzungumzwa kuhusiana na suala hili la kujiwekea malengo lakini mimi hapa leo ningependa kulizungumzia katika mtazamo wa ndege maarufu aitwaye Tai, jinsi anavyoendesha maisha yake kwa kuwa kiumbe anayesifika zaidi Duniani kutokana na umahiri wake wa kutimiza lengo lolote lile analojiwekea la kuwinda kwa ufanisi mkubwa.

TUNAJIFUNZA MBINU ZIPI KUTOKA NA TABIA ZA NDEGE HUYU TAI?

Pamoja na nguvu na uwezo mkubwa aliokuwa nao Tai wa kuona na kuruka juu angani lakini anazo pia mbinu za ziada anazozitumia katika kutekeleza malengo yake wakati wa mawindo. Mbiu hizo baadhi nitazitaja hapa chini;

(1) Tai haishi kwa hamasa wala mihemko bali yeye hujijengea mazoea mazuri tokea utotoni akiwa kinda.
Tofauti na walivyo ndege wengine kama Kunguru ambao ni mpaka pale wanapoona mzoga ndipo hupata hamasa na kuanza kushangilia kwa kuitana, Tai yeye tayari anajua kabisa wajibu wake kila siku ni kuwinda kitoweo hai siyo mizoga. Tai wanaanza kujifunza kutoka kwa mama zao namna ya kuwinda na kuruka juu angani wakiwa na wiki 10 – 12 na baadae kuishi maisha yao yote katika mazoea hayo waliyofunzwa.

SOMA: Njia 10 za kuhamasika na kuendelea kubakia na hamasa hiyo kwa muda mrefu ujao.

Kwa upande wetu sisi Binadamu huwa tunafanya makosa makubwa sana tunapojikuta tukihusudu sana HAMASA kama njia kuu ya kupata mafaniko na kusahau kujijengea MAZOEA ambayo ndiyo hasa kiini cha mafanikio ya watu wengi unaowaona wamefanikiwa.

Unapojijengea mazoea ya kufanya jambo fulani, jambo hilo hunasa katika akili yako ya ndani. Jambo unalolifanya kama mazoea kila siku huwezi kuacha kulifanya hata siku moja, lakini lile unalolifanya kwa hamasa ya muda mfupi, siku ukija kuamka huna hamasa hutaweza kulifanya. Si kama nasema hamasa(mhemko) ni kitu kibaya hapana, bali iambatane na  kujijengea tabia ya kutenda jambo kidogokidogo kila siku.

Mfano mzuri sana ni ni wale watu wanaofanya mazoezi ya viungo maarufu kama watu wa ‘gym’. Watu hawa huwa hawaoni kama ni kazi ngumu hata kidogo kuhudhuria gym kama ilivyo kwa watu wengine wa kawaida wasiokuwa na mazoea hayo kutokana na mazoea waliyokwishajijengea taratibu kwa muda mrefu. Kwa yule anayekwenda gym siku mojamoja kutokana tu na pengine amehamasika baada ya kumuona baunsa aliyetuna kifua akadhani na yeye anaweza akawa hivyo siku hiyohiyo, mara hamasa hiyo itakapopoa na yeye unakuwa ndiyo mwisho wake wa kuonekana gym.

SOMA: Je wajua siri nyingi za mafanikio zimejificha kwenye mambo haya 4 madogomadogo?

(2) Tai hawana wivu wa kijinga
Ukifanikiwa kuwaona Tai wadogo wanapokuwa wakijifunza kuruka na kuwinda unaweza kucheka kwa jinsi wanavyofanya makosa. Huanza kwa kuruka kidogokidogo kwenye miti ya karibukaribu huku wakiwatazama mama zao vile wanavyoruka na kuwinda wakijua kabisa kwamba kwao hakuna maisha bila ya kujua kuruka juu na kuwinda.

Tabia hii ya ndege Tai kujifunza kwa weledi na umakini mkubwa haiwaruhusu kabisa kuwa na kitu kinachoitwa WIVU WA KIJINGA, wala tabia nyinginezo za wizi na kunyanganyana mizoga kama wafanyavyo kunguru kwa kuwa kila mmoja  anakuwa na stadi zinazomwezesha kujitafutia chakula mwenyewe.

Na sisi binadamu yafaa sana tuige tabia hii ya tai ya kujifunza kwa bidii kutoka kwa wale waliofanikiwa pamoja na wale waliotuzunguka, ni njia zipi rahisi wanazozitumia mpaka wanafanikisha mambo yao kwa ufanisi na wala siyo kuanza kuwaonea vijicho na husuda au kutafuta mbinu chafu za kuwashusha au kuwaangamiza. Wivu ni mbaya sana kwani unazuia kabisa mtu kujifunza.

(3) Uwezo wa kuona lengo lake kabla(VISION)
Macho yenye nguvu ya Tai(Ana uwezo mara 8 zaidi ya ule wa binadamu) humwezesha kuona lengo (Kile anachotaka kuwinda) mfano Sungura aliyeko umbali wa maili 2 kutoka alipo yeye kabla hata ya sungura mwenyewe kushtuka kama ameonwa.

SOMA: Ingawa mipango si matumizi lakini haiepukiki kwenye maisha na biashara.

Binadamu na sisi tunapaswa kujijenga uwezo wa kuyaona maisha yetu miezi/miaka kadhaa ijayo mbele(na haya ndiyo malengo yenyewe). Ingawa ni kweli kuna mambo hutokea yenyewe tu bila ya kuyapanga lakini mengi ni yale  ambayo tunakuwa tumechagua wenyewe yawe jinsi yanavyotokea. Mbinu hii inamwezesha mtu kubadilisha njia anazotumia kuyafikia malengo yake kulingana na umbali au mazingira mengine yeyote yale atakayokutana nayo njiani kabla ya kulifikia lengo lenyewe, sawa tu na Tai afanyavyo, mfano kupunguza kasi, kushuka kidogo, kupanda kidogo, ilimradi tu aweze “kutarget” kitoweo chake kwa usahihi.

(4)Tai huwa haangalii fursa moja tu.
 Tai chakula chake kikubwa ni samaki, lakini usije ukafikiri anaweza kufa njaa ikiwa atakosa kabisa samaki hapana. Tai anakula pia wanyama wengine kama vile, sungura, watoto wa nguruwe mwitu, ndege wengine, nyoka, kobe, nguchiro, vindama vya mbuzi, vicheche na akizidiwa sana anao uwezo hata wa kuwabeba watoto wa binadamu.

SOMA: Fursa za mafanikio kamwe hazitakaa ziishe lakini pia hazichumwi mtini kama embe.

Maisha yanatakiwa mtu ubadilike kulingana na mazingira uliyopo. Ijapokuwa malengo yako unayajua lakini ni lazima katika mapambano ya kuyafikia utumie stratejia  mbalimbali zinazoendana na mazingira yale uliyopo. Lengo la Tai ni kujipatia mlo lakini si lazima atumie samaki tu peke yake, halikadhalika na wewe inawezekana unayo malengo ya kupata kiasi fulani cha pesa, si lazima uuze mchicha tu uliozoea kuuza ndippo upate kiasi hicho cha pesa, ukiona hata inawezekana kwa kuuza kahawa ukapata hicho kiasi, basi wewe nenda kauze kahawa ili mwisho wa siku lengo lako liweze kutimia lakini si kubadilisha gia angani kwa kubadilisha au kuyaacha  malengo yako kirahisirahisi kabla hujayatimiza na kuweka mengine kabla ya muda kutimia.

Je na wewe 2020 Ungependelea uishi kama ndege yupi? Tai au Kunguru? Binafsi jibu langu nitakupa siku nyingine.

Asante sana na tukutane tena wakati mwingine

Mwanaviwanda/Industrialist
Peter Augustino Tarimo


The 2020 Tanzania Industrial Revolution is Possible, Play your Part !


..................................................................................................


1.     Mwaka 2020 njia  za kupata Vitabu na huduma zetu zote zimerahisishwa mara dufu baada ya maboresho ya hali ya juuu;

2.     Kujipatia vitabu vya karatasi wasiliana nasi au fika BRIGHT BOOKS & STATIONERY,  MBEZI(Kibanda cha mkaa). Kwa softcopy lipia kwa namba, 0765553030 au 0712202244, na utatumiwa ndani ya dk.5 tu

3.     KITABU CHA DUKA LA REJAREJA 2020 KIMEONGEZEWA MAMBO MENGI MAZURI, HEBU YACHEKI KWA KUBONYEZA JALADA HAPO CHINI;



KITABU CHA DUKA LA REJAREJA



1.     UNAWEZA PIA KUFAHAMU ZAIDI KUHUSU KITABU CHA MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI KWA KUBOFYA JALADA HAPA CHINI;

KITABU CHA MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI


KUPATA MAELEZO YA KINA KUHUSU KITABU CHA MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA BONYEZA JALADA HAPO CHINI;

KITABU: MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYPENDA KUITOA


0 Response to "MWAKA 2020 ISHI KAMA TAI, USIKUBALI TENA KUISHI KAMA KUNGURU"

Post a Comment