KIJANA WA UMRI MDOGO ANAWEZA KUANZISHA BIASHARA KUBWA IKAFANIKIWA? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KIJANA WA UMRI MDOGO ANAWEZA KUANZISHA BIASHARA KUBWA IKAFANIKIWA?

KIJANA MDOGO TAJIRRI BIILIONEA
Tunaendelea na maswali kutoka kwa msomaji  wetu wa Songea mkoani Ruvuma na Swali lake la pili aliuliza kama ifuatavyo;

Ahsante na kuna kauli zipo mitaani kwamba wenye umri mdogo hawawei kufanya biashara kubwa kwa mafanikio, ni kweli??

JIBU:
Siyo kweli kabisa na ni uzushi mtupu kwani duniani na hata hapa Tanzania ipo mifano ya vijana wengi waliofanikiwa katika biashara zao, kupata utajiri au kuwa mamilionea na hata mabilionea wangali hawajafikisha umri wa miaka 30.

Sula la ni umri gani mtu  anaweza akaanza kufanya biashara linategemea vigezo mbalimbali  kikiwemo  kigezo cha masomo au shule, vinginevyo kama tutakavyoona katika makala hii, mtu hata akiwa na umri wa miaka 15 anaweza akaanzisha biashara na akafanikiwa kufika mbali.


Ikiwa kijana bado anasoma si jambo zuri kujiingiza katika biashara ingawa  pia kuna baadhi ya watu ambao waliacha shule na kwenda kujiingiza katika biashara zilizowapa mafanikio makubwa. Lakini ukumbuke watu kama hao ni wachache sana.  Katika watu 100 labda wanaopata bahati hiyo hawazidi 10. Elimu itabakia kuwa muhimu daima. Ieleweke kuwa hata hao walioacha shule ‘drop outs’ siyo kama waliacha wakiwa mambumbumbu, hapana, wengi huwa wanakuwa tayari wameshajitambua.

Tuchukulie mfano wa hapa hapa kwetu vijana walioanza biashara na kufanikiwa wakiwa na umri mdogo, Mohammed Dewji alitajirika akiwa na umri mdogo sana, ingawa utajiri  huo chimbuko lake ni baba yake lakini fedha za baba yake zilikuwa ni kama mtaji tu.

Mohammed  Dewji Mo

Mo akiwa na umri wa miaka 25  pekee baada ya  kuhitimu masomo yake ya chuo kikuu huko nchini Marekani, alianza kazi katika kampuni ya baba yake kama mkuu wa idara ya pesa  wakati huo ikiwa na mapato  ya dolla za Kimarekani milioni 30 tu, lakini  baada ya kuchukua uthibiti  wa kampuni hiyo aliweza kuifanya kampuni hiyo kufikisha mapato yanayokadiriwa kufikia  dola bilioni 1.5 katika kipinddi cha miaka 15  pekee.


Hebu fikiria katika umri huo wa miaka 25 tu alivyoweza kuifanyia mapinduzi makubwa na ya kushangaza kampuni ya baba yake iliyokuwa ikijihusisha na uuzaji tu wa bidhaa katika maduka lakini kutokana na ubunifu wake mkubwa sasa kampuni hiyo  imejikita katika biashara za aina mbalimbali zikiwemo viwanda vikubwa vya bidhaa za chakula na sabuni.

Dunia nzima sasa inamtambua Mohammed Dewji, hata Jarida mashuhuri la Forbes likamtangaza  kuwa Mtanzania wa kwanza kuwa Bilionea, jarida hilo pia lilimtaja Mo kuwa Mwafrika bilionea kijana  zaidi mwaka jana 2016 akimiliki utajiri unaozidi dola bilioni 1.

Kijana mwingine wa Kitanzania Patrick Ngowi muanzilishi wa kampuni ya vifaa vya umeme jua solar(Helvetic group), alianza biashara akiwa na umri mdogo sana wa miaka 15  na dola za Kimarekani $50 tu. Alipofikisha miaka 18 alikopeshwa mtaji na wazazi wake wa dola zingine $1,800 alizozitunza akiwekeza kwa uangalifu mpaka  alipogeuka na kuwa milionea kabla hata hajatimiza umri wa miaka 30.


Ladi Delano kijana wa Kinaigeria akiwa na umri wa miaka 22 tu na kampuni yake ya ‘Bakrie Delano Africa’ aliweza kuwa biilionea katika umri huo mdogo kabisa alipokuwa akiishi nchini China mwaka 2004.


Mfano mwingine wa kuvutia kutoka nje ya Tanzania ni wa mwanzilishi wa mtandao wa kijamii Facebook, Mark  Zuckerberg mnamo Mwaka 2004  January  akiwa na wanachuo wenzake bwenini  katika chuo kikuu cha Havard Marekani walianzisha mtandao huo na kumbuka alikuwa na umri wa miaka 20 pekee. Alikuwa bilionea kwa mara yake ya kwanza kabisa akiwa na umri wa miaka 23 tu mnamo mwaka 2008.

Mmiliki wa facebook Mark Zuckerberg

Wengine waliokuwa mabilionea wakiwa na umri mdogo ni pamoja na mwanzilishi wa mtandao wa snapchat  Evan Spiegel aliyekuwa na umri wa miaka 25 mwaka 2015, Mwanzilishi wa Google, Larry Page aliyekuwa bilionea kwa mara ya kwanza mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 30 pekee. Bill Gates alitangazwa bilionea kijana zaidi mwaka 1987 alipokuwa na umri wa miaka 31 tu.Kwahiyo ndugu yangu kutoka Songea sasa wasiwasi wako umepatiwa majibu na ikiwa wewe ni kijana basi angalia kama  bado upo masomoni au tayari umekwishamaliza masomo yako. Na hata ikiwa unasoma bado, hilo haliwezi kukuzuia wewe kuanza kujiandaa kuwa mjasiriamali kisaikolojia. Anza kujijenga kimawazo  pamoja na kuanza  kujifunza namna ya kujiwekea akiba  kwani akiba ni muhimu sana hasa pale utakapokuja kuanza kufanya biashara au kuwekeza.   

Ndugu msomaji, kama una swali au ungependa kupata ushauri wowote ule kuhusiana na ujasiriamali au kuanzisha biashara yako, usisite kutuma swali/maswali yako kwa njia z meseji au e-mail, tutakujibu na tunaweza pia kuyaweka hapa bloguni majibu kwa manufaa ya wasomaji wengine bila kutaja utambullisho wako labda iwe ni kwa ridhaa yako tu.

Usikose swali la tatu kutoka kwa msomaji huyu wa Songea Kesho.

..................................................................................................

Kwa vitabu vyako vya ujasiriamali na biashara katika lugha ya kiswahili, tembelea SMART BOOKS TANZANIA

Mawasiliano ni  0712202244   au   07655533030, Peter Augustino

2 Responses to "KIJANA WA UMRI MDOGO ANAWEZA KUANZISHA BIASHARA KUBWA IKAFANIKIWA? "