SEMINA SIKU YA 5: MCHANGANUO WA BIASHARA YA KUSAGA UNGA WA DONA-HATUA KWA HATU | JIFUNZE UJASIRIAMALI

SEMINA SIKU YA 5: MCHANGANUO WA BIASHARA YA KUSAGA UNGA WA DONA-HATUA KWA HATU


mchanganuo wa biashara ya dona
Kabla hatujaendelea na semina yetu kwanza nikuombe sana radhi ndugu msomaji wangu kama ulikuwa ukifuatilia mfululizo wa somo hili toka siku ya kwanza kutokana na siku ya jana kushindwa kuweka somo kama tulivyoahidi. 

Kulikuwa na kuharibika kwa transofa maeneo yetu hivyo kwa siku nzima ya jana hadi leo hii jioni nikashindwa kuwasha pc(compyuta) kwa ajili ya kuhamishia masomo kwenye simu. Kwa hiyo siku ya leo nalazimika kuweka masomo ya siku 2 na kesho tutamalizia kama kawaida sehemu ya mwisho.


Katika siku hii ya 5 tutaandika Sura mbili, sura ya

6. Mpango wa Uendeshaji na Sura ya
7. Utawala
Tuanze na sura ya 6;


6.0 Mpango wa Uendeshaji
Kwenye sura hii ya Utekelezaji  kwa kawaida huwa inahusiana hasa na jinsi biashara inavyofanya kazi(itakavyoendesha mambo mbalimbali) kila siku. Hapa chini ni vipengele vidogo mbalimbali unavyoweza kuvitumia katika sura hii;

1.   Hatua mradi ulipofikia mpaka sasa hivi
2.   Mchakato mzima wa uzalishaji utakavyokuwa
3.   Teknolojia/maelezo ya kiufundi
4.   Vihatarishi vya mradi
5.   Eneo
6.   Vifaa na gharama mbalimbali
7.   Malighafi na vyanzo vyake
8.   Masuala ya kisheria
9.   Sera ya mikopo nk.

Kwa upande wangu mimi kwenye mchanganuo huu wa USADO Milling kama unavyoona nimechagua tu baadhi ya vipengele hivyo vidogo kulingana na mahitaji ya biashara hii na nilielezea vitu vifuatavyo;

Mradi ulipofikia
Nimetaja vitendo mbalimbali muhimu vinavyotakiwa kutekelezwa ili mradi uweze kuanza na kila kimoja nikaeleza kimefikia wapi mpaka sasa hivi. Unaweza kucheki katika mchanganuo huo vitendo hivyo.

Vihatarishi vya mradi
Biashara inaweza ikakumbana na hatari au vikwazo mbalimbali ambavyo biashara nyingine mpya hukutana nazo katika uchumi wa soko lenye ushindani mkali. Na ikiwa basi hatari hizo hazitaweza kubainishwa na kushughulikiwa mapema basi biashara inaweza ikafa muda mfupi. Katika Mchanganuo huu nimeainisha hatari kubwa 4, USADO Milling inazoweza kukumbana nazo na jinsi ya kuzishughulikia.

Mahitaji ya Kisheria
Katika kipengele hiki nimetaja taasisi mbalimbali USADO Milling inazowajibika moja kwa moja kujisajili au kulipia tozo mbalimbali zinazotakiwa na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Maelezo ya Kiufundi.
Hapa nimeelezea Mifumo mikubwa 4 ambayo mahindi hupitia kabla ya kupata dona safi na salama. Pia mambo mengine ya kiufundi niliyoainisha hapa ni pamoja na uwezo wa mota ya mashine ya kusaga ambao ni Horse Power 40 saizi ya kinu namba 100, kiasi cha umeme Kilowatts 29 kwa saa pamoja na taarifa nyinginezo kama vile chanzo cha mashine hizo ambacho ni taasisi ya SIDO tawi la Vingunguti Dar es salaam.

Eneo.
Hapa nimeelezea jinsi eneo walilochagua USADO Milling la Mbezi mwisho lilivyokuwa la kimkakati kutegemeana na soko wanalolilenga na mikakati yao kwa ujumla. Mambo mengine ya kiufundi niliyoyaelezea katika Sura hii ni pamoja na;

·      Uoshaji wa mahindi
·      Ufungashaji unga
·      Usambazaji
·      Malighafi
·      Vifaa na mashine
·      Mapato na gharama mbalimbali

Na hapa ndio mwisho wa Sura ya 6 ya Mpango wa biashara hii ya USADO Milling, Karibu kwenye Sura ya 7, “Utawala na Nguvukazi”


7.0 Utawala na Nguvukazi.
Kama kawaida Sura inaanza na muhtasari mdogo unaoandikwa mwishoni na nitaacha kwanza nafasi ya aya moja hivi. Halafu nitazingatia vipengele vidogo vinavyounda sura hii ambavyo mara nyingi huwa ni hivi hapa chini;

7.1 Mfumo wa uongozi
7.2 Timu ya uongozi na wafanyakazi
7.3 Mpango wa mishahara

Mimi nilianza na kipengele kifuatacho;

7.1 Muundo wa Utawala
Hapa nimeelezea kwa maneno tu na siyo kuchora chati ya utawala kwa kuwa timu ya wafanyakazi wa USADO Milling bado ina watu wachache. Nimetaja kila kiongozi, wadhifa wake kwenye kampuni, historia yake kitaaluma na kikazi pamoja na uzoefu aliokuwa nao kulingana na majukumu atakayokuwa nayo kwenye kampuni.

7.2 Pengo la Utawala:
Hapa nimeelezea mapungufu yaliyopo katika nafasi mbalimbali za kiuongozi na kiutendaji. Ni nafasi gani zinahitajika kujazwa na ni lini nafasi hizo zitajazwa. Pia nimeeleza njia mbadala zitakazotumika ili kujaza pengo lililopo.

7.3 Mpango wa Mishahara
Katika kipengele hiki kidogo nimeanza na maelezo kisha nikachora jedwali linaloonyesha kiasi cha mishahara ya wafanyakazi wote kwenye kampuni kwa kila mwaka kwa miaka yote mitatu. Nilianza kwa kujumlisha mishahara ya mfanyakazi mmoja mmoja kila mwezi kisha kwa mwaka. Namba hizi nitakuja kuzitumia pia kwenye ripoti ya Faida na Hasara hapo baadae

Na hapa ndio mwisho wa Sura ya 7 ya Uongozi au Utawala. Sura inayofuata ni Sura ya Fedha.

SEMINA SIKU-4                SEMINA SIKU-6
                                                                                                               

0 Response to "SEMINA SIKU YA 5: MCHANGANUO WA BIASHARA YA KUSAGA UNGA WA DONA-HATUA KWA HATU"

Post a Comment