Sura hii ya Fedha ni ndefu lakini ni
muhimu katika mpango wa biashara, nimeweka mkazo sana katika Ripoti ya Faida na
hasara kwani ndiyo chanzo cha namba katika ripoti nyingine zote mbili za
Mtiririko wa fedha(cash flow) na Mizania ya biashara(Balance sheet)
8.0
Mpango wa Fedha
Kama zilivyo Sura nyingine zote zilizopita hii nayo kuna
muhtasari mdogo unaogusa zile sehemu muhimu zote za Sura yote. Lakini kabla
hatujaendelea hebu kwanza tuone ni vipengele gani vidogo vinavyounda sura nzima
ya fedha;
7.1
Dhana/makisio muhimu
7.2
Tathmini ya mauzo ya kurudisha gharama (Break Even Analysis)
7.3
Makisio ya faida na hasara
7.4
Makisio ya mtiririko wa fedha
7.5
Makisio ya mali na madeni (mizania ya biashara)
7.6
Sehemu muhimu za biashara
8.1
Makisio muhimu
Kwenye makisio muhimu nimeorodhesha tu vile vigezo (assumptions)
nilizotumia katika kuamua hesabu zangu ziwe vipi. Kwa mfano ukuaji wa mauzo
mwaka wa pili na wa tatu nilitumia kigezo cha kuongezeka kwa asilimia 25% na
asilimia 50%, haya ni makisio (assumptions) kulingana na tafiti.
Pia kukisia vitu kama wafanyakazi 3 mwaka wa kwanza, kodi ya
mapato na riba ya mkopo kama mpango huu ungehusisha mkopo pia vyote hivyo ni
makisio muhimu ambayo ningepaswa kuandika hapa kwa kifupi kusudi msomaji wa
mpango huu wa USADO Milling atambue hesabu zangu zimefikajefikaje pale zilipo
na wala sikuzitoa hewani tu.
8.2 Tathmini ya Mauzo yatakayorudisha Gharama zote kwa
mwezi (Break Even Analysis)
Kipengele hiki kidogo ingawa nimekiweka hapa lakini kimsingi
kinapaswa kuandikwa baada ya kumaliza kipengele kinachofuata cha Ripoti
ya faida na hasara kwasababu data zake zote inabidi zitokane na ripoti
hiyo. Hata hivyo nitaeleza namna nilivyokokotoa lakini ukumbuke data hizo
zimetokana na kipengele kinachofuata baada ya hiki.
“Break Even Analysis” ni tathmini ya kiasi cha mauzo yanayohitajika
ili kurudisha gharama zote zilizotumika katika kipindi fulani, inaweza ikawa
mwezi, mwaka au kipindi kingine chochote kile ila mwezi ndiyo hutumika mara
nyingi zaidi.
Namba zote zinazotumika kwenye tathmini hii
zinapatikana kutoka katika jedwali la Ripoti
ya Faida na Hasara, hivyo ni vizuri kuifanya tathmini hii baada ya
kukamilisha jedwali hilo.
Ili kukokotoa Mauzo hayo tutahitaji kuwa na
vitu 3 muhimu vifuatavyo;
· Wastani
wa gharama za kudumu kwa mwezi
· Asilimia
ya Gharama za mauzo kwenye mauzo
· Kanuni
ya kukokotoa mauzo hayo(Break even
Formula)
Katika jedwali la Faida na Hasara wastani wa
gharama za kudumu kwa mwezi ni zile gharama za uendeshaji kwa mwezi ambazo ni
shilingi 827,000
ukitazama
jedwali la faida na hasara kwenye mchanganuo wako wa USADO, nimechukua jumla ya
gharama za uendeshaji kwa mwaka sh. 9,924,000 kisha nikagawa kwa miezi 12 kupata
za mwezi mmoja.
Asilimia
ya Gharama za mauzo kwenye Mauzo, nimechukua jumla ya
gharama zinazobadilika za mauzo sh. 55,062,400
kutoka katika jedwali la makisio ya faida na hasara mwaka wa kwanza kisha
nikagawa kwa Mauzo ambayo ni sh.
75,942,000. Hizi ukichukua za mwezi au za mwaka asilimia utapa
hiyohiyo moja ambayo nimepata asilimia 72.5%
au
0.725
Kanuni
ya kukokotoa “Break Even Sales” zipo nyingi kulingana na
data/taarifa unazopewa, kwa mfano hapa tayari tuna mauzo, gharama za mauzo na
gharama za kudumu kama ilivyokuwa kwa ‘case’ yetu hapa nitatumia kanuni
ifuatayo;
(Nikisema
Break Even sales namaanisha Mauzo ya kurudisha gharama zote zilizotumika yaani
mapato yamelingana na gharama, hamna faida wala hasara)
Chati ya mauzo hayo nimeitengeneza kwa
kutumia data za “Mauzo vs Faida” na data hizi nimezipata kwa kutumia kanuni
(formula) hii hapa chini;
Faida = Mauzo – Gharama za mauzo –
gharama za kudumu
Kisha nikatengeneza jedwali la Mauzo vs
Faida,
Mauzo
|
0
|
5,000,000
|
10,000,000
|
15,000,000
|
20,000,000
|
25,000,000
|
Faida
|
- 827,000
|
548,000
|
1,923,000
|
3,298,000
|
4,673,000
|
6,048,000
|
Lakini kumbuka kila thamani ya gharama za
mauzo kulingana na data zetu pale juu ni asilimia 72.5% au 0.725 ya Mauzo
Hivyo Fomula yetu itakuwa kama ifuatavyo
Faida = Mauzo – 0.725Mauzo – 827,000
Baada ya hapo katika kila chumba nilitafuta thamani ya faida kwa
kutumia fomula yetu hapo juu katika kila mauzo, mfano nikiweka 0 kila penye
mauzo, faida itakuwa kama ifuatavyo;
Faida = 0 – (0.725 X 0) – 827,000 = - 827,000
Mauzo yakiwa 5,000,000 Faida itakuwa kama ifuatavyo;
Faida = 5,000,000 – (0.725 x 5000,000) – 827,000 = 548,000
Na kuendelea hadi viboksi vyote vya faida kwenye jedwali
vimejaa. Sasa Nikichora chati kwa kutumia data zangu hizo utaona mahali faida
itakapokuwa 0 ndipo Break
even point ilipo na hapo ndipo mistari yote 2 ule wa mauzo na wa faida
hukutana. Tazama chati hiyo hapa chini;
8.3
Makisio ya Faida na Hasara.
Katika ripoti hii ya faida na hasara
nitatumia hesabu ndogondogo ambazo zimeshajitokeza kwenye vipengele vingine vya
mchanganuo huu huko nyuma. Ukichunguza mchanganuo wetu huu tangu mwanzoni mpaka
sasa utagundua kuna sehemu kadhaa nimekuwa nikigusa hesabu au namba. Kwahiyo
katika sehemu hizo zote ndogondogo sasa hapa ndio nitazichukua na kuzitumia
kwenye Sura hii kuu inayohusu fedha.
Sura zilizogusa mahesabu au namba ni hizi
zifuatazo;
1. Sura ya pili, Maelezo
ya Biashara katika kipengele kidogo cha ‘2.4’ Kianzio kwenye majedwali ya
kianzio na Mizania ya biashara.
2. Sura ya ‘5.0’
kipengele kidogo cha ‘5.3’, Makisio ya mauzo na gharama za mauzo
3. Kwenye kipengele cha
6.0 cha Uendeshaji katika majedwali ya vifaa, malighafi na gharama
4. Sura ya ‘7.0’
kipengele kidogo cha ‘7.3’, Uongozi na Wafanyakazi kwenye jedwali la mpango wa
mishahara
Katika Makisio ya faida na hasara kuna vitu
vikubwa 5 vifuatavyo,
1. Mauzo
2. Gharama za mauzo (zinazobadilika)
3. Gharama za uendeshaji(za kudumu)
4. Kodi
5. Faida halisi
1. Mauzo
yapo kwenye makisio ya mauzo sura ya 5 kama nilivyoeleza hapo juu na nimekisia
mauzo ya mwaka mzima.
2. Gharama
za mauzo (zinazobadilika) zinapatikana katika sura hiyohiyo ya 5 kwani huwa
zinaambatana na mauzo, ni zile gharama za moja kwa moja za mahindi yanayotumika
katika uzalishaji wa dona pamoja na gharama zote za moja kwa moja
zinazoambatana na na uzalishaji huo kama, vibarua, umeme, vifungashio na umeme
wa kusagia.
3. Gharama
za uendeshaji za kudumu; hizi ni zile gharama za kila mwezi ambazo hata
kama hamna uzalishaji lakini bado zitalipwa kama vile mishahara ya wafanyakazi
wa kudumu, pango la eneo, uchakavu wa vifaa kama mashine nk. Gharama hizi
tunazipata katika sura ya 6 kwenye kipengele cha Uendeshaji kwenye jedwali la
gharama za kudumu.
4. Kodi
ya mapato, imekisiwa kulingana na viwango mamlaka husika inazotoza biashara
nyingine zinazofanana na hii.
5. Faida
Halisi: Hapa ndiyo hitimisho la taarifa hii ya mapato na matumizi ya USADO
Milling. Faida halisi nimeipata baada ya kutoa vitu vyote 3 vilivyotangulia
kutoka kwenye Mauzo.
Kwa kawaida Ripoti hii nitaanza na makisio ya
kila mwezi kwa miezi yote 12 ya kwanza, kisha ya mwaka 1 na miaka 2 inayofuata.
(a)
Makisio ya kila mwezi, miezi yote 12 ya mwaka wa 1
Ili kukisia miezi nitahitaji “Spreadsheet” /
“graph paper” au programu ya kompyuta kama vile Microsoft Excell au hata naweza
tu kutumia Microsoft word kuchora jedwali lenye miezi 12 ambalo ndilo
nitakalotumia kukisia namba zangu. Kama ningeamua kutumia karatasi basi
ningechora jedwali lenye safu zilizolala (rows) na zilizosimama (columns) mfano
wa grafu.
Jedwali langu zima litaonekana kama hili hapa
chini isipokuwa mimi hapa sijaweka miezi yote 12 kutokana na udogo wa nafasi na
kwa ajili ya kuonekana vizuri bila ‘kuzoom’,
nimeweka tu mpaka mwezi wa 5 ambao ni Julai; Jedwali zima unaweza kuliona
katika mchanganuo kamili wa USADO Milling
Kwenye safu zilizosimama (columns), kuna miezi 12. Mwaka wa USADO unaanzia mwezi Machi, hivyo nitaanza kuhesabu mwezi wa kwanza kuttoka “Machi” na kumalizika Februari.
Katika
safu zilizolala (rows), kuna vitu vifuatavyo;
1) Safu
ya kwanza kabisa nimeweka mauzo. Mauzo tayari katika sura ya Mikakati kipengele
kidogo cha 5.3.1 nilishakisia miezi yote na hapa kazi ni kuyaweka tu, kama
uonavyo hapo juu, mwezi januari ni sh. 5,620,000
mwezi Julai sh. 6,030,000 na
kuendelea…..mpaka mwezi Desemba sh. 7,830,000
ingawa jedwali limeishia tu Julai
2) Safu
inayofuata nimeweka Ghama za Mauzo, nazo tayari nilishazipata kwa miezi yote
12, ni kuziweka tu.
3) Safu
ya 3 ni Faida Ghafi, Faida ghafi nimechukua mauzo nikatoa gharama za mauzo.
4) Safu
ya 4 nikaweka asilimia ya faida ghafi kwa mauzo ambayo kutokana na mauzo na
gharama zake kutofautiana kila mwezi basi kila mwezi una asilimia tofauti mfano
Machi ni asilimia 26.3%,
Mei 21.2% na Julai 22.7%
5) Inafuata
safu ya Gharama za uendeshaji. Hizi nazo nilikwishakisia katika sura ya 6
ambazo nilizitaja kuwa ni pango, mishahara, matangazo, umeme & maji, tozo
mbalimbali, uchakavu na dharura. Jumla yake naweka pale chini kabisa ya vitu
vyote hivyo vilivyotajwa
6) Faida
kabla ya kodi na riba, hii ni safu inayopatikana baada ya kuchukua Faida ghafi
niliyoipata pale juu namba 3 na kutoa jumla ya Gharama zote za uendeshaji namba
5.
7) Inafuata
Riba ya mkopo ambayo inatokana na mkopo ikiwa USADO Milling wangelikuwa wameomba
mkopo mahali. Lakini katika Mpango huu tunaambiwa Isabella na Maurine walitoa
fedha zao wenyewe mfukoni walizodunduliza hivyo nimeweka sifuri pale (0) kila
mwezi.
8) Safu
ya Kodi ya mapato, Hii imepatikana kutokana na makisio ya yaliyofanyika
kulingana na utafiti kwa biashara nyingine zinazofanana na hii ya USADO.
9) Faida
Halisi, safu hii nimechukua Faida kabla ya kodi na Riba niliyokwishapata hapo
juu namba 6 kisha nikatoa Riba na Kodi. Jibu lake ndio FAIDA HALISI.
10) Safu
ya mwisho kabisa katika jedwali hili la Faida na Hasara ni asilimia ya faida
halisi kwa mauzo ambayo nimechukua faida halisi nikagawa kwa Mauzo kisha
kuzidisha mara 100. Na nimefanya hivyo kwa miezi yote 12 kama unavyoweza kuona
hapo katika mchanganuo wako wa USADO Milling.
Kwa ujumla jedwali hili linatuthibitishia
kanuni isemayo;
FAIDA
HALISI = MAUZO – GHARAMA ZOTE - KODI
(b)Makisio
ya mwaka wa kwanza.
Ninaposema mwaka wa 1 au nikisema 2020 kwa
biashara hii ya USADO Milling ni kitu kilekile. Baaada ya kumaliza kazi ya
kukisia miezi yote 12 maana yake na ya mwaka wa kwanza pia nakuwa tayari
nimeshamaliza.
Hapa ukijumlisha mauzo yote ya miezi 12
utapata jumla ni sh. 75,942,000 ambayo ndiyo mauzo ya USADO
ya mwaka mzima wa 2020 na unaona nimeweka pale chini katika jedwali la mwaka,
halikadhalika ukijumlisha safu zingine zote zilizolala (rows) utapata thamani
iliyowekwa katika jedwali hili kama unavyoona.
Chakufanya tu ni kujumlisha kila safu
iliyolala miezi yote 12 kisha majibu yake unayaweka katika jedwali la mwaka wa
1 kama ifuatavyo;
MUHIMU: Mpaka kufikia hapo watu wengi wanakuwa
wameshamaliza kipengele hiki cha fedha ikiwa mchanganuo wako huna ulazima wa
kukisia hesabu za miaka 2 inayofuata, pengine umeandika tu kwa ajili ya
uendeshaji wa biashara yako hamna mdau au taasisi yeyote ile iliyokutaka
uwasilishe mpango wa biashara.
(c)Makisio
ya Miaka 2 inayofuata: mwaka wa pili na wa tatu.
Kama utakumbuka wakati nikikisia mauzo na
gharama za mauzo katika sura ya 5.0 nilikisia mauzo ya mwaka wa kwanza 2020 kwa
kujumlisha mauzo ya miezi yote 12 kisha nikasema kwa miaka miwili inayofuata
yaani 2021 na 2022 nitatumia kanuni ya ongezeko la mauzo kwa asilimia na
nilipata mauzo ya mwaka wa 2 baada ya kukisia ongezeko la asilimia 25% ya mwaka
wa 1 na asilimia 50% mwaka wa 2 kupata mauzo ya mwaka wa tatu.
Nikapata mwaka wa pili kuwa ni sh. 94,927,500 na
mwaka wa tatu sh. 142,391,250.
Halikadhalika kwa upande wa gharama za mauzo pia nimefanya hivyohivyo kama
jedwali linavyoonyesha hapa chini.
Gharama
za Uendeshaji mwaka wa 2 na 3.
Kumbuka hapa nataka makisio ya mwaka wa 2 na
wa 3 zaidi kwani mwaka wa kwanza tayari nimeshapata kila kitu. Gharama za
uendeshaji ni rahisi kukisia na huwa hazibadiliki sana kwa mfano pango
ulilolipa mwaka jana si rahisi mwaka huu liwe limepanda na hata mishahara ni
hivyohivyo.
Kwa hiyo nitaangalia tu zile gharama ambazo
kulingana na biashara kukua au kusinyaa zinaweza kubadilika kwa mfano vitu kama
gharama za mishahara, pango umeme, maji, na fedha za dharura. Hapa mtu unatumia
tu akili yako ya kuzaliwa“common sense”
kama mtu unayetarajia kuifanya hiyo biashara.
1) Kwa
mfano katika biashara hii ya USADO Milling mishahara mwaka wa pili na wa tatu
utaona itaongezeka kutoka sh. 4,800,000
mwaka
wa 1 mpaka sh. 7,200,000
mwaka
wa 2 kutokana na sababu kwamba kuna Meneja atakayeajiriwa kuanzia mwaka huo.
Mwaka wa 3 pia ataongezeka mtu mmoja na mishahara nayo itaongezeka na kuwa sh. 12,000,000
2) Pango
la eneo la biashara kwa mwaka wa 2 litaendelea kubakia vile vile lakini litaongezeka
mwaka wa 3.
3) Gharama
za matangazo mwaka wa pili zimebakia vilevile sh. 1,200,000 lakini mwaka wa 3
zitaongezeka mpaka sh. 1,500,000
na
hii inatokana na kampuni kukua hivyo shughuli za matangazo nazo kuongezeka
4) Gharama
za umeme na maji zitaongezeka kila mwaka kutokana na sababu kwamba shughuli za kiwanda
zinakisiwa kukua, vifaa mbalimbali kama vile taa, feni, heater na bomba la maji
vinatarajiwa kufanya kazi mara dufu tofauti na mwaka wa kwanza.
5) Fedha
za dharura, matengenezo na tozo mbalimbali pia zinakisiwa kuongezeka kwasababu
biashara ikikua changamoto nazo huongezeka pamoja na tozo za serikali.
6) Gharama
za Riba kwenye mchanganuo huu hatuna kwasababu kampuni haikukopa.
7) Kodi
ya mapato nayo nimekisia itaongezeka kidogo mwaka wa 3 kutokana na biashara
nayo kukua.
Baada
ya kukisia gharama zote za uendeshaji na kupata jumla yake nitakokotoa faida
kabla ya kodi na riba kwa kuchukua Faida ghafi kisha nitoe jumla hiyo ya
gharama za uendeshaji kwa miaka yote 2.
Pia
nitatoa kodi ya mapato kama nilivyofanya katika mwaka wa 1 na kupata FAIDA HALISI. Mpaka hapo nitakuwa
nimekwishamaliza kukokotoa Faida na Hasara kwa miaka yote mitatu na jedwali
letu sasa litaonekana kama ifuatavyo;
MUHIMU
SANA:
Kumbuka jedwali la Faida na Hasara ndio
msingi wa majedwali ya Ripoti nyingine zote 2 zinazofuata za “Mtiririko wa
fedha” na “Mizania ya biashara” kwani karibu vitu vyote vya ripoti hizo
hutegemea namba kutoka katika jedwali hili, hivyo ni vizuri kuhakikisha jedwali
hili linakisiwa kwa umakini.
Na pia kama umeandika mpango wako wa biashara
unaweza ukaweka jedwali hili tu peke yake likatosha kuwakilisha mawazo yako
mazima kwenye kipengele cha fedha kwa ujumla. Na isitoshe hii ndiyo Ripoti
rahisi zaidi kukokotoa moja kwa moja bila hata ya kuhitaji utaalamu mkubwa.
8.4 Makisio ya mtiririko wa fedha.
(1)Miezi
12 ya mwaka wa 1
Katika Ripoti hii pia naanza na makisio ya
miezi 12 ya mwaka wa kwanza kama tulivyofanya kwenye faida na hasara, kisha nitatafuta
jumla ya miezi yote 12 kukamilisha makisio ya mwaka mzima wa kwanza. Baada ya
hapo sasa nitakisia miaka 2 inayofuata.
MUHIMU:
Lakini kuna kitu kimoja hapa nataka ujue mapema kabla hatujaendelea, Kuna
vipengele katika ripoti hii wakati unapokuwa ukivikokotoa, moja kwa moja pia
unakuwa ukikamilisha na baadhi ya vipengele katika ripoti ya 3 ya Mali na
Madeni (Mizania).
Na hii ndio sababu tunasema kwamba ripoti
hizi zote 3 zinategemeana na kuhusiana, makosa katika ripoti moja husababisha
ripoti nyingine 2 pia kuwa na makosa na hesabu hazitaoana. Pia vipengele vya
ripoti hii vingi vinatokana na jedwali lile la Faida na Hasara tulilomaliza hivi punde.
Ripoti ina jedwali lenye sehemu kuu 2, upande
wa juu ni wa Fedha taslimu zinazoingia(Fedha
ingia) na upande wa chini ni wa fedha taslimu zinazotoka(Fedha toka). Juu kabisa kuna kianzio na
chini kabisa safu mbili zilizolala kuna Mtiririko wa fedha pamoja na salio la
mwisho kwa kila mwezi. Hapo chini nimeweka miezi 5 tu, jedwali kamili unaweza
kuliona katika mchanganuo kamili wa USADO Mlilling.
8.5 Makisio ya mali na madeni (Mizania ya Biashara).
Jedwali la ripoti ya Mali na Madeni nayo
imegawanyika katika sehemu kuu 2, sehemu ya kwanza ni ya juu ambayo hukaa
Rasilimali (Mali) au Asseti, Sehemu ya pili ni upande wa chini ambao huwekwa
Mtaji wa wawekezaji pamoja na Madeni (vyanzo vya Mali hizo)
Tuanze
na makisio ya kila mwezi kwa mwaka wa 1
Baada ya kukamilisha zile ripoti 2, ripoti
hii ya tatu nayo inakuwa imekwishakamilika kwani nitakuwa nikitumia namba
kutoka majedwali mengine kuikamilisha.
Nitachora jedwali letu lenye safu
zilizosimama (columns) 13, safu moja itatumika kuweka namba za kuanzia kutoka
katika lile jedwali la Mizania ya mwanzo kabisa wakati nikikisia Mahitaji na
chanzo cha mahitaji sura ya 2, huku safu 12 zikiwa ni za miezi 12. Safu
zilizolala (rows) zinawakilisha hesabu mbalimbali (accounts)
Ripoti hii tofauti na zile mbili ya Faida na
hasara na ile ya Mtiririko wa fedha, ili kupata makisio ya mwaka mzima wa
kwanza sitajumlisha safu zilizolala (rows), bali nitachukua safu nzima
iliyosimama (column) ya mwezi wa 12. Kwa upande wa miaka 2 inayofuata nitafanya
makadirio kwa kutumia asilimia ya mauzo ya kila mwaka. Katika jedwali lifuatalo
nimeweka hadi mwezi wa 4 na miezi yote 12 inapatikana katika Mchanganuo kamili
wa USADO Milling.
Ikiwa Hesabu zako utakuwa umezifanya kwa usahihi,
utaona jumla ya mtaji na deni utakayopata hapo upande wa chini, inalingana
sawasawa kabisa na jumla ya (rasilimali) Mali uliyopata upande ule wa juu bila
hata ya kulazimisha na huo ndio ushahidi kuwa Ripoti hizi 3 zinashirikiana.
8.6 Sehemu muhimu za biashara.
Kuna uwianao wa aina nyingi lakini hapa
nimeweka baadhi yake tu kwa kuziorodhesha. Jedwali zima lenye sehemu hizo zote
lipo katika mchanganuo mzima wa USADO Milling.
Asilimia
ya Mauzo
Huu ni uwiano unaowezesha mtu kujua sehemu
mbalimbali mfano gharama za mauzo, faida ghafi, gharama za uendeshaji na faida
halisi ni asilimia ngapi ya mauzo kwa kugawa vitu hivyo kwa mauzo kisha
unazidisha mara 100. Hukuwezesha kulinganisha biashara husika na nyingine za
washindani.
1)
Asilimia ya Faida kwa mali zote/Return on Assets (ROA)
Uwiano huu unachukua Faida halisi kisha
unagawa kwa Jumla ya mali zote mara 100
2)
Faida halisi kwa mtaji wa wawekezaji / Return on Investment (ROI),
huu ni uwiano muhimu unaomwezesha mwekezaji kuwa na matumaini kwamba fedha zake
zitarudi, unachukua faida halisi unagawa kwa mtaji wa mwekezaji mara 100. Kwa
USADO nimepata ni asilimia 20% mpaka 22%
3)
Gharama za mauzo/bidhaa za stoo/Inventory Turn Over.
Uwiano huu unachukua Gharama za mauzo unagawa
kwa wastani wa salio la Malighafi za stoo, hupima biashara inauza haraka kiasi
gani, uwiano mkubwa, 5 mpaka 9 ni ishara kwamba biashara inauza faster zaidi,
mzigo haukai. Katika mpango wa USADO Milling nilipata 8.3 kwa mwaka 2020 ambao
ni mzuri
4)
PAY BACK PERIOD (Muda wa kurudisha mtaji)
Haya ni makadirio ya muda kianzio chote
kitarudi na hupatikana kwa kuchukua kianzio na kugawa kwa Faida halisi. Jibu
lake ndiyo muda mtaji wote unakisiwa kurudi
44,600,000
/ 10,655,600= 4.18
Sawa na miaka 4 na miezi 2
Mwisho wa Sura hii ya 8 kesho tutamalizia na Sura ya 9. Kwa swali lolote lile au maoni unakaribishwa. Asante.
SEMINA SIKU-5 SEMINA SIKU-7
0 Response to "SEMINA SIKU YA 6: MPANGO WA FEDHA MCHANGANUO WA BIASHARA KIWANDA CHA DONA (USADO MILLING"
Post a Comment