MSHINDANI WAKO KIBIASHARA ANAPOANZA KUKUHUJUMU BADALA YA KUSHINDANA KIHALALI UFANYE NINI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MSHINDANI WAKO KIBIASHARA ANAPOANZA KUKUHUJUMU BADALA YA KUSHINDANA KIHALALI UFANYE NINI?

MSHINDANI WAKO ANAPOGEUKA KUKUHUJUMU
Safu yetu ya USHAURI leo tumepata swali la msomaji mmoja kutoka kule Mkoani Mbeya na mimi kama kawaida nitaliweka swali hilo hapa kama lilivyotumwa bila kuongeza wala kupunguza chochote isipokuwa tu sitataja jina lake kamili kwani hajaniruhusu kufanya hivyo.


SWALI.
Kaka  pole  na kazi  naitwa  HY  ni mwalimu . Kwa sasa nipo mbeya nimeanzisha biashara  ya spare  za  pikipiki  yaani duka la spare  za pikipiki.  Ila ndani  ya Muda mfupi  mwalimu mwenzangu  kafungua biashara  hiyohiyo  mlango  wa pili  ndani ya jengo  hili hili.  Sasa yeye  amekua  na tabia  ya kuhonga mafundi  wangu  na kuwaweka kwake  hadi  sasa  mafundi watatu  wamehamia  kwake.  Na nimempata fundi  mwingine  ila nahisi  nae  ataondoka  maana  ni rafiki  na mafundi  walio  toka kwangu.  Naomba  ushauri  wako nifanye  nini  ili  niendelee???  Nakosa lugha  nzuri ya kueleza  shida yangu  ila  kwa kuwa wewe  ni mtaalamu  najua  utanielewa.


MAJIBU YA SWALI/USHAURI
Kwanza Pole sana ndugu yangu kwa mtihani huu unaokusibu katika biashara yako. Ingawa hapa nitakupa majibu ama ushauri juu ya namna ya kukabiliana na ushindani katika biashara kwa ujumla lakini kwa kesi yako kuna vitu nitaongezea kidogo kutokana na sababu kuwa huyu jamaa(mshindani wako) ambaye umesema ni mwalimu mwenzako anachokifanya siyo ushindani wa kawaida wa kibiashara uliozoeleka bali ni HUJUMA(sabotage).

Hujuma hizi amezificha nyuma ya mgongo wa ushindani na hujuma za namna hii wakati mwingine mtu anaweza hata akatumia mbinu za aina mbalimbali mfano kumwaga kinyesi cha binadamu mlangoni pa biashara yako  usiku kusudi tu ikifika asubuhi wateja wataharuki na kupaona kwenye biashara yako kama kituo cha polisi vile. Tukio la namna hii binafsi niliwahi kulishuhudia mahali ila kwa bahati nzuri mtuhumiwa alinaswa na kumtaja aliyemtuma ikagundulika kumbe alikuwa mshindani wake kibiashara. Sasa huwezi ukasema eti mtu wa namna hii anachokifanya ni ushindani wa kawaida wa kibiashara hata kidogo.


Kwanza kwenye hili la kuwahonga mafundi wako napenda tu nikutie moyo kwamba, hebu kuwa mvumilivu kwanza, hafiki mbali huyu, atahonga wangapi?  Je, wakifika 10 atawalipa nini? Na hata kama atakuwa akiwafukuza wakishakuwa wengi, si mwisho wa siku watamshitukia? Haki ni haki tu mwishowe wewe ndiye utakayeibuka kidedea na kila mteja kuwa upande wako. Kwanza wateja huwa wana tabia ya kusimama upande wa yule mwenye haki wakishagundua kuna mchezo mchafu kama huo. Atahonga mafundi lakini hataweza kamwe kuwahonga wateja, wewe jifunze tu mbinu za “kuwahonga” wateja kwani ndiyo kila kitu.

Akimhonga fundi wako au mfanyakazi na yeye akakubali wewe wala usiwe na hofu ingawa inaweza kukuuma sana kwani wateja wengine humfuata mtu kulingana na ujuzi alionao, afterall watafuta kazi ni wengi kuliko kazi zenyewe, wewe jipange tafuta mwingine na mwisho atagundua mbinu anayoitumia si endelevu ataachana nayo. Wewe cha kufanya ni ‘kustiki’ kudumu na mbinu nitakazokwenda kukushauri hapa chini ambazo ndizo zinazotumiwa duniani kote na makampuni yaliyobobea katika biashara za aina mbalimbali. Narudia tena, mbinu yake hii chafu itakuumiza kwa muda mfupi tu na kama malengo yako ni ya muda mrefu utashinda!

MBINU HALALI NA HALISI ZA KUKABILIANA NA USHINDANI MKALI KWENYE BIASHARA YAKO, SIYO HUJUMA LAKINI.

1.Fanya utafiti kujua Nguvu na Udhaifu wako na pia kwa upande wa washindani wako.

Njia halisi na halali mtu katika sekta yeyote ile ya biashara anazoweza akazitumia katika kukabiliana na ushindani mkali wa biashara na hatimaye kuibuka mshindi zinaanzia kwenye Utafiti wa biashara na soko lako kwa ujumla, pale unapoanza kulijua vizuri soko lako ni lipi pamoja na kuwasoma barabara Washindani wako wa moja kwa moja na hata wale wasiokuwa wa moja kwa moja kwamba wanafanya kitu gani, Nguvu na Udhaifu wao ni upi. Kisha na wewe pia unajichunguza Nguvu na Udhaifu wako upo katika vitu gani.


Kwa kifupi Nguvu ni yale mambo yote kwenye biashara unayoweza kuyafanya vizuri na kwa ukamilifu zaidi kuifanya iende mbele na Udhaifu ni vitu au masuala yote usiyoweza kuyafanya vizuri na ambayo yanaweza kuirudisha biashara yako nyuma. Hapa chini nitakuorodheshea mifano ya vitu hivi viwili, Nguvu na Udhaifu kwa ujumla ambavyo vinaweza kuwa katika biashara yeyote na wewe sasa utaangalia biashara yako hii ya vifaa vya ujenzi nguvu na udhaifu wake ni upi na kwa upande wa mpinzani wako pia Nguvu zake na Udhaifu upo wapi. Kila biashara ni lazima iwe na vyakwake.

NGUVU.(Strength)
·       Mtaji mkubwa wa kutosha.
·       Wafanyakazi walio na ujuzi
·       Uharaka wakati wa kutoa huduma.
·       Unafuu katika bei.
·       Huduma tofautitofauti kwa mteja.
·       Eneo zuri lenye watu wengi.
·       Thamani zaidi kwa mteja.
·       Kuwahi kufungua biashara mapema.
·       Kutoa zawadi kwa wateja.
·       Huduma ya usafiri wa bidhaa za wateja

Nguvu kwenye biashara vinaweza kuwa ni vitu vingi na unaweza ukataja hata elfu moja au zaidi ukipenda, itategemea ni katika mazingira yapi au ni aina gani ya biashara unayoifanya ilimradi tu kitu chenyewe ni chanya kinachoiongezea nguvu biashara yako ya kusonga mbele.

Udhaifu(Weakness)
·       Udhaifu unaweza kuwa ni kati ya vitu vyote tulivyotaja hapo juu kwenye Nguvu lakini kinyume chake mfano;
·       Mtaji kidogo.
·       Wafanyakazi wasio na ujuzi au wachache.
·       Kutoa huduma polepole mno.
·       Bei kubwa inayowakimbiza wateja.
·       Eneo baya
·       Kuchelewa kufungua
·       Huduma mbaya kwa wateja
·       Lugha mbovu
·       Mpangilio mbaya wa bidhaa
·       Kukosa uzoefu nk. na vile vitu vyote vinavyoweza kuizorotesha biashara.


Ufanyeje Utafiti kuvijua vitu hivi.
Uafiti wa biashara kama nilivyoelezea kwa kina sana katika Kitabu cha Michanganuo ya Biashara na Ujasirimali siyo kazi ngumu kuifanya  na wala huhitaji mtaalamu au kampuni ikufanyie kama biashara yako ni ndogo tu au ya kati. Wajasiriamali wa kawaida mitaani pasipo wala kujua huwa tunafanya utafiti kwenye biashara zetu kila mara.

Mfano mzuri ni dada mmoja anayefanya biashara ya kuuza mihogo ya kukaanga alinifuata siku moja na kutaka nimshauri, kwamba jirani na kwenye biashara yake kuna babu mmoja ambaye naye anafanya biahsra kama yak wake ya kuuza mihogo. Lakini jambo la ajabu alisema kwamba babu huyo kila siku anapoona tu hyu dada akimuuzia mteja macho humtoka pima utadhani mjusi kabanwa na mlango, huwa hatulii atazunguka mpaka kwenye kona moja ambayo anaweza kuona vizuri kabati la huyo dada kujua mihogo imeuzika kiasi gani.


Sasa huyu dada akawa anashangaa na kuhisi labda huyu babu ni mshirikina na vile vituko vyote labda huwa ndio njia za kumloga ili asiuze biashara idode. Jibu rahisi nililompa yule dada ni kuwa, wala huyu babu siyo mchawi hata kidogo ila kile anachofanya ndiyo mbinu yake ya kumtafiti mshindani wake na pengine hata masikini babu wa watu hajui kama anachokifanya kuwa ni utafiti. Hii spirit ya kuwatafiti washindani wetu huwa imepandikizwa katika akili zetu ni vile tu watu wengi hawajui kuitumia kwa faida, wanatafiti bila kuchukua hatua.

Mfano mwingine ni katika mapenzi, hivi ukigundua mpenzi wako ana mchepuko utafanya kitu gani kwanza kabisa kabla hujachukua hatua yeyote ile ya kuukomesha? Cha kwanza si utafiti kumjua huyo mwenzako yukoje, ana nguvu zipi na udhaifu wake upo wapi? Sasa biashara nayo ni hivyohivyo, halikadhalika na kwenye vita ni hivyo pia.

2.Tambua Siri yako ya Ushindi ni ipi(Competitive Advantage)
Siri yako ya Ushindi kwa maneno mengine, Faida yako ya kiushindani si kitu kingine bali unaangalia tu katika ile orodha ya Nguvu ulizopata pale juu, chagua ile unayoweza kuimudu zaidi na ambayo mshindani wako/washindani wako hawaiwezi kama wewe. Hapa ni lazima ufahamu kwanini mteja afanye biashara na wewe na kumuacha mshindani wako.Ukiweza kujibu swali hili tayari unakuwa umeshapata siri yako ya ushindani na utaitumia katika mikakati yako yote ya masoko    


Mfano labda wewe katika duka lako hilo la spea za pikipiki mtaji wako ni mkubwa kulinganisha na la mshindani wako. Sasa nguvu hiyo ya mtaji mkubwa unaweza kuitumia kikamilifu pamoja na yeye kuhangaika kukuibia mafundi.

Komaa na kuendelea kuleta spea tofautitofauti ambazo yeye hana uwezo wa kuzileta mwishowe utakuta hata mafundi wake wakirudi tena kwako kununua spea ambazo yeye hana. Japo wapo wateja watawafuata mafundi waliowazoea kule, lakini wengine pia hawatajali kigezo hicho wao shida yao kubwa ni upatikanaji wa spea bora kwa bei wanayotamani, na wewe sifa hizo unazo.

Fungua duka lako muda wote wa kazi kila siku hutakosa kuuza. Wakati yeye akihangaika kutafuta fedha za kuwalipa kundi la mafundi aliowanunua, wewe endelea kumpatia mafunzo huyo fundi wako mpya uliyemleta, mlipe stahili zake vyema isijekuwa labda wanarubuniwa kutokana na wewe kuwabana mno. Lakini pia hakikisha unaulinda mtaji wako kama mboni ya jicho lako kwani biashara bila mtaji haiwezi kusogea mbele.


Huyu mshindani wako alishagundua kuwa udhaifu wako mkubwa upo katika eneo hili la mafundi ndio maana akatumia mbinu hiyo sasa na wewe inabidi uonyeshe kuwa udhaifu huo unaweza kuukwepa kwa kutafuta na kushikilia nguvu nyingine unayoimudu zaidi.

3.Chagua Eneo lako unalolimudu zaidi(Niche)
Kipengele hiki hakitofautiani sana na kile kilichopita cha siri yako ya ushindi isipokuwa tu ni kwamba hiki ni kipana zaidi na unaangalia eneo kubwa katika biashara siyo kipengele kimoja. Tuchukulie mfano wa biashara nyingine ya kuuza vifaa vya ujenzi. Badala ya kuuza vifaa vyote vya ujenzi wewe unaamua kudili na vifaa vya aina moja tu au mbili mfano unasema mimi nitauza sementi tu au mabati tu au mimi nitauza vifaa vya umeme tu nk. Kuchagua eneo kutakufanya wewe ubobee au uwe mahiri na wateja watakutafuta wewe tu na kuwaacha washindani wako.

4. Tengeneza Ushirikiano.
Kuwa na mtandao na wafanyabiashara kama ya kwako lakini wasijekuwa ni washindani wako wa moja kwa moja. Kwa kesi hii ya dula la spea za pikipiki, unaweza kujenga ukaribu na watu kama mafundi. Ili kuwalinda wasirubuniwe kuwa mbunifu, tafiti kile kinachowavutia wahamie kwa huyo mpinzani wako, lazima kipo ila ikiwa utapata uhakika kuwa ni kweli anawarubuni kwa kuwahonga fedha nyingi wewe usijibu kwa kuwapandishia dau endelea tu kuvumilia kama nilivyokushauri pale mwanzoni.


Kama ni sababu zingine basi jitahidi na wewe kuzidumisha. Hakikisha hata kama na huyo fundi mwingine atarubuniwa dukani paendelee kuwa wazi na mtu atakayekuwa anaendelea kuuza spea  kama kawaida usifunge kwa kukosa fundi, mapato yako hayatokani na fundi tu bali pia na mauzo ya spea.

5.Tengeneza Mahusiano mazuri na Jamii inayokuzunguka.
Huu ni mkakati mzuri kwani utakujengea jina na wateja zaidi wataambizana kwa mdomo mtaa mzima kuwa unauza spea nzuri kwa bei wanayoimudu. Usionyeshe waziwazi chuki yako kwa huyo mshindani wala kutoa malalamiko kwa watu kiholela, waache wateja na wanajamii watagundua wenyewe

6. Dumisha chochote kilichokuwa na thamani na kuachana kabisa na vile vinavyokuletea hasara.
Vitu vyenye thamani ni mambo yote yale yanayowafanya wateja waje kununua. Mambo mengine yote unayoona hayana tija wala kumfanya mteja kuja kununua yatupilie mbali kabisa zikiwemo fikra za chuki kwa huyo mpinzani wako. Acha kufikiria kila mara jinsi utakavyolipa kisasi kwa kurudisha mabaya kwa huyo mshindani na badala yake jikite tu katika mbinu za kitaalamu za kukabiliana na ushindani huku ukiendelea kuwa mvumilivu. Nguvu hasi hazitakusaidia kitu na zaidi zitazidi tu kukudidimiza.
  
………………………………………………………

Swali hili la msomaji wetu wa Mbeya lingeweza kujibiwa kwa asilimia 100 kama angelisoma kitabu changu kiitwacho MAFANIKIO YA BIASHARA YA DUKA LAREJAREJA. Kwa mfano katika sura ya 2 ukurasa wa 41 ipo mada isemayo, “Tathmini siri yako ya Ushindi”, Katika ukurasa wa 41 ipo mada nyingine isemayo, “Mbinu za kuwa juu kushinda washindani wao” na Katika ukurasa wa 47 pia ipo mada, “Kushindana na Maduka makubwa” Mada zote hizi tatu hakuna zilichoacha kuhusiana na namna ya kudili na Ushindani kwenye biashara.



Kwa vitabu vingine mbalimbali katika lugha ya kiswahili tembelea Smart Books tz

Ikiwa unapenda kujifunza kuandika mpango/mchanganuo wa biashara yako kwa urahisi kabisa jiunge na programu yangu katika Wasap iitwayo Michanganuo Online ambapo tunajadili kila siku jinsi ya kuandaa michanganuo bunifu ya biashara zinazolipa hatua kwa hatua. Kiingilio ni sh. elfu 10 na tunakutumia pia masomo na kila kitu tulichojifunza katika kipindi cha mwaka wote wa 2018.Kujiunga tuma ujumbe wasap 0765553030 na ikiwa hutumii wasap tutakutumia masomo na vitabu kupitia email. Unaweza pia kupiga namba 0712202244



0 Response to "MSHINDANI WAKO KIBIASHARA ANAPOANZA KUKUHUJUMU BADALA YA KUSHINDANA KIHALALI UFANYE NINI?"

Post a Comment