INGAWA MIPANGO SI MATUMIZI LAKINI HAIEPUKIKI KWENYE MAISHA NA BIASHARA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

INGAWA MIPANGO SI MATUMIZI LAKINI HAIEPUKIKI KWENYE MAISHA NA BIASHARA


Binafsi napenda kuzungumzia vitu kutokana na uzoefu wangu mwenyewe na hasa katika mambo ninayoandika katika blogu hii ya jifunzeujasiriamali. Katika kampeni tunazoanzisha hapa, tangu mwaka jana nimekuwa nikitoa taarifa zake kwa wale wanaofuatilia hatua kwa hatua kwa kadiri mimi mwenyewe ninavyotekeleza kampeni hizo kwa upande wangu huku nikiwasihi pia wasomaji nao kupima mwenendo wa uteelezaji kwa upande wao.

Siyo lazima kila mmoja alingane na mwenzake katika kiwango cha utimizaji wa malengo lakini angalao kila mtu anapaswa kujitathmini ikiwa anapiga hatua ama la. Siku chache kabla sijatoa makala ya mwisho katika blogu hii niliandika makala ya kuwakumbusha wadau wote wa blogu hii kwamba, Ni robo ya mwaka sasa, je malengo yao waliyojiwekea Januari yalikuwa katika mstari sahihi kama walivyokusudia au walikuwa tayari wameshayaacha na kushika mambo mengine tofauti?

SOMA: Salamu zangu 2018 kukutakia heri na mafanikio ya kweli.

Nakiri kweli kwamba baada ya hapo, ghafla sikuonekana tena katika blogu wala mitandao mingine ya kijamii niliyokuwa nimezoea kuonekana kila mara kinyume kabisa na malengo yangu niliyokuwa nimejiwekea Januari. Kwa waliokuwa wamesoma ujumbe wangu huo wa mwisho bila shaka walistaajabu kuona  “Mhubiri anashindwa kuyaishi yale anayohubiri”,  Kama anayoandika ni ya kweli mbona sasa yeye hayatimizi, ona sasa tulimwambia mipango siyo matumizi, anakataa,

Dhamira yangu kuu mimi na blogu hii kwa ujumla mwaka huu ilikuwa ni kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya Mzunguko chanya wa fedha ndiyonjia bora zaidi ya kutimiza malengo yako mwaka 2018, na moja kati ya malengo madogomadogo tuliyojiwekea ni kuhakikisha kila mwezi tunajadili mchanganuo mmoja bunifu ndani ya group la wasap la MICHANGANUO ONLINE pamoja na mada mbalimbali kuhusiana na mzunguko wa fedha katika biashara zetu na mifukoni pia kila siku.

Ukiniuliza vipi malengo hayo kama ninayatimiza nitakujibu ndiyo, japo siwezi kukuambia kama nayatimiza kwa asilimia mia moja. Na hii iko hivyo kila mahali duniani, kila taasisi na kila mtu, hata serikali zenyewe haziwezi zikatimiza malengo au mipango zinayojiwekea “exactly” kama zilivyoipanga. Kwa mfano mimi mwenyewe binafsi majuzi katika kampeni yetu hii niliugua kiasi sikuweza kutimiza ipasavyo majukumu yangu yote ya kila siku na hio likasababisha na shughuli zangu kwenye mitandao ya kijamii kusita kwa muda pia.

SOMA: Punde kabla hujakata tamaa ya maisha hebu soma hapa kwanza.

Huwezi kuandika wala kufikiria vizuri ili hali unaumwa na kama ujuavyo shughuli zinazohusiana na maudhui kukasimu kwa mtu ghafla ni vigumu kama hukuwa umefanya maandalizi ya kutosha, hata hivyo nashukuru kwenye group letu la MICHANGANUO ONLINE bado kuna wadau ambao tayari walikuwa wameshaanza kutoa michango yao kuhusiana na mada mbalimbali hasa ya ufugaji wa kuku kwa kweli nawashukuru walikuwa wanafanya kazi kubwa kuendelea kuchangamsha group lisisinzie. 

Hili linanikumbusha siyo mimi tu na hata wewe pia kama ulikuwa hujafahamu  umuhimu wa kufanya kazi kama timu, basi ujue umuhimu huo upo na ni mkubwa hasa ikiwa utataka kutengeneza mfumo ambao haukutegemei wewe kama wewe kuwepo pale eneo la tukio moja kwa moja ndipo mambo yaweze kwenda.

SOMA: Jifunze nguvu ya ushirika(mastermind group)

Binadamu tunaweka mipango, tunapanga malengo na hivyo ndivyo tumekuwa tukifanya karibu katika kila jambo tulifanyalo, jana nimemsikia mdhibiti mkuuu wa hesabu za serikali Profesa Musa Assad akizungumzia bungeni jinsi ambavyo wanafanya kazi kubwa kuhakikisha mipango inayopangwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano  inatimizwa na serikali, alitaja baadhi ya maeneo ambayo wahusika hawakuweza hata kutimiza mipango iliyowekwa kwa asilimia 50%.

Ni kweli inawezekana kunakuwa na uzembe mahala pengine lakini kwingine ni sababu tu ambazo zisingeliweza kuzuilika. Nimemsikia pia Raisi msaafu wa awamu ya nne Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho kikwete wakati akiwa na mwenzake Rais wa sasa Mh. Dokta John Pombe Magufuli wakati wa ufunguzi wa Taasisi yake ya Jakaya Kikwete Foundation.

Kikwete katika malengo ya taasisi yake nadhani ni manne aliyoyataja kuwa ni Afya hasa mama na mtoto, Kilimo vijana na kina mama, Mabadiliko ya hali ya nchi na Utawala bora alitamka bayana kwamba haiwezekani kutimiza kila lengo kwa wakati mmoja, na watakachokifanya ni kutimiza kidogokidogo wakianza kwanza na lengo la Afya ya mama na mtoto. Hapa Kikwete anaonyesha ni kwa jinsi gani kutekeleza mipango kunahitaji subira na malengo.

Ninachotaka kusema hapa tu ni kwamba, juu ya yote ingawa mipango tunayojiwekea maishani tunaweza tusiweze kuitekeleza kama tulivyojipangia lakini mipango kamwe haiwezi kuepukika katika shughuli zetu za kila siku hapa duniani. Ninaposema mipango namaanisha malengo, ni kitu kile kile hata ikiwa kuna tofauti kidogo.

Angalia ni sababu zipi zinazokwamisha usiweze kutekeleza mipango yako, je unaweza ukazirekebisha mara moja na kuendelea kusonga mbele? Vipi kama ni ugonjwa, umepona? Kama ni uzembe tu, umerekebisha haraka?. Baada ya kurekebisha kile kilichokukwamisha kwa muda kutekeleza mipango yako sasa ni wakati wa kuendeleza mapambano mpaka umefikia mwisho.

Kampeni yetu ya Mzunguko chanya wa fedha ndiyo njia bora ya kutimiza malengo mwaka 2018 ipo palepale na wala haijatetereka licha ya misukosuko ya hapa na pale, Leo tunaendelea na somo letu la “NAANDIKA HATUA KWA HATUA MCHANGANUO WA BIASHARA YA UFUGAJI WA KUKU WA NYAMA sehemu ya 4” ambayo tutaangalia hesabu au mpango wa fedha kwa undani kabisa.

SOMA: Naanza hatua kwa hatua kuandika mchanganuo wangu wa biashara ya ufugaji wa kuku wa nyama(BROILERS)

Michanganuo hii tunayoijadili katika hili group la watsapp ni ya kipekee, pamoja na kwamba unaweza ukaona ni ya kawaida tu kwa kuitaja lakini ndani yake ina ubunifu mkubwa wenye lengo la kumfanya anayeisoma kujijengea mawazo ya kijasiriamali yatakayomwezesha kuendesha biashara yake kwa ufanisi mkubwa zaidi na hivyo kusababisha mzunguko wake wa fedha kuwa chanya muda wote.

Ikiwa hutumii watsapp siyo tatizo kwani masomo haya yote pia huwa tunayatuma yote kwa njia ya email pamoja na kuyaweka katika blogu maalumu inayoweza kufikiwa na mtu aliyejiunga na GROUP hilo tu.

KARIBU SANA KWENYE GROUP LA MICHANGANUO ONLINE

WHATSAPP: 0765553030
SIMU:            0712202244

0 Response to "INGAWA MIPANGO SI MATUMIZI LAKINI HAIEPUKIKI KWENYE MAISHA NA BIASHARA"

Post a Comment