JINSI KIWANDA KIDOGO KINAVYOWEZA KUKUTOA KIMAISHA NA KUWA TAJIRI WA KUTUPA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

JINSI KIWANDA KIDOGO KINAVYOWEZA KUKUTOA KIMAISHA NA KUWA TAJIRI WA KUTUPA

jinsi kiwanda kidogo kinavyoweza kukutajirisha
Kwa haraka haraka mtu anaposikia kuhusiana na kuwekeza katika viwanda moja kwa moja akili yake inaweza kumpeleka katika uwekezaji ama kuanzisha kiwanda mithili ya kiwanda cha Dangote cement Mtwara, kumbe kiwanda hata ukiwa tu unafahamu jinsi ya kutengeneza icecream unaweza kufungua kiwanda chako kidogo kwa ajili ya kutengeneza icecream za watoto na watu wazima ukauza mtaani kwako na hata nje ya mtaa unakoishi.

Viwanda ndiyo mhimili mkubwa katika chumi za nchi kubwakubwa na zilizoendelea tofauti na nchi kama hizi za kwetu ambazo mhimili mkuu ni kilimo. Hakuna shaka yeyote kwamba uzalishaji wa bidhaa viwandani ni muhimu sana kwa nchi yeyote ile iwe imeendelea ama ni nchi iliyoko dunia ya tatu, kwani viwandani ndiko hupatikana vifaa mbalimbali kama pembejeo za kilimo, zana za uvuvi, madawa na kemikali za kukuzia mimea, dawa na kemikali za kuuwa wadudu waharibifu, mashine mbalimbali, vipuri vya magari, bidhaa mbalimbali, madawa na vifaa vya hospitalini nk.


Kwa ujumla ni kwamba karibu kila sekta nyingine zote duniani zinategemea uzalishaji wa viwanda ili ziweze kufanya kazi sawasawa. Kwa hiyo ikiwa unao mpango wa siku moja kuja kumiliki kiwanda basi ni vyema ukaanza hata sasa kwa kuanza na kiwanda kidogo halafu baadaye utakapopata nguvu zaidi kimtaji ukafungua kiwanda kikubwa kama walivyofanya matajiri wengi wakiwemo kina Bakhresa, Reginald Mengi, Mohamed Dewji, Alihaj Ali Dangote na wengineo.

Nasema hivyo kutokana na sababu kwamba kuanzisha kiwanda kikubwa kunahitaji uwekezaji wa fedha na rasilimali nyingi lakini na ambao pia ikiwa bidhaa unazozalisha zinahitajika kwa wingi unaweza kutengeneza utajiri mkubwa ndani ya kipindi kifupi sana.

Siri 7 ni kwanini kiwanda kinaweza kumtajirisha mtu haraka.
1. Kiwanda hutumia mashine kuzalisha bidhaa kwa wingi na kwa haraka zaidi kushinda mikono ya binadamu. Tuchukulie mfano hata wa juisi ya maembe, ukikamua juisi ya embe kwa kutumia mashine ya blenda itakuchukua muda mfupi zaidi kuliko kama vile ungeamua kutwanga kwa kutumia kinu na kuchuja kwa kitambaa, au kutwanga mahindi ya kande kwa kutumia kinu ni zoezi gumu na linalogharimu muda mwingi kuliko kukoboa mahindi katika mashine.


2. Kiwanda kina uwezo wa kutengeneza bidhaa nyingi kwa wakati mmoja ambazo unaweza ukazisambaza kwa watu wengi. Na hivyo kuwa na wateja wengi wanaonunua bidhaa zako jambo litakalokupa faida nyingi kwa wakati mmoja tofauti na biashara tuseme labda ya kuuza bidhaa katika eneo moja tu.

3. Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha bidhaa zilizokuwa na ubora ule ule bila ya kushuka hivyo kusababisha soko liwe la uhakika.

4. Wateja popote pale duniani wanayo tabia ya kuamini zaidi zile bidhaa zinazotoka viwandani zikiwa na nembo pamoja na alama zilizothibitishwa na mamlaka mbalimbali za ubora na usalama.

5. Kiwanda kina uwezo wa kufanya kazi kila siku na wakati mwingine usiku na mchana kutokana na kutumia mashine zinazoendeshwa kwa nishati, hivyo uzalishaji ni mkubwa na faida nayo huwa kubwa pia.

6. Kiwanda kina uwezo wa kuzifanya bidhaa zinazoharibika upesi kudumu kwa muda mrefu zaidi na hivyo kuepusha hasara itokanayo na kuoza kwa mazao hasa ya kilimo.

7. Kiwanda kilichosajiliwa na kupewa vibali vyote vinavyostahili hupewa ushirikiano pamoja na usaidizi stahiki kutoka serikali kuu na serikali za mitaa kwa jambo lolote lile linalohusiana na maendeleo ya kiwanda.

Hatua 7 za uanzishaji wa kiwanda kidogo
Unapotaka kuanzisha kiwanda hata ikiwa ni kiwanda kidogo, inafaa mtu kufuata taratibu angalau zile muhimu ili kuhakikisha kiwanda chako hakiji kufungiwa na serikali au mamlaka husika. Taratibu nyingi au sheria itategemea ni kiwanda cha aina gani unachotaka kuanzisha. Kwa mfano kiwanda kidogo cha sabuni taratibu zake zitakuwa tofauti na taratibu za uanzishaji kiwanda tuseme labda cha kutengeneza sofa au fenicha.


Viwanda nyeti kama vile viwanda vya bidhaa zinazohusisha moja kwa moja afya na usalama wa binadamu au mazingira taratibu zake ni lazima zizingatiwe kwa umakini na ni vigumu kuanzisha kiwanda kama hicho bila kuzingatia ipasavyo sheria na taratibu za kuanzisha kiwanda husika.
Kiwanda kidogo siyo lazima kiwe na mashine nyingi
Kiwanda kidogo
1. Hatua ya kwanza kabisa ukishaamua ni kiwanda cha bidhaa gani unachotaka kuanzisha, fanya kwanza utafiti(upembuzi yakinifu) wa soko la bidhaa yako pamoja na masuala yote yatakayohusika kuanzia mtaji utakaohitajika, eneo la kuweka kiwanda chako, usajili na vibali kama vinahitajika, malighafi zitakazotumika, kiasi utakachozalisha, msaidizi/wasaidizi wa kazi kama wapo pamoja na ujuzi utakaohitaji kuwa nao kuhusiana na shughuli za kiwanda chako.

2. Hatua ya pili ni kuandaa mpango wa biashara kulingana na utafiti ulioufanya katika hatua iliyotangulia.

3. Tafuta pesa kwa ajili ya uanzishaji na uendeshaji wa kiwanda chako kwani shughuli yeyote ile ya uzalishaji hata iwe ndogo kiasi gani, bila ya kuwa na mtaji haiwezekani kuanzisha. Tumia mtaji wako uliokuwa nao, mkopo au fedha kutokana na mchango wa mbia.

4. Hatua ya nne, fuatilia leseni na vibali vinavyohusika kama kiwanda chako ni lazima kiwe navyo, ikiwa ni kiwanda kisichohitaji vibali basi unaweza kufuatilia leseni tu ya kawaida ya biashara. Kulingana na ukubwa na aina ya kiwanda utakachoanzisha, unaweza kujikuta unalazimika kwenda katika  taasisi mbalimbali kama vile BRELA, TRA, Ofisi za biashara za manispaa yako, TFDA, TBS, SIDO, NEMC nk. Mlolongo wa taasisi hizi usikutishe kwani kwa mfano ikiwa kiwanda chako ni cha vitu kama vyakula vile vya kawaida kama vitafunwa huna haja ya kwenda hata TFDA


5. Hatua tano ni kuandaa eneo na vifaa vya vitakavyotumika wakati wa uzalishaji kwenye kiwanda chako. Vipo viwanda kwa mujibu wa sheria vinatakiwa viwe kwenye maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya viwanda na kuna viwanda vingine unaweza ukafungua eneo lolote lile ilimradi pana nafasi ya kutosha. Nunua mshine au vifaa vinavyotakiwa.

6. Hatua ya sita, anza uzalishaji wa bidhaa zako

7. Hatua ya 7 na ya mwisho, tangaza na kuuza bidhaa zako.

Mwanzo wa ngoma ni lele, leo umeanzisha kiwanda kidogo, baada ya muda ukishapata mtaji unaweza ukaanzisha kiwanda cha kati na hatimaye ukamiliki kiwanda kikubwa kabisa. Unaweza kupata mafunzo na muongozo zaidi kutoka mashirika au taasisi mbalimbali zinazohusiana na uanzishaji wa viwanda vidogovidogo kama SIDO, VETA nk.

……………………………………………………………………...

Mpenzi msomaji wa makala katika blogu yako hii, kama unapenda kujifunza masomo ya biashara na ujasiriamali kwa kina kabisa, unaweza ukajipatia moja kati ya vitabu vyetu hapa, SMART BOOKS TANZANIA, pia kwa huduma zetu nyingine tunazotoa fungua ukurasa wa HUDUMA ZETU

Na kama ulikuwa hujakisoma kile kitabu cha JINSI YA KUJIFUNZA ELIMU YA PESA NA MAFANIKIO, bofya hayo maandishi ili uweze kukipakua bure bila malipo yeyote.

Mwandishi na mhamasishaji wako;
Peter A. Tarimo
0712202244

0765553030

1 Response to "JINSI KIWANDA KIDOGO KINAVYOWEZA KUKUTOA KIMAISHA NA KUWA TAJIRI WA KUTUPA"