UTAFITI WA SOKO LA BIASHARA YAKO/UPEMBUZI YAKINIFU -1 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

UTAFITI WA SOKO LA BIASHARA YAKO/UPEMBUZI YAKINIFU -1

Unapoanzisha biashara ama kutaka kuboresha biashara ya zamani, utafiti ni jambo la lazima endapo mtu utataka upate mafanikio, ingawaje ni jambo linalogharimu pesa na muda mwingi, lakini gharama hizo haziwezi kamwe kuzidi hasara ambayo mtu  unaweza akaipata endapo utapuuzia ama kukwepa jambo hili. 

Neno upembuzi yakinifu "feasibility study"  lina maana sawa na Utafiti isipokuwa upembuzi yakinifu lina maana pana zaidi. Kwa mfano unaposema utafiti wa masoko unamaanisha kipengele kimojawapo cha upembuzi yakinifu katika kipengele cha soko pekee. Vipo vipengele vingine kama vile, bidhaa/huduma, tekinolojia, fedha, na utawala.

Vilevile upembuzi yakinifu wapo watu wengine huuweka katika aina za michanganuo/mipango ya biashara ijapokuwa vitu hivi viwili vina tofauti kidogo kama tutakavyoona huko mbele.

Lengo  kuu la kufanya utafiti/upembuzi yakinifu ni kupata picha  halisi ya biashara itakavyokuwa siku za baadaye na hivyo  kwa kutathmini kila hatua utakayopitia  unaweza kubaini kama biashara  husika italipa au la,  na hivyo kukufanya  uamue kuendelea nayo au  kuiacha. Vile vile  kwa kubaini kabla  matatizo ambayo  yataweza   kuja  kujitokeza  mbele  ya safari, unaweza   ukapanga  mapema  mikakati ya  kukabiliana  nayo.

Utafiti/upembuzi yakinifu  hukupatia  taarifa  za   msingi  zinazohusiana  na wazo lako la biashara.  Yapo  mawazo mengi ya biashara, mengine yanafaa na mengine hayafai, kupata  wazo  fulani la biashara haimaanishi  kwamba litaleta mafanikio/faida. Sababu kubwa ya wajasiriamali wengi kuanguka  mara  waanzishapo biashara ni  kuwekeza fedha zao na muda  katika biashara  ambazo hawajazifanyia utafiti wa kina.

Umuhimu  mwingine wa kufanya utatifi wa biashara ni katika kuandaa Mpango ama Mchanganuo wa Biashara.  Kama ilivyoelezwa katika kitabu cha JIFUNZE MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI,  msingi mkuu wa mpango wa biashara  ni yale yale majibu unayoyapata kutoka katika utafiti wa biashara  na masoko/upembuzi yakinifu ulioufanya.

Tofauti yake tu ni kwamba; kwenye utafiti/upembuzi yakinifu, unaorodhesha  na kuainisha njia  mbalimbali za kufanya biashara,wakati kwenye  mchanganuo wa biashara  unaonyesha vitendo vinavyotakiwa kufanywa kusudi  wazo la biashara  lililopendekezwa liweze  kugeuzwa kuwa  biashara  halisi. Vilevile  tofauti nyingine  ni  kwamba utafiti/upembuzi ndio huanza kufanyika kwanza kabla mchanganuo haujatengenezwa na kutekelezwa

Wakati mwingine  utafiti wa biashara hufanywa na makampuni ya ushauri wa kibiashara, chagua kampuni yenye uzoefu na biashara unayotaka kuifanya. Pia ukumbuke kuwa, unapompa mtaalam afanye kazi hii haimaanishi na  wewe hautashiriki, hapana, kila hatua inabidi  uhusike, fahamu kila kitu kinachofanyika na wakati mwingine uhoji matokeo ya utafiti wenyewe.

Upembuzi yakinifu umegawanyika katika vipengele vikuu 3 vifuatavyo:-
1.  Ufafiti  wa soko na bidhaa/huduma unayotaka kuuza.
2.  Utafiti wa maswala ya kiufundi na Utawala.
3.  Utafiti wa maswala ya fedha.

Badala ya kutumia njia ya kitaalamu sana kufanya  utafiti, mfanyabiashara ndogo ndogo, asiyekuwa na utaalamu mkubwa  wala fedha za kutosha kuajiri kampuni ya utafiti anaweza akajibu maswali yafuatayo  na akawa ametimiza  lengo lake la kujua ikiwa biashara anayotaka kuifanya au kuipanua itamlipa  aendelee nayo  ama aachane nayo.

Majibu hayo  atayapata kwa kufanya utafiti usiokuwa rasmi kwa kuingia mitaani na kuuliza watu maswali mbalimbali, wanaweza wakawa wale wanaofanya  biashara kama ya kwake, wauzaji wa jumla, wauzaji wa rejareja, wataalam wa biashara, pamoja na kusoma machapisho mbalimbali yanayoelezea sekta anayotaka kuifanya. Maswali hayo yamepangwa kufuatanana na   mtiririko  wa vipengele vile vitano yaani maswali yanayohusu Bidhaa/Huduma, soko,  teknolojia/ufundi, maswala ya kiutawala /management  na  Maswala ya fedha.

SOKO.
·       Soko  lako ni lipi?
·       Walengwa wako ni kina nani?
·       Fahamu  tabia  za wateja wako ni zipi.
·       Wapo wateja wangapi?
·       Kuna changamoto gani zinazokabili soko hilo?
·       Ni gharama kiasi gani itakayotumika kulifikia soko  hilo?
·       Ni nani mshindani wako wa moja kwa moja?
·       Bidhaa  zako zinafanana au kutofautiana vipi na za washindani wako?
·       Ni nini siri yako kuu ya mauzo?
·       Je  washindani wako wana weza kukuiga kirahisi?
·       Washindani  wako wanachukuliaje ujio wako katika soko?
·       Ni nani washindani wako wasiokuwa wa moja kwa moja?

2 Responses to "UTAFITI WA SOKO LA BIASHARA YAKO/UPEMBUZI YAKINIFU -1"

  1. Asante sana kwa maarifa haya ambayo si rahisi kuyapata katika mfumo wetu wa elimu.
    mbarikiwe saana na msikate tamaa tunawafuatilia kwa ukaribu sana sana.
    hakika mnafanya kazi nzuri sana.

    ReplyDelete