MWANAMKE NA MAMA MJASIRIAMALI WA SHOKA NINAYEMFAHAMU ZAIDI DUNIANI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MWANAMKE NA MAMA MJASIRIAMALI WA SHOKA NINAYEMFAHAMU ZAIDI DUNIANI

Ukiniuliza ni mwanamke gani duniani mjasiriamali wa shoka ninayemfahamu zaidi kuliko wengine wote hapa duniani, moja kwa moja picha ya mama yangu mzazi, Fabiola Augustino Tarimo hunijia akilili. Kuelekea maadhmisho ya siku ya mama Duniani kesho jumapili, kumbukumbu zangu za awali kabisa katika maisha yangu ya utoto zinanikumbusha jinsi mama alivyokuwa akihangaika na biashara ndogondogo kusudi mimi na ndugu zangu wengine tuweze kupata mahitaji yetu muhimu yakiwemo mahitaji ya chakula, nguo, ada za shule na hata matibabu.

Ingawa kwa mama ninazo kumbu kumbu nyingi nzuri na zinazonisisimua sana ninapozikumbuka lakini kwa leo naona nijikite zaidi kwenye kumbu kumbu za mama yangu kama Mwanamke na mama Mjasiriamali wa shoka ambaye naweza nikasema kwangu mimi ndiye mwanamke ninayeweza kumpa nafasi ya kwanza kabisa katika kumbukumbu za maisha yangu yote kama shujaa wa kuigwa mfano (Role model) wangu katika Ujasiriamali na shughuli za biashara hapa duniani.


Sina lengo la kubeza umuhimu au juhudi za baba la hasha, naye alikuwa akijitahidi kivyake lakini kusema ukweli, juhudi zake tu mwenyewe bila ya mama hali ingelikuwa ngumu sana. Maisha hayakuwa rahisi, na kipato cha baba hakikuwa kikubwa cha kuiwezesha familia kumudu mahitaji yote kwa ukamilifu. Hii ndiyo sababu iliyomfanya mama aamue kujikita katika ujasiriamali na hasa biashara ndogondogo kwa ajili ya kuikimu familia.

Mpaka leo hii nikitazama katika mkono wangu wa kulia chini kidogo ya kiwiko lakini kabla ya goti la mkono, kuna doa la alama  fulani kama vile ya mtu aliyewahi kuungua na moto hapo zamani, alama hii sasa imefifia kidogo lakini wakati nikiwa mtoto mdogo ilikuwa ikionekana dhahiri. Mama wakati huo nikiwa mdogo aliwahi kunisimulia kwamba alama ile ilitokana na yeye kukaa juani masaa mengi mno wakati akiwa mjamzito, alinisimulia kwamba wakati nikiwa tumboni mwake alikuwa akifanya biashara za kuuza mazao mbalimbali ya chakula kama mahindi, maharage na ndizi.

SOMA: Utamu wa lugha ya mama hauna mfano.

Mama alisema kwamba, ilimbidi kusafiri umbali mrefu wakati mwingine hata kulala hukohuko kutokana na shida kubwa ya usafiri iliyokuwepo, alikwenda maeneo ya mbali kama Arusha, Moshi mjini na Himo kwa ajili ya kupata nafaka akauze maeneo ya Mkuu Rombo, Mashati, Useri na Tarakea. Wakati huo usafiri uliokuwa ukitumika ni wa malori na magari ya wazi hivyo njiani jua lilikuwa kali sana na ikawa ndiyo sababu kubwa ya mimi kupata baka la alama niliyokuwa nayo mpaka sasa hivi mkononi mwangu.

Kumbukumbu yangu kubwa zaidi na ambayo mpaka leo hii haijafutika akilini ingawa ilitokea nilipokuwa mdogo sana, ni ile njaa ya mwaka 1984, mwaka huo kulitokea njaa kali sana kote nchini Tanzania na nchi za jirani. Vyakula na hasa nafaka vilikuwa adimu sana hata serikali ya awamu ya kwanza wakati huo chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikaamua kuomba msaada wa mahindi ya njano kutoka nchini Marekani yaliyojulikana kwa jina maarufu kama mahindi ya Yanga. Mama wakati huo ndipo nilipotambua ujasiri wake.

Tukio ambalo siwezi kulisahau, japo wakati linatokea sikuwepo nyumbani, nilikuwa kwa bibi lakini wakaja kunisimulia dada na kaka zangu ni lile la mama siku moja kuamua kuinjika jikoni chungu kilichokuwa na chakula feki ili tu, aweze kuwaaminisha watoto wake kisaikolojia kwamba chakula kipo, kumbe alikuwa anakwenda kukitafuta.


Alikatakata shina la chini kabisa karibu na mizizi la mgomba kilugha huitwa(matonga) akajifanya ni viazi na kuviweka kwenye chungu kisha akainjika jikoni pamoja na kutia magadi, juu aliweka mfuniko na juu ya mfuniko akaweka jiwe, aliwaonya wanawe wasifunue, wachochee moto mpaka pale atakaporejea. Baada ya muda alirejea mkononi ameshika mfuko uliokuwa na unga. Kilichoendelea hapo kaka na dada zangu wanajua wenyewe.

Ujasiriamali wa mama haukuishia hapo, pia kipindi chote tukisoma mimi na ndugu zangu alikuwa mashuhuri kijijini kwa biashara ya kutengeneza na kuuza kwa jumla kinywaji maarufu cha mbege, ambacho ni mchanganyiko wa ndizi mbivu zilizochemshwa, kutiwa maji na kukamuliwa pamoja na kimea cha ulezi uliopikwa, wenyeji huita, kutisha mbege.

Nakumbuka mara nyingi nilivyokuwa nikimsaidia kukamua mbege masaa ya jioni baada ya kutoka shuleni. Wakati huo huo pia mama alikuwa akijishughulisha na kilimo na tulipokuwa shambani wote ndipo nilipojifunza masuala mengi kuhusiana na ujasiriamali.


Kitu cha ajabu sana nilichogundua kutoka kwa mama ni kwamba, kumbe ujasiriamali mtu anaweza akajifunza mwenyewe kutokana na mazingira na uzoefu anaopitia katika maisha yake. Kumbuka mama aliishia darasa la 2 enzi za mkoloni lakini kanuni muhimu za msingi za biashara na ujasiriamali alizifahamu kupita hata mtu aliyefika chuo Kikuu.

Mama mara kwa mara tulipokuwa shambani mimi na ndugu zangu alikuwa akituambia maneno haya,

 “Mwanangu ili uweze kupata kitu chochote kile kizuri maishani ni lazima jasho likutoke kwanza”,-Mama 
  
Katika biashara yeyote ile , mtaji ni kitu cha kuchunga sana wanangu, hakikisha unapokula usile mtaji bali kula faida tu” –Mama

Siwezi kusahau pia jinsi mama alivyotutia moyo wanawe pale tulipoanzisha jambo au biashara yeyote ile, nilipoanza kufuga kuku na kilimo cha bustani wakati nikiwa bado nasoma, mama alinipa support kubwa, baba alipogundua nimekata miti yake shambani kwa ajili ya kujengea banda la kuku alikasirika sana na kufikia hata hatua ya kunichapa lakini mama alijitahidi kwa udi na uvumba kumpoza hasira asinichape, mpaka ikafika hatua baba naye akaamua kuniunga mkono kwa kazi zangu baada ya kuona zinaleta manufaa kwangu na pale nyumbani kwa ujumla.


Mama aliona uchungu sana baada ya kugundua sikuweza kwenda kuuza mbogamboga zangu sokoni kutokana na muda wote wa mchana kuwa niko shuleni, yeye mwenyewe alitafuta muda, akazichuma na kunipelekea sokoni, niliporudi kutoka shuleni jioni alinipatia fedha zote alizoniuzia mbogamboga, mayai au nyanya na kwa kweli nilifurahi mno!


Namshukuru sana mama yangu, ndiye aliyeanza kunifundisha ujasiriamali tangu hata sijaanza shule, alinifundisha kwamba maisha ni kufanya kazi na siyo kukaa bure. Mama ametufanya katika familia yetu wote kuwa wajasiriamali, dada zangu, kaka na ndugu zangu wengine wote leo hii wapo waliofanikiwa kimaisha kupitia ujasiriamali na yote ni kutokana na kuiga mfano mzuri kutoka kwa mama yetu. Mungu azidi kumlinda na kumpa maisha marefu zaidi.

0 Response to "MWANAMKE NA MAMA MJASIRIAMALI WA SHOKA NINAYEMFAHAMU ZAIDI DUNIANI"

Post a Comment