CHUMA ULETE ANAVYOWATESA WENYE MADUKA NA WAFANYAKAZI WAO DAR | JIFUNZE UJASIRIAMALI

CHUMA ULETE ANAVYOWATESA WENYE MADUKA NA WAFANYAKAZI WAO DAR

Ni kisa nilichokishuhudia mwenyewe kwa macho yangu.

Joyce, siyo jina lake halisi, alikuwa ndiyo kwanza ana wiki mbili tu tangu aanze kazi ya kuuza duka la tajiri yake jina pia siwezi nikalitaja hapa kwani hajaniruhusu. Duka hilo la vinywaji  baridi mchanganyiko na vileo kama bia lilikuwa karibu kabisa na mahali nilipokuwa nikifanya shughuli zangu kwa wakati huo.

Wateja wa aina mbalimbali walikuwa wakifika mara kwa mara katika ‘pub’ hiyo hasa nyakati za jioni kwa lengo la kupoza makoo yao.

Siku hiyo kuna kaka mmoja umri wake ni wa makamo hivi, alifika hapo na baada ya kukaribishwa na yule mhudumu yaani Joyce aliketi na kisha akaagiza kinywaji (Bia)na kuanza kunywa. Lakini kama ilivyokuwa ada kwa wateja wengi  hasa wa jinsia ya kiume wanapokwenda katika maeneo vinapouzwa vileo, wengi wao huwa na malengo zaidi ya kupoza koo. Yule kaka alianza kumtongoza yule mhudumu naye baada ya kubaini nia yake hakufanya ajizi akaanza kupanga mikakati ya “kumchomoa noti”.

Joyce kwa kweli katika wiki nzima ile alikuwa akisikika na majirani wa pale nikiwamo na mimi mwenyewe akilalamika sana juu ya hali ngumu ya maisha, alikuwa akihangaika sana juu ya namna atakavyoweza kupata pesa kwa ajili ya kulipa pango la chumba cha kuishi alichopanga ambacho ilionekana muda ulikuwa mbioni kumalizika. Kwa kweli hata kile kilichokuja kutokea pale hakikunishangaza sana kwani Joyce alikuwa tayari kwa lolote ilimradi tu azipate pesa kwa ajili ya kulipa pango hilo.

Basi kaka yule aliendelea kuburudika na kinywaji chake huku maongezi ya hapa na pale na Joyce yakiendelea. Baada ya kitambo kidogo kupita majirani tulishitushwa na kilio cha Joyce aliyekuwa akilalamika kwamba pesa zake zote za mauzo ya tangu jana yake usiku, zaidi ya shilingi elfu sabini zilikuwa zimetoweka kutoka katika droo ya pesa katika mazingira ya kutatanisha.

Huku mikono ikiwa kichwani na machozi kweli yakimlengalenga, Joyce aliwafanya wengi wa watu waliokuja kushuhudia tukio lile waamini kuwa ni kweli lilikuwa limetokea.

Mtuhumiwa wake mkuu aliyedai kuwa ndiye mhusika wa kuzichukua pesa zie kimiujiza alikuwa ni yule mteja wake, kijana aliyekuja pale kujiburudisha na bia. Huku akiwa ameketi palepale kwenye kiti kama alivyokuja, kaka yule alipigwa na bumbuwazi asijue la kufanya, hata kujitetea ilikuwa ni shida kwa jinsi Joyce alivyokuwa akipiga makelele.

Kwa amaelezo ya Joyce ni kwamba yule kaka mara tu baada ya kufika na kukaa pale kwenye kiti, alitazama kwenye droo na aliziona pesa zote zikiwa salama, lakini alidai kwamba baada ya kukaa muda fulani alitazama tena katika droo na kukuta hamna kitu, pesa zote zimetoweka. Alipoulizwa ikiwa kuna muda wowote alitoka pale kaunta akaenda nje na kumuacha yule kaka peke yake pale alijibu kuwa wala hakutoka kabisa na yule kaka wala hakuinuka hata mara moja pale alipokuwa ameketi.

Aliendelea kusisitiza kuwa kaka yule ni lazima atakuwa mchawi na huo utakuwa ndio mchezo wake kwenda katika biashara za watu akijifanya anakunywa kumbe lengo lake ni kuchukua mauzo kwa njia za kimiujiza(chuma ulete)

Joyce alikataa kata kata kwamba labda fedha hizo zilikuwa zimechukuliwa na mtu mwingine hapo kabla, labda na  vibaka wanaopitapita wakati alipojisahau. Watu tulishindwa kusuluhisha kwani  Joyce alikuwa akidai arudishiwe fedha  za bosi wake kwani asingekuja kumuelewa pindi ambapo angerudi.

Watu tuliokuwa pale tulishindwa  kusuluhisha, ikabidi sakata lihamie kwa mjumbe, mjumbe naye hakuliweza ikabidi yafike polisi. Kule polisi, sijui tuseme ndiyo ujanja au ni kitu gani, walimfundisha abadilishe maelezo aliyokuwa akiyatoa kutokana na sababu kwamba eti serikali haijihusishi na masuala ya kishirikina. 

Walimwambia ikiwa alitaka ile kesi iweze kufika mahakamani basi alikuwa hana budi kuyaondoa kabisa maneno yaliyohusiana na ushirikina au chuma ulete na badala yake aeleze kwamba, pesa zilipotea baada ya mtuhumiwa kufika pale na kuanza kumtomasa tomasa akiwa ndani ya kaunta ya vivywaji.

Kusema ule ukweli, mimi mwenyewe binafsi mazingira ya tukio nilivyoyaona, kulikuwa hakuna kabisa uwezekano wa mtu kuweza kuiba pesa ilihali mhudumu akiwa palepale hata ikiwa alimsogelea kiasi gani kwani kulikuwa hakuna uwezekano wowote wa kuweza kuifikia droo ya pesa. Hata hivyo akiwa palepale alipokuwa ameketi alisachiwa na hakukutwa na hata senti tano zaidi ya fedha zake mwenyewe alizokuwa nazo mfukoni.

Huku akiwa haamini macho yake yule kaka alijikuta akitinga mahakamani, na kesi ikaanza kusikilizwa, wiki zilipita na hata miezi, kesi si mchezo, iliwagharimu wote wawili si mtuhumiwa tu na hata yule mlalamikaji, Joyce naye hata ikawa siku zingine hafiki mahakamani. Lakini mwenye haki ni mwenye haki tu yule kaka wa watu hakukosa mahakamani hata siku moja,  hata hakimu baada ya kuona mlalamikaji haonekani ikabidi  atumiwe ujumbe wa kuitwa mahakamani.

Mwishoni ilionekana dhahiri kabisa kwamba mlalamikaji hakuwa na ushahidi wowote ule wa maana bali alikuwa tu akilazimika kuhudhuria mahakama kusudi tajiri yake aamini kweli kama pesa aliibiwa, mwisho kabisa na kibarua chenyewe kiliota nyasi sambamba na kukatwa mshahara wake pesa alizodanganya kaibiwa kichumaulete. Huku mahakamani nako yule kijana aliachiwa huru. Watu walimshauri akamfungulie kesi ya udhalilishaji lakini akasema yote anamwachia Mungu.

Biashara nyingi hususani zile za rejareja mtindo huu wa wasaidizi kusingizia Chuma ulete, au masuala ya kishirikina kuwa ndiyo chanzo cha biashara kuzorota au pesa kupotea  umeota mizizi sana. Bosi usipokuwa mwerevu na wewe ukawa ni mtu rahisirahisi tu wa kuamini upumbavu huo basi unaweza ukajikuta ukiingia mkenge. Hawakukosea waliosema Wajinga ndio waliwao” Usikubali kuwa mjinga wa kuamini vitu vya karne zilizopita, tena visivyokuwa na ushahidi wowote wa kisayansi.


Kuwa makini na wasaidizi/wafanyakazi wako, tengeneza mfumo thabiti wa mahesabu ya biashara yako, tenganisha fedha za biashara na matumizi yako binafsi pamoja na kupata maarifa na mbinu sahihi juu ya biashara unayoifanya, ndiyo muarobaini wa ko wa kupambana na “Mdudu Chuma ulete” hatimaye ukaweza kumshinda.

0 Response to "CHUMA ULETE ANAVYOWATESA WENYE MADUKA NA WAFANYAKAZI WAO DAR"

Post a Comment