NI KITABU GANI HAUTAKISAHAU MAISHANI?: LEO NI SIKU YA VITABU DUNIANI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

NI KITABU GANI HAUTAKISAHAU MAISHANI?: LEO NI SIKU YA VITABU DUNIANI

Shaaban Robert

Ingawa Watanzania tunasifika kwa tabia ya uvivu wa kusoma vitabu Duniani, tangu miaka ya nyuma lakini tabia hiyo unapoilinganisha siku hizi na miaka iliyopita hali sasa imezidi kuwa mbaya. Angalao miaka kuanzia ya 90 kurudi nyuma watu walikuwa na muamko wa kusoma vitabu.

Pengine kudorora huko kwa usomaji wa vitabu kumetokana na ujio wa mtandao wa intaneti na simu za mikononi ambapo watu hutumia muda wao mwingi wa ziada katika vitu hivyo. Kwenye vitabu kuna maarifa mengi, waandishi kabla hawajaandika hufanya utafiti mwingi ndiyo maana hakuna mtu duniani anayeweza kuvibeza vitabu.


Zamani kulikuwa na vitabu vingi vizuri, siyo tu vilivyokuwa vikisomwa mashuleni kwa ajili ya mitihani, bali hata na vile vya riwaya vilivyolenga kutoa burudani na mafunzo kwa jamii. Mimi binafsi ukiniuliza ni kitabu gani siwezi kukisahau, ukweli ni kwamba vingi vilinisisimua lakini Vitabu vya akina Marehemu Ben R.Mtobwa, Elvis Musiba, Agoro Anduru na Shaaban Robert haviwezi kamwe kufutika akilini mwangu. 


Kwa upande wa shule ya msingi, kulikuwa na vitabu vya  kusoma kwa Kiswahili kama sikosei ni kuanzia  Darasa la tatu vilivyokuwa  na hadithi  za kusisimua kama vile hadidhi ya Sadiki na Sikiri, “Sikiri mimi masikini” “Hadithi ya Pazi” , “Kibanga ampiga Mkoloni”, “Ndoto ya Kimweri” na vinginevyo vingi.



Ukija sekondari kulikuwa na vitabu  vya kujifunza kiingereza vya British Councel  form one na two, kulikuwa na aina nyingi na tulikuwa tukiazima library ya shule baada ya kumaliza kusoma unarudisha, ukipoteza unalipishwa mwisho wa temu. Kitabu ninachokikumbuka sana  kilikuwa kinaitwa “Dear Jane” “Pele, kilichokuwa kikizungumzia soka” “Hawa the bus Driver” nk.. 

Vitabu vingine ni vile vya  Literature au fasihi, form three na four. Kulikuwa na vitabu vya kusisimua kama vile “Is it Possible”, “The River Beteen” , “Three Suitors One Husband”  Things Fall Apart” “No longer At Easy” “Song of Lawino” “Mashairi ya Saadan Kandoro” “Shida” “Rosa Mystika” “Ngoswe Penzi Kitovu cha Uzembe”  Kusadikika" "KULI" cha Adam Shafi Adam na vinginevyo vingi.
 
Shafi Adam Shafi

Umahiri wa watunzi vitabu wa zamani ni wa hali ya juu na utalithibitisha hilo kwa kuona watu wakikumbuka vitabu vyao kwa majina na wahusika, mfano ni kama vile vitabu vya Mtobwa na Musiba mpaka kesho utakuta watu wakikutajia wahusika wakuu katika kazi zao kwa kuwataja Joram Kiango kwa upande wa Mtobwa na Willy Gamba kwa upande wa Musiba. Vilikuwa kama filamu vile wakati ukivisoma. Pia vilikuwa na uhalisia wa maisha ya kawaida ya watu mfano ni vitabu vya riwaya hasa vile vya kiingereza vya mtunzi Agoro Anduru kama “TEMTATION” Hakika unapokuwa ukikisoma unaguswa kama kwamba matukio yale ni ya ukweli. 

Vitabu vingine vizuri vya kukumbukwa ni vya waandishi, Mohamed Said Abdullah(Duniani kuna watu), Profesa Chachage S. Chachage(Makuwadi wa soko huria) Faraji Katalambula, Beka Mfaume(TUFANI), Vuta Nkuvute(Shafi Adam Shafi), Amri Bawj, Hemed Kimwanga(Kazikwa yu hai) pamoja, John Simbamwene na wengineo wengi.

Kuna haja ya vitabu hivi kurudishwa tena hata kwa njia ya mtandao, kwa mfano ungewekwa utaratibu wa kuviweka kwenye intaneti kila mtu akawa na uwezekano wa kuvisoma, hata kama ikiwa ni kwa kuvilipia.

Juu ya yote ni kitabu cha Think and Grow Rich, kitabu hiki ndiyo kitabu maarufu zaidi duniani na kilichowahi kusomwa na watu wengi zidi. Upekee wa kitabu hiki unatokana na sababu kwamba kinamfundisha mtu namna ya kuondokana na umasikini. 

Kwa kweli mimi binafsi nasema hiki ndiyo kitabu cha pili muhimu zaidi kwangu na ninachokipenda baada ya msahafu wa dini yangu. Mapenzi yangu katika kitabu hiki yalinifanya kuzipa baadhi ya kazi zangu hasa kitabu kikubwa cha Michanganuo ya Biashara na Ujasiriamali pamoja na Tovuti na Blogu hii jina, "KUELEKEAUTAJIRI" 

Ukisoma Think and Grow Rich katika  kila mwanzo wa sura waliweka sentesi hii, "The .....step to Riches" Kwa mfano sura ya pili, "Hatua ya kwanza kuelekeautajiri" hivyo hivyo na sura zote zinazofuta. Kwa hiyo na sisi tuliamua kutumia neno hili, "kuelekeautajiri" kama "kauli mbiu yetu"(slogan).

Tulitumia jina hilo "KUELEKEAUTAJIRI" kwa nia njema tu ya kuwahamasisha watu katika kupigana na umasikini lakini cha kusikitisha ni kwamba, baadhi ya wasomaji walituelewa vibaya, kila walipokutana na jina hili kwenye intaneti au vitabu walihisi labda kuelekeautajiri ni miongoni mwa taasisi au vyama  vyenye utata vinavyopingwa na jamii.

Tuligundua hilo baada ya baadhi ya wasomaji kutupigia simu mara kwa mara na kutuuliza kama sisi ni vyama hivyo au kama tunaweza kuwaunganisha navyo.,

Majibu yetu kila mara yamekuwa kuwaelimisha kwamba hatuhusiani kabisa na vyama au taasisi za namna hiyo na sisi lengo letu ni kuelimisha wafanyabiashara hasa wale wadogowadogo mbinu mbalimbali za kijasiriamali katika kukuza biashara zao. Lakini pamoja na kuwaelimisha hivyo bado baadhi ya watu wakaendelea kupiga simu wakiwa na wasiwasi labda tunawadanganya.

Hali hii imetulazimu kubadilisha kabisa(rebranding) Majina ya Kitabu chetu cha Michanganuo na Ujasiriamali, tovuti na blogu hii unayosoma sasa hivi; Majina hayo sasa yatakuwa kama ifuatavyo;

Kitabu 'KUELEKEAUTAJIRI' sasakitaitwa "MICHANGANUO YA BIASHARA NA UJASIRIAMALI"

Tovuti na Blogu hii zilizokuwa zikiitwa Kuelekeautajiri.com na kuelekeautajiri.blogspot.com sasa zitaitwa jifunzeujasiriamali.com na jifunzeujasiriamali.blogspot.com.

Mabadiliko hayo ni katika jalada na majina tu. yaliyokuwemo ndani hayajabadilika.

Marejeo: Picha zilizotumika katika makala hii ni kwa hisani ya blogu na tovuti zifuatazo, 

  1. Hapa kwetu(hapakwetu.blogspot.com)
  2. Maisha na Mafanikio(ruhuwiko.blogspot.com)
  3. Jamii forum
  4. Jamvi la simulizi za kusisimua(facebook)
  5. Kitoto(kitoto.wordpress.com na
  6. Michuzi Blog.



0 Response to "NI KITABU GANI HAUTAKISAHAU MAISHANI?: LEO NI SIKU YA VITABU DUNIANI"

Post a Comment