SHILINGI 500 MPYA YA SARAFU NI MAJANGA KWA WAFANYIBIASHARA! | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SHILINGI 500 MPYA YA SARAFU NI MAJANGA KWA WAFANYIBIASHARA!



“Mwanzoni nilifikiri ni utani  tu lakini baada ya ugomvi ule kukolea ndipo nilipobaini kumbe ulikuwa ni ugomvi dhahiri”  Anasimulia Shaban Saleh ambaye hivi karibuni katika duka moja maeneo ya Buguruni Malapa jirani na stendi ya daladala nusura mwenye duka na mteja wake wazichape “kavu kavu” kisa kikiwa ni sarafu mpya ya shilingi mia tano ambayo imeletwa mbadala na ile noti ya zamani ya shilingi 500, na ambayo pia ililalamikiwa mno kwa ubora wake hafifu.

Kisa kilianza hivi, Mteja baada ya kufika dukani alimpa mkononi yule muuzaji sarafu moja huku akimwambia, “Nipe sigara moja aina ya embsi . Muuzaji pasipo kuitazama ile sarafu na huku kama kawaida yake akidhani ni sarafu aliyoizoea ya shilingi miambili, aliitupilia katika droo lake la pesa na kisha  haraka haraka akachomoa sigara aina ya embasi na kumkabidhi yule mteja pasipo kumrudishia chenji. Mteja alikaa kimya akisubiri chenji yake lakini alishangaa kumuona muuza duka naye akiwa kimya bila dalili yeyote ya kumrudishia chenchi yake.

Ndipo yule mteja alipoamua kumuuliza muuzaduka chenji yake na ugomvi ukaanzia palepale, muuzaduka akishikilia kwamba sarafu aliyopewa ilikuwa shilingi mia mbili, iweje aseme ni shilingi mia tano?. Kwa upande mwingine yule mteja alijitahidi kumuelewesha muuzaji kwamba alichompa ni shilingi mia tano kwa msisitizo kiasi kwamba alitaka hata kuingia ndani hadi kwenye droo ya pesa akaionyeshe pesa yake lakini muuzaduka akamzuia.

Katika hali ile ya taharuki kubwa watu walianza kusogea karibu, na kuanza kumshauri muuza duka akubali kukagua pesa zake . Ilibainika kumbe yule muuzaduka hata uwepo wa kitu kinachoitwa sarafu ya mia tano hakuwa nao sembuse  kukubali kuwa alipewa shilingi mia tano na mteja. Ilibidi juhudi za ziada zifanywe na wale wasuluhishi akiwemo bwana huyu Shaaban kumuelimisha juu ya uwepo wa sarafu mpya y ash. 500 na ndipo muuza duka sasa alipokubali, na alipoangalia vizuri katika droo lake la pesa aligundua kulikuwa na sarafu mpya inayong’aa  lakini isiyokuwa na tofauti kubwa na sarafu ya shilingi mia mbili.


Watu wengi walitoa maoni yao wakisema kwamba sarafu hii mpya ya sh. 500 itaibua sintofahamu kubwa hasa kwa wafanya biashara hata kuliko ilivyokuwa kwa noti inayoondolewa kutokana na kwanza, kufanana mno na ile ya shilingi mia mbili kwa ukubwa na hata kwa umbo, “Ni heri hata wangeiwekea pembe mithili ya ile sh. 5 ya zamani ingelikuwa afadhali” Alisema mwananch mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja katika eneo la tukio. Pili wengine wanadai itakuwa mzigo kutokana na kuwa zamani hata benki waliweza kukupa hata mia tano za shilingi elfu hamsini na ukazibeba bila usumbufu lakini kwa sasa hivi haitawezekana hata kutembea na shilingi elfu kumi za sarafu mifukoni mwa nguo tena.


0 Response to "SHILINGI 500 MPYA YA SARAFU NI MAJANGA KWA WAFANYIBIASHARA!"

Post a Comment