KWANINI KUFANIKIWA KIFEDHA SI DHAMBI NA KILA MTU ANASTAHILI AFANIKIWE? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KWANINI KUFANIKIWA KIFEDHA SI DHAMBI NA KILA MTU ANASTAHILI AFANIKIWE?


Ni lengo la kila mtu maishani mwake siku moja kuja kuwa milionea au kumiliki pesa na utajiri, ingawa mara nyingi watu wengi huogopa kuliweka lengo hili wazi. Mtu tangu utotoni huota ndoto za kuja kuwa na maisha mazuri yaliyokuwa bora kama vile, kujenga nyumba nzuri, kuwa na vitegauchumi vya aina mbalimbali, kuwa na familia bora, kusomesha watoto shule nzuri, kula vizuri nk.

Ijapokuwa kila binadamu tangu kuzaliwa dhamira yake kubwa ni kufanikiwa maishani, lakini hilo si watu wengi wanaopenda kuliweka wazi, sababu ambayo pengine ndiyo inayosababisha kweli kushindwa kupata mafanikio kifedha au kutajirika.

SOMA: Maajabu ya kufikiri mambo makubwa na kwanini ujiwekee malengo makubwa maishani.

Unajua dhamira au lengo si tu linapaswa kuwekwa rohoni bali ikibidi hata wakati mwingine ulitamke waziwazi watu wakusikie ndipo kweli litokee kuwa kweli. Kujidai eti utajiri ni dhambi ilhali mioyoni tunatamani kuupata huo ni unafiki mkubwa.


Lakini pamoja na ukweli huo dhahiri kuwa kila mtu angependa afanikiwe, inakuja kutokea kuwa asilimia kubwa ya watu huja kuishia kuwa na maisha ya kawaida na wengine kutumbukia kwenye lindi la umasikini mkubwa kiasi ambacho hata mlo wa kila siku inakuwa vigumu kuupata. Ni asilimia ndogo tu ya watu ambao ndoto zao huja kugeuka kuwa kweli. Ukichunguza sababu inayofanya hali hii kutokea unaweza ukapata majibu mengi tofautitofauti.

Moja ya sabaubu kubwa inayotajwa sana na watu kuwa ndiyo inayochangia kuwepo kwa hali hiyo ya watu wachache kuwa na maisha mazuri ili hali wengi wakiishi maisha ya umasikini ni jinsi watu wanavyojiwekea malengo yao. Wale wanaofanikiwa huweka malengo makubwa maishani mwao huku wakifikiria mambo makubwa na kamwe hawakubaliani na kuishi maisha ya kawaida ya umasikini yaliyozoeleka na watu wengi.


Wanafanya kazi kwa nguvu zao zote huku wakitumia kwa uangalifu mkubwa pesa wanazopata zisipotee ovyo bila kuzalisha. Wanaweka vitegauchumi vingi kuhakikisha mtiririko wa fedha kwao unakuwa chanya siku zote. Kwa upande wa wale wasiofanikiwa, wanaridhika mno na hali walizokuwa nazo na wakati mwingine huogopa hata kumiliki pesa nyingi wakifikiri kuwa utajiri ni dhambi au ni hatari, wezi na majambazi wanaweza kuwavamia muda wowote. Hujiwekea malengo mafupi na wanapopata pesa huhakikisha zinakwisha kabla hawajazizalisha wala kuwekeza chochote.

Hizo ni baadhi ya sababu chache tu nilizotaja, lakini kuna sababu nyingine nyingi tu unazoweza kukutana nazo endapo utaamua kutafuta chimbuko la ni kwanini watu wengine huwa matajiri wa kutupa wakati wengine hubakia kuwa masikini. Sasa hebu tukaone kile tulichodhamiria kujifunza leo.

Sababu za wewe kuwa na mafanikio kimaisha, kuwa milionea au kumiliki pesa nyingi na utajiri
Kwanza kabisa kabla sijazitaja sababu zenyewe, tukubaliane kabisa kwamba kuwa tajiri siyo dhambi, ilimradi tu utajiri au fedha hizo ni halali, hujazipata kwa njia za mkato au kuwadhulumu watu wengine maisha au mali zao. Nadhani watu wa dini mbalimbali hilo bila shaka yeyote wataniunga mkono.

1. Ukiwa na maisha mazuri(tajiri) unagusa maisha ya watu wengine.
Kabla sijaendelea kwanza napenda nikuulize kitu kimoja, “umewahi kukumbana na tatizo lolote lile hasahasa la kiafya kama ugojwa kwa, ndugu yako, mpendwa wako wa karibu au rafiki lakini kwa bahati mbaya akafa au kupata madhara makubwa kimaisha kwa sababu tu ya kukosekana uwezo kifedha wa kushughulikia tatizo lake?”

Ikiwa hujawahi kukutana na hali kama hiyo, mimi nimekwisha kutana nayo, na nakueleza ndugu yangu, usiombee yakukute kwani ni hali inayoumiza  mno moyo na kutia simanzi kubwa. Lakini vipi ikiwa upo katikati hali kama hiyo na kisha akatokea mtu mmoja tajiri au tu hata tuseme mtu mwenye uwezo kifedha akaamua kutoa msaada kwa ajili ya kuokoa uhai wa huyo mpendwa wako, utajisikiaje?

Katika hali ya kawaida kwa kweli binadamu wengi tunaamini kwamba matajiri wengi au watu waliofanikiwa zaidi kimaisha ni wenye roho mbaya na uchoyo, watu wabaya wasiostahili kuuona ufalme wa Mungu. Lakini tunasahau mambo mengi mazuri matajiri hao ambayo huyafanya.

SOMA: Siri matajiri wasiyopenda kuitoa.

Kwanza fahamu kuwa tajiri kama ataamua kuishi jinsi vile watu wengine wa kawaida wanavyotaka aishi basi utajiri wake hautaweza kudumu hata miaka miwili, utamalizika. Si kama nawatukuza matajiri, hapana ila nataka tu kusisitiza umuhimu wa watu kutokuendelea kukubali kuwa masikini.

Watu masikini na wale wa hali za kati mara nyingi huwa tunalalamika tukidai kupatiwa misaada na ruzuku wakati matajiri wao muda mwingi hufikiria namna ya kutekeleza mambo, kufanya vitu kivitendo zaidi. Kuna mifano ya watu matajiri kama vile, Bill Gates. Bill Gates amewahi kutoa mailioni ya dola kupambana na malaria ili kuokoa maelfu ya Waafrika wanaotaabika na kufa kila siku kwa ugonjwa uaotibika kirahisi tu.

Ukija hata hapa Tanzan tunao watu kama kina Mzee, Reginald Mengi, Said Salim Bakhresa na wengine wengi wakiwemo hata matajiri wadogowadogo katika mitaa tunamoishi, husaidia watu wakati mwinge kimya kimya hata pasipo watu wengine kugundua kuwa wametoa misaada. Sasa unaweza kuona ni kwa jinsi gani pesa zina umuhimu na ni kwanini kila mtu anatakiwa kuzipata.

SOMA: Je, ungependa uwe kama Regnald Mendi, Said Salim Bakhresa, Mohamed Dewji au Rostam Aziz?

2. Ukiwa tajiri unawaambukiza na watu wengine kuwa matajiri.
Hebu jaribu kuchunguza watu matajiri, utajiri wao wananufaika nao wao wenyewe tu na familia zao?. Jibu nadhani litakuwa hapana. Kwanini, kwa sababu matajiri huanzisha miradi ya kibiashara na makampuni ambayo huajiri watu wengine wengi na watu hao wengine pia huwa matajiri kupitia miradi hiyohiyo. Hebu fikiria tena, ni watu wangapi wametajirika au maisha yao kuwa bora zaidi kupitia kuuza bidhaa za Mohamed Enterprises, Azam, IPP, Microsoft, IBM, Cocacola, Pepsi na wengineo wengi?

3. Ukiwa tajiri unakuwa na uwezo hata wa kusikilizwa na Serikali kwa jambo lenye manufaa ya umma.
Wewe utakuwa shahidi kwani ni juzijuzi tu hapa tumeona Rais wa nchi, John Pombe Magufuli akimuita ikulu Mmiliki wa kiwanda cha simenti cha Dangote, Alhaji Aliko Dngote ambaye pia ndiye mtu tajiri zaidi BaraniAfrika kutokana na malalamiko ya kiwanda hicho juu ya mikataba yake kibiashara na serikali kutoenda vizuri. Angelikuwa mtu masikini angepata ‘attention’ kiasi kile?. Hivyo unaweza ukaona ni kwa namna gani unapokuwa na uwezo kifedha unavyoweza kuathiri hata maamuzi ya serikali.

Mfano mwingine nitakaokupa, hebu tazama uchaguzi wa Marekani uliomweka Donald Trump Madarakani, Trump inasemekana hakuwahi hata kuwa mjumbe wa nyumba kumi kule Marekani zaidi ya kuongoza kampuni zake binafsi za biashara, lakini uliona jinsi alivyoweza kuathiri maoni na mitazamo ya Wamarekani mpaka mwishowe wakakubali wenyewe kumpa Urais? Ingelikuwaje kama asingekuwa na kitu?

Mwisho, tunapaswa kukubaliana na ukweli kwamba, umasikini unaumiza, unamfanya mtu kuwa mnyone, unamnyima mtu fursa nyingi na hata wakati mwingine unamnyima mtu fursa ya uhai wake mwenyewe aliopewa na Mwenyezi Mungu kama mfano nilioanza kukupa pale mwanzoni mwa makala hii.

SOMA: Ni nini hasa unachohitaji ili uweze kufanikiwa kiuchumi?

Lakini ipo njia moja tu halali ambayo binadamu tunaweza tukaitumia kuondokana na umasikini huo na kuwa na maisha bora yaliyojaa mafanikio. KUFANYA KAZI NA HASA BIASHARA, nasema biashara kwasababu hata kazi ya ajira inahesabika ni biashara kutokana na kwamba mwajiriwa anauza nguvu na muda wake kwa mwajiri kwa ujira wa FEDHA. Ili kufanya biashara kwa ufanisi mkubwa na hatimaye mtu uweze kuwa na mafanikio ya pesa hauna budi kuhakikisha unakuwa na maarifa sahihi mengi kuhusiana na jinsi ya kufanya biashara.


.............................................................................................

Kwa vitabu vizuri vya Ujasiriamali, biashara na maendeleo binafsi tembelea SMSRTBOOKSTZ.

Jiunge na BLOGU YA MASOMO YA SEMINA YA MICHANGANUO YA BIASHARA kwa kubonyeza maandishi hayo. 

0 Response to "KWANINI KUFANIKIWA KIFEDHA SI DHAMBI NA KILA MTU ANASTAHILI AFANIKIWE?"

Post a Comment