KWANINI HURUMA NA UPENDO WA WAZAZI WENGI KWA MTOTO HUPITA KIASI? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KWANINI HURUMA NA UPENDO WA WAZAZI WENGI KWA MTOTO HUPITA KIASI?

Wazungu husema ni Unconditional Love”, upendo usiokuwa na masharti.Kuwa mzazi maana yake ni kwamba umpende mwanao kuliko hata ulivyowahi kujipenda wewe mwenyewe maishani mwako.

Naandika makala hii kutokana na kisa kimoja kinachonihusu binafsi, nami kutokana na kwamba kilinigusa mno basi nikaona ni vizuri kukielezea hapa kama njia ya kupunguza mhemko niliokuwa nao juu ya tukio lenyewe pia kumshirikisha yeyote yule hasa  ambaye ni mzazi.

Wiki jana wakati nikiwa katika mihangaiko yangu, nilipigiwa simu na mke wangu akinijulisha juu ya matokeo ya kijana wangu Frank anayesoma chekechea. Mama yake alikuwa amekwenda shuleni anakosoma kuchukua matokeo ya mtihani wao wa mwisho wa mwaka. Nilishangaa!.

Mwanangu Frank ni mtundu, siyo ule utundu wa kawaida, bali ni utundu ambao kila mtu anayemuona hushangaa. Siwezi nikaelezea kwa kina sana namna alivyokuwa mtundu lakini inatosha tu kusema kuwa ni mtundu. Kilichonishangaza mimi na hata mama yake ni matokeo yake ya mtihani wa kwanza shuleni, katika watoto 60 aliweza kushika namba ambayo sikuweza kuamini kabisa licha ya utundu aliokuwa nao. Aliweza kuwamo katika watoto 10 wa mwazo. Matokeo yale yalinifanya nifikirie kwa kina sana juu ya namna ambavyo wazazi tunapaswa kuwafunza maadili mema watoto wetu.

Frank kuna wakati  fulani alikuwa akifanya kosa huwa nilikuwa nikimtandika kwa lengo kwamba hatarudia tena kosa lile,  lakini kwa mshangao hata siku haitapita utakuta kesharudia tena kosa lilelile. Kitendo cha kuwa namchapa mara kwa mara niligundua kilikuwa kinamfanya mtoto awe anakuwa na tabia ya ukatili zaidi badala ya kujirekebisha.

Kila nilipomchapa baadaye  nilikuwa nikiingiwa na huruma ninapomtazama, “kalivyokuwa kadogo!”, kisha najisemea moyoni, “Mbona hata mimi nilipokuwa mtoto nilikuwa nikifanya makosa kama yeye”  Sikuwa napenda kabisa kumtandika  bali nilidhani nisipofanya vile ndiyo nilikuwa namharibu zaidi.

Baada ya kugundua kumuadhibu haimbadilishi, niliamua sasa kutumia mbinu nyingine, kumchukulia kwa upendo kila anapofanya kosa, badala sasa ya kuwa mkali nikawa kwanza naonyesha kuchukizwa na kile anachokifanya kisha najaribu kumfanya ajue kwamba kile alichokifanya ni makosa, siyo sahihi. 

Kidogo kidogo sasa naona mbinu hii inazaa matunda na mtoto ameanza kujiamini na kupunguza ule utundu aliokuwa nao. Hii haiondoi kabisa uwezekanao wa kumtandika, ila simtandiki kila mara tena hata kwa ‘vikosa’ ambavyo  najua hata mimi nilikuwa navifanya nilipokuwa mtoto.

Siku moja alifanya kosa kubwa shuleni kwake ambalo kwa vyovyote vile alijua baba akija tu ni lazima atamchapa ikiwa ni pamoja na kwenda mpaka shuleni pengine kumuadhibu mbele ya mwalimu na wanafunzi wenzake, mama yake alimsikia akitamka, “leo naomba baba asije tu nyumbani” kwa woga wa kuja kuchapwa.

Nilipofika nyumbani, alikaa mbali kabisa na mimi, baada ya mama yake kunielezea sikuonyesha kabisa kukasirika, bali nilimuita kwa upole na kuanza kumuuliza taratibu ni kwanini alikuwa amefanya vile (alikuwa na tabia ya kuwapiga wenzake makonzi kichwani na siku hiyo mwalimu aliandika kikaratasi kwa mzazi ili aende shuleni kuonana naye).

Ijapokuwa ni mtoto mdogo kabisa, kwa kweli alionyesha kujutia kosa mno! Akaniambia “Baba sirudii tena nisamehe”. Nusura machozi yanitoke, nikamkumbatia na kumuambia, “mwanangu nakupenda sana usiwe tena unafanya makosa”

Baada ya kugundua hakukuwa na uharaka sana wa kufika pale shuleni kwa ajili ya kosa lile, nilimwambia na mama yake wala asiongozane naye moja kwa moja kwenda kwa mwalimu siku iliyofuata, bali atakwenda kuonana na mwalimu wakati wake, mtoto mwenyewe hajui kama wameonana. Yote hiyo ilikuwa ni kumfanya mtoto ajiamini na kutokuhisi kuwa anahukumiwa.

Upendo wa bure pekee hapa duniani ni ule wa wazazi, wa wengine wote waliobakia ni lazima uulipie gharama...

Kwa kweli nimegundua kwamba hata wazazi wengi wanaowafanyia watoto wao ukatili wa kutisha baada ya kufanya makosa, wengine si kama wanapenda bali ni mihemko inayotokana na hasira huku wakidhani kwa kuwapa adhabu kali basi watajirekebisha kumbe ni kinyume chake. Si kama hawawapendi bali wanakosa tu subira na kutokutambua kwamba mtoto popote pale na katika vizazi vyote hufanya makosa na wanachohitaji zaidi ni kuelekezwa kwa upendo zaidi kuliko hasira.

Frank nimeona hamna namna nyingine ya kumfanya  apunguze utundu zaidi ya kumuonyesha upendo wa hali ya juu pamoja na kumuombea Mungu. Na kwa kweli ameonyesha mabadiliko makubwa sasa na anapenda kujisomea awapo nyumbani. Kila mzazi angependa mtoto wake awe na tabia njema, lakini changamoto hujitokeza, ni kwa namna gani utamfanya afuate yale yaliyokuwa mazuri tu na kuacha mabaya.

Mawasiliano mazuri na mtoto huku ukimtia moyo kuzungumza yale anayofikiri yeye kuwa ni sahihi itakusaidia kutambua kwanini mtoto anafanya makosa na itakuwa rahisi kumrekebisha kwa njia ya kumuelimisha taratibu. Imani pia inasaidia, unapokwenda na mtoto katika nyumba ya ibada, iwe ni Kanisani au Msikitini huku ukianza kumfundisha taratibu kuwa, kuna Mungu na huwa hapendi watoto wawe wakorofi nayo inasaidia sana.

Huruma na Upendo vilivyopitiliza kwa watoto kila kiumbe hasa sisi binadamu tunavyo, lakini usipokuwa makini unaweza ukamharibu mtoto aidha kwa kuchelea kumfundisha tabia njema au kwa kutumia njia zisizokuwa sahihi za kikatili mno ukijaribu kumrekebisha.

Nimegundua ukiwasiliana naye vizuri kwa upendo unamjengea uwezo wa kujiamini na pia uwezo mkubwa zaidi wa kufikiri na kujifunza masomo ya shuleni na pia yale yaliyomo kwenye jamii inayomzunguka.

Kuna nukuu hii maarufu kutoka kwa mtu mmoja aitwaye ‘Kevin whately’ isemayo;

From the time you are a tiny baby, a parent's love is usually unconditional. Whatever you do, your parents think you are the tops, but when their memory goes, you stop recouping the love you've put in” Kevin Whately

Anamaanisha kwamba; 
Tangu ukiwa mtoto mchanga, Upendo wa mzazi hauna masharti, chochote kile ulichokifanya, wazazi wako walikichukulia kwa umakini mkubwa, lakini kadiri kumbukumbu zao zinavyopotea ndivyo na wewe unavyoacha kukumbuka upendo uliojengewa”

Nyingine ni kutoka kwa Bill Ayers nayo inasema hivi;
“Your kids require you most of all to love them for who they are, not to spend your whole time trying to correct them.”- Bill Ayers

Akimaanisha kwamba; 
“Watoto wako wanachohitaji zaidi kutoka kwako, ni wewe kuwapenda kama walivyo, na siyo kupoteza muda wako wote ukijaribu kuwarekebisha”.


Wimbo huu hapa chini uliimbwa na mwanamuziki Jim Reeves, “But You Love Me Daddy”(Lakini unanipenda baba) akijibizana na mwanawe wa miaka mitano 5. Jim alikuwa akimweleza mwanawe kwa lugha ya upendo kabisa jinsi anavyomsababishia maudhi mengi huku mwanawe huyo akimjibu, “Lakini baba si unanipenda?”

Video ya wimbo "Lakini unanipenda baba";

Audio ya wimbo, lakini unanipenda baba;


Mashairi ya wimbo “Lakini unanipenda baba” katika kiswahili.

Uso wako wa miaka mitano
Unatia aibu kwa uchafu
Lakini unanipenda baba


Unatupa tupa ovyo midoli yako
Na unapiga sana kelele
Lakini unanipenda baba.

Unajua mwanangu
Unaweza  ukawa mbaya sana
Lakini unanipenda baba

Unaniamsha alfajiri
Wakati ninapotaka kuendelea kulala
Lakini unanipenda baba


Sasa unakula biskuti
Wakati nakukataza
Lakini unanipenda baba
“Ndiyo sababu unaniambia hivyo”

Na umekuwa mgumu sana kukanya
“Kwakuwa  wewe ni wangu wa miaka mitano
Kwasababu unanipenda baba

Nikuvishapo nguo
Unakwenda kucheza na mtoto wa mbwa
Lakini unanipenda baba

Ninapokuwa napiga simu
Huniachi peke yangu
Lakini unanipenda baba

Unamhuzunisha dada yako
Kwa kumvuta nywele zake
Lakini unanipenda baba

Unakwaruza sakafu
Na kuandika katika mlango
Lakini unanipenda baba


Unauliza maswali ya kijinga
Sasa unajua kwamba ni kweli
Lakini unanipenda baba
Sasa unajua kwamba unanipenda

Unakuwa mgumu sana kukanya
Kwasababu wewe ni wangu wa miaka mitano
Kwasababu unanipenda baba.
........................................................................................................

Ungependa pia kusoma makala hizi juu ya watoto?




                         

0 Response to "KWANINI HURUMA NA UPENDO WA WAZAZI WENGI KWA MTOTO HUPITA KIASI?"

Post a Comment