Napenda kuanzisha biashara ila sina mtaji wala pesa za kununua vitabu kujiendeleza, nifanyeje? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

Napenda kuanzisha biashara ila sina mtaji wala pesa za kununua vitabu kujiendeleza, nifanyeje?

KITABU CHA MIPANGO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI
Katika kipengele chetu cha Ushauri leo kuna msomaji mmoja ameuliza swali, "Napenda kuanzisha biashara ila sina mtaji wala pesa za kununua vitabu kujiendeleza, nifanyeje?". Nami kama kawaida huwa napenda kuliweka swali kama lililvyoulizwa bila ya kubadilisha chochote hata spelling.Hii husaidia kutunza uhalisia wa swali lenyewe kwa msomaji.


Unajua katika mitandao hii ya kijamii kuna aina fulani ya uandishi unaotokana na matumizi ya simu za kisasa smartphone kwa mfano utakuta penye “Z” mara nyingi panawekwa ‘X’ kimakosa kutokana na ukaribu wa herufi hizo, lakini ndio imekuwa kama kawaida mtu ukikuta hivyo mara moja unatambua mwandishi alimaanisha ‘z’ na wala siyo ‘x’. Vilevile katika safu hii hatutaji jina la muulizaji swali pasipo ridhaa yake ndio maana tunaamua tu kuweka herufi yeyote kwenye nafasi ya jina.

Swali lake original aliuliza hivi;

mimi ningependa kkufanya biashara ila shida mtaji  pamoja na hayo hata psa ya kununua vitabu vya kujifunzia juu yaujasliamali sina nifanyeje. naomba ushauri

MAJIBU KWA SWALI HILO NI HAYA HAPA;

Hellow B , 
Kwanza nikushukuru sana kwa kufuatilia makala zangu na nimefurahi pia kusikia kuwa unapenda sana kuanzisha biashara ila tatizo ni mtaji na kukosa pesa za kununulia vitabu vya ujasiriamali kwa ajili ya kujifunza na kujiendeleza zaidi. Nikutie moyo kwani mpaka hapo ulipofikia ijapokuwa bado uwezo wako wa kuanzisha biashara ni mdogo, umepiga hatua kubwa tu kwa kuweza kusoma makala katika blogu yetu hii ya jifunzeujasiriamali.

Usijikune usipofikia kama ukweli huna fedha za kununulia vitabu zaidi, na inawezekana kuwa ni kweli hauna kwani umesema hata biashara haujaanza bado kutokana na kuwa mtaji huna. Huwezi ukanunua kitabu cha sh. Elfu 5 au hata elfu 10 wakati kipato hakiruhusu, ni lazima kwanza upiganie mahitaji yako yale ya msingi kama binadamu.


Mimi ningekushauri kama unapenda kuja kuanzisha biashara, endelea kwanza kusoma makala mbalimbali kwenye blogu yetu ya jifunzeujasiriamali pamoja na kusoma makala tunazokutumia kwa njia hii ya email, bado makala hizi zinaweza kuwa msaada mkubwa kwako kwani nyingi zinalenga kumjengea mjasiriamali mdogo uwezo wa kupata mtaji kwa njia za kawaida kabisa bila kukopa wala kumdhulumu mtu. Na habari njema ni kuwa makala hizo hulipi hata senti tano zaidi tu ya kulipia bundle katika simu yako ya mkononi au kompyuta unayotumia kusomea.

Ikiwa utakuwa ukifanyia kazi kwa vitendo yale yote utakayojifunza ndani ya makala hizo, taratibu utajenga uwezo wa kijasiriamali na kuanzisha biashara ndogo. Kidogokidogo biashara yako hiyo ndogo itakua na utajikuta mwenyewe tu ukihitaji kujifunza zaidi na wala hutajali gharama bali utanunua vitabu zaidi kwani utakuwa ndio wakati wake umefika.


Na kwa sababu sasa utakuwa ukiingiza kipato kidogo utaweza kugawa kipato hicho asilimia fulani kwa ajili ya kujiendeleza kimaarifa, ubongo pia unahitaji kuendelezwa na kulishwa sawa tu na kama ilivyokuwa kwa mwili wako au hata unavyozitunza nywele zako, kucha, kope, na viungo vyote vya mwili kwa ujumla ili viendelee kupendeza siku zote za maisha yako hapa duniani.

.... ..........................................................

Hilo ndilo jibu nililompatia msomaji mwenzetu huyu. Lakini kwa faida ya wasomaji wengine wote pia ningependa kuongezea hapo mambo machache kidogo kuhusiana na suala hili la usomaji vitabu hasa vitabu vya ujasiriamali, biashara na mafanikio kwa ujumla.


Mara nyingi  baadhi ya watu wanaponunua vitabu kutoka kwangu nikifanikiwa kuonana nao ana kwa ana huwa wananiuliza hivi, “Bwana Peter, hivi nikimaliza kusoma kitabu chako hiki chote ndio nitakuwa nimekuwa mjasiriamali kamili?” Huwa nacheka na kuwajibu,

hapana ujasiriamali ni mchakato usiokuwa na mwisho na kila unapomaliza hatua fulani mbele kuna hatua nyingine inayofuata cha msingi ni kujua kwanza ABC za Ujasiriamali kupitia kitabu kama hiki cha kwangu halafu mbele ya safari siyo lazima uendelee kujifunza kupitia vitabu peke yake, kuna njia nyingi za kujifunza ikiwemo njia ya UZOEFU kwa fani au tasnia uliyopo.”

Hata walioandika vitabu si kama kila kitu walipata kwenye vitabu hapana, vingine ni uzoefu wao  katika kile walichoandika.


USIWE MTUMWA WA VITABU!
Unaweza kunielewa vibaya lakini hii napenda sana kuitumia kwa sababu ni watu wengi mno hulalamika tokea wameanza kufuatilia vitabu hivi vya biashara na mafanikio miaka imekatika mingi na maktaba zao zimejaa lakini cha ajabu hamna hatua zozote walizopiga kiuchumi kama walivyotarajia. Kama uliwahi kusoma kitabu changu ninachotoa bure kisemacho, JINSI YA KUJIFUNZA ELIMU YAPESA NA MAFANIKIO KWA UFANISI” unaweza ukanielewa vizuri zaidi.


Vitendo ndio kila kitu, mafanikio ya kiti chochote hayatajali umejifunza kwa kiasi gani kama haujachukua hatua kutekeleza mchakato fulani, tuseme labda umejifunza jinsi ya kutengeneza sabuni za aina mbalimbali, ikiwa ujuzi huo utaufungia kichwani bila kuutia katika matendo, utaishia tu kumlalamikia mkufunzi aliyekufundisha kutengeneza sabuni huku ukidai kala pesa zako bure, kumbe kosa ni la kwako hukuchukua hatua za kufanya biashara ya kutengeneza sabuni.

WENGINE HUULIZA, “NITANUNUA VITABU VINGAPI ILI KUWA MJASIRIAMALI KAMILI NILIYEFANIKIWA?


Sikinzani hata kidogo na dhana ya kujifunza kila siku ila tu ninachosisitiza ni kwamba,

 “Usikimbilie kununua zana mpya wakati zile ulizokuwa nazo bado hujajua hata kuzitumia vizuri”

Ninashauri hivi, ikiwa uliwahi kununua vitabu fulani vya ujasiriamali, hakikisha angalao unavisoma vizuri na kujaribu kuweka katika vitendo haraka yale uliyojifunza humo kisha sasa ndipo uamue kununua vitabu vingine vipya.


Kuna walio tayari na uwezo wa kujifunza vitu vipya kila wakati, hawa sina shaka nao, lakini wapo ambao inachukua muda kujifunza mada moja au tuseme somo moja, ni vizuri wakajijengea uwezo taratibu kwa kujifunza material walizokuwa nazo kwanza huku wakiweka kipaumbele katika utekelezaji na wakanunua kozi au vitabu vingine hatua kwa hatua kusudi kuepuka hali ya kukata tamaa njiani baada ya kuona hawaelewi au kufanikiwa jinsi vile ambavyo wangependa wafanikiwe.


Kwa mfano hauwezi ukasomea kozi au somo la kupamba sherehe mbalimbali na keki za harusi wakati bado hujajifunza hata jinsi ya kupika keki zenyewe za harusi. Anza na mambo ya msingi kwanza halafu panda ngazi taratibu kwa vitendo ndipo utaweza kuona matokeo bora kabisa katika kila unachokifanya.

0 Response to "Napenda kuanzisha biashara ila sina mtaji wala pesa za kununua vitabu kujiendeleza, nifanyeje?"

Post a Comment