BIASHARA NDOGONDOGO 7 ZILIZO NA FAIDA KUBWA UNAZOWEZA KUANZISHA BILA MTAJI KABISA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

BIASHARA NDOGONDOGO 7 ZILIZO NA FAIDA KUBWA UNAZOWEZA KUANZISHA BILA MTAJI KABISA

Unapojikuta katika hali ya kutokuwa na mtaji kabisa wa fedha, unaweza kufikiria njia nyingi sana za ni namna gani utakavyoweza kuendesha maisha yako ya kila siku. Ukiwa katika hali kama hiyo, mtaji wako pekee unakuwa ni nguvu zako ulizokuwa nazo kama huna ugonjwa wowote unaokusumbua, ujuzi, maarifa au elimu uliyo nayo pamoja na uzoefu ulioupata siku za nyuma.

Sasa zipo biashara unazoweza kuzifanya hata ikiwa hauna kabisa mtaji kwa maana ya fedha, ingawa hauwezi kabisa kabisa kusema ipo biashara isiyotumia mtaji kwa kuwa hata nguvu na ujuzi kitalamu huhesabiwa kama ni mtaji mojawapo. Orodha ile ya biashara nitakazozitaja hapa ya biashara zisizohitaji mtaji wa pesa kabisa ni tofauti na nyingine niliyowahi kutaja tena katika blogu hii iliyokuwa inaziorodhesha  biashara zilizokuwa na faida kubwa na yaharaka mara 2 ya mtaji utakaowekeza.

Vile vile hapa sizungumzii zile biashara unazoweza kuanzisha bila mtaji wa pesa kwa maana ya kutumia mbinu mbalimbali kama vile kukopa mali kutoka kwa wasambazaji na wauzaji wa jumla kisha na wewe baada ya kwenda kuuza rejareja unarudi kuja kuwalipa fedha zao, itategemea bidha hizo unakwenda kuuzia wapi, ikiwa huuzii katika fremu au chumba cha kulipia labda unauzia nyumbani au kutembeza mitaani sawa itakuwa ni biashara isiyotumia mtaji.

Au kutoa huduma kama vile za kiushauri wa kitaalamu ambazo mtu ingawa unaweza usitumie mtaji wa pesa lakini unajikuta ukihitaji pesa kwanza za kuandaa ofisi nk. Au biashara ya kwenye mtandao wa intaneti ambayo ni lazima kwanza uhakikishe unayo kompyuta, moderm au simu ya kisasa ya mkononi kama smartphone na shilingi lfu moja, mbili za kuweka bando la intaneti . Biashara kama hizo badala ya kusema hazihitaji kabisa mitaji tunaweza kuziita ni biashara za mtaji kidogo au za uwekezaji mdogo kwa sababu haiwezekani kabisa uanzishe bila senti tano mfukoni.

SOMA: Biashara ndogo za kufanya Dar bila kulipa pango

Katika orodha yangu hii namba moja 1, nitaifanya kuwa ndiyo ya mwisho, ilitakiwa kuwa ya kwanza lakini kutokana na upekee wake naona tuiache kwanza mpaka mwishoni ndipo niitaje.

1.    Udalali wa vitu, nyumba, vyumba, viwanja na mashamba; Hapa nazungumzia ule udalali wa ngazi ya chini kabisa mitaani, siyo ule wa ngazi za makampuni yaliyosajiliwa kisheria ingawa kama ukishaanza chini ni lazima baada ya kupata mtaji sasa ukumbuke kwenda kujisajili kisheria serikalini. Kwa kuanza unaweza kutafuta mtaani unakoishi watu wenye vitu mbalimbali wanavyokodisha au kuuza kisha unakwenda kuwatafuta na watu wanaohitaji vitu hivyo halafu baada ya kuwaunganisha wanakupa malipo kidogo toka kila upande au upande mmoja.

Kuna mtu mmoja yeye hakuwa na mtaji wowote ule ila alikuwa tu na aidia ya maswala ya material na vifaa vya ujenzi vya kujengea nyumba kama vile, tofali, paving blocks, vigae/tiles, baluster na ventilation blocks. Aliwafahamu vyema pia wauzaji na watengenezaji wa vifaa hivyo vya ujenzi, bei za vifaa na material hizo, na kila kitu kuhusiana navyo.

Kando kando ya ukuta wa nyuma yake uliopakana na barabara ya Morogoro road yanakopita magari na watu wengi alipamba ukuta huo kwa vipande vilivyovunjika vya vifaa hivyo alivyookota wanakotengeneza pamoja na kuweka bei zake na namba yake ya simu kama matangazo kwa wateja kwamba yeye anauza vitu hivyo.

Wateja wanaohitaji humpigia simu wakishapatana bei huwaambia wasubiri kidogo aende eneo anakotengenezea ili awachukulie, kumbe yeye huku anakwenda kwa watengenezaji. Hapo hupatana kabisa na mtu wa gari wanakwenda kupakia tayari kwa kupeleka saiti kwa mteja. 

2.    Biashara ya utoaji wa huduma mbali mbali kama vile biashara ya huduma ya kuangalia watoto wadogo wakati wazazi wao wakiwa kazini(babysitting au home daycare), hii unaweza ukaifanyia nyumbani kwako lakini katika kiwango cha watoto wachache tu kuanzia labda mmoja mpaka watatu ukitumia vifaa na eneo la nyumba unayoishi,  kisha baadae unaweza ukatafuta vibali na leseni kwa ajili ya kuanzisha kituo kamili cha kuangalia watoto wengi zaidi.

Huduma nyingine unayoweza kutoa bila kuwa na mtaji wa pesa ni, biashara ya udobi, kufua na kupiga pasi nguo za watu ukiwa majumbani mwa watu hao, unakwenda wewe mwenyewe na vifaa vyote ni vya kwao. Au hata unaweza kwa kutumia vifaa vyako vya nyumbani ukawatangazia majirani na watu wanaohitaji huduma hiyo wakaleta nguo zao hapo nyumbani unapoishi.


Huduma ya kufundisha na ushauri, yanaweza kuwa masomo ya ziada ya shule(tuition) ama ujuzi wowote uliokuwa nao na ambao kuna watu wengine wanaohitaji kujifunza kama vile muziki, ujasiriamali, mapishi, kutarizi, utengenezaji wa vitu kama mishumaa, batiki, sabuni, unga wa lishe nk. Unaweza kuwafundisha wateja wako mmojammoja majumbani mwao au ukawaita eneo unaloishi na kuwapa masomo kisha wakakulipa. Vifaa kwa mfano malighafi za kutengenezea vitu ni mteja mwenyewe atakayenunua.

3.    Biashara ya kuokota na kuuza vitu chakavu kama vile chupa za plastiki, vyuma chakavu, chupa na mikebe ya kuwekea vitu iliyotupwa pamoja na vifusi kutoka majengo yaliyobomolewa. Kuna biashara pia ya kuzoa na kuuza mchanga kutoka kwenye mifereji ya barabara au maeneo yanayoruhusiwa.  Usije ukaaona waokota makopo na chupabarabarani ukadhani wote ni machizi, wapo wajanja hata kukushinda wewe uliyeko ofisini.

4.    Kuuza mbolea na mifupa ya ngombe au kuku. Sehemu za machinjio ya wanyama kama kuku, ngombe na mbuzi. Kile wanachotupa kama uchafu, wapo watu wanaokihitaji kwa mfano mbolea kwa ajili ya kuoteshea mbogamboga na mimea, mifupa na damu kwa ajili ya kulishia wanyama kama kuku, samaki nk. Unaweza kutafuta kwanza oda kutoka kwa watu wanaohitaji kisha na wewe unakwenda kuchukua na kuwapelekea, wakakulipa pesa.

5.    Biashara ya kuuza mabaki ya vyakula mahotelini na kwenye migahawa. Tafuta kwanza watu wanaohitaji mabaki hayo ya vyakula na wengi ni wale wanaofuga wanyama kama mbwa, paka, kuku, bata na nguruwe, halafu kazi yako inakuwa ni kupita maeneo mbalimbali wanakopika na kuuza vyakula kama kwa akina baba na mama lishe, migahawa, baa na mahoteli mbalimbali. Waombe wawe wanakupa yale mabaki ya vyakula vinavyobaki na kama hawana kazi navyo watakupa na wewe ukaviuze kwa wateja uliokwishawapata.

6.    Utengenezaji wa mapambo na bidhaa ndogondogo kwa kutumia malighafi zitokanazo na vitu vilivyotupwa majalalani kama vile maua, midoli, vyungu vya maua kwa kutumia udongo nk. Biashara ya kuuza miche ya maua na miti mbalimbali, hii unaweza kuotesha miche ya mimea ya maua na miti mbalimbali ambayo mbegu zake unaweza kuzipata bure au kuokota kwenye miti, na kwa kutumia karatasi za nailoni zilizotupwa na makopo au chupa unapanda miche na kuiuza kandokando ya barabara ambako huchajiwi kodi na mtu yeyote ilimradi tu umepanga kwa unadhifu pasipo kuharibu au kuchafua mazingira.

7.    *AJIRA.
Biashara ya mwisho unayoeza kuifanya wakati hauna kitu chochote kile mfukoni na ambayo nilisema ilipaswa kuwa ya kwanza lakini kutokana na kwamba ni biashara iliyo katika mjadala mzito ikiwa ni biashara kweli ama siyo biashara ni biashara ya ajira.

Kwa upande wangu mimi nafikiri pengine na kuna watu wengine wanaoamini hivyo, ajira au kazi nayo ni biashara kama zilivyokuwa biashara zingine kutokana na sababu kubwa kwamba, mwajiriwa anauza nguvu au ujuzi wake kwa mwajiri. Ili biashara iitwe biashara ni lazima kuwe na bidhaa au huduma halafu muuzaji na mnunuzi.

SOMA: Ajira siyo laana, bali chanzo kizuri zaidi cha mtaji wa biashara.

Kwa mantiki hiyo basi, ikiwa hauna mtaji wowote ule mfukoni hiyo ndiyo fursa nzuri zaidi ya kutafuta ajira yeyote ile unayoweza kuifanya kulingana na uzoefu, ujuzi au taaluma uliyokuwa nayo. Hata kama ikiwa huna vitu vyote hivyo, basi uza nguvu zako kwa kutafuta zile kazi ambazo ni nguvu zako tu ndizo zinazotakiwa kama vile kubeba mizigo(ukuli), kulima, shughuli za ujenzi kama kubeba zege, kuwasaidia mafundi, kufagia barabara, kupiga debe, kazi za ndani(housegirl & houseboy) kazi ya kufyatua matofali, kazi ya uuzaji na kutangaza bidhaa(sales and marketing) maarufu kama kazi za promosheni, kazi ya kuuza, kazi ya kuuza mgahawani nk.

Halafu sasa kitu kimoja cha kuvutia zaidi ni kwamba ajira ni chanzo kizuri sana cha mtaji wa kuanzisha biashara zingine za kawaida kama za uuzaji wa bidhaa au utoaji wa huduma kwani kwa kutumia akiba ya mshahara utakaoupata unaweza ukaanza biashara yako.
   
Kwa ufupi sana nimejaribu kuorodhesha zile biashara ambazo mtu anaweza akazianzisha pasipokuwa na shilingi hata moja mfukoni. Hata hii ya 7 ambayo nimesema ipo katika mjadala nayo nimejitahidi sana kutaja zile kazi ama ajira ambazo kwa kweli hata hazihitaji utaalamu au ujuzi wa kuzifanya bali nguvu za mtu mwenyewe tu au akili ya kuzaliwa.

......................................................................................................

Ndugu msomaji wa blogu hii, ninaamini katika makala tunazokuletea mara kwa mara humu hukosi kitu cha kujifunza chenye manufaa kwako. Nakuomba endelea kusoma makala zetu kila wakati lakini pia jitahidi uweze kupata na moja ya vitabu vyetu hivi au semina na mafunzo mbalimbali tunayoyatoa, zijue huduma hizo kwa kubonyeza hayo maandishi au katika menu pale juu bonyeza palipoandikwa HUDUMA ZETU.

Hata ikiwa hujawa tayari kununua kitabu au kulipia semina na mafunzo basi pata angalao kitabu chetu tunachotoa bure bila malipo yeyote kwa kubonyeza maandishi yafuatayo, JIUNGE NA BLOGU HII kupata vitabu vizuri bila malipo kwa kuweka jina, email na namba yako ya simu katika kisanduku.


Kitabu rahisi kabisa unachoweza ukakinunua na ambacho kwa kweli ni kitabu kila mtu aliyewahi kukisoma hushindwa kuelewa ni kwanini tukiuze bei rahisi kiasi hicho ukilinganisha na yale yaliyokuwemo ndani yake ni MIFEREJI 7 YA PESA NA SIRI MATAJIRI WASIYOPENDA KUITOA, kitabu hiki unakipata kwa shilingi elfu 3 tu ndani ya email yako. Jaribu leo kusoma kitabu hiki usipoona tofauti na vitabu ulivyowahi kusoma vya ujasiriamali na maendeleo binafsi hakika nitakurudishia pesa yako. 

2 Responses to "BIASHARA NDOGONDOGO 7 ZILIZO NA FAIDA KUBWA UNAZOWEZA KUANZISHA BILA MTAJI KABISA"