SI KILA MUOKOTA MAKOPO NI KICHAA,WAPO WANAOTENGENEZA NOTI KUSHINDA KARANI WA BENKI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SI KILA MUOKOTA MAKOPO NI KICHAA,WAPO WANAOTENGENEZA NOTI KUSHINDA KARANI WA BENKI

Chupa za maji ya kunywa zilizokwishatumika, juisi na hata makopo na mikebe mbalimbali ya bidhaa zilizokwishatumika mara nyingi hutupwa katika majaa na kisha baadae huchukuliwa na mamlaka husika kwa ajili ya kwenda kutupwa kwenye madampo makubwa  ya takataka katika miji na majiji mbalimbali.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni baada ya ongezeko kubwa la viwanda vya kutengeneza maji ya kunywa na vinywaji baridi, kumekuwa na uhitaji wa kuzirudisha tena viwandani chupa hizo(recycling) kusudi ziweze kutumika tena na tena kama njia mojawapo ya kupunguza uchafuzi wa mazingira. Chupa hizi na mifuko ya nailoni baada ya kukusanywa na kurudishwa viwndani, huchambuliwa, kuoshwa, kusagwa na hatimaye kuyeyushwa tena kwa ajili ya kuunda chupa au vyombo vingine vya plastiki.

Mchakato huo wote huhitaji watu wa kukusanya chupa hizo mitaani, kazi ambayo watu wengi wamekuwa wakiifanya kwa ujira kidogo, kwa wastani chupa kiasi cha kilo moja huuzwa siyo zaidi ya shilingi 150 mpaka 200. Unaweza kukuta mtu kafungasha furushi kubwa la chupa lakini akikuambia kiasi cha fedha atakachokwenda kupata utashangaa. 

Hata hivyo ukizingatia kwamba gharama wanayotumia kuzipata ni kidogo na sana sana utakuta ni ule muda wao wanaoutumia tu, basi kiasi hicho cha fedha wanachopewa ni haki wala hawadhulumiwi. Ujira kidogo unaotokana na shughuli hii umesababisha ionekane na baadhi ya watu kuwa  ni kazi “kichaa” isiyolipa na inayostahili kufanywa na wale wenye ugonjwa wa akili tu. Hata wengine hudiriki kusema kwamba kila anayeokota chupa(makopo) basi ni sharti avae ‘maguo’ machafumachafu.

Nilikuwa miongoni mwa watu wanaoamini kauli hizo hasi lakini siku moja kwa mshangao mkubwa nilijikuta nabadilisha kabisa mtazamo wangu juu ya kazi hii “kichaa” baada ya kukutana na mtu mmoja mwanaume  aliyekuwa akiifanya kazi hii. Nilifanya naye mahojiano yasiyokuwa rasmi kwa kujaribu kumdodosa ni vipi kazi ile iliweza kumsaidia kimaisha baada ya kumuona alikuwa tofauti sana na waokota chupa wengine. Kwanza alionekana nadhifu, nguo zake zilikuwa safi, mkononi alishika fuko la kadiri, siyo kubwa sana na chupa alizookota alichagua zile zilizokuwa katika hali nzuri peke yake. Zaidi ya hapo, tofauti na waokotaji wengine, yeye hakuziponda chupa kabla ya kuzitia kapuni bali aliziweka kwa utaratibu zikiwa nzima.

Katika mahojiano nilibaini kuwa muokota chupa yule ni baba wa watoto watatu, anaishi na mkewe na wote anawatunza vyema kutokana na kipato anachopata kwa kazi hii, “mimi kila siku ni lazima niwabebee mke wangu na wanangu vipaja viwili vitatu vya kuku wakatafune, na mke wangu hubadilisha khanga kila anapohitaji, nimejenga japo ni kigogo na nina kakiwanja eka mbili Chanika” Aliniambia kwa kujidai. 

Lakini bado nilikuwa na maswali  kibao kichwani niliyohitaji kuyajua majibu yake, kwanza ni vipi anaweza kutengeneza pesa kiasi hicho zinazomuwezesha kufanya mambo ambayo hata mtu mwenye ajira ya wastani ama biashara ndogo ni vigumu kuweza kumiliki vitu anavyomiliki huku familia ikimtegemea. Nilikuwa na mashaka ikiwa ni hii kazi ya kuokota chupa za maji pekee iliyokuwa ikimuweka mjini. Alinihakikishia pasi na shaka yeyote kuwa kazi yake ilikuwa ni ile ile ya kuokota chupa za maji zilizokwisha tumika, bali yeye kinachomsaidia kuweza kutengeneza pesa nyingi ni ubunifu wa kipekee aliouanzisha.

Wakati waokota chupa wengi soko lao hutegemea wanunuzi wa jumla wanaonunua kwa ajili ya viwanda vinavyokwenda kuyeyusha kwa ajili ya kutengeneza upya chupa za maji, yeye hufanya tofauti kabisa. Amechagua soko lake tofauti. Katika maduka ya kawaida ya vyakula mara nyingi wale wenye maduka huhitaji chupa tupu kwa ajiliya kuwekea vitu mbali mbali mfano, mafuta ya taa, mafuta ya kula na hata wengine huhitaji kwa ajili ya kuhifadhia dawa za asili. Ili mtu uweze kuzipata kutokana na siku hizi kuwa hazizagai ovyo, inakubidi ufanye kazi ya ziada na hata kama utaokota basi ili upate nyingi ni lazima ukubali kuzunguka kwa muda mrefu mitaani  huku jua likikuwakia.

Baada ya baba huyu wa watoto watatu kubaini uhitaji mkubwa wa chupa hizi katika maduka na kwa watu wanaofanya shughuli mbalimbali zinazohitaji chupa tupu kwa bei rahisi, basi aliamua yeye kuziokota na kuwapelekea, na badala ya kuziuza kwa bei rahisi kimafungu kama wafanyavyo wale wanaokwenda kupima kwenye mzani, yeye huuza chupa moja ndogo ya robo lita kwa shilingi kati ya 50 mpaka 100, ile ya nusu lita huiuza kati ya sh. 100 mpaka 150 na ya lita moja sh. 100 mpaka 200. Kwa mtindo huo huweza kujipatia kiasi kikubwa cha fedha kwa siku tofauti na kama angeamua kuziuza kwa kilo.
Muokota chupa akiwa amebeba furushi la chupa za plastiki akipeleka kuuza kwa kilo.
Na ili kuziongezea dhamani zaidi wakati mwingine huzisafisha kwa maji safi ya moto na sabuni ambapo ni zile wanazotoa oda wateja malumu kama vile wanaozitumia kwa ajili ya kuwekea vinywaji mbali mbali kama  juisi, togwa na mbege. Anasema kwa zile chupa anazoosha bei yake huongezeka kidogo mfano badala yash. 50 huuza sh. 100 kila chupa. “Huwa nakuwa sina haraka, nyumbani nimelundika kiasi kikubwa cha chupa ambazo naziuza taratibu taratibu, sina ‘presha’ na biashara” alijigamba mgeni wangu huyu.


Nilibaini kumbe kweli siyo kila unayemuona akiokota vitu chakavu akili zake zimeruka, wengine wana mipango na mikakati mizuri kushinga hata wenye biashara rasmi za mitaji mikubwa. Wanatunza familia zao kwa kazi hizohizo na hata kujiwekea akiba kwa ajili ya kuja kufungua miradi mikubwa zaidi hapo baadaye. Kwa hiyo chunga usije ukawacheka!

Chanzo cha picha iliyotumika ni: jumamtanda.blogspot.com

0 Response to "SI KILA MUOKOTA MAKOPO NI KICHAA,WAPO WANAOTENGENEZA NOTI KUSHINDA KARANI WA BENKI "

Post a Comment